Nchi yetu Tanzania inashikilia nafasi ya pili barani Afrika kwa idadi ya mifugo, lakini changamoto kubwa ni ubora wa mifugo hiyo.
Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia ya 2024, Tanzania Economic Update: Harnessing the Opportunity for a Climate-Smart and Competitive Livestock Sector in Tanzania, moja ya sababu kuu zinazochangia kutokuwepo kwa mifugo bora kama ng’ombe, mbuzi, nguruwe, na kondoo nchini ni upungufu wa madume bora ya kuzalisha.
Kama taifa, tumeshindwa kuzalisha mbegu bora za wanyama kama ng’ombe, mbuzi, nguruwe, na kondoo. Kuzalisha madume ya mbegu bora ni sayansi inayohusisha kupandisha mbegu zenye ubora maalum ili kuhakikisha mnyama anayezaliwa anakuwa na sifa bora zinazotarajiwa.
Zoezi hili linaweza kufanikishwa na taasisi zetu za Serikali kama vile Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Shirika la Ranchi za Taifa (NARCO), na Kituo cha Kitaifa cha Upandishaji kwa Chupa (NAIC).
Ni muhimu kwa Serikali kuziwezesha taasisi hizi kifedha, kiteknolojia, na kiutalaamu ili ziwezekuzalisha mbegu bora za wanyama wa nyama na maziwa. Hii itasaidia kuondoa mifugo hafifu isiyokidhi vigezo vya kimataifa, kupunguza athari za mazingira zinazotokana na mifugo duni, mbayo haiwezi kidhi vigezo vya kimataifa.
Kuna njia mbili kuu za kuboresha ubora wa mifugo yetu hapa nchini.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tanzania Inahitaji Sera Mpya ya Mifugo, Uvuvi?
Njia ya kwanza ni kuagiza mbegu bora kutoka nchi zenye mazingira yanayofanana na yetu na zinazozalisha mbegu zenye ubora wa hali ya juu. Mfano mzuri ni nchi kama Afrika Kusini, Botswana, Namibia, na jirani yetu Kenya, ambazo zina mbegu bora kama ng’ombe wa Boran.
Tukileta mbegu hizi na kuhakikisha zinalindwa, kuendelezwa, na kusambazwa kwa wafugaji wakubwa na wadogo, tunaweza kupunguza changamoto ya uzalishaji wa wanyama kwa kuzaliana wao kwa wao, au inbreeding kwa kimombo, jambo ambalo ni tatizo kubwa linalosababisha udhaifu wa mifugo yetu.
Njia ya pili ni kuboresha aina za mifugo yetu ya asili kama vile Mpwapwa, Zebu, na Ankole. Tukiboresha sifa zao za kizazi na kuzisambaza kwa wafugaji katika maeneo mbalimbali ya nchi, tunaweza kuondoa mifugo dhaifu isiyo na tija.
Mifugo bora huonyesha sifa za kiuchumi kama ukuaji wa haraka, ukubwa wa mwili, uwezo wa kuzaa watoto wakubwa na wenye afya, pamoja na kinga dhidi ya magonjwa. Uboreshaji huu si tu utainua tija ya sekta ya mifugo, bali pia utaimarisha maisha ya wafugaji kwa kuongeza kipato na kupunguza gharama za uzalishaji.
Tunatambua changamoto za kusambaza mbegu bora katika nchi yetu ni kubwa, hasa kufikia maeneo ya mbali kama Bukoba na Mtwara. Hata hivyo, uwekezaji katika vituo vya uzalishaji wa mbegu bora kwa kila mkoa, au kanda, ni suluhisho linaloweza kuleta mafanikio makubwa.
SOMA ZAIDI: ‘Ukoloni wa Ndani’: Kwa Nini Watu Waishio Maisha ya Kiasili Wanaendelea Kuteseka Tanzania?
Njia nyingine ni kushirikisha sekta binafsi. Baadhi ya wafugaji wakubwa binafsi wamekuwa wakiagiza madume bora kutoka nchi kama Kenya na Afrika Kusini.
Serikali inaweza kushirikiana na wafugaji hawa kwa kuruhusu mifugo yao bora kupandishwa na majirani zao, au kushirikiana na taasisi kama TARILI na NAIC ili kuhakikisha mbegu hizo zinathibitishwa ubora wake na kusambazwa kwa wafugaji wengine.
Ushirikiano huu unaweza kufungua milango kwa upatikanaji wa mbegu bora kwa wafugaji wadogo na kuongeza tija ya sekta nzima.
Ripoti ya Benki ya Dunia tuliyoitaja hapo juu inaonyesha kuwa ili sekta ya mifugo iweze kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa, kuna haja ya kuwekeza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 546 kuanzia mwaka huu 2024 mpaka 2029.
Uwekezaji huu, pamoja na mambo mengine, utaimarisha programu za kuboresha mifugo ya asili kama Mpwapwa, na kuhakikisha mbegu hizi bora zinamfikia kila mfugaji nchini, hivyo kuinua sekta ya mifugo na ustawi wa kiuchumi kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: Matarajio ya Serikali Kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Kusimamia Usafirishaji Mifugo
Tukiboresha ubora wa wanyama wetu, mlaji atanufaika kwa kupata nyama bora na maziwa zaidi, kipato cha mfugaji kitaongezeka, pato la taifa litakua, na zaidi ya yote, tutapata fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa uchumi wetu.
Wafugaji tunatoa wito kwa mamlaka husika kuwekeza zaidi katika sekta ya mifugo. Uwekezaji kwenye madume ya mbegu bora unaweza kuleta mapinduzi makubwa kutoka kwenye ufugaji wa jadi kuelekea ufugaji wa kisasa wenye tija.
Tusiridhike na bora mnyama, bali tujenge msingi wa kuwa na mnyama bora!
Albert Rweyemamu ni mfugaji anayefanya kazi na Royal Farm iliyopo Misenyi, Bukoba. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia rweyemamualbert@gmail.com au X kama @AlbertRweyemam6. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.