The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vijana wa Tanzania: Uwezo Usiochochewa au Kizazi Kinachosahaulika?

anzania itanufaika zaidi endapo kama vijana wake wengi watashiriki kwenye chaguzi kama wagombea na wapiga kura pia.

subscribe to our newsletter!

Pengine hii ni aina nyingine ya changamoto ambayo Tanzania, katika medani za siasa, inakumbana nayo kutokana na uhaba wa vijana ambao wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi, kuanzia ngazi ya kitongoji mpaka ngazi ya taifa. 

Tafiti zinaonesha kwamba kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa mfano, ni asilimia 64 pekee ya vijana walioshiriki katika uchaguzi huo. Takwimu zinaonyesha kuwa ushiriki wa vijana ulikuwa kama wapigaji kura, na asilimia ndogo zaidi ikijitokeza kama wagombea kwenye nafasi mbalimbali za uongozi. 

Kwenye takwimu hizo, asilimia 35 ilikuwa ni vijana waligombea nafasi za mwenyekiti wa kijiji, nafasi za udiwani (asilimia 27), na nafasi za ndani ya vyama vyao vya kisiasa (asilimia 24), huku asilimia 14 wakihudumu kama wajumbe wa mabaraza ya serikali za mitaa. 

Mgawanyo huu unaonyesha namna idadi kubwa ya vijana hushiriki katika mchakato wa kidemokrasia, lakini ni wachache tu wanaochukua nafasi za uongozi au kugombea katika chaguzi.

Siyo kwamba haieleweki ni kwa nini hakuna mlingano baina ya takwimu za vijana wanaopatikana katika taifa na vijana wanaojitoa mbele kuwania nafasi za uongozi na ushirikiano unaopatikana kutoka kwa vijana wenzao katika upigiwaji wa kura. 

SOMA ZAIDI: Uzoefu wa Wanasiasa Wakongwe na Ushauri Wao kwa Wagombea Vijana, Wanawake Kuelekea Chaguzi 

Wanaogombea nafasi za uongozi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa pesa za kuwawezesha kushiriki katika kampeni kwani mchakato huo unahitajika pesa nyingi na pasipo kuwa na pesa zoezi la ushiriki linakuwa gumu. 

Pia, uaminifu mdogo kuanzia ngazi za vyama kwa kivuli cha ukosefu wa uzoefu na kusababisha vijana kukosa nafasi za kuwania uongozi na mwisho wake kuonekana watu walewale ambao wamekwisha zoeleka. Swali ni lini vijana hawa watapata uzoefu kama hawapewi nafasi? 

Upande wa pili, kwa vijana ambao wanategemewa kwenda kupiga kura, nao wamekuwa na maoni yao kadhaa kwa nini hawajitokezi kwenda kupiga kura pale inapotakiwa kufanya hivyo, wengi wao wakisema “Hata kama nikipiga kura, hakuna kitakachobadilika kwa maana kila kitu kimeshapangwa.” 

Kwa hiyo, haoni haja ya kwenda kupiga kura. Wengine husema kwamba ni maslahi ya kiongozi na siyo kwa manufaa yetu sisi wanajamii, wameshuhudia mara kadhaa viongozi kubadilika pindi wakishapata kura na kutotimiza yale ambayo wameahidi kwenye jamii zao. 

Lakini je, hili suala linahitaji kuendelea kuwa hivi na nani anapaswa kulibadili pasipo kuchukuliwa hatua? Tukiyapa mgongo matatizo yetu, tukitegemea yaje kutatuliwa na mtu mwingine ambaye hatujui atakuja lini, kutokea wapi na saa ngapi je ni sawa? Tunahitaji kuanza sasa.

SOMA ZAIDI: Ni Hatari Kwa Nchi Kuwa na Vijana Wanaodhani Wanaweza Kuishi kwa Kusifia Wengine Badala ya Kufanya Kazi

Ni muda wa kuweka tofauti zetu pembeni na kuangalia namna ya kujenga taifa lililo imara zaidi, ikiwepo uzingatiaji wa uwepo wa vijana katika ngazi tofauti za uongozi, na hii haina maana wakabidhiwe tu mkononi pasipo kukidhi vigezo na masharti stahiki vya kuwepo mahala husika ni muhimu kujiridhisha kuwa kiongozi anayekuwepo nafasi husika amefikia vigezo vinavyotakiwa.

Lakini pia, upatikanaji wa taarifa ni jambo la msingi zaidi kwa kila pande ili kuelewa nani anatakiwa kufanya nini, wapi na kwa muda upi suala husika linatakiwa kufanyika. Kwa mfano, suala la elimu ya uraia siyo tu kupatikana shuleni bali hata kwenye jamii wanatakiwa kuwa wanufaika wa hii elimu ya uraia. 

Hii itawasaidia wananchi kutambua mazingira yao ya demokrasia na kitu kipi cha msingi wanatakiwa kufanya ili kuweza kuboresha elimu yao ya msingi ya demokrasia. 

Vyama vya siasa, ambavyo ndiyo msingi wa vijana, au njia kuu ambayo wanapitia, vinahitajika kuimarisha zaidi misingi ya demokrasia na ukuzaji wa vijana ili waweze kuwa wakomavu na kutambua majukumu yao. 

Tujiepushe na uteteaji kuwa sisi chama chetu kinafanya tayari wakati takwimu zinaonesha kabisa upatikanaji wa vijana kwenye nafasi kadhaa kuwa ni mdogo na hata wale ambao wamekuwepo imekuwa ni sura zilezile ambazo zimezoeleka kuonekana.

SOMA ZAIDI: Je, Tuwatazame Vijana Kama Kundi Maalumu Tanzania?

Uangaziaji wa sera na mikakati ambayo inalenga moja kwa moja ushiriki wa vijana ni jambo ambalo wanajamii pamoja na Serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine, kuwekea mkazo ili kuweza kuimarisha ushiriki wa vijana. 

Hakuna maana kutengeneza sera ambazo zinamhusu kijana pasipo ushirikishaji wa kijana mwenyewe kuanzia mwanzo, na mwisho wa siku kijana kuwa kama mtekelezaji wa sera ambazo hajashiriki hata kuitengeneza na kutoona umuhimu wake kwa maana haimgusi moja kwa moja.

Ushiriki wa vijana kwenye chaguzi ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu kwani tunahitaji taifa lililo bora zaidi na mimi, kama mmoja wa vijana, nitafurahi zaidi kukiwa na uwakilishi mkubwa wa vijana wengi zaidi katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuakisi tunachohitaji kukiona katika Tanzania tuitakayo.

Kelvin Expellah ni mshauri wa masuala ya utetezi na uchechemuzi kutoka Twaweza East Africa. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia consultantke@twaweza.org. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts