The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waiangukia Serikali Kuharakisha Mchakato wa Urejeshwaji wa Mabaki ya Ndugu Zao Kutoka Ughaibuni: ‘Tumehangaika vya Kutosha’

Familia hizo zimekuwa zikiendesha jitihada hizo kwa miaka, zikiingia gharama za mamilioni, na sasa wanaitaka Serikali iyape kipaumbele madai yao na kuwapa msaada stahiki.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Familia za Watanzania wanaopigania urejeshwaji wa mabaki ya ndugu zao kutoka ughaibuni wameitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuuharakisha mchakato huo licha ya kuwa baadhi ya nchi zinazoshikilia mabaki hayo, kama vile Ujerumani, zimekubali kuyarejesha nchini Tanzania kwa ajili ya taratibu zingine.

Familia hizi ni zile zinazohusisha watu kama vile Mangi Meli wa Moshi, Mangi Lobulu Kaaya wa Meru, Chifu Songea Mbano wa Songea na Sindato Kiutesha Kiwelu wa Moshi ambao ndugu zao wamekuwa wakipigania urejeshwaji wa mabaki yao, hususani mafuvu, kutoka Ujerumani walikopelekwa baada kunyongwa na mkoloni huyo aliyeitawala kikatili Tanganyika kwa takriban miongo minne.

Mabaki ya watu hao ni baadhi ya maelfu ya mabaki ambayo Ujerumani inayashikilia kwenye makumbusho zake, vyuo vikuu na kwenye baadhi ya taasisi binafsi za watu na ambayo ndiyo msingi wa vuguvugu na kampeni kubwa inayoendelea duniani ya kuilazimisha Ujerumani kuyarudisha mabaki hayo kwa ndugu za wale iliyowaua wakati wa ukoloni wake Tanganyika na sehemu nyingine za Afrika.

Ndugu wa familia hizi, hususani wale ambao kupitia vipimo vya vinasaba wamefanikiwa kugundua sehemu yalipo mabaki ya mababu zao, wameiambia The Chanzo kwamba mamlaka nchini Ujerumani zimewahakikishia kwamba ziko tayari kurejesha mabaki hayo nchini, na kwamba wanasubiria tu maelekezo kutoka Serikali ya Tanzania, na hivyo kuzitaka mamlaka husika kutoa maelekezo hayo kuharakisha zoezi hilo.

“Kwa kuwa Ujerumani wapo tayari kurudisha mabaki ya babu zetu, tunaamini Serikali ikiingilia kati itakuwa ni haraka zaidi kuliko tunavyofanya sisi [kama ndugu],” John Mbano, kitukuu cha Chifu Songea Mbano, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano kwa njia ya simu. “Kule mafuvu ni mengi. Hatuwezi kusema Serikali iyalete yote kwa pamoja, hilo siyo rahisi. Serikali ishirikiane na sisi familia za hao watu. Nafikiri itakuwa ni rahisi sana kulifanikisha hili.”

John Mbano (kushoto), kitukuu cha Chifu Songea Mbano, akiwa nchini Ujerumani kama sehemu ya jitihada za familia yake kugundua yalipo mabaki ya babu yao huyo na kuyarejesha Tanzania. PICHA | CHARLOTTE WIEDEMANN/X.

Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania umesema hauwezi kulizungumzia suala hili, ikimtaka mwandishi atafute majibu kutoka Serikalini. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, ambaye suala hili liko chini yake, hakupatikana kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi licha ya jitahada mbalimbali.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kunufaika na Uwepo wa Watu Kama Joe Chialo, Waziri Jijini Berlin Mwenye Asili ya Tanzania?

Hata hivyo, Serikali imeonekana mara kadhaa ikifanya vikao na baadhi ya wadau, wakiwemo wawakilishi wa familia ambazo mabaki ya babu zao yako Ujerumani, katika kile kinachoonekana kuwa ni juhudi za kufanikisha urejeshwaji wa mabaki hayo nchini Tanzania na kuhitimisha miongo kadhaa ya usumbufu na majonzi.

Juhudi hizi za wanafamilia pia zinakuja takriban mwaka mmoja tangu Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, azuru Tanzania hapo Oktoba 30, 2023, ambapo, pamoja na mambo mengine, aliomba msamaha kwa ukatili ambao watu wake waliufanya walipokuwa Tanzania, kipindi hicho Tanganyika.

Hatukati tamaa

Mbano, 36, ni kitukuu cha Chifu Songea Mbano, aliyekuwa kiongozi wa Wangoni ambaye Ujerumani ilimnyonga, pamoja na viongozi wenzake wa kimila 66 kwa kukataa kusaliti watu wao na kusalimu amri kwa ukoloni wa Mjerumani. 

Chifu Mbano anasadikika kwamba alikuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa watu wake kiasi cha Mjerumani kudhani kwamba akikubali utawala wao kazi ya wakoloni ingekuwa rahisi, lakini kiongozi huyo jasiri alikataa na kuungana na watu wake kwenye kupinga uvamizi huo wa Mjerumani.

Mbano ameiambia The Chanzo kwamba licha ya kuhangaika kwa miaka na miongo kadhaa, bado familia yake haijafanikiwa kujua yalipo mabaki ya babu yao huyo, lakini amesema hilo haliwakatishi tamaa na wataendelea na juhudi hizo mpaka wagundue mahala yalipo mabaki hayo na kuyarudisha nchini Tanzania.

“Watanzania wengine hawawezi kuelewa umuhimu wa mabaki hayo, ila sisi kama familia ndiyo tunaumia hasa, na tunajua yana umuhimu gani kwetu,” alisema Mbano. “Unajua jambo lililotushangaza ni kuwa Ujerumani [wananchi] hawajui kabisa kama babu zao walifanyia watu ukatili, na hapa tumeshirikiana na shirika moja huko Ujerumani kuandaa makala juu ya nini hasa kilichotokea.”

SOMA ZAIDI: Ukombozi wa Tanzania Unahitaji Kwanza Mapinduzi ya Maarifa

Makala anayozungumzia Mbano inaitwa Kaburi Wazi, au The Open Grave, kwa kimombo, iliyoongozwa na Agnes Lisa Wegner wa Ujerumani na Cece Mlay kutoka Tanzania, inayoangazia juhudi za Mbano kupigania urejeshwaji wa mabaki ya babu yake kutoka Ujerumani. 

Makala ya Kaburi Wazi ni ushirikiano kati ya watengenezaji filamu kutoka Tanzania na Ujerumani yenye lengo la kuchochea urejeshwaji wa mabaki ya mababu wa Kitanzania nchini kwao. PICHA | KABURI WAZI.

Filamu hiyo iliyotoka mwaka huu wa 2024, na ambayo ilioneshwa nchini Tanzania hapo Juni 28, 2024, katika jumba la Ajabu Ajabu, pia inaangazia juhudi za Felix Kaaya za kupigania urejeshwaji wa mabaki ya babu yake, Mangi Lobulu Kaaya.

Tumehangaika sana

Tofauti na Mbano, Felix aliieleza The Chanzo kwamba juhudi zao za kufahamu yalipo mabaki ya babu yao zimefanikiwa, na kilichobaki sasa ni kuhakikisha yanarudishwa Tanzania ili kumuwezesha babu yao huyo kupata maziko rasmi yanayoendana na mila na desturi za jamii yao.

“Ni kwa miaka zaidi ya 40 sasa tunapambana ili kujua mwili huo ulipelekwa wapi,” Felix Kaaya, 70, alisema. “Nilienda Ujerumani kufuatilia baada ya kukabidhiwa jukumu hili, lakini sikufua dafu. Ndipo nikaamua kushirikiana na shirika moja la Kijerumani kufanya utafiti ndipo ikabainika kuwa mwili wa Mangi Kaaya ulipelekwa nchini Marekani.”

Lobulu Kaaya alikuwa mrithi wa Mangi Matunda Kaaya wa Meru aliyefariki mwaka 1896. Hata hivyo, Lobulu alinyongwa na Wajerumani mnamo mwaka 1900 na fuvu lake kupelekwa nchini Ujerumani. 

Felix Kaaya, kitukuu cha Lobulu Kaaya, ameiambia The Chanzo kwamba kwa sababu sasa wanajua mabaki ya babu yao yako wapi, kinachohitajika ni Serikali za Tanzania, Ujerumani na Marekani kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha fuvu hilo linarudi kwa familia.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

“Tumehangaika sana na tumechangishana sana hadi huyo Mjerumani alipokuja kutupa majibu kuwa mabaki ya babu yetu yalipelekwa Marekani,” alisema Felix. “Hivyo, hapa tusubiri hatua za kidiplomasia sasa, na nafikiri Serikali yetu itaweza kutusaidia.”

Gharama

Moja ya sababu zinazozisukuma familia hizi kuitaka Serikali kuharakisha mchakato wa urejeshwaji wa mabaki ya babu zao ni gharama wanazopaswa kuingia katika jitihada zao za kutafuta mabaki ya wapendwa wao hao na kuyarudisha nchini Tanzania.

Wanafamilia wanaingia gharama kubwa za safari, chakula na malazi wanapokwenda nchini Ujerumani kufuatilia mabaki ya ndugu zao, na wakati muda mwingine hupokea michango kutoka kwa wasamaria wema, kwa kiwango kikubwa gharama hizi huchangiwa na wanafamilia husika.

Mtaa jijiji Berlin, Ujerumani, wapewa jina la Maji Maji kama heshima kwa waathirika wa Vita ya Maji Maji iliyoendeshwa na Watanganyika dhidi ya uvamizi na kiloni wa Kijerumani. PICHA | IMANI NSAMILA/X.

Anaeli Gerlad Moshi ni kitukuu cha Mangi Meli wa Old Moshi ambaye yeye na ndugu zake wametumia miaka 60 iliyopita kutafuta fuvu la babu yao huyo ambaye mwaka huu wa 2024 imetimia miaka 124 tangu anyongwe na Wajerumani na fuvu lake kupelekwa Ujerumani.

Anaeli, ambaye tayari ameshakwenda Ujerumani mara tatu kufuatilia mabaki ya babu yake bila mafanikio, anaiomba Serikali ya Tanzania kulipa suala hilo kipaumbele kwani kama familia wametumia gharama kubwa hadi sasa kufuatilia mabaki ya babu yao huyo bila mafanikio.

SOMA ZAIDI: Angela Merkel: Sauti Iliyovuma, Kuheshimiwa Barani Ulaya na Kwengineko

“Kuna mashirika ya Ujerumani yamekuwa yakitusaidia kidogo, lakini kwa kiasi kikubwa tunachangishana ili kuweza kupata fedha kwa ajili ya mapambano hayo yote ninayokwambia,” Anaeli aliiambia The Chanzo. “Serikali ikiingilia kati tutafurahi sana kwani hili suala tulikuwa tunalifanya kifamilia pekee yetu.”

Wito huu pia umeungwa mkono na Zablon Kiwelu, kitukuu cha Akida Sindato Kiwelu, ambaye alikuwa mshauri wa Mangi Meli, ambaye pia aliuawa na Wajerumani na fuvu lake kuchukuliwa na kupelekwa Ujerumani. Tofauti na Mangi Meli, fuvu la Kiwelu linajulikana lilipo, na sasa familia inasubiria taratibu za kulileta nyumbani zikamilike.

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts