Masuala ya utwaaji wa ardhi yanadhibitiwa na sheria, ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Sheria makhsusi ni pamoja na Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji, na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, zote za marejeo ya mwaka 2022. Sheria sambamba na hizo ni pamoja na zinazohusu mazingira, madini, uthamini wa ardhi, na kadhalika.
Ardhi ya Tanzania imegawanywa katika maeneo matatu: ardhi kuu, ardhi ya vijiji, na ardhi iliyotengwa. Hati ya kumiliki ardhi iliyopimwa inatolewa kwa jina la Rais kama muangalizi, au msimamizi, wa ardhi yote nchini. Na kwa mantiki hiyo, Rais anaweza kutwaa ardhi yeyote, kwa kufuata utaratibu.
Kikatiba, kila mtu ana haki ya kumiliki mali, ikiwemo ardhi. Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mmiliki wa jumla wa ardhi yote ya Tanzania kwa niaba ya Jamhuri.
Kanuni za kimsingi za Sera ya Taifa ya Ardhi ni pamoja na kuhakikisha umikilikaji sawia wa ardhi. Vilevile, kuhakikisha fidia inalipwa kwa usawa na kwa wakati ikiwa ardhi ya mtu itatwaliwa na mamlaka au mtu/kampuni, kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji wa Ardhi.
Aidha, kanuni nyingine muhimu ni ushiriki wa wananchi kikamilifu na kwa uwazi katika usimamizi wa ardhi, na maamuzi yanahohusu ardhi kama mali yao.
Kauli ya Rais kuhusu fidia
Mkanganyiko ulioletwa na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watu wanaodai fidia ya ardhi wangoje kukamilika kwa shughuli za maendeleo ulihitaji tafakuri. Kwamba, ikiwa unadai fidia, usiharakishe, kwa kuwa kipaumbele ni maendeleo ya jumla. Ya kwako binafsi yasubiri. Kivyovyote vile, sheria hazimuungi mkono Rais. Vilevile, masharti ya mikopo ya uwekezaji hayaafiki maelekezo hayo ya Rais.
SOMA ZAIDI: ‘Maendeleo ya Watu’ Lazima Yahusishe Ulipaji Fidia wa Haraka Kwa Watanzania
Haibishaniwi kwamba Rais anaweza kutwaa ardhi, kwa mujibu wa sheria, kwa maslahi fulani ya umma. Maslahi hayo ni pamoja na matumizi ya Serikali au umma, kwa maendeleo ya kilimo, viwanda au huduma za kijamii.
Ardhi inaweza kutwaliwa na Rais kwa madhumuni ya kujenga mji, bandari au kiwanja cha ndege, uchimbaji wa madini au mafuta, ama kwa matumizi ya mtu binafsi ambaye, kwa maoni ya Rais, anafaa apewe ardhi kwaajili ya maendeleo ya kilimo.
Aidha, Rais atahitaji idhini ya Bunge na amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, ili kutamka kwamba ardhi fulani itatengwa kwa matumizi ya umma. Mfano, ujenzi wa mradi mkubwa wenye faida kiuchumi.
Ili Rais atwae ardhi, wakazi wa eneo lile watapewa notisi – si chini ya wiki sita – kutoka kwa Waziri wa Ardhi kwamba ardhi yao inakusudiwa kutwaliwa kwa matumizi fulani. Taarifa kwa wananchi lazima iwe inajitosheleza, shirikishi, na ikubaliwe.
Kuhusu fidia
Serikali inatakiwa kutoa fidia kwa kila mtu ambaye ardhi yake itatwaliwa kwa maelekezo ya Rais. Serikali, kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi, inatakiwa kulipa fidia kwa wote walioathiriwa na utwaaji wa ardhi. Fedha za fidia, kwa madhumuni hayo, lazima ziidhinishwe na Bunge.
Kwa upande mwingine, kwa makubaliano na mtu ambaye ardhi yake imetwaliwa, Rais anaweza kumpa ardhi nyingine. Aidha, ardhi hiyo lazima iendane na isizidi thamani ya ardhi yake ya awali. Vilevile, kumpa mtu ardhi nyingine hakutaathiri stahiki nyingine.
Mfano, fidia ya usumbufu, maendeleo katika ardhi yake ya awali na zaidi, kwa mujibu wa sheria.
Malipo ya fidia kutokana na utwaaji wa ardhi yatazingatia thamani ya ardhi wakati wa kutwaliwa, hasara inayotokana na kuhama, faida za kijamii, ikiwemo umbali wa kufuata na kupata huduma za kijamii.
Sheria zetu, hata hivyo, haziko bayana kuhusu tathmini ya mtaji wa kijamii, ufikiwaji wa huduma za kijamii kati ya awali na baadaye, na vilevile masuala ya kiutamaduni na kiimani.
Katika kutathmini ardhi, thamani ya ardhi katika soko itazingatiwa. Fidia ya usumbufu, usafiri, kupoteza faida kama malazi na gharama zote zinazohusiana na kuiendeleza ardhi. Wataalamu wanashauri vilevile kuzingatia mtaji wa kijamii, au social capital kwa kimombo, kama watu, urahisi wa kufikia huduma za kijamii kama shule, soko, hospitali na maji kama nilivyogusia hapo juu.
SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo 852 Mbarali Waiburuza Serikali Mahakamani Wakitetea Ardhi Yao
Dhana ya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii kabla ya uwekezaji inalenga kuondoa uwezekano wa kutwaa ardhi kwa ajili ya uwekezaji alafu ikageuka kuwa mateso kwa wananchi.
Ndiyo maana, kwa mfano, uwekezaji wowote mkubwa lazima uwe umetengewa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za kimazingira na kijamii, ikiwemo fidia kwa watu watakopoteza maslahi katika ardhi zao.
Ardhi ya vijiji
Iwapo Rais atahitaji kuhamisha ardhi ya kijiji kuwa ardhi kuu au ardhi iliyotengwa, atamuelekeza Waziri kufanya hivyo, kwa maslahi ya umma, uwekezaji, na kadhalika.
Waziri atatoa taarifa kwa umma na kuchapisha katika Gazeti la Serikali ardhi inayotakiwa kuhamishwa.
Waziri atabainisha kiasi na mipaka ya ardhi ya kijiji itakayohamishwa, sababu za kuhamisha ardhi, tarehe na notisi ya siku sitini kwa wamilikaji wa ardhi hiyo.
Aidha, ardhi ya kijiji haitahamishwa isipokuwa pale ambapo kuna makubaliano kuhusu kiasi, aina na muda wa fidia kati ya Serikali/halmashauri ya Kijiji na Kamishna wa Ardhi ambaye ni mwakilishi wa Waziri na Rais. Makubaliano hayo lazima yatokane na mwafaka wa wanakijiji kupitia vikao rasmi, ambavyo vitaikaimisha halmashauri jukumu la kuafikiana na Kamishna wa Ardhi.
SOMA ZAIDI: Wadau wa Ardhi Waitaka Serikali Kuheshimu Maamuzi ya Mahakama
Ni wajibu wa Serikali, au mtu ambaye ardhi inatwaliwa kwa niaba yake, kuhakikisha analipa fidia kwa wanakijiji. Kanuni ni ileile, fidia iwe ya kujitosheleza na ilipwe kwa wakati. Kumbe, kauli kwamba ardhi ikitwaliwa kwa maendeleo au uwekezaji fidia huja baada ya faida ni uongo!
Mifumo ya malalamiko
Migogoro ya ardhi inatatuliwa kupitia Mahakama zetu za ndani, kwa upande mmoja. Mtu yeyote mwenye sababu ya kuamini kwamba ardhi yake imetwaliwa kiubatili ana haki ya kuwasilisha shauri mahakamani.
Kuna mabaraza ya ardhi na Mahakama Kuu kitengo cha ardhi. Yote, kwa pamoja, yanashughulikia migogoro ya ardhi kwa ngazi tofauti tofauti.
Vilevile, kuna mifumo makhsusi iliyowekwa na taasisi kama Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia. Taasisi hizi zina vitengo makhsusi kutokana na nafasi yao kama wakopeshaji kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Wameweka mifumo hiyo ili iwasaidie kuwekeza kiuwajibikaji.
Benki ya Dunia ina mfumo wa malalamiko yanayotokana na athari za uwekezaji kupitia asasi ya International Finance Corporation (IFC). Asasi hiyo inafanya kazi chini ya mfumo wa malalamiko unaojulikana kama Compliance Advisor Ombudsman. Jamii, au watu, walioathiriwa na uwekezaji wanaweza kuwasilisha malalamiko yao iwapo uwekezaji umefanyika bila kuwapa fidia ya ardhi iliyotwaliwa kwaajili hiyo.
SOMA ZAIDI: Ukiukwaji wa Haki ya Ardhi kwa Wenyeji wa Ngorongoro Umekuwa Kero
Benki ya Dunia, kupitia asasi yake hupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi wa ama kusitisha mradi, au kuitaka Serikali illipe fidia kwa waathirika. Kikawaida, masharti ya kuwapa watu fidia au nafuu zingine za kisheria huwa sehemu ya makubaliano ya mkopo. IFC itamtaka mteja wao kuzingatia kanuni fulani fulani za uwekezaji ambazo zitahakikisha jamii, au watu, walioathiriwa na mradi wanapata nafuu za kisheria kwa wakati.
Vilevile, Benki ya Maendeleo ya Afrika inao mfumo wake wa malalamiko ambao, pamoja na mambo mengine, unahakikisha kwamba wateja wao wanazingatia viwango fulani, sera na taratibu za uwekezaji.
Moja ya tunu zao ni kutoa nafuu na fidia kwa jamii ambazo zimeathiriwa na mradi. Kupitia Independent Review Mechanism chini ya Compliance Review and Mediation Unit, Benki ya Afrika huhakikisha malalamiko yote yanayohusu uwekezaji kuhusu jamii zilizopata athari yanasikilizwa na kutatuliwa.
Uzembe na upotoshaji
Kauli ya Rais kuhusu fidia, kwa ujumla, ni ya kizembe na kiupotoshaji. Nilidhani kwamba ameelekezwa vibaya. Lakini baadaye nikaamini ni msimamo wake maana, hata baada ya watu kuonesha mshangao na kuikosoa kauli yake, hajaomba radhi au kutengua kauli ile. Haipendezi kwa Rais kukosea mara kwa mara na akaendelea kuona ni sawa.
Fidia ni takwa la kisheria na vilevile kiutu. Kwa kuwa hakuna mbadala wa utu wa mtu, huwezi kuwalaghai watu kwamba unawaletea maendeleo kwa kuwanyang’anya ardhi na makazi yao na ukawaacha bila kitu.
Utu wa mtu unalindwa kwa kupewa hifadhi stahiki ya jamii na hakikishio la usalama wake na mali zake. Ni vema viongozi wakapima madhara ya kauli zao kwa watu na kwa watendaji wa chini yao kabla hawajazitoa.
Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.