Tunafahamu, yapo mambo mengi bado hayaendi sawa kwenye nchi hii ya Tanzania, na mihangaiko ya kila siku ya maisha inatulazimisha wengi kujikita kwenye kile kisichoenda vizuri badala ya vile vinavyoenda vizuri, angalau kwa ulinganifu. Lakini amini, usiamini, kwenye mwaka huu wa 2024, yapo mambo kadhaa yaliyoing’arisha Tanzania.
Chukulia hili la kuimarika kwa Shilingi, kwa mfano, ambalo limekuwa gumzo kwenye siku chache zilizopita, huku kila mmoja akionekana kutafuta majibu ya nini kimepelekea Shilingi ya Tanzania kuimarika dhidi ya baadhi ya fedha za kigeni, hususan Dola ya Kimarekani.
Kuimarika kwa Shilingi maana yake ni kwamba mwananchi anapungukiwa na maumivu anapobadilisha fedha zake za Kitanzania kwenda fedha kama ile Dola ya Kimarekani kwani tofauti inakuwa siyo kubwa kama inavyokuwa pale ambapo Shilingi inakuwa imedorora.
Hali inapokuwa hivi faida zinakwenda kwa mwananchi wa kawaida, kama vile kuweza kununua bidhaa nchi za nje kwa bei nafuu, na taifa kwa ujumla kwenye jitihada zake za kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na watu wake.
Pia, kama ambavyo imedhihirika, hali inapokuwa kama hivyo kunakuwa na upatikanaji wa kutosha wa fedha za kigeni, hususan Dola za Kimarekani, ambazo ni nyenzo muhimu za ufanyaji wa biashara na shughuli nyingine za kiuchumi nje ya mipaka ya Tanzania.
SGR kuanza kazi
Mbali na hili la kuimarika kwa Shilingi, ni muhimu kukumbuka kwamba ilikuwa ni mwaka huu wa 2024 ndipo Tanzania, kwa mara ya kwanza, ilizindua rasmi matumizi ya Reli ya Kisasa ya Umeme, maarufu kama SGR, na kuvuta hisia za wengi ndani na nje ya nchi.
Safari ya kwanza ya treni iliyobeba abiria ilifanyika June 14, 2024, kwa kuwabeba abiria waliotoka Dar es Salaam hadi Morogoro kisha kutoka Morogoro kurejea tena Dar es Salaam.
SOMA ZAIDI: Stesheni Za Reli Ya SGR Zapewa Majina Ya Marais Tanzania
Kuanza kufanya kazi kwa miundombinu huu muhimu kutakuwa na faida kubwa kwa Watanzania kwenye uwezo wao wa kuharakisha safari zao na mizigo yao, hali inayotegemewa kutoa mchango mkubwa kwenye kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Faida hizi za kiuchumi na kijamii, bila shaka, zitazidi kuongezeka pale mpango wa kujenga reli ya treni ya umeme yenye mtandao wa kilomita 1,219 za njia kuu utakapokamilika na kuanza kwa matumizi yake. Mpango huu una awamu tano ambazo zinaanzia jijini Dar es Salaam hadi jijini Mwanza.
Bwawa la Nyerere larindima
Lakini, kama ambavyo umeona hapo, hii ni treni ya umeme, na utekelezaji wake utakuwa ni wa kusuasua endapo kama Tanzania haitahakikisha upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu.
Ndiyo maana ni muhimu pia kutaja hapa mradi mwingine muhimu ulioanza utekelezaji mwaka huu wa 2024 ambao si mwingine bali ule wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
Mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme kwenye bwawa hilo uliwashwa mwezi Februari mwaka huu na kuingiza megawati 235 kwenye gridi ya taifa, hali iliyopunguza kiasi makali ya mgao wa umeme.
SOMA ZAIDI: Deni la Taifa Kuendelea Kuwa Gumzo 2023?
Mitambo mingine ya umeme kutoka kwenye bwawa hilo imeendelea kuwashwa, ambapo mpaka Disemba 12, 2024, mradi huo ulikuwa unazalisha megawati 1,175 kati ya 2,115 zinazotakiwa kuzalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa.
Hatuwezi kusisitiza vya kutosha hapa namna upatikanaji wa uhakika, kwa bei nafuu, wa nishati ya umeme unavyoweza kuboresha maisha ya kila siku ya Mtanzania na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwenye michezo hakupoi
Kwenye tasnia ya michezo kwa mwaka 2024, mambo yalikuwa si haba pia. Vilabu vyake vya soka, hasa Simba na Yanga, viliendelea kufanya vizuri kwenye uga wa kimataifa, lakini timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ndiyo ambayo imeitoa Tanzania kimasomaso.
Taifa Stars ilifanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 itakayofanyika nchini Morocco. Hii ni baada ya ushindi wa bao kwa sifuri kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya Guinea, mchezo ambao ulifanyika Novemba 19, 2024, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, uliopo jijini Dar es Salaam.
Taifa Stars iliungana na vinara wa Kundi H, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambao walikuwa na alama 12, hatua ambayo iliifanya kuwa miongoni mwa mataifa matatu ya Afrika Mashariki yaliyofuzu AFCON 2025. Mataifa mengine yaliyofuzu ni Uganda na DRC.
SOMA ZAIDI: Tumeanza Vibaya AFCON 2025 Lakini Hatujuti
Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kufuzu kushiriki michuano ya AFCON baada ya kushiriki mwaka 1980 (Nigeria), 2019 (Misri), na 2023 (Ivory Coast). Katika awamu zote hizo ilizoshiriki, Tanzania imekuwa ikiishia kwenye hatua ya makundi tu.
Ndugulile WHO
Jambo jingine lililoing’arisha Tanzania kwa mwaka huu wa 2024 ni kuchaguliwa kwa Mtanzania Faustine Ndugulile kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Ukanda wa Afrika.
Ndugulile, aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni (CCM), aliiheshimisha Tanzania kwa kutwaa nyadhifa hiyo muhimu ya kulitumikia moja kati ya mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa (UN).
Hata hivyo, Ndugulile, aliyepata kuhudumu kama waziri, hakuweza kuishi kuutumikia wadhifa huo kwani alifariki mnamo Novemba 27, 2024, ambapo Tanzania ilitangaza kumteua Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kuchukua nafasi yake.
Matukio mengine yaliyoin’garisha Tanzania kwa mwaka huu wa 2024 ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kutangazwa kuwa uwanja wa ndege wenye viwango vya juu vya ubora na usalama barani Afrika kwenye shindano la kimataifa linalojihusisha na kupima ubora wa viwanja vya ndege duniani.
Je, unafahamu tukio jingine lililopaisha heshima na hadhi ya Tanzania kimataifa ambalo hatujafanikiwa kuliorodhesha hapa? Unaweza kutuwekea kwa kuandika hapo chini na kuwawezesha wasomaji wengine kunufaika kwa kulifahamu.
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza, unaweza kumfikia kupitia matonyingamakaro@gmail.com.