Msongo wa mawazo, sonona na changamoto mbalimbali za afya ya akili zimekuwa zikiwatatiza watoto na vijana wadogo wengi hata kuwasababisha kufikia hatua ya kuchukua uhai wao.
Kutokana na kukua kwa kasi kwa janga hili, yatupasa kutathmini namna ya kuepuka changamoto hii na kuvunja muendelezo wake kwa vizazi vyetu endelevu.
Wataalamu wa afya ya akili wanaamini kuna mambo ambayo tukiyazingatia kwa watoto wetu katika hatua za ukuaji wao, itawasaidia kuhimili changamoto mbalimbali za maisha ambazo zinaweza kupelekea msongo wa mawazo na magonjwa Kama sonona na unyogovu.
Moja ya njia hizi ni kuwa karibu na kuwafahamu watoto wetu ili tutumie aina ya malezi inayowafaa. Tuwekeze juhudi za makusudi kuwa karibu na watoto wetu ili tuweze kujenga mahusiano thabiti. Hii itakuwa chachu ya malezi bora kwa watoto wetu.
Mahusiano na watoto wetu yatatusaidia kujua aina sahihi ya malezi ya kuyafuata ili kuwafanya watoto hawa kuwa watu wa mfano kwenye jamii zetu, na kupalilia mabadiliko chanya hata kwa vizazi vyao.
Malezi ya kimamlaka
Tunazo aina nyingi za malezi kama vile malezi ya kimamlaka na uongozi, malezi ya kutelekeza, malezi ya kiutawala na mabavu na malezi ya bora liende. Wataalamu wa afya ya akili wanasema kuwa aina bora ya malezi yatakayomsaidia mtoto aweze kukua katika misingi imara na ni malezi ya kimamamlaka na uongozi.
SOMA ZAIDI: Sababu za Kukupa Wasiwasi Juu ya Msichana wa Kazi Nyumbani
Hii ni aina ya malezi ambapo mzazi, au wazazi, wanachanganya udhibiti – kusimamia kanuni na kutoa mwongozo – na huruma, kujali pamoja na ufatiliaji wa mara kwa mara. Mtoto anawekewa mipaka na sheria wazi, huku akionyeshwa upendo, msaada, kusikilizwa maoni yake na kupewa muongozo kwa ukaribu.
Pia, watoto wanaadabishwa kwa njia zinazompa nafasi ya kujifunza kutokana na makosa pale ambapo wanakuwa wamekosea. Tujilazimishe kuwapa nafasi ya kujitetea, hii itatusaidia kupata mwanga wa safari yao ya kifikra na mtazamo wao juu ya tukio husika mpaka kufikia hatua iliyopo.
Lakini pia tuwape mtazamo wetu ili wapate taswira ya namna wengine tulivyoona na kuchukulia tukio husika ukiachana na mtazamo wao.
Mtindo huu wa malezi utawasaidia watoto wetu kukua wakijiamini, kujithamini, kujitambua na kujikubali. Lakini pia wataweza kujitegemea, kukabiliana na changamoto za maisha na kufanya maamuzi sahihi, wakizingatia hisia za watu wengine watakaoguswa kwa namna moja ama nyingine na maamuzi ama matendo yao.
Msaada wa kisaikolojia
Kila mtoto anahitaji upendo, ushauri na ushirikiano kutoka kwa mzazi wake ili aweze kukua vizuri kiafya, kiakili na kihisia.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Umuhimu wa Malezi Mazuri Kwa Watoto Wetu?
Jambo moja ambalo wazazi wengi, hasa katika jamii zetu za Kiafrika, hususani hapa Tanzania, tunalikosa, ni desturi ya kuwapeleka watoto kwa wataalamu wa saikolojia pale mtoto anapoonesha dalili za magonjwa ya afya ya akili, au pale mtoto anapoonesha anahitaji msaada na mwongozo wa maisha.
Tufahamu kwamba, mtaalam wa saikolojia anaweza kumsaidia mtoto kugundua kipaji chake, uwezo wake ndani na nje ya shule, pamoja na upekee alio nao. Lakini pia humsaidia kujiamini na kufahamu jinsi gani ya kukabiliana na changamoto za kijamii na kiafya kiujumla.
Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi, watoto na vijana wanaweza kujieleza zaidi juu ya yale yanayowasibu kwa mtu ambaye si wa karibu yao hasa mtaalamu wa saikolojia endapo mzazi hakujenga msingi na desturi ya kufanya mazungumzo na mtoto wake tangu akiwa mdogo.
Kwa nafasi kubwa zaidi sisi kama wazazi yatupasa tuwe msaada wa kwanza wa kisaikolojia kwa watoto wetu. Kwa mfano, tuweke jitihada katika kutatua matatizo ya kihisia kwa kuwasikiliza mawazo yao, chanzo cha huzuni kwao, na kuwapa ushauri namna ya kuondokana na wasiwasi na woga.
Lishe bora
Lishe bora ni mlo kamili ambao unajuimisha vyakula vyote vya wanga, protini, mafuta, madini chumvi, na vitamini. Fikiria ubongo wa mtoto kama treni ya mwendokasi, au SGR.
SOMA ZAIDI: Njia Saba Wazazi Tunaweza Kupita Kufanikisha Uadabishaji Chanya kwa Watoto
Ili iendeshwe kwa kasi na ufanisi, inahitaji umeme mwingi na wenye ubora. Hivyo ndivyo lishe bora inavyofanya kwa ubongo wa mtoto, ni kama umeme wenye nguvu unaomwezesha kukua, kujifunza, na kufikiri kwa nguvu.
Lishe bora huujenga ubongo vizuri na huchochea shughuli za ubongo ili mtoto afikiri vizuri, ajifunze haraka, na akumbuke vitu kwa urahisi. Tafiti zinaonyesha kwamba ubongo wenye afya nzuri unasaidia binadamu kupigana na magonjwa ya akili kuliko ubongo uliodhoofika kwa kukosa virutubisho muhimu.
Ukiacha lishe bora, mazingira bora pia ni muhimu kwenye makuzi ya mtoto kwani hufanya kazi kama mfumo wa ulinzi kwa mtoto – yanamlinda mtoto na vile vitu vinavyoweza kumdhuru.
Mazingira ya familia na jamii yenye urafiki na upendo humpa mtoto nafasi ya kujifunza jinsi ya kuhimili hisia zake kwa njia nzuri na kuamini kwamba watu wa kumsaidia na kumsikikiza wanapatikana katika mazingira yake, na hivyo kuwa huru na mwepesi kuomba ushauri na kujieleza kwa wale wanaomzunguka hata akiwa kijana.
Nguvu ya upendo
Mtoto anajifunza jinsi ya kukabiliana na matatizo na mfadhaiko kwa ufanisi. Fikiria mtoto anayekua katika familia yenye upendo na mazingira ya utulivu. Anahisi yupo salama, amezungukwa na watu wanaompenda, na anafursa za kujifunza na kukua.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Baba Anapaswa Kumsindikiza Mama Kliniki Kipindi cha Ujauzito?
Mtoto huyu ana uwezekano mkubwa wa kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha kuliko mtoto anayekua katika mazingira yenye ukatili na ukosefu wa upendo.
Mtoto huyu ana uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na matatizo ya afya ya akili. Nani mwenye jukumu la kutengeneza mazingira salama? Jibu ni rahisi, sisi wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Tumalize kwa kusema kwamba, kizazi kijacho bila matatizo ya afya ya akili kinawezekana. Lakini, inahitaji juhudi za pamoja, tunahitaji kuwekeza katika malezi bora, mazingira yenye upendo na usalama, na elimu kuhusu afya ya akili tangu watoto wakiwa wadogo.
Tuongeze uelewa wa afya ya akili, tuondoe ubaguzi, na tuhakikishe kila mtoto anaweza kupata msaada anaohitaji. Pamoja, tunaweza kujenga kizazi chenye afya ya akili, chenye furaha, na chenye uwezo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.