Search
Close this search box.

Nishati Safi ya Kupikia: Wanaoongea ni Wengi Lakini Bosi ni Hela

Watu wasio na uhakika wa kula, wakipata chakula watakipika kwa nishati ya bei ya chini zaidi.

subscribe to our newsletter!

Ndoto yangu ilikuwa nije kuwa mwanamuziki wa Hip-hop. Ndoto ikafa lakini mapenzi yangu na muziki wa huo yanaishi mpaka leo, na moja kati ya nyimbo zangu bora kabisa ni pamoja na ule wa Stimu Zimelipiwa wa Joh Makini. Kwenye wimbo huo, msanii anaimba:  Wanaongea wengi lakini bosi ni hela

Mstari huo umenishawishi kuchangia mawazo yangu juu ya mjadala wa nishati safi ya kupikia hapa nchini, mjadala ambao umeshika kasi sana siku za hivi karibuni, hususan baada ya kupata msukumo mkubwa kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan. 

Kwa sasa, inakadiriwa kwamba ni asilimia nane tu ya Watanzania wote ndiyo wanatumia nishati safi ya kupikia. Malengo ya Serikali ni kuwa ifikapo mwaka 2033, angalau asilimia 80 ya Watanzania wote watumie nishati hiyo.

Kwa wasiofahamu, nishati safi ya kupikia ni nishati kutoka kwenye vyanzo dumivu, na matumizi yake kwa shughuli za kupikia hayana athari, au athari kubwa tuseme, kwa mazingira, wala afya ya watumiaji. Umeme, unaotokana na vyanzo jadidifu kama vile upepo, jua na joto-ardhi, ni mfano sahihi.

Hata hivyo, Tanzania imejumuisha gesi kama nishati safi, ingawaje gesi yetu ni mithani; yaani haidrokaboni kama yalivyo mafuta. Japo si chafu kama mafuta ila si safi kwa sababu inatiririsha hewa ukaa na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

Kulinda mazingira

Sababu ya kwanza ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kutaka kulinda mazingira dhidi ya ukataji miti kwa ajili ya mahitaji ya kuni na mkaa, unaosababisha ukame na mmong’onyoko wa udongo. Hiyo ni hoja ya kisayansi, haiwezi kukanushwa kwa maneno matupu. 

SOMA ZAIDI: Ukata Unavyokwamisha Matumizi ya Nishati Mbadala Dodoma

Hata hivyo, kabla ya kuibeba kama ilivyo, ni muhimu kujua kuwa misitu mingi ipo vijijini, na wanavijiji wanatumia zaidi kuni, hasa zile zinazodondoka zenyewe bila kukatwa na mtu wakati watu wa mjini wanatumia zaidi mkaa.

Wakati fulani tuliambiwa zaidi ya asilimia 50 ya mkaa wote unaozalishwa nchini unatumika Dar es Salaam. Taarifa hizi zituongoze kujiuliza, je, jitihada za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupeleka umeme vijijini zitapunguza matumizi ya mkaa? 

Majibu ni hapana, takwimu za hivi karibuni zimetuonyesha kuwa Dar es Salaam ndiyo mkoa uliouganishwa zaidi na umeme kuliko mikoa yote nchini. Hivyo, kama kufikiwa na umeme ndiyo kutumia nishati safi ya kupikia, matumizi ya mkaa yalipaswa kuwa chini Dar es Salaam, kuliko mkoa mwingine wowote. 

Kinyume chake, Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa matumizi ya mkaa na hivyo kufanya kuwapelekea watu umeme kutokuwa sawa na kuwapa nishati safi ya kupikia.

Bosi ni hela

Pengine tujiulize ni kwa nini mikoa yenye umeme ndiyo mikoa inapika kwa nishati chafu. Majibu anayo Joh Makini: Wanaongea wengi lakini bosi ni hela. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya Watanzania milioni 15 wanaishi kwenye dimbwi la umasikini. 

SOMA ZAIDI: Daktari Bingwa Muhimbili Awasihi Watu Kuacha Kutumia Kuni, Mkaa Kupikia

Mpango wa kupunguza idadi ya Watanzania masikini ndani ya miaka kumi ijayo ni muhimu, na ndiyo utaamua kama mpango wa kutaka kuongeza idadi ya watumia nishati safi ya kupikia kutoka asilimia nane hadi asilimia 80 ya Watanzania wote utawezekana ama utabaki kwenye maandishi.

Watu wasio na uhakika wa kula, wakipata chakula watakipika kwa nishati ya bei ya chini zaidi. Ni rahisi kwa mchumi wa chuo kikuu kusema nishati nafuu ni gesi, akakupa na namba kwa kusema unahitaji mkaa wa Shilingi 1,000 tu kupika ugali. 

Baada ya ugali kuiva ule moto unaoteketea bila matumizi ni hasara, na zile Shilingi 1000 za kila siku ukizijumlisha ni gharama kubwa kuliko mtungi wa gesi wa Shilingi 52,000 unaoweza kuuzima baada ya kupika; kudhibiti upotevu wa nishati. Ni rahisi kusema hivi.

Hata hivyo, nani anayo Shilingi 52,000 mara moja gesi iishapo? Lakini wengi wanamudu mkaa wa Shilingi 1,000, kesho itajisumbukia yenyewe, siyo kwamba hawaijali kesho, wanajali ila hawana hela. Ni suala la maisha halisi, siyo uwingi wa maneno ya motisha. Kama ni maneno, wanaoongea ni wengi, lakini bosi ni hela. 

Turudi kwenye umeme. Wakazi wa Dar es Salaam ni mfano tosha kuwa Mtanzania anaogopa kupika maharage kwenye umeme; anatumia umeme wake kuwasha taa, kuangalia runinga na kuchaji simu. Siyo kupika makande.

Dira

Mwaka 1999, wakati taifa linazindua Dira 2025, malengo ilikuwa ni kupandisha pato la mwaka la Mtanzania kufikia Dola za Marekani 3,000. Leo imebaki mwaka mmoja kutamatisha Dira 2025, na wastani wa pato la Matanzania ni Dola za Marekani 1,200.

SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania

Tumeshindwa kufikia malengo kwa asilimia 60. Hatujafikia hata nusu ya tulichokusudia. Tulishindwa kukuza pato la Mtanzania, kabla ya kuibuka kwa UVIKO-19 na vita ya Ukraine.

Utakuwa uongo kusingizia UVIKO-19, ama vita ya Ukraine, ama ya Palestina kuwa ndiyo imefanya tusifikie malengo. UVIKO-19 na hizo vita zimeibuka miaka 20 baada ya utekelezaji wa Dira 2025. Vivyo hivyo, tutakuwa waongo kama tutaamini kuwa tunaweza kufikia malengo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kilichosalia kutamatisha Dira 2025. 

Tulishakosea miaka 25 iliyopita, tunayo nafasi ya kujisahihisha miaka 25 ijayo.

Taifa letu linaandaa Dira 2050. Je, tutakwenda kuandika namba kubwakubwa kuwa ifikapo 2050 pato la Mtanzania liwe Dola za Kimarekani 8,000 ama tutaweka malengo halisi na kuyatafsiri kwa vitendo? 

Muda utaamua, na majibu yake ndiyo yataamua kama tutafika ama hatutofika kwenye nishati safi ya kupikia.

Mikakati ya kutaka watu wote tupikie gesi, ama umeme, iendane na mikakati ya kuongeza pato la Mtanzania. Ni wajibu wa Serikali kusimamia utajiri wa nchi na kuugawanya kwa watu wake. Wengi tutaongea kuhusu nishati safi ya kupikia lakini mwisho wa siku, bosi ni hela. 

Maisha bora kwa kila Mtanzania ni ongezeko la pato la mtu mmoja mmoja; awe na hela ya kuamua apikie gesi au umeme.

Clay Mwaifwani ni mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 758 850 023 au claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *