The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ubakaji Unavyowajaza Hofu Watoto wa Kike Mjini Magharibi, Z’bar: ‘Tunaogopa, Hatuko Salama’

Serikali inasema inafanya kila linalowezekana kurekebisha hali hiyo, lakini inakiri kwamba bila ushiriki wa jamii na familia, juhudi hizo zinaweza kushindwa kufanikisha malengo yake.

subscribe to our newsletter!

Mjini Magharibi, Zanzibar. Asha* ni mwanafunzi wa darasa la nne katika moja ya shule za msingi zilizopo mkoani hapa anayelazimika kuishi na kumbukumbu mbaya inayoendelea kuitesa nafsi yake, nayo si nyingine bali ni kubakwa na kulawitiwa na mtu ambaye, licha ya kutekeleza uhalifu wa aina hiyo, ameendelea kubaki uraiani, akiwa huru.

Binti huyu mwenye umri wa miaka tisa, mkazi wa Shaurimoyo, mkoani hapa, alifikwa na kadhia na aibu hiyo mapema mwaka huu wa 2024, ambapo mhalifu wake alimkamata kwa nguvu na kisha kwenda naye porini na kumfanyia ukatili huo. Hii, anakiri Asha, ni kumbukumbu ambayo hatamani iendelee kubaki akilini mwake.

“Nilikuwa natoka dukani jioni, [kijana huyo] akaniita na kisha kuniambia njoo nikutume, akanibeba na kunibana mdomo, akanipeleka msituni, na kunibaka mbele na nyuma, niliumia sana,” alieleza Asha wakati wa mahojiano yaliyofanyika shuleni kwao.  “Baadaye, akanipeleka barabarani na kuniacha hapo, watu wakaniona, wakanipeleka hospitali na polisi.”

“Watu wengi walijua, na hata wakati mwingine watoto hapa shuleni wananichokoza kuwa nimebakwa, [wakifanya hivyo] huwa naona aibu,” amesema Asha, binti mwenye kimo cha wastani, sura ya maji ya kunde, akionekana kuwa na woga mwingi, huku akitetemeka na kuifikicha mikono yake.

Kisa cha Asha ni kielelezo cha hatari inayowakabili watoto na wanawake wengi visiwani Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo watoto na wanawake wengi wanaripotiwa kuwa katika hatari kubwa ya ukatili wa kijinsia.

Mjini Magharibi

Wakati tatizo hili linaripotiwa kuwepo kwenye maeneo mbalimbali ya visiwa hivi vinavyotambulika kwa harufu yake ya marashi ya karafuu, hakuna sehemu tatizo hili limeripotiwa kuwa kubwa zaidi kama ilivyo kwa mkoa wa Mjini Magharibi, mkoa unaoweza kuuita ‘Dar es Salaam’ ya Zanzibar.

SOMA ZAIDI: Ukatili wa Wenza Kusambaza Picha na Video za Faragha Baada ya Kuachana Waliza Wanawake Zanzibar

Ukiwa na jumla ya wakazi wapatao 893,169, wanaume wakiwa 427,977 na wanawake ni 465,242, kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mjini Magharibi ndiyo mkoa wenye watu wengi zaidi visiwani Zanzibar, angalau mara nne ya mikoa mingine, hali inayoweza kuelezea, kwa sehemu, kwa nini inaongoza kwenye tatizo hilo.

Taarifa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, kwa mfano, zinaonesha kuwa wakati matukio ya udhalilishaji kwa Zanzibar nzima yalikuwa 1,369 kwa mwaka 2019, Mjini Magharibi pekee ilikuwa na matukio 324. Kwa mwaka 2023, Zanzibar nzima ilisajili matukio yapatayo 1,954, huku Mjini Magharibi pekee ikiwa na matukio 557.

Hali ya ubakaji kwa miaka mitano kwa mkoa wa Mjini Magharibi.

Ripoti ya Takwimu za Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani ya Januari hadi Disemba mwaka 2023 pia inaonesha kuwa Mjini Magharibi inaongoza kwa vitendo vya ubakaji kwa kuwa na matukio 564 yaliyoelezwa kuwaathiri wasichana wenye umri chini ya miaka 16.

Kushamiri huku kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti kunaifanya Mjini Magharibi kuwa eneo la hatari kwa watoto na wanawake, huku wengi wao wakivamiwa au kuhadaiwa mara kwa mara na wanaume kabla ya kubakwa, kulawitiwa na kufanyiwa aina zingine za ukatili wa kijinsia, na kuwajaza wengi wao hofu kuhusu maisha na usalama wao.

Hofu na mashaka

Hawa ni pamoja na Mwajuma,* mwanafunzi wa darasa la sita katika moja ya shule za msingi iliyopo mkoa wa Mjini Magharibi, ambaye mwaka 2023 alinusurika chupuchupu kufanyiwa ukatili wa aina hiyo alipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwao, akitokea shuleni.

“Ilikuwa Alhamisi [wakati] narudi [kutoka shuleni],” Mwajuma, anayetumia usafiri wa daladala kwenda na kurudi shuleni na mwenye ndoto ya kuwa mhandisi majengo, anasimulia. 

SOMA ZAIDI: Wanawake Zanzibar Wataka Uwakilishi Baraza la Maulamaa: ‘Hatuko Huru Kueleza Shida Zetu kwa Wanaume’

“Sasa, [nilikuwa] nataka nifike nyumbani haraka, nikapita kwenye vichochoro, nikakutana na huyo kijana,” aliendelea kusimulia binti huyo. “Nilikuwa peke yangu, akanifukuza, akanikamata, na kunipeleka kwenye kichochoro, huku akianza kunivua nguo.”

Mwajuma, anayesoma masomo ya mchana na kulazimika kurudi nyumbani jioni sana, aliiambia The Chanzo kuwa alijikaza na kujipapatua, huku akipiga kelele kujiokoa kutoka kwa mshambuliaji wake, na alinusurika tu baada ya kutokea kwa mtu, hali iliyomfanya mshambuliaji wake akimbie. Tukio hilo, hata hivyo, limemjaza Mwajuma hofu kubwa kuhusu usalama wake.

“Bado naogopa sana,” Mwajuma, mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto wanne, aliiambia The Chanzo. “Muda mwingine natamani nipate simu, niwe nampigia mjomba aje anichukue barabarani, au nasubiri mtu anayepita nifuatane naye.”

Kwa upande wake, Amina* alibakwa na rafiki wa kiume wa rafiki yake aliyekuwa akimsindikiza mara kwa mara kwa mwanaume huyo kwenda kuchukua pesa, hali iliyomuacha na maumivu makali ya kimwili na kihisia ambayo anaendelea kuyauguza mpaka hivi sasa.

“Tulikuwa tunakwenda mara mbili kwa wiki, Jumatatu na Alhamisi,” Amina, 14, anaeleza, huku akiwa ameinamisha kichwa chini kwa aibu. “Siku moja, nikapita pale wakati natoka shuleni, nikamuona yule anayempa rafiki yangu pesa, akaniita, akaniambia njoo uchukue pesa ukampe shoga yako, nilipofika akaniziba mdomo, akanibaka.”

Hofu miongoni mwa watoto na wanawake mkoani hapa inaongezeka zaidi wakikutana na wadhalilishaji wao mtaani baada ya kukaa siku kadhaa mahabusu, kwani, wakati wapo wanaohukumiwa kwenda jela, baadhi ya wanaume wanaohusika kutekeleza vitendo hivi hufanikiwa kurudi mtaani katika mazingira waathirika wao hawawezi kuyaelezea.

SOMA ZAIDI: ‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

Taarifa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, kwa mfano, zinaonesha kwamba kati ya kesi zote za ubakaji zilizoripotiwa visiwani humo kwa mwaka 2023, 117 watuhumiwa walihukumiwa. 

Kesi sita watuhumiwa waliachiliwa huru. 214 zinaendelelea mahakamani. 192 zipo kwenye upelelezi. 25 zipo kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali; na sita zimeondolewa mahakamani.

Ushiriki wa familia

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu, aliiambia The Chanzo kwamba wao kama taasisi ya usimamizi wa sheria wanafanya kila linalowezekana kumfanya kila mtu anayeishi mkoani humo, wakiwepo watoto na wanawake, kuwa huru na salama kwenye kuishi na kufurahia maisha yao.

Mwenendo wa ushughulikiwaji wa kesi za ubakaji kwa mkoa wa Mjini Magharibi.

Hata hivyo, Mchomvu alibainisha kwamba kukabiliana na tatizo la udhalilishaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia kunahitaji zaidi ya polisi kufanya kazi zao sawasawa, akitaja ushiriki kamili wa familia na jamii kama uamuzi muhimu sana kwenye kukomesha vitendo hivyo.

“Kesi ikija, siku ya pili unakuta [familia] wameshakubaliana [kuyamaliza],” alidokeza Mchomvu, akikusudia kufichua sababu zinazopelekea kushamiri kwa tatizo hilo. “Lakini pia, ushahidi wa matukio haya [ni changamoto], yanakosa sana ushirikiano kwenye jamii. Hapo huwezi kumzuia mshtakiwa mahabusu ikiwa hakuna ushahidi.”

Amina alithibitisha hili wakati wa mahojiano yake na The Chanzo kwa kusema kwamba baada ya kumwambia bibi yake kama amebakwa, mlezi wake huyo alimpatia tu dawa, huku akimsihi wasiipeleke kesi hiyo polisi.

SOMA ZAIDI: Zanzibar Yachunguza Tukio la Mtuhumiwa Kufariki Mikononi Mwa Vyombo vya Ulinzi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Siti Abbas, ameiambia The Chanzo kwamba Serikali inafanya kila linalowezekana kuwafanya watoto na wanawake kujihisi salama kuishi kwenye maeneo yao husika, ikiwemo kuweka kamera kwenye maeneo mbalimbali.

“Lakini, waowaharibu watoto hawawaharibu kwenye sehemu ya watu kuona,” aliongeza Siti. “[Kwa hiyo,] usalama wa wasichana ni ulinzi wao wenyewe, majirani zao na hata wazazi, kwa sababu mwisho wa siku madhara makubwa yanawakuta watoto na siyo Serikali.”

Ushiriki wa familia pia umegusiwa na mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, Zulpha Bashir Mbwana, ambaye ameiambia The Chanzo kwamba ili jitihada zinazochukuliwa na taasisi kama vile Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla kufanikiwa kwenye kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia, familia zitapaswa kubadilika, na kushiriki kikamilifu.

Uwazi kwa watoto

“Hakuna taasisi kubwa ambayo inaweza ikatibu gonjwa hili, au tatizo hili, kama majumbani,” Zulpha ameiambia The Chanzo. “Baba na mama kuwa wawazi kwa watoto wetu. Watoto wetu wanatakiwa waelezwe ukweli wa mambo majumbani, fulani akikutania hivi, akikushika hivi, usiruhusu, kwa sababu ndiyo mwanzo wa kubakwa na kudhalilishwa.” 

Swali linalobaki ni je, wazazi na walezi wanawapatia watoto wao elimu hii ya msingi ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa miili na maisha yao, na kama wanafanya, hilo linafanyika kwa kiwango na kwa uwazi wa aina gani? 

Kwa mujibu wa Sajda Sharifu, mwanafunzi wa darasa la tano kutoka Shule ya Msingi ya Jang’ombe iliyopo mkoa wa Mjini Magharibi, wazazi na walezi hawafanyi vya kutosha kuwapatia watoto elimu hii.

Sajda Sharifu, mwanafunzi wa Darasa la Tano, Shule ya Msingi Jang’ombe, anatamani wazazi na walezi wangekuwa wanafanya zaidi kwenye kuwapatia watoto wao elimu inayoweza kuwasaidia kujilinda dhidi ya vitendo vya ubakaji. PICHA | NAJJAT OMAR

Akijitolea mfano yeye mwenyewe ambaye anasema amekuwa akisikia kuhusu matukio ya ubakaji zaidi kwenye vyombo vya habari kama redio kuliko kutoka kwa wazazi wake, binti huyu ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa wa wazi kwa watoto wao, na kuwapatia elimu inayoweza kuwasaidia kujilinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

“Muda mwingine wazazi hawatusikilizi [tukiongea] kuhusu udhalilishaji,” Sajda, 10, aliiambia The Chanzo. “Tunafundishwa sana shuleni ila siyo nyumbani. Wazazi nao inatakiwa watusikilize na kutufundisha.”

*Siyo jina lake halisi.


Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts