Hivi karibuni, nilikuwa natembelea akaunti mbalimbali za vyombo vya habari kujua kilichotokea, au kuripotiwa, lakini nikakutana na kitu ambacho, nadhani, hakuna mhariri aliyekipitia kabla ya kuruhusu kichapishwe mtandaoni.
Zilikuwa ni picha za wachezaji watatu; wawili wanaosakata soka Tanzania na mmoja ambaye yuko barani Ulaya. Maandishi chini ya picha hiyo yalikuwa yanasoma, “Matapeli wa usajili msimu huu.” Niliposoma, nikaona wameitwa jina baya la matapeli kwa sababu hadi sasa hawajafunga bao, au mwenendo wao si mzuri.
Unahitaji kuwa na hoja nyingi kuthibitisha watatu hao ni matapeli iwapo watakwenda mahakamani kudai kuwa wamedhalilishwa na kudai fidia. Na sidhani, na siamini, kama hoja za kimpira zinaweza kuhalalisha chombo cha habari kimuite mchezaji “tapeli.”
Tukio hilo limetokea wakati maofisa habari wawili wa klabu za Simba na Yanga, Ahmed Ali na Ali Kamwe, mtawalia, wakiwa wametishiwa kufikishwa mahakamani baada ya kutoa maneno ambayo waathirika wamedai yamedhalilisha, kupotosha umma, na kuchafua bniashara zao.
Kamwe ametishiwa kushtakiwa mahakamani na kutakiwa aombe radhi baada ya kutoa maneno ambayo mdai, kampuni ya Sandalandi inaoidhamini jezi ya Simba, anasema yamechangia kushusha mauzo ya jezi za klabu hiyo, hivyo kutaka alipwe Shilingi bilioni tatu kama fidia ya kuharibiwa biashara yake.
SOMA ZAIDI: Wageni Hawakuzi Soka la Tanzania, Wanalitangaza
Ali naye ametishiwa na klabu ya Yanga kutokana na maneno aliyosema kuhusu kiungo wa klabu hiyo, Pacoume Zouzoua, kuwa ameshamaliza mkataba Yanga, hana mpango wa kuuongeza, na amechoshwa na sindano kila siku “kama anazuia mimba” na kwamba Simba wanaangalia kama anawafaa Simba, na wakiona hawafai watawaachia Yanga kama walivyofanya kwa Cloutus Chama.
Hakuna shaka, wote wawili walitoa kauli hizo bila uangalifu, hasa wakizingatia kuwa klabu hizo mbili zina utani wa jadi kiasi kwamba wanaona wanaweza kusema lolote likachekesha na kupita kama upepo.
Ndivyo ilivyofanyika kwa wale wachezaji watatu waliopachikwa jina la matapeli bila ya mhariri kuangalia athari zake iwapo watachukua hatua ya kwenda mahakamani.
Mpira biashara
Kilichopo kwa sasa ni kwamba mpira wa miguu unazidi kuwa biashara, na hivyo wadau wengi wanaingia kwa lengo la kushirikiana na klabu na taasisi zinazojihusisha moja kwa moja na mpira ili wafanye biashara.
Kampuni hizo zinaweka mabilioni kwenye mpira zikitegemea kuwa fedha zilizowekezwa zitarudi na faida, hivyo ziko makini kuangalia mwenendo wa mauzo na mambo mengine mengi yanayoendana na biashara zao zilizohusishwa na mpira wa miguu.
SOMA ZAIDI: Wanaohoji Rangi ya Njano Yanga Wako Sahihi. Viongozi Wawasikilize
Klabu nazo ziko makini kuhakikisha wadau wake wanapata taarifa sahihi kuhusu mambo yanayoendelea ndani yake na nje kwa kuwa taarifa zisizo sahihi zinaweza kuvuruga wanachama, mashabiki na wadau wengine.
Hii inaweza kuwapelekea kuanza kufikiria kuwaondoa viongozi, kuanza kuzomea wachezaji ambao habari zao zimepotoshwa kwamba hawataki kuendelea kubakia kwenye klabu waliyopo sasa, na wakati mwingine kusababisha hata mashabiki kususia kwenda viwanjani.
Kwa hiyo, utani wa Simba na Yanga unazidi kuwekewa mipaka tofauti na ulivyokuwa mwanzo wakati klabu hazikuwa zikiajiri wanasheria wengi kwa ajili ya kushauri jinsi ya kuenenda.
Na iwapo pande zote mbili zitakomalia mashauri yake hadi kwenda mahakamani, ni dhahiri kuwa wadaiwa watakuwa kwenye wakati mgumu kwa kuwa kuendesha shauri tu ni kazi moja, achilia mbali kushinda kesi. Unashinda wakati ukiwa umechoka sana baada ya hekaheka za mahakamani.
Fikiria kwamba wawili hao wamepoteza ajira kwa sababu yoyote ile, itakuwaje kwao iwapo mashauri hayo yataendelea kuwepo mahakamani? Hakuna klabu itakayoendelea kusimamia kesi kwa njia ya kugharamia mawakili au mambo mengine.
Tusifike huko
Kwa hiyo, haitakiwi ifike huko. Ni lazima wasemaji na wadau wengine katika tasnia ya michezo waanze kuwa makini na tabia zao wanapozungumzia masuala ya klabu nyingine.
SOMA ZAIDI: Lini Tutamsikia Toni Kroos wa Tanzania?
Imekuwa ni tabia ya wanahabari wote wa klabu kuzungumzia klabu nyingine badala ya kutoa taarifa zinazohusu klabu zao. Ofisa habari anaweza kuwa anatoa taarifa inayotakiwa ichukue nusu saa, lakini akatumia dakika kumi kuzungumzia ubaya kwa kitu kama hicho kinachofanywa na klabu nyingine.
Kwa kawaida, mtu wa habari anapotoa taarifa hutakiwa asiruhusu jambo jingine lolote litawale taarifa yake na ndiyo maana wale wanaojua vizuri jambo hilo, hulazimika hata kukataa maswali yanayohusu jambo jingine lisilohusiana na taarifa yake kwa hofu kuwa ndio linaweza kupata nafasi zaidi ya lile alilokusudia.
Ndiyo maana taarifa za hao wasemaji wa klabu zinazotembea sana mitandaoni ni zile za kukashifu upande mwingine badala ya ile aliyokusudia ya kuutaarifu umma maendeleo ya klabu yake. Mitandaoni watu wanapenda kucheka, hivyo, ukiwapa vichekesho watacheka na kukukubali, wakati kile muhimu ulichotaka wakipate hawana habari nacho.
Uofisa habari ni fani ambayo ina miiko na mwongozo wake na ndiyo maana hata Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) huwa na mafunzo maalumu kwa watu wa tasnia hiyo.
Tishio hilo kwa Kamwe na Ali ni ishara tu kwamba huko tunakokwenda ni kugumu sana, kwa sababu watu mbalimbali wanaotaka kujihusisha na mpira wa miguu wanazidi kuingia, na hivyo unatakiwa umakini mkubwa na weledi badala ya kufanya mambo kwa mazoea.
SOMA ZAIDI: Prince Dube Anapitia Ugumu wa Mbappe
Na kwa sababu mpira una fedha kwa sasa, si ajabu ukakuta wanasheria wanaojipa kazi ya kutafuta makosa ya kiuandishi, ya utoaji taarifa na mambo mengine, ili wawataarifu wanaodhani wameathirika na kuwashawishi wafungue kesi za madai.
Katika hali hiyo, wale wanaoropoka kuhusu chapa za klabu nyingine, kuwasema vibaya viongozi, au mashabiki wengine, wanaweza kujikuta katika hali ngumu sana kama sakata la Kamwe na Ali halitakuwa ilani kwao.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.