Mali ya umma si mali ya mtu yoyote yule. Angalau huu ni mtazamo tulionao wananchi tulio wengi. Ni mtazamo huu, naamini, ndiyo unaotusukuma kuharibu miundombinu kama vile ya maji na umeme kwa malengo ya kujipatia manufaa binafsi. Hatuuoni umiliki wetu kwenye miundombinu hiyo; chetu, kwa ufupi, ni kile kilichopo mifukoni mwetu tu!
Kwa kweli, mali ya umma si mali ya mtu yoyote yule. Ndiyo maana haishangazi kuona wananchi wenye hasira kali tukijichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga na kuwaua, muda mwingine kwa kuwachoma moto, watu wanaosadikiwa kuwa vibaka – wa kuku, viatu kwenye nyumba za ibada, bodaboda, kutaja mifano michache tu.
Sisisisi, tunaokerwa sana na wizi wa kuku na bodaboda, tunashindwa kuonesha hasira zetu hizo kwa wizi wa fedha na mali nyingine za umma, wizi unaoripotiwa kila mwaka na mamlaka kama vile Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kimsingi, ni sisisi tunaokuwa tayari kuwa wapambe na machawa wa wezi hawa kwenye jamii zetu na hata kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa sababu walio na madaraka wamefanikiwa kuutambua ukweli huu mtakatifu, kwamba wananchi hatukerwi sana na matumizi mabaya ya fedha na mali zingine za umma na wale waliokabidhiwa mamlaka ya kupanga matumizi ya rasilimali hizo kwa faida ya watu wote, ufisadi umeendelea kutamalaki Serikalini, ukilitumbukiza taifa na watu wake chini zaidi kwenye shimo la umasikini.
Utekelezaji sifuri
Ufisadi huu unajidhihirisha kwa namna tofauti tofauti, lakini leo naomba nijikite kwenye uundwaji wa kamati na tume za ki-Rais, zinazoundwa kwa lengo la kutafuta majibu ya matatizo mbalimbali yanayotusibu kama nchi, zikitumia fedha, muda na rasilimali nyingine nyingi za walipa kodi, ili tu mwisho wa siku mapendekezo yao yajaze nafasi kwenye makabati ya ofisi za umma, kukiwa na utekelezaji sifuri.
SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: Je, Ufisadi Unatokana na Udhaifu wa Serikali au ni Tatizo la Kijamii?
Ni uamuzi wa busara na hekima sana kwa kiongozi kuunda timu ya wataalamu kuangalia jambo fulani kwa undani kabla ya kumpatia kiongozi huyo taarifa sahihi zitakazomuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya taifa lake na watu anaowaongoza. Inathibitisha ule usemi kwamba mtu hawezi kujua kila kitu, na hakuna ubaya katika kutafuta ushauri na maarifa.
Lakini kama ambavyo tunapaswa kupongeza timu hizi za wataalamu zinapoundwa, vilevile tunapaswa kuhoji pale kiongozi aliyeunda timu hizi, au Serikali yake, anapoonekana kutokufanyia kazi, au kuchelewa kufanyia kazi, au kufanyia kazi nusu-nusu, mapendekezo yaliyotolewa na timu hizo kubadilisha mambo mbalimbali kwa lengo la kuboresha ustawi wa nchi na watu wake.
Mtu mwingine anaweza kuja na tafsiri tofauti ya hatua kama hiyo, lakini ukiniuliza mimi, nitasema kwamba kufanya hivyo ni kufuja tu fedha na mali zingine za umma kwa njia tofauti.
Serikali inawekeza vya kutosha – kifedha na kimuda – kwenye kuendesha na kufanikisha michakato hiyo, na kusipokuwa na utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa huo unakuwa ni uwekezaji mbaya, usiowanufaisha wanahisa – wananchi –, na hivyo ni lazima tuache kufanya aina hizo za uwekezaji.
Hapa Tanzania, Serikali, kwa nyakati tofauti, imeunda kamati na tume mbalimbali ambapo, wakati kuna mapendekezo ya baadhi yao yametekelezwa kwa kiwango fulani, nyingi zimetoa mapendekezo ambayo mpaka leo utekelezaji wake haujafanyika na wenye jukumu la kufanya hivyo wamejikausha kama vile hawapaswi kutoa maelezo yoyote juu ya kushindwa kutekelezwa kwa mapendekezo hayo.
Rais Samia
Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan pekee, vikosi kazi, kamati na tume mbalimbali zimeundwa na nikifanya tathmini, sioni kama uwekezaji tuliofanya kwenye kufanikisha michakato hiyo umezaa matunda yaliyotarajiwa na wengi.
SOMA ZAIDI: Tume Yataka Sheria Itungwe Itakayoruhusu, Kusimamia Upelelezi Binafsi
Hizi ni pamoja na Tume ya Kuchunguza Usawa wa Kijinsia na Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Mpaka wakati naandaa safu hii machache yalikuwa yanajulikana kuhusu ile ya kuchunguza usawa wa kijinsia au mapendekezo ya ile ya haki jinai yangeanza lini kutekelezwa.
Mbali na tume, Rais Samia pia ameunda vikosi kazi kadhaa kwa lengo la kushughulika na masuala mbalimbali mahususi. Hivi ni pamoja na Kikosi Kazi cha Kushughulikia Nishati Safi ya Kupikia; Kikosi Kazi cha Kupata Mbinu za Kumaliza Utapiamlo na Udumavu; na Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa, kutaja vile vichache tu ninavyovifahamu.
Nafahamu machache sana kuhusu kikosi kazi cha nishati safi ya kupikia na kile cha utapiamlo, na jitahada zangu za kujielimisha hazikufua dafu maana kuna habari chache sana mtandaoni kuvihusu, isipokuwa zile zinazohusu kutangazwa kuundwa kwake. Upo uwezekano kwamba timu hizi zimekamilisha kazi zao na sasa mapendekezo yao yameanza kutekelezwa.
Lakini kwa kile cha vyama vya siasa, nafahamu kwamba utekelezaji wa mapendekezo yake haujafanyika, na hata kile Serikali ilichokitekeleza, kama vile kuzifanyia marekebisho ya sheria za uchaguzi, ikisema huko ni kufanyia kazi mapendekezo hayo, wadau wamekikataa, wakisema kwamba kilichorekebishwa hakiakisi maoni waliyoyatoa wakati wa mchakato wa ukusanyaji wa maoni.
Sasa, Rais Samia ameunda Tume ya Kutathmini na Kushauri Kuhusu Masuala ya Kodi kufuatia mzozo mkubwa unaoendelea kuripotiwa kuwepo kati ya wafanyabiashara na mamlaka za kikodi, kama vile Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA). Ni matumaini yangu kwamba uwekezaji wa kifedha na kimuda utakaofanyika kufanikisha kazi ya tume hii hautaenda na maji, na hivyo mapendekezo yake yatatekelezwa ipasavyo.
Kila kitu kinawezekana
Sikiliza, upo uwezekano kwamba Rais Samia amepanga kutekeleza mapendekezo ya vikozi kazi, kamati na tume zote alizounda, pengine ni suala la muda tu. Ndiyo, upo huo uwezekano. Lakini, kama kuna chochote tunaweza kujifunza kutoka kwenye historia, upo pia uwezekano wa mapendekezo hayo kutotekelezwa kabisa.
SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi
Marais wawili kabla ya Samia, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, walishindwa kufanyia kazi Mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1994, na mpaka leo mapendekezo hayo hayajafanyiwa kazi.
Mkapa pia aliunda Tume ya Warioba ya Rushwa, ya mwaka 1997, ambayo alishindwa kutekeleza mapendekezo yake ambayo yameendelea kubaki bila kufanyiwa kazi hadi leo hii. Bila kusahau Serikali kushindwa kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya.
Kwa hiyo, kama hatua zote mbili zinawezekana, yaani kutekelezwa na kutotekelezwa, nini kitaamua hatua ipi iishinde nyingine? Maoni yangu ni kwamba itategemea na msukumo wananchi watakaoutoa kufanikisha hatua yenye manufaa kwao, yaani, mapendekezo ya tume za Rais kutekelezwa.
Kukosekana kwa msukumo huo kutaamua ushindi wa hatua nyingine ambayo haina maslahi kwa Watanzania, yaani, mapendekezo kuendelea kukaliwa, huku utekelezaji wake ukiwa sifuri.
Wapo miongoni mwa wananchi wenzetu, wakisaidiwa na wadau wengine kama vile asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kidini, vyombo vya habari na washirika wa maendeleo, wanaoisukuma Serikali itekeleze mapendekezo ya tume na kamati mbalimbali yanayolenga kujenga Tanzania ya haki, jumuishi na usawa kwa wote.
Jukumu letu ni kujiunga na wananchi na wadau hawa katika kusukuma gurudumu hili na kufanikisha malengo yake. Ni kwa maslahi yetu binafsi tunapaswa kuziunga mkono juhudi hizi, ikiwemo kuhakikisha kwamba fedha na mali zetu kama walipa kodi hazifujwi kupitia uundwaji wa vikosi kazi, kamati na tume ambazo mapendekezo yake yanakuja kudharauliwa.
Tunapaswa kuhakikisha kwamba kila uwekezaji tunafanya unaleta tija tunayoitarajia. Vinginevyo, tukatae uwekezaji huo.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.