Wiki iliyopita, niliona video ya kituo kimoja cha televisheni kikifanya mahojiano na Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Wallace Karia, kuhusu mambo mbalimbali ya uendeshaji soka nchini, hasa suala la idadi ya wachezaji wa kigeni.
Mwandishi wa kituo hicho alikuwa akimuhoji Karia kutaka kuona kama ongezeko la wachezaji wa kigeni limesaidia kukuza wachezaji wazawa. Kwa sasa, Ligi Kuu ya Bara inaruhusu klabu kusajili wachezaji 12 wa kigeni na inaruhusiwa kutumia idadi yoyote kati yao katika kikosi kinachoanza.
Uhuru huo umesababisha hadi klabu ambazo kiuchumi hazijatengemaa kuona wachezaji wa kigeni ndio wanaoweza kuzipa timu zao matokeo mazuri, na kwa hiyo, kumekukuwa na ongezeko la wachezaji hao kila mwaka.
Kwa mujibu wa Karia, wachezaji wa kigeni wamesaidia kuifanya ligi yetu kuwa bora zaidi, na kwamba wameleta ushindani kwa wachezaji wazawa, ushindani ambao utasaidia kukuza viwango vyao na hivyo timu ya taifa kuwa bora Zaidi.
Karia aliwasifu mabeki wa Tanzania kuwa wamefanikiwa kupambana dhidi ya wageni na ndiyo maana timu nyingi zinatumia mabeki wa hapahapa Tanzania na kutaka wachezaji wa maeneo mengine kupambana kwa jinsi hiyo.
Ukiangalia mabeki waliopambana ni pamoja na Dickson Job na Ibrahim Bacca na Bakari Nondo, ambao wamekuwa wanakosekana kwa nadra kwenye kikosi cha Yanga na Taifa Stars, Mohamed Hussein “Tshabalala”, Shomary Kapombe, Mwamnyeto na Abdulrazak Mohamed, wanaotamba kikosi cha Simba na Taifa Stars na Lusajo Mwaikenda wa Azam.
SOMA ZAIDI: Wanaohoji Rangi ya Njano Yanga Wako Sahihi. Viongozi Wawasikilize
Lakini timu nyingine zenye uwezo bado zinasajili mabeki kutoka nje, hata kama ni wa bei ya chini kulinganisha na wale wanaosajiliwa na klabu za Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars.
Sina uhakika kwamba mabeki wazawa ndio waliofanya kazi kubwa ya kujiingiza kwenye vikosi vya kwanza vya klabu zao na hivyo Taifa Stars, lakini nachojua ni kwamba ni utamaduni wa dunia nzima kuwa na safu ya ulinzi ya wachezaji wazawa, labda tu pale mgeni anapokuwa na kipaji cha aina yake.
Klabu nyingi duniani hupendelea kusajili washambuliaji na viungo kutoka nje ya nchi kwa kuwa vipaji vyao ni nadra na hivyo huwa na bei kubwa kulingana na mabeki. Kama mabeki hawatofautiani sana, kuna sababu gani ya kukimbilia nje kumsajili mchezaji ambaye atakugharimu fedha nyingi?
Mapungufu ya kisera
Kwa hiyo, si kwa ushindani wao uwanjani bali na nguvu za kawaida za sokoni zinazoamua.
Nadhani kitu kikubwa hapa ni kutokuwa na sera imara ya kukuza wachezaji wetu na baadaye.
Ukiangalia ligi zinazoongoza kwa ubora Afrika utaona mataifa ya kaskazini ndio yanaongoza, yaani Misri, ambayo ni namba moja, Algeria (2), Morocco (3) na Sudan (4), huku Tunisia ikiwa imetupwa nafasi ya nane, chini ya Tanzania, Afrika Kusini na Angola.
Ligi hizi hupangwa katika orodha hiyo ya ubora kutokana na ubora wake kwa ujumla, kiwango cha ushindani na kiwango cha mvuto wa wachezaji waliopo kwenye ligi hizo pamoja na hatua za juu ambazo klabu zake hufikia katika mashindano ya Afrika.
SOMA ZAIDI: Lini Tutamsikia Toni Kroos wa Tanzania?
Hata hivyo, ubora huo hauweza kutofautiana kulingana na vigezo anavyotumia mpangaji kwa kuwa wako wanaoongeza sifa kama ubora wa miundombinu, umaarufu, mafanikio ya kibiashara, uendeshaji na usimamizi. Lakini ubora huo huweza kubadilika vigezo kwa kadri ligi zinavyokuwa, kuibuka kwa ligi mpya na mzunguko wa kawaida wa mafanikio.
Kwa kutumia kigezo kama wachezaji wa nje kuongeza ubora na ushindani, kwa nchi za kaskazini mwa Afrika, ambazo ndizo zinaongoza kwa mafanikio katika bara hili, idadi ya wachezaji wa kigeni haizidi watano, ukiachana na Sudan ambayo hali ya kisiasa bado haijatulia.
Misri inaruhusu wachezaji wanne tu wa kigeni kwa msimu mmoja, wakati Algeria ndio imeruhusu msimu huu kuwa na wachezaji hadi watano kutoka watatu, huku Morocco ikiendelea kuwa na wachezaji watano.
Iwe na mashindano ya timu za taifa au klabu, Morocco, Misri na Algeria ndio zimekuwa zikibadilishana ubingwa, labda kwa nadra sana timu za taifa za Afrika Magharibi ndio huingilia kati. Hali ni hiyohiyo katika ngazi ya klabu ambako hutawaliwa na mataifa hayo ya Afrika Kaskazini.
Programu za maendeleo
Ukiangalia kwa umakini, utagundua kwamba mataifa hayo yana programu nzuri za watoto na maendeleo ya vijana, huku mifumo yao ya kijamii ikiweza kudhibiti udanganyifu wa umri na hivyo nchi kuwa na uhakika na kizazi kinachopikwa kuanzia chini.
Na Serikali za nchi hizo husaidia maendeleo hayo kwa kujenga miundombinu inayoweza kutumiwa vizuri na watoto na vijana, mafunzo kwa walimu na vituo vya ubora, kama ambavyo mfalme wa sasa wa Morocco ameufanyia mchezo wa mpira wa miguu na mingine.
SOMA ZAIDI: Prince Dube Anapitia Ugumu wa Mbappe
Kwa hiyo, nchi hizi hazijawa pale juu kwa bahati, bali kwa mipango ya dhati ya kuendeleza michezo. Hivi sasa timu zetu za taifa, Taifa Stars na ile ya chini ya miaka 20 zimefuzu kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika.
Mafanikio haya yanaweza kutupumbaza kwa kuwa Tanzania sasa imekuwa mshiriki wa kawaida wa AFCON. Lakini ukiangalia kwa makini ni kulegezwa kwa ushindani wa kufuzu ambao sasa ni mataifa 54 ya Afrika kuwania nafasi 24, takriban nusu ya idadi yote.
Kwa maneno mengine, kwa sasa kutofuzu ni vichekesho kwa kuwa nafasi ni kubwa mno tofauti na miaka michache iliyopita wakati mataifa 54 yalipokuwa yakiwania nafasi 16 tu, au 12, au hata nane wakati Tanzania ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980.
Kujipumbaza
Kwa hiyo, kuchukulia mafanikio ya kufuzu AFCON na klabu zetu kufika hadi fainali ya mashindano ya Afrika kuwa ni kukua kwa soka letu ni kujipumbaza kwa kuwa hao wanaoziwezesha klabu kufuzu hawajapikwa hata kidogo na mfumo wetu. Ni watu waliokuja kutafuta fedha tu, na wanachofanya ni kulitangaza soka letu tu na si kulinyanyua.
Na hata kuchukulia kufuzu mfululizo kucheza AFCON kuwa ni kuendelea kwa soka letu, bado ni kujipumbaza kwa kuwa fainali hizo sasa zimerahisishwa sana. Ni nadra sana siku hizi kukutana na mataifa mawili kama Algeria na Ivory Coast kwenye kundi moja.
Ukikutana na Morocco kundi moja, basi wapinzani wengine ni ama Burundi, Uganda, Ethiopia na hata Djibout. Hapo itakuwa ni kichekesho nchi kutokuwa moja ya timu mbili zilizovuka hatua ya makundi.
SOMA ZAIDI: Mwamuzi Omary Mdoe Anastahili Adhabu Kali
Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na sera imara ya maendeeleo ya soka letu kuliko kutegemea maajabu halafu kuyatumia hayo kama kielelezo cha kukua kwa soka letu.
Hatuhitaji kubahatisha wakati wa kuzungumzia maendeleo yetu, bali maelezo thabiti yanayoonyesha kulifanyika kitu fulani, halafu kikazaa kitu kizuri katika soka letu. Kama akina Che Malone (Simba), Gibri Silla (Azam), Pacome Zouzoua (Yanga) na Stephane Aziz Ki (Yanga) wametokea katika shule za soka, kwa nini wetu wasitokee huko?
Na kwa nini hao nyota watokee shule za soka au ni mfumo uliowalazimisha kwenda huko? Tunahitaji kuwa na maelezo ya kutosha ili hata kujitathmini iwe rahisi.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.