The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Falsafa ya CHADEMA ya ‘Nguvu ya Umma’ na Itikadi ya Ujamhuri: Je, Upo Ulinganifu?

Falsafa ya CHADEMA ya nguvu ya umma inaendana na itikadi ya ujamhuri, iliyoibuliwa na chama hicho kwa mazingira yao ya Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Wapendwa CHADEMA,

Je, ni jambo lisilo la kawaida kwa mimi kuwaandikia kwa njia hii, ni nani hukiandikia chama cha siasa, tena kinachoongoza upinzani Tanzania, barua ya wazi kama hii?

Nimetumia muda wa takriban miaka tisa, nikisoma na kuandika kuhusu mapambano yenu, ikiwemo mbinu, mafanikio na vikwazo mnavyokumbana navyo. Hata hivyo, sijawahi fikiria kuwa hili linanipa haki ya kuwaandikia na bado sifikirii hivyo. 

Ni rahisi kuwaambia watu wengine kuhusu nyinyi. Lakini ningeweza, ama ninaweza, kuwaambia nini kuhusu nyinyi? Je, nyinyi na wazalendo wenzenu hamjatosheka na watu kama mimi, watu wanaojiona wanatoka tabaka la waliobahatika, weupe, wanaume kwa wanawake, Waingereza wanaothubutu kuwakaripia?

Ninataka kuwa tofauti hapa kwa kukuzungumza nanyi jambo linalowahusu. Jambo lenyewe ni kuhusu hasa mawazo yenu. Katiba yenu inaweka bayana kwamba itikadi yenu ni ya mrengo wa kati-kulia. Mnathamini biashara binafsi, soko huria, Serikali ndogo na jamii iliyowazi. 

SOMA ZAIDI: Tunaitathmini Vipi Mikutano ya Hadhara Inayoendelea ya CHADEMA?

Nimewasikia viongozi wenu wakitetea misingi hii kwenye mikutano ya hadhara na kwenye kumbi mbalimbali za mikutano ya chama ngazi ya tawi na hata kwenye miji mikuu ya nchi za Magharibi, hasa barani Ulaya.

Wengi huchukulia kuwa huo ndiyo mwisho wa habari yenu wakati sivyo ilivyo kiuhalisia. Pia, katiba yenu inabainisha kwamba mna kile kinachoitwa ‘falsafa ya nguvu ya umma.’ 

Jambo hili limefafanuliwa kwa sentensi chache tu lakini naona likielezwa kwa ufasaha katika hotuba za viongozi wenu, wanaharakati wa demokrasia wanaowaunga mkono kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii hasa X, zamani Twitter, na hata katika wito wenu wa Katiba Mpya. Hamuhitaji niwaambie kile wanachosema wengine au kile mnachoamini. 

Lakini ningependa kuwaonyesha njia nyingine ya kuona kile ambacho mawazo yenu yanafanana nacho. Kama rafiki anayewainulia kioo, ningependa kuwapa mtazamo mwingine kuhusu nyinyi.

Ujamhuri

Mtazamo wenyewe ni kwamba, nadhani, falsafa yenu ya nguvu ya umma inaendana na itikadi ya ujamhuri, au Republicanism, kwa kimombo, mliyoiibua wenyewe kwa mazingira yenu ya nyumbani. 

SOMA ZAIDI: CHADEMA Yamuandikia Tena Barua Spika Wakimtaka Kutekeleza Azimio la Baraza Kuu

Hapa simaanishi mawazo ya kile chama cha siasa cha Republican kule Marekani. La hasha! Ninamaanisha maono ya siasa ambayo yanaunganisha wanafikra wengi na kwa rika nyingi. 

Ninamaanisha mkondo wa mawazo ya kisiasa ulioibukia Ugiriki na Roma ya kale, lakini ambao umefufuliwa na kuboreshwa kwa nyakati na kwenye maeneo mengi tangu wakati huo na kisha kuvumbuliwa upya kwenye baadhi ya maeneo duniani. 

Ninamaanisha mfumo wa kisomi ambo hutumiwa na kundi la wanafalsafa wa siasa kutafasiri na kuzitolea majawabu changamoto za kisiasa kwa sasa.

Wanajamhuri hawafanani. Wamekuwa wakiungwa mkono na wahafidhina na wale wenye itikadi kali kuelekea kushoto na kulia. 

Wamejumuishwa kwenye ushawishi na utetezi wa mambo mbalimbali, kama vile kupinga ufalme, ukoloni, ujamaa, utumwa na ubepari. Wamekuwa watetezi wakuu wa demokrasia na pia wamekua wakipambana vikali na Serikali za watu wachache kwa maslahi ya wachache. 

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Namna Gani CHADEMA Inaenda Kudai Katiba Mpya?

Hata hivyo, kuna maudhui ambayo hujirudia rudia miongoni mwao na hivyo kuwaungisha wote kwa pamoja. Kwa kawaida, Wanajamhuri wanaunganishwa na dhamira yao ya kukataa kutawaliwa.

Dhana ya uhuru

Kutawaliwa, kama wanavyoelewa, ni kuwekwa chini ya matakwa ya mtu mwingine kiholela mithili ya mtumwa anavyotiishwa kwa matakwa ya bwana. Sehemu moja ya fikra za kijamhuri ni ile inayohusianisha kutawaliwa na uhuru. 

Fikra hii ilianzishwa na mwanafalsafa Cicero na wengine katika miaka ya mwisho ya jamhuri ya Roma ya kale na kisha kufufuliwa na mwamko wa watu wenye siasa kali. 

Kuwa huru, kwa maoni yao, ni kutotawaliwa. Mtu anaweza kuwa hayuko huru, kwa ufahamu huu, hata kama hakuna mtu anayemuingilia, ikiwa tu kuna mifumo ya kitaasisi inayowawezesha watawala kuingililia uhuru huo wakati wowote wanapoona wafanye hivyo.

Wanajamhuri mamboleo na wananadharia wa kileo kama vile Philippe Pettit waliojikita katika mkondo huu wa mawazo, wanashawishi na kubainisha umuhimu wa kubuni na kuwa na katiba zinazolinda uhuru na kuzuia kuibuka kwa madikteta. 

SOMA ZAIDI: Ilikuwa Ni Lazima CHADEMA Ipoteze, Suala Lilikua Ni Nini Wanapoteza

Wanafikra hawa wanapata msukumo kutoka kwa wale wa Jumuiya ya Madola, hasa James Madison, ambao huchukulia katiba ya Marekani kama kielelezo chao. 

Wanashawishi kwamba ni muhimu kuhakikisha katiba zinazoundwa zinadhibiti na kuweka mgawanyo wa mamlaka baina ya mihimili ya dola kuwadhibiti kila wakati wale wanaoweza kuwa madikteta.

Ufisadi

Eneo jingine la kifikra linalowaunganisha wanajamhuri wote ni lile linalohusianisha kutawaliwa na ufisadi. 

Ufisadi machoni pao siyo tu kwamba ni jambo baya litendwalo na viongozi, ama maofisa, binafsi; ni kutawala kwa maslahi ya sehemu fulani badala ya maslahi ya wote. 

Aina hii ya ufisadi wa kimfumo, kwa mtizamo wa Wanajamhuri, huwezeshwa na kuendelezwa kwa kutawaliwa na sehemu hiyo ndogo kwa maslahi ya wachache. 

Mawazo haya yaliasisiwa na mwanafalsafa Socrates na kutoa msukumo kwa wanafikra wa jumuiya ya madola. 

Mmoja wao alikuwa mwanafikra wa Kiitaliano wa karne ya 16, Niccolò Machiavelli anayejulikana sana leo kwa imani ya siasa za nguvu zisizo na huruma zinazotetewa katika kitabu cha The Prince

SOMA ZAIDI: Jinsi Sakata la Viti Maalumu Linavyoiweka Chadema Katika Njia Panda

Hata hivyo, Machiavelli aliweka mawazo yake haya kwenye maandishi yake mengine maarufu yanayowaangalia wananchi walio wengi dhidi ya wachache wenye mamlaka. 

Aliwachagua wachache –il grande– kama kundi linalotawala kwa maslahi yake na wengi– il popoli– kama chombo cha utawala wao. Machiavelli alitetea kuanzishwa kwa taasisi za kiraia kwenye jamhuri ambazo zitawapa wananchi wa kawaida uwezo wa kudhibiti utawala na Serikali ya wachache.

Mawazo haya yamejitokeza tena kwa namna tofauti tangu wakati huo na kupitiwa upya na bodi ya wananadharia wa siasa kwa siku za hivi karibuni. Wanaona njia ya kufikiri katika mawazo haya ambayo tunahitaji. 

Wanatumia njia hiyo kukosoa aina nyingi za ufisadi wa kimfumo uliokithiri ambao wao, na mimi, tunauona kote ulimwenguni. Pia, wanaitumia kueleza maono ambapo tawala za watu wachache zinadhibitiwa na wananchi wanaliokombolewa kupitia nguvu ya umma.

Mawazo haya ya kijamhuri yametolewa kutoka kwa wanafikra huko Ulaya na Amerika ya Kaskazini. Yamefanyiwa mapitio na wanazuoni, hasa katika vyuo vikuu vya Ulaya na Amerika ya Kaskazini.

Mawazo hayajui mipaka

Hata hivyo, mawazo hayajui mipaka. Ukosoaji wa ufisadi wa Serikali ya wachache, umuhimu wa uhuru kwa maana ya kutotawaliwa, na dira ya kuwezesha umma kuwa na nguvu inayotolewa na wanazuoni hawa, huweza kupata umuhimu katika muktadha tofauti.

SOMA ZAIDI: Ni Miaka 61 ya Uhuru Kweli?

Misingi mbalimbali ya kikatiba wanayotoa ni nyenzo muhimu kwa watetezi na wanamageuzi wa demokrasia ya kiliberali mahali popote. Misingi hii haielezwi tu na wasomi wa leo kutoka mataifa ya kusini kama vile Camila Vergara na Lawrence Hamilton

Toussaint Louverture au, Black Spartacus, kiongozi wa mapinduzi ya Haiti ya karne ya 18 ya kupinga utumwa na ukoloni, aligeuza mawazo ya kijamhuri ya Ulaya dhidi wakoloni wa Ulaya, huku akikosoa utumwa dhalimu walioupenda.

Vivyo hivyo, wazalendo wa Afrika na Caribbean walibeba mawazo ya kijamhuri wakati wa kupambana na ukoloni wakitaraji kujenga mfumo mpya wa kidunia usiyo na mabavu ya kimataifa. 

Mfano mzuri ni wazo la kujitegemea la Julius Nyereye, hata kama mfumo wa utawala aliokuja kuutengeneza ulichukua sura nyingine tofauti na ile ya kijamhuri. Mkondo wa mawazo ya kijamhuri ni mtambuka na umesambaa kiasi ya kuwa na ukinzani. 

Hi ni kwa sababu hakuna itikadi inayoweza kunyumbulisha mawazo yote iliyo nayo kwa mara moja. Hata hivyo, falsafa ya CHADEMA ya ‘nguvu ya umma’ inashabihiana sana na ujamhuri nilioeleza hapo juu.

SOMA ZAIDI: Je, Demokrasia ni Sharti Au Matokeo ya Maendeleo ya Kiuchumi?

Nyinyi CHADEMA huiona historia ya Tanzania kuwa ni historia ya kutawaliwa na Wajerumani, Waingereza, na hata tawala za baada ya uhuru zilizofuata. 

Mliona tawala za Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete zilivyogubikwa na kuzuka kwa mfululizo wa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wachache ambao waliteka Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kutawala kwa maslahi yao –ya pesa– wenyewe.

Aidha, mliona miaka ya John Pombe Magufuli kama utawala wa dikteta na wapambe wake na ukuaji wa dola mpya ya kifisadi iliyojikita kwenye upendeleo na matakwa ya mtu mmoja.

Mabadiliko ya katiba

Mnaona kwamba suluhu ya matatizo ya Tanzania iko katika mabadiliko ya katiba, mabadiliko ambayo yatapunguza madaraka ya rais, yatadhibiti mamlaka holela ya dola na yatakayozuia kuibuka kwa ufisadi uliokithiri kila mara. 

Mnasema kwamba mageuzi kama haya yataleta ukombozi wa pili. Mnaona njia ya ukombozi huo kuwa ukombozi wa umma kupitia chama chenu na kuundoa mfumo wa utawala mbovu. Falsafa yenu ya ‘nguvu ya umma’ ni ujamhuri asilia kwa wakati mmoja.

SOMA ZAIDI: Wakazi wa Dar Walilia Katiba Mpya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia

Ninawapa mtazamo huu kuhusu nyinyi wenyewe si kwa nia ya kuwashushia hadhi mawazo yenu kwa kuyalinganisha na ya kijamhuri. Falsafa yenu ni ya asili na ya kipekee. Haiwezi, na wala haipaswi, kushushiwa hadhi kwa kuigeza na falsafa za wengine.

Ninawapa hii kama rasilimali. Chukueni mawazo ya kijamhuri kama kisima cha mawazo ambamo mnaweza kuchagua na kuchukuwa ya kwenu. Fanyeni ulinganifu ambao unaweza kuifanya falsafa yenu ya ‘nguvu ya umma’ ieleweke na wengine. Itumieni mpendavyo.

Mimi, kwa upande wangu, nitakuwa nikiwashirikisha wengine kile wanachoweza kujifunza kutokana na mawazo yenu kama chama.

Nitakuwa nikiwaambia jinsi falsafa yenu inavyowaongoza katika ukosoaji wenu wa ufisadi mkubwa, vita vyenu dhidi ya udikteta, uhamasishaji wenu wa Katiba Mpya na mapambano yenu kwa njia ya ‘nguvu ya umma.’

Dan Paget ni mhadhiri wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia D.Paget@sussex.ac.uk au X kama @pandaget. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *