Wadau wa sekta ya uziduaji nchini wameitaka Tanzania kuwa na tahadhari katika suala la mhamo wa nishati, kwani linaweza kuleta athari kwa jamii na watu wenye kipato cha chini ambao hawajaandaliwa mazingira mazuri.
Haya yanajiri wakati ambapo ajenda mbalimbali za kimataifa zimehamasisha mataifa kuachana na matumizi ya nishati ya kisukuku na kuhamia kwenye nishati jadidifu. Wadau hawa wamesema kuwa, ikiwa mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania, yataharakisha mchakato huu bila kuwa na mikakati ya kutosha, kuna hatari ya kuathiriwa kiuchumi kwa wananchi wa kawaida.
Wakizungumza katika Jukwaa la Uziduaji linalofanyika jijini Dodoma, kuanzia Novemba 5 hadi 6, 2024, wadau wameonyesha kuwa kama taifa, tunapaswa kujithamini, kujua ni wapi nafasi yetu ilipo, na jinsi gani tunaweza kujiweka katika mazingira bora ya kuhama, badala ya kukimbizana na ajenda zinazotolewa.
“Tunatambua kwamba kuna shinikizo la kimataifa la kuhama kutoka katika nishati ya mpito kwenda kwenye nishati jadidifu. Tunajua kwamba mabadiliko haya hayatafanana kwa kila nchi,” alisema Shaidu Nuru, mtaalamu wa jiolojia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
“Ukianza kumlinganisha Tanzania na mataifa haya ambayo yamepiga hatua kwenye suala la nishati lakini pia yamepiga hatua katika suala la viwanda, itakuwa ni ngumu sana, kwa hiyo tunafahamu kwamba ni shinikizo na ni ajenda ya kitaifa lakini siyo kwamba nchi zote zitafika katika nafasi sawa, kasi sawa na wakati sawa. Tunajua kwamba kutakuwa na badiliko la taratibu kutoka nishati mpito kwenda kwenye nishati safi lakini itachukua muda,” aliongeza.
SOMA ZAIDI: Nishati Safi ya Kupikia: Wanaoongea ni Wengi Lakini Bosi ni Hela
Jukwaa la Uziduaji huandaliwa kila mwaka na Jukwaa la Asasi za Kijamii ambazo zinashughulikia masuala ya madini, mafuta na gesi nchini Tanzania (HakiRasilimali) kwa lengo la kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, kuchunguza njia za kuunda na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, na kuleta mabadiliko ya sera.
Kwa mwaka 2024 limeandaliwa chini ya kauli mbiu inayosema Kukuza Maendeleo Endelevu: Sekta ya Uziduaji Tanzania na mhamo wa Nishati huku likikutanisha wadau wa sekta ya madini mafuta na gesi takribani 214 kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, alisisitiza kuwa licha ya shinikizo la kimataifa la kuhamia kwenye nishati safi, Tanzania inapaswa kuwa na mkakati wa kujizatiti ili kuendana na uhalisia wa maisha ya kiuchumi ya wananchi wake.
“Tunapojadili, tuangalie kila mtu mchango wake kulingana na hali yake, kwa mfano kama leo tunasema mafuta ni mabaya, na wakubwa huko wanasema ni lazima tuhame kwenye matumizi ya mafuta, lakini tujiulize hadi leo, ni nani anatumia mafuta zaidi kuliko mwingine?” alisema.
Aidha, alieleza changamoto za utekelezaji wa ajenda ya nishati safi kwa nchi za Afrika, akisisitiza kuwa, kabla ya kuhamia kwenye nishati safi, ni muhimu kuelewa kuwa hali ya kiuchumi ya kila nchi ni tofauti na itahitaji hatua mbalimbali kutekeleza mabadiliko haya kwa ufanisi ili kutosababisha athari kwa uchumi na maendeleo ya watu.
Ajenda ya mabadiliko ya kaboni ya chini inayohusiana na Makubaliano ya Paris inakusudia kuleta mabadiliko makubwa katika mahitaji ya madini, ugavi wa nishati, na teknolojia za nishati. Inalenga mataifa kuachana na matumizi ya makaa ya mawe, mafuta, na gesi chafu na nishati nyingine zinachangia uchafuzi.
SOMA ZAIDI: Ukata Unavyokwamisha Matumizi ya Nishati Mbadala Dodoma
Hii inatajwa kuwa inaweza kusababisha changamoto katika mtiririko wa uwekezaji na kusababisha kuporomoka kwa mapato katika nchi zinazochipuka zinazozalisha rasilimali hizi, kama vile Tanzania.
“Tujaribu kuangalia hali ya dunia kwenye nishati ya kisukuku. Marekani kwa sasa inaongoza katika uzalishaji wa nishati kisukuku, China na Urusi wanazalisha, na mashariki ya kati pia wanazalisha. Tunajua kwamba matumizi ya gesi asilia yanaongezeka,” alieleza Priva Clemence, mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la EnergyCARDS.
Clemence aliuwa akichangia mada iliyohusu Maendeleo ya Nishati Kisukuku au Nishati Mpito Katika Zama za Uendelevu kwa kimombo The Future of Fossil Fuels in the Age of Sustainability.
“Swali si kama Tanzania ihame sasa, bali ni jinsi gani tunaweza kujiandaa na mabadiliko haya. Hilo ndilo swali ambalo wadau wanapaswa kujiuliza. Unapozungumzia matumizi ya LNG (liquefied natural gas) na gesi, tunahitaji kuweka sera bora za kuvutia uwekezaji na kuongeza uzalishaji wa rasilimali hizo,” aliongeza Clemence.
Takwimu kutoka Wizara ya Nishati zinaonyesha kuwa, kati ya nishati inayozalishwa nchini, 65% inatokana na kuni, 26.2% ni mkaa, na 8.8% ni mchanganyiko wa gesi ya petroli ya lita (LPG), umeme, na vyanzo vingine.
Naye mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Godwin Lema alisema kuwa jambo la msingi ni kujiridhisha na changamoto zisizotarajiwa baada ya kuchukua hatua ya kuhama au kutokuhama katika matumizi ya aina ya nishati.
“Tunapozungumzia watu, pia tunazungumzia uchumi na mambo mengine muhimu. Hatupingi maendeleo, lakini tunapozungumzia masuala ya mazingira, tunapaswa kuwa na uwiano bora,” alisema Lema.
SOMA ZAIDI: Daktari Bingwa Muhimbili Awasihi Watu Kuacha Kutumia Kuni, Mkaa Kupikia
Kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka 2017/18, matumizi ya nishati ya kuni yamekithiri hasa maeneo ya vijijini ambapo asilimia 84.8 ya kaya hutumia nishati hiyo ikilinganishwa na maeneo ya mijini ambapo matumizi ni asilimia 17.4. Mahitaji ya nishati ya kuni vijijini ni makubwa kwa kuwa ni nishati pekee inayopatikana kwa gharama nafuu.
Aidha utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 60.5 ya kaya katika maeneo ya mijini hutumia nishati ya mkaa, ikilinganisha na asilimia 11.5 ya kaya katika maeneo ya vijijini.
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.