Maandamano ya chama cha upinzani CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Septemba 23, 2024, hayakufanikiwa, haya yakiwa ni maandamano ya tatu kutokea ndani ya miezi miwili hasa juu ya matukio ya utekaji nchini. Maandamano mengine yaliibuka ghafla huko Lamadi, Simiyu na pia Makuyuni, Arusha, yote yakipinga masuala ya watu kupotea na kupotezwa, hasa watoto.
Tukiongezea na maandamano yaliyofanywa na Wamasai wa Ngorongoro kupinga unyanyasaji katika ardhi ya Ngorongoro inakua jumla ni maandamano manne ndani ya miezi miwili. Hata hivyo, maandamano ya CHADEMA hayakufanikiwa, ingawaje wengi wanaamini kwamba yameacha mafunzo na maswali mengi yatakayochonga muelekeo wa siasa zetu nchini.
Wahafidhina wa msimamo mkali ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wanaoamini katika kuongoza nchi kwa misingi ya ukandamizaji, watatumia kilichotokea Septemba 23 kama kielelezo muhimu cha kuonesha kuwa ukandamizaji ni njia sahihi.
Kwa wahafidhina wengine wa msimamo wa kati hasa Serikalini, wanaoamini kuwa watu lazima waoneshe shukrani ya “kupewa uhuru,” wao watatumia maandamano hayo kuendelea kutaka wapinzani waisifie Serikali na kukosoa kwa ruhusa ya Serikali na kwa namna bora ambayo serikali ingependelea.
Kwa watekaji wanaoonekana kupoa kukiwa na fukuto la kisiasa, labda watarudi kazini kuendelea kufanya wazazi kufariki kwa mifadhaiko ya kutoona watoto wao, wake kubaki wajane wasioeleweka na familia kubaki zikiomboleza kusikokoma. Hii ni furaha yao. Bahati mbaya, na Mungu atusaidie Watanzania, hakuna dalili zozote zinazoonesha kuna kuguswa kwa dhati juu ya malalamiko ya watu. Hakuna kujali. Kuna kupuuzwa, na hakuna dalili kwamba kutakuwepo na kujali.
Kwa Polisi, hasa viongozi wao, nategemea kuwaona wakiingilia zaidi siasa, jambo ambalo mstaafu Kikwete alitahadhirisha chama chake mnamo 2013. Polisi wataonekana zaidi kwenye siasa hasa kutokana na kuwa kuna manufaa kadha wa kadha wanayopata, ikiwemo heshima ya kipekee wanayopewa, kuongezewa na kupelekewa bajeti mbalimbali na kwa haraka na pia kujipa umuhimu. Suala la kujipa umuhimu linaweza kusababisha mivutano mikali na wenzao.
Kwa mahusiano ya vyama vya upinzani, taarifa ya chama cha ACT Wazalendo ya kushauri CHADEMA iache maandamano yake ni sababu nyingine kwa nini CHADEMA na ACT hawatakutana meza moja kwa dhati, labda kupitia matukio.
SOMA : Falsafa ya CHADEMA ya ‘Nguvu ya Umma’ na Itikadi ya Ujamhuri: Je, Upo Ulinganifu?
Kwa ACT, siwaoni wakiweza kujisafisha juu ya watu kutokuwaamini. Taarifa yao ilikua ni makosa ya kimahesabu, Wazungu wangesema political miscalculation. Wamejiongezea mzigo wa kutoaminika kama chama cha upinzani bila sababu. Hata hivyo, kama lengo lilikua ni kuonesha wako sambamba na Serikali, basi lengo hilo litalipa.
Kwa CHADEMA, kiongozi wa chama, Freeman Mbowe, aliweza kubadilisha kufeli kwa jana kuwe na mafanikio kadhaa, ingawa kumeacha maswali ambayo CHADEMA lazima wayajibu.
Mbowe kujitokeza katika maandamano yale na mtoto wake, wakati kuna sintofahamu kali na vitisho , ameacha alama muhimu. Kwanza, kaonesha utu wake katika majonzi ya watu. Kwa sababu unauliza kwa nini Mbowe na mtoto wake walikamatwa? Jibu ni moja tu: ni kwa sababu walikua wanapinga Watanzania kutekwa na kupotezwa, kaonesha uongozi.
Pili, kwa watu waliokua wakisema viongozi wanaficha familia zao na kutaka wengine waandamane, Mbowe kazima sauti zao. Kwa joto lile la kisiasa, ni jambo lisilofikirika kwamba Mbowe angekuja na binti yake, ambaye sio mwanasiasa. Hili ni jambo litakalobadilisha uelekeo, hasa ndani ya CHADEMA. Kama masomo yote ya Mbowe kwa wanachama hasa vijana hayakuingia, somo la jana kila mtu anapata maksi 100, lilikua ni darasa tosha la siasa.
Tatu, taarifa kutolewa kuwa Mbowe kakimbia mkoa na yeye kuonekana, ni jambo litakalosukumizwa chini ya kapeti, lakini ni la muhimu. Wahafidhina wanaoamini katika ukatili wamekua wakitumia taarifa za uongo ili kupanda madaraja ya kusikilizwa na wakubwa wao, na wanasikilizwa.
Lakini tuhoji kwa nini CHADEMA hawakufanikiwa jana?
Utegemezi kwa watu mashuhuri
Moja ya jambo ambalo lilionekana kutokea Septemba 23 ni watu wengi walikua wanategemea Mbowe, Tundu Lissu, Godbless Lema, Joseph Mbilinyi,Sugu, John Mnyika, na watu wengine mashuhuri kutokea ndio hamasa ya maandamano kutokea.
SOMA ZAIDI: Utata Kupotea Kwa Kiongozi Mwingine wa CHADEMA. Polisi Rukwa Wasema Hakuna Utekaji
Hata hivyo, kwa upande mwingine, hata kama wewe ni polisi, umepewa kazi ya kusimamisha maandamano, hao ndio watu wa kwanza na wengine mashuhuri wa mtandaoni utakaowadhibiti, na polisi walifanya kazi hiyo.
Hakukuwepo na matumizi ya nguvu kupita kiasi, kama vipigo na kutesa, hata katika ukamataji wa Lissu aliyekamatwa nyumbani kwake. Hili lilikuwa ni jambo jema, ingawa siyo sababu ya polisi kuminya haki ya CHADEMA kukusanyika kwa amani.
Tukumbuke pia hawa watu mashuhuri wamekuwa wakipitia katika msongo mkubwa, hasa juu ya usalama wao. Binadamu yeyote anaweza kuvumilia kwa sehemu. Lazima tuwaangalie kwa jicho la huruma na kujali, na kuwapumzisha kidogo.
Baada ya mauaji ya kikatili ya Mohamed Ali Kibao, viongozi wengi wa CHADEMA wamepata msongo, hofu na simanzi kubwa, ingawa wengi wameendelea kuonesha ujasiri mkubwa pia. Inabidi kuelewa wao ni watu wanaweza kufanya mpaka sehemu, ila sio vyote.
Wachambuzi wengi wameendelea kuwatupia lawama Watanzania kuwa hawajitokezi haki zao zinapominywa, lakini matukio ya miezi miwili yanaonesha siyo kweli. Uzoefu unaonesha muitikio wowote wa kiraia huanzia ngazi za chini, na siyo juu kwenda chini.
Sasa, kwa CHADEMA, ngazi yao ya chini ya kwanza ni wanachama wake, halafu ndipo inafuatia umma. Msingi mkubwa wa siasa za mashinani ni wahamasishaji jamii.
Wahamasishaji jamii hawa ni watu wenye imani kubwa juu ya itikadi, jambo, na wana uwezo wa kujenga mahusiano na kuishawishi jamii inayowazunguka. Mara nyingi hujitolea kwa hali na mali, bila kutegemea chochote.
Kutokana na msisitizo mkubwa wa siasa za vyama kuwekwa kwa watu mashuhuri, wahamasishaji jamii ni kama wamepoteza uelekeo. Wengi wao ni watu ambao wako tayari kujitolea kila wakati, kujitoa, na kujitokeza, hawa ndio waliotakiwa kuleta namba inayohitajika kusema kuna tukio limetokea.
Wahamasishaji jamii kwa vyama vingi wameishia kukutana na mifadhaiko, hata uwezeshwaji unapokuwepo kwao haufiki. Siyo kwamba Septemba 23 hakukua na wanachama wa CHADEMA waliojitokeza na kujionesha, wengi wao walibaki peke yao.
Katika shughuli yeyote ya kijamii wahamasishaji jamii wangetakiwa wao ndio kuwa na jukumu la kuhamasisha na kuwa kiungo kwa wanachama wa mwanzo, na hapa ni kuangalia kila mhamasishaji jamii ana watu wangapi, na namna wanavyoyasoma mazingira. Uwepo wa viongozi na watu mashuhuri ungekuwepo kuvutia umma kwa ujumla.
Na hii pia itapunguza ulazima wa kutangaza eneo la kuanzia au kutangaza eneo la kukutania na kuwa lazima liwe hilo hilo.
Labda ni wakati sahihi CHADEMA kurudi kuimarisha siasa kupitia wamhamasishaji jamii, watu wenye imani na siasa za CHADEMA na kuepuka wao kukutana na ukatishwaji tamaa hasa kwa kutokuwa maarufu. Na kama kuna fursa nao wapewe kipaumbele.
SOMA ZAIDI: Tunaitathmini Vipi Mikutano ya Hadhara Inayoendelea ya CHADEMA?
Lakini, CHADEMA inahitaji mkakati wa muda mrefu wa shughuli zake zote – iwe mikutano ya ndani, mikutano ya nje, na maandamano. Mfano majuzi wengi walijiuliza inakuwaje viongozi wote walikamatwa majumbani kwao, jambo ambalo kila mtu alikua akilitegemea.
Kutoaminiana
Toka chaguzi za ndani ya CHADEMA zianze, kumekuwepo na kutoaminiana kukubwa ndani ya chama, huyu akimshuku huyu na yule. Na pia taarifa za rushwa zikitolewa kutoka chama tawala kwenda kwa CHADEMA zimezidisha zaidi hali hii.
Inawezekana hali hii ndiyo iliyoleta ugumu hata wa kuwasiliana na kuaminiana katika kuwasiliana. CHADEMA ina jukumu la kuamua kuendelea katika hali ya kutoaminiana ambapo hakuna cha msingi kitakachotekelezeka, au kuvunja ndoa na watu wanaowafanya wasiaminiane.
Lakini pia mifarakano ya ndani ya chama inaonesha kuwa haisaidii kuimarisha taasisi, zaidi sana kuivunja. Wakati vyama vingine vina nafasi ya hata kufarakana, CHADEMA haina hiyo anasa, wanahitaji kurekebisha mambo.
Uwepo wa wahafidhina wa msimamo mkali ndani ya Serikali na chama tawala unaonesha kuwa wengi wao watasukuma kutaka kuona mabavu zaidi yakitumika Tanzania.
Kutumika kwa mabavu zaidi itakua ni kukosea tena kwa mahesabu ya kisiasa. Kwanza itaendelea kushusha umaarufu wa viongozi lakini pili, hakuna mtu ana uhakika kiuhalisia ni kiasi gani cha ukatili, jamii ya Watanzania wanaweza kuhimili. Labda wanajua waumini wa siasa za mabavu na ukatili.
SOMA ZAIDI: CHADEMA Yamuandikia Tena Barua Spika Wakimtaka Kutekeleza Azimio la Baraza Kuu
Kwa ujumla, hekima za kisiasa zinahitajika na ni muhimu, ingawa sidhani kama hili ni jambo ambalo linavutia viongozi kwa sasa. Hii inamaanisha kunahitaji ubunifu katika vyama vya siasa kujenga taasisi ambazo zinaweza himili ukatili na uvunjaji wa haki toka kwa wale waliopewa dhamana.
Lakini, ukijumlisha hali ya dunia ilivyo, nchi zilizoendelea zinapambana kukataa watu kutoka Afrika, tunahitaji kuwa na taifa ambalo kila mtu anaweza kuishi, watoto wanaweza kukua na kulelewa na wazazi wao bila kufikiri ni saa ngapi watekaji watafika, vijana wanaweza kutimiza ndoto zao bila kuwaza kupotezwa. Tunahitaji kuwa na taifa ambalo sio lazima uwe chawa wa Serikali ndiyo maisha yako yawe ya uhakika.
Bahati nzuri na mbaya, kwa wengi wetu, hatuna nchi nyingine, itabidi tu kuifanya nchi yetu iwe bora kwa wote, na sio kwa watu wachache, au kwa wale wenye uwezo wa kutoa sifa njema kama mzee wetu, Profesa Palamagamba Kabudi, bali watu wote, na Mungu atusaidie!
Tony Alfred K ni mchambuzi na mwandishi anayefanya kazi na The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tony@thechanzo.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.