Wazo la mwisho lililokuwa kichwani mwake ni afike katika eneo la Michezani, eneo lenye majengo marefu ya ghorofa, ajirushe labda ingeweza kumnusuru na wimbi la mawazo na aibu iliyomfika. Hii ni baada ya picha za faragha za *Alua (29) kusambazwa katika mitandao ya kijamii na aliyekuwa mume wake. Hakuwahi kuwaza katika maisha yake kama angewahi kufika katika hali hii.
“Hata sikufirikia kama picha za miaka mitatu nyuma anazo na atazisambaza kuniaibisha na kunivua utu wangu,” anaeleza Alua macho yake yakiwa ni kama mtu asiyeamini maisha yake yalivyobadilika.
Alua aliolewa mnamo mwaka 2019 na kupata mtoto mwaka 2020, hata hivyo mwaka 2021 ulikua mgumu zaidi katika maisha yake baada ya aliyekuwa mume wake kuamua kumdhalilisha.
“Nilikuwa natoka chuo, nikapigiwa simu na rafiki yangu akaniambia niingie WhatsApp kuna kitu kanitumia, ile nataka kuingia tu, nikaona simu ya dada yangu akaniambia nirudi nyumbani haraka huku analia,” anaeleza Alua huku sauti yake ikijaa hisia kadri tunavyo ongea.
Alivyoiitizama simu yake ni kama dunia ilivunjika vipande vipande akishuhudia, picha zake za utupu huku sura yake ikionekana zilizagaa kila kona.
“Kwanza nilitumiwa hizo picha na watu kama 20 na nilipoona nilisikia moyo wangu kama unatoka,” anaeleza Alua ambaye alikwenda hadi Facebook kuona jina la ukurasa uliotuma picha zile. “Nilipokwenda nikakuta watu wanazogoa kuhusu mimi na ni ukurasa mpya ulikuwa unaitwa Homa ya Jiji”.
SOMA: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria
Changamoto hii ilimpata Alua akiwa nyumbani kwao baada ya ndoa yake na mumewe kuvunjika kwa kukosekana maelewano. Alua anaeleza kuwa baada ya kuachana, mume wake hakuwa tayari kumuacha aende.
“Alikuwa anasema mara nyingi nitakuonesha na nitakufanyia kitu kibaya ila sikuwa nafikiria kuwa zile picha za toka tuanze mahusiano anazo na angeweza kuniposti na kunidhalilisha,” anaeleza Alua katika hali simanzi.
“Dunia iliniinamia na nilitaka kujiua nilishakwenda hadi pale michezani kutaka kujirusha ila nikasema yatapita. Yamepita kidunia, ila kwangu sijawahi kupona na sitawahi kupona ndio maana nilihama chuo na kuondoka nyumbani,” aliendelea kueleza Alua.
Haikuwa aibu yangu bali hata familia
Moja ya jambo linalofanya iwe vigumu kuona kuwa kuna matukio ya watu kufanya ukatili kwa kuvujisha picha za faragha na utupu za watu waliokuwa karibu nao ni mtindo wa maisha ya Zanzibar ambapo dini, mila na desturi, imefanya kuwe na hali ya kuficha siri, ni hali hii iliyomfanya Alua asite kutafuta msaada kokote kwani alihisi atazidi kujidhalilisha.
Suala la Alua linafanana kidogo na lile la *Hafia (23), mwanafunzi aliyekatisha masomo yake ya ualimu mwaka 2023. Sababu kubwa ya kukatisha masomo ni aibu na msongo wa mawazo uliomkumba baada ya video yake ya faragha akiwa na aliyekuwa mwenza wake kuwekwa kwenye makundi vya WhatsApp mwaka 2023. Hafia hakuwa anajua kama kuna video ya namna hiyo, kwani ilirekodiwa bila ya yeye kufahamu.
“Sikuwa najua kama amenirekodi, tulipogombana na kila mtu kuendelea na maisha yake miezi mitatu baadae nitakuta hiyo video kwenye makundi mtandaoni,” anaeleza Hafia, msichana mrefu mweupe aliyevalia baibui na mtandio rangi ya choroko aliyekuwa anasimulia huku akiinamisha sura kwa maumivu.
“Kila mtu alinitumia na hakukuwa na hata kukataa maana ni kweli ni mimi na niliumia zaidi maana video ilikuwa haioneshi sura ya huyo aliyekuwa mtu wangu, sasa aibu ikawa yangu na familia yangu,” aliendelea kusimulia.
“Nilikuwa silali, usingizi hauji na nawaza sijui nife au nitoroke nyumbani ,nakumbuka mama yangu alikuwa akisema kufanya siri haikukutosha hadi ukaona uweke ushahidi,” Hafia anasema maneno yale yaliniumiza sana na kuona maisha yake yamefikia mwisho.Baba yake ambaye ni mwalimu wa madrasa aliamua kumkana na kumfukuza Hafia nyumbani kwao.
“Aibu ile ilikuwa kubwa na baba akanifukuza na nikaondoka na kuhamia huku shamba kwa mama yangu mdogo na sikuendelea tena kusoma niko ndani tu hadi leo, watu wanasema sitaolewa tena na bado naitwa majina mabaya,” alimaliza Hafia.
Utafiti uliofanywa katika uandishi wa makala hii, pamoja na tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wasichana na wanawake wanaoipitia udhalilishaji wa kusambazwa kwa picha na video zao za utupu mtandaoni wengi wanapitia msongo wa mawazo na kama ilivyokuwa kwa Hafia na Alua wengi hufikiria kutaka kujiua.
Sheria
Moja ya changamoto kubwa inayo onekana kuwakumba waathirika wengi wa vitendo vya ukatili huu, ni kuwa wengi wao huwa ni vigumu kufika katika vyombo vya sheria. Kwa Tanzania, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ndiyo inayodhibiti usambazaji wa ponografia katika jamii na kutoa adhabu ikiwemo faini na kifungo kisichopungua miaka saba.
Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar linaeleza kuwa ni nadra kupata kesi za watu kushtaki juu ya changamoto hizo kutoka kwa wenza walioachana.
“Kwa kipindi ambacho mimi nimekuwa hapa hakuna taarifa juu ya malalamiko ya wahanga wa vitendo hivyo kushtaki na ni kwa sababu wanaona aibu na kudhani wanaendelea kusambaza taarifa hizo,” anaeleza Hamad Khamis Hamad ambaye amekuwa Kamisha wa Jeshi la Polisi Zanzibar kwa takribani miaka mitatu.
SOMA: Kilichojificha Nyuma ya Kuvuja kwa Video za Utupu Mitandaoni
Asha Abinallah ni Katibu Mtendaji wa taasisi ya Tech and Media Convergency akiwa pia mwanaharakati wa masuala ya matumizi sahihi ya kidijitali Asha anakiri kupokea kesi mbalimbali kutoka Zanzibar.
“Toka mwaka 2018 tumepokea kesi 76 zinahusisha masuala ya kuvunjiwa kwa faragha kwa wanawake na wasichana na kati ya hizo 11 ni kutoka Zanzibar jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuenea kwa haraka,” anaeleza Abinallah.
Moja ya waathirika wa ukatili huu aliyeamua kuchukua hatua za kisheria ni *Khadija (24) Mkaazi wa Mjini Magharibi. Khadija na mama yake walivunja ukimya na kuchukua hatua za kutaka msaada wa kisheria baada ya mwanaume aliyekuwa nae kwenye mahusiano kumtumia video yake ya faragha iliyerekodiwa kwa siri na kumtishia kuwa ataisambaza mtandaoni.
“Alikuwa mchumba wangu kumbe alinirikodi video tukiwa chumbani tulipogombana, akanirushia na kuniambia ukiniacha nitaziposti hizi kwenye mitandao,” anaeleza Khadija, huku akisimulia zaidi namna alivyoendelea kulazimika kutimiza matakwa ya mtu huyo.
“Tuligombana na mimi nikaendelea na maisha yangu ila alikuwa akinitishia nikaonane nae au ataziweka mtandaoni, nikawa nakwenda ili nisiabike alikuwa anasema atazifuta ila hakuzifuta.”
Khadija ni mtoto wa pili kwenye familia yenye watoto wanne, anaishi na mama yake ambaye ni mjane aliyefiwa na mume wake mwaka 2020. Moja ya jambo lililomuwezesha Khadija kupata msaada ni usikivu wa mama yake.
“Mwanangu aliniambia juu ya jambo hilo, niliumia sana zaidi pale niliposikia wanakuwa wanamfanya watu wawili nilitamani kufa ila nikajikaza,” alieleza mama yake Khadija ambaye aliamua kufika Ofisi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto kuomba msaada.
“Nilikwenda kushtaki kwa Mkurugenzi na wakatuma polisi akakamatwa na picha zikafutwa na mtoto wangu akawa salama,” alieleza mama Khadija.
Kubadili Mtazamo
Warda Hemed Mansour ni Mkurugenzi wa Ubunifu kutoka taasisi ya The Launch Pad inayotoa msaada na elimu kuhusu mitandao salama, Warda anaeleza kuwa pamoja na kuwa kuna nyezo za kisheria, kama mwathirika wa matukio haya aliruhusu kurekodi au alijirekodi basi na yeye anakuwa na jinai ya moja kwa moja.
“Wakati tunawapa ushauri tunawaambia kupiga picha wewe mwenyewe na kutuma kwa mtu, wewe ndio unakuwa mtuhumiwa wa kwanza kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao,” anafafanua Warda huku akieleza kuwa waaathirika wengi hukosa motisha ya kuendelea na kesi hizo baada ya kuziwasilisha kuomba msaada.
Kwa nchi Jirani kama Kenya na Afrika Kusini zinavifungu mahsusi katika sheria zao ambazo zinaangazia suala la kusambaza picha za faragha za wengine. Sheria ya Filamu na Uchapishaji ya Afrika Kusini inakataza kusambaza picha za faragha bila ridhaa, na kwa Kenya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni inakataza uchapishaji au usambazaji wa picha au video za faragha za mtu mwingine.
Warda anaeleza kuwa pamoja na hitaji kubwa la kutoa elimu kwa jamii, hasa juu kutojirekodi video za utupu na faragha, kuna umuhimu pia wa kuangalia sheria hasa pale zinapofanya waathirika wa matukio haya kuhofia kujitokeza na kupata msaada.
SOMA: TCRA: Uhalifu ni Uhalifu Tu Hata Ukifanyika kwa Njia ya Simu
Mkurugenzi Idara Ya Maendeleo Ya Jamii Jinsia Na Watoto Zanzibar, Siti Abbas Ali, anaeleza pia umuhimu wa kulinda utu wa watu changamoto hizi zinapotokea.
“Ni vyema wanawake na wasichana kuwa makini na kuacha kutuma au kujirikodi, ila pia ni vyema kuwepo na uwazi wa kuripotiwa kwa matukio haya pale tu vitisho vinapoanza kabla ya kusambazwa ili kupunguza athari zinatomuharibia mtu utu wake,” anasisitiza Siti.
Moja ya taasisi iliyopokea kesi mbalimbali za ukatili Zanzibar,niChama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA, Mkurugenzi wa taasisi hii Dk. Mzuri Issa, anaeleza umuhimu wa jamii kubadilika juu ya kutatua changamoto hii inayoendelea kushamiri.
“Jamii ichukue suala hili kama ni bahati mbaya na kuacha tabia ya kuwaona wahanga wa vitendo hivyo ni wakosaji pale haya yanapotokea,” anaeleza Dk.Mzuri.
*Siyo jina lake halisi
Wewe ni mmoja wa waathirika wa matukio haya ya ukatili kupitia mitandao? Unaweza kupata msaada wa karibu kwa kuwatafuta Launch Pad +255676333935
Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najjatomar@gmail.com.
One Response
Hii imekuwa changamoto ata kwa wanawake wa bara mara wanaume wengi sasa hivi unakuta lazima aombe kwanza picture zako za uchi ata kwenye mahusihano inatakiwa kutolewa elimu kwa wanaume na wanawake