The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Matukio ya Mauaji Yawasukuma Wakazi wa Mkonze, Dodoma Kushinikiza Kujengewa Kituo cha Polisi

Kata hiyo yenye wakazi 45,000 imeshuhudia matukio ya mauaji takribani sita ndani ya mwaka huu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Ilikuwa majira ya saa nane usiku, Pendo Mwakibasi, 41, alipokea simu kutoka kwa mama yake mzazi kuwa mdogo wake aitwae Mwamvita Mwakibasi, 33, amevamiwa nyumbani kwake.

Usiku huo wa Septemba 6, 2024, Pendo alifunga safari na kuelekea kwa mdogo wake aliyekuwa akiishi katika mtaa wa Muungano A, kata ya Mkonze, jijini Dodoma. Alipofika alikuta mdogo wake na mtoto wake, Salma Ramadhan, aliyekuwa akisoma darasa la sita wakiwa wamevamiwa. 

“Nilikuta chumba chote kimetapakaa damu,” alisema Pendo kwa uchungu wakati akiongea na The Chanzo, Oktoba 8, 2024, alipokuwa kituo cha polisi Dodoma akifuatilia kesi ya mauaji ya mdogo wake. “Kitanda chote kilikuwa kimetapakaa damu. [Mwamvita] damu zilikuwa zinamtoka shingoni, puani na masikioni. Na mtoto wake damu zilikuwa zinatoka sehemu za mbavu, puani na masikioni.”

Pendo anaendelea kueleza kuwa Salma, 12, alibakwa pia, lakini Mwamvita hakuingiliwa kimwili kwa kuwa alikuwa kwenye siku zake.

“Tulimkuta na nguo zake akiwa amezivaa vilevile. Inaelekea walivyomuona mama yuko katika hali ile hawakuhangaika naye,” alisema Pendo akiwa amekaa kwenye jiwe, ameegamia gari na mkononi akiwa ameshikilia simu.

Upendo Mwakibasi ambaye ni dada wa Mwamvita akiwa nje ya kituo cha Polisi Dodoma.

Baada ya kukutana na hali hiyo Pendo anasimulia kuwa aliwaita majirani na kuomba msaada wa kuwapeleka majeruhi hospitali.“Tulifanikiwa kuwapeleka hospitali, lakini kwa bahati mbaya wakawa wamefariki. Walifariki baada ya kufika hospitali,” alisema Pendo huku akiwa ameinamisha kichwa chini.

Pendo anadai kuwa familia yao bado haielewi chanzo cha mauaji hayo kwani mdogo wake alikuwa ni mtu wa kufurahi na kila mtu, na kwa muda mrefu hawakuwahi kusikia kitu chochote kibaya kilichokuwa kinamhusu ndugu yake huyo. 

Mwamvita Mwakibasi enzi za uhai wake.

SOMA ZAIDI: LHRC: Uchunguzi Uharakishwe Mauaji ya Katibu CCM Kilolo

Kutokana na tukio hili, Jeshi la Polisi Dodoma liliwakamata watu wanne kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, ambapo watatu kati yao walifunguliwa kesi namba 23436 ya mwaka 2024 mbele Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, na ikatajwa kwa mara ya kwanza Septemba 19, 2024. 

“Watu hao walisema wenyewe [wakishauwa] wanakinga damu,” alisema Pendo akinukuu maelezo aliyopewa na polisi. “Tukauliza damu wanaipeleka wapi wakatutajia mkubwa wao [aliyewatuma] wametuambia lakini bado hatujamthibitisha. Ina maana wao walichofanya walikinga damu na kuondoka nayo.”

Mtoto Salma Ramadhani enzi za uhai wake.

Pendo anaendelea kusema, “vifo hivi vimetuhuzinisha sana, siyo vya haki. Tunajua kufa kupo, na kila mtu atakufa lakini kuna vifo vingine kama hiki cha Mwamvita na mwanae ni vifo ambavyo vimetuumiza kama familia.”

Mauaji ya Mwamvita na mwanaye siyo tukio pekee lilitokea kwenye kata ya Mkonze. Julai 21, 2024, kwenye korongo moja uliokotwa mwili wa mwanamke aliyefahamika kwa jina la Angela Stephano, 23, ukiwa ndani ya kiroba.

Mwili huo ulipatikana katika mtaa wa Chinyika ulikuwa umefungwa kwenye nailoni na maboksi, kisha kuwekwa kwenye kiroba hicho. 

Oktoba 14, 2024, The Chanzo ilifika katika kata ya Kizota kuzungumza na mama wa mwanamke huyo, anayefahamika kwa jina la Marry Msuya.

Nilikutana na Marry, 48, majira ya saa nne asubuhi akiwa dukani kwake akiendelea na pililikapilika za kupika chakula kwa ajili ya wateja wake. Mama huyu mwenye watoto sita alikuwa amesuka rasta, na kuvalia dera la rangi ya chungwa, alisema mtoto wake aliyeuwawa alikuwa akiishi kata ya Mkonze, mtaa wa Michese.

Kabla ya tukio hilo kutokea, mtoto wake alikwenda nyumbani kwake kumsalimia, anakumbuka alimuambia kuwa amepata kazi kwenye duka la vipodozi. Baada ya mtoto wake kurudi anapoishi, simu yake haikupatikana tena.

Mama huyu anasimulia kuwa aliendelea kumtafuta mtoto wake bila mafanikio. Ndipo siku moja alipokea ujumbe kutoka kwenye namba ya simu ya mtoto wake aliyekuwa akimtafuta, ujumbe uliosema simu yake ni mbovu, wawasiliane kwa njia ya ujumbe mfupi. 

“Nikamuambia mtoto wako anaumwa akanitumia Shilingi 25,000, mimi sikuwa na wasiwasi wowote,” alisema mama huyo. “Baada ya muda tumekaa akatuma ujumbe [tena] anaomba 50,000, alimtumia mdogo wake. Mdogo wake akaniambia mama Angel ameomba 50,000 nikamuambia ya nini?”

“Nikimpigia [simu] anasema tuchati. Nikamuambia mdogo wake embu nipe hizo jumbe nisome. Angela anapenda kuchanganya L kwenye R, [niliposoma] nikamuambia hizi jumbe siyo Angela anayeziandika.”

Hali hiyo ilimpa wasiwasi mama huyu na ndipo alipochukua uamuzi wa kwenda kwenye eneo ambalo mwanaye alikuwa anakaa kwa ajili ya kufahamu hali yake. Alipofika alikuta chumba cha mwanaye kimefungwa na alipowauliza majirani aliambiwa kwamba ni muda umepita hawamuoni na namba yake haipatikani. 

Marry Msuya mama mzazi wa Angela Stephano aliyevaa gauni la njano akiwa na mwandishi wa The Chanzo Jackline Kuwanda.

Baada ya kufuatilia aligundua kuwa vitu vya binti yake havikuwemo tena mule ndani, na akaelezwa kwamba kuna mtu alivichukua. Kuanzia hapo Marry anaeleza kuwa alianza kufuatilia ili kujua ni wapi vilipo vitu vya mtoto wake, baadhi ya watu wakamwambia kuwa itakuwa ni ngumu kuvipata tena lakini wakampa namba za mtu aliyedaiwa kuvichukua. 

SOMA ZAIDI: Familia ya Kibao kwa Rais Samia: Bado Tunaamini Hatua Zinaweza Kuchukuliwa Dhidi ya Waliohusika na Mauaji ya Mzee Wetu

“Wakaniambia bwana huyo kijana ni tapeli mkubwa kachukua simu za watu, kachukua 1,000,000 ya mama mmoja. Lakini huyo kaka huwezi kumpata kwa sababu ni mwizi,” alisimulia mama huyo.

“Nikawaambia hata kama kamuua mtoto wangu basi hata nipate mifupa nikazike. Wakanipa namba, nikapiga akapokea mwanamke. Nikampa kijana aongee naye, akamuuliza wewe ni mke wa Jackson [Magoti]? Akasema hapana. Akamuambia kuna kazi hapa tumefanya tuna 400,000, akamuambia nitumie, akasema siwezi kutuma nataka kuja mpaka mahali ulipo.”

Marry aliongozana na huyo kijana hadi alipokuwa mwanamke aliyepokea simu, walipofika walikuta simu anayoitumia ni ya mtoto wake anayemtafuta. “Nikamuuliza simu [hiyo] umetoa wapi, akasema mimi nimepewa na Jackson [Magoti].”

Wakati anaendelea kumtafuta binti yake Marry alipata taarifa kutoka kituo cha polisi Dodoma kuwa kuna mwanamke ameokotwa akiwa amefariki. Alipofika kituo cha polisi aliulizwa ikiwa anaweza kumtambua mwanaye?

“Nikawaambia kama ni wa kwangu nitamtambua,” alisema mama huyo machozi yakiwa yanamlenga. “Nikaambiwa kuna nguo ziko hapa. Walivyonitolea zile boksi [nilijua ni mwanangu] maana nilimuambia awe anatandika boksi chini ya godoro. Walivyotoa nguo nikawaambia basi mtoto ni wa kwangu.”

Asubuhi na mapema alidamka kwenda mochwari ya hospitali ya rufaa Dodoma kuthibitisha kama ni mwili wa mtoto wake. Akakuta kweli ni mtoto wake, licha ya kuwa ulikuwa umeharibika kutokana na kukaa muda mrefu.

“Tulivyoenda hospitali kwa sababu maiti ilikuwa imekaa muda mrefu ilikuwa ni siku ya 11 walipima wakasema imeganda, kwa hiyo walimpasua wakawa wamechukua kila kiungo kidogo kidogo nikaambiwa vinapelekwa kwa Mkemia Mkuu, lakini mpaka leo sina majibu ya Mkemia Mkuu.”

Angela Stephano enzi za uhai wake.

Marry alieleza kuwa mtuhumiwa wa mauaji ya mwanaye, Magoti, 34, alikamatwa, na alipohojiwa alieleza kuwa amuua binti huyo kwa kumnyonga kwa sababu alimtongoza, akakubali, lakini akakataa kushiriki naye tendo la ndoa. 

SOMA ZAIDI: Takribani Mwaka Tangu Wapendwa Wao Wauwawe Kikatili, Familia Hizi Zataka Haki Kutendeka

Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo inadaiwa alisafirishwa hadi jijini Mwanza kwa sababu huko nako alikuwa anadaiwa kuhusika na mauaji mengine, na alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu. 

Kaburi la Angela Stephano lilipo Nkonze, Dodoma.

Kituo cha polisi

Haya ni baadhi tu ya matukio ya mauaji yaliyotokea kwenye kata ya Mkonzi. Kwa mujibu wa diwani wa kata hiyo, David Bochela, kwa mwaka huu takribani matukio sita ya mauaji yameripotiwa. 

Novemba 6, 2024, The Chanzo ilifika katika kata ya Mkonze yenye idadi ya watu 45,000, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, na kuzungumza na wakazi wake. Katika mazungumzo hayo ilibainishwa kuwa kata hii haina kituo cha polisi hata kimoja. 

Wakazi wa kata hii walieleza kuwa kukosekana kwa kituo cha polisi kunapelekea watu kufanya uhalifu kwenye kata hiyo bila hofu, lakini pia wananchi wanashindwa kwenda kuripoti matukio ya uhalifu na kuyafuatilia kwa sababu wanalazimika kufuata huduma za kipolisi katika kituo cha polisi Dodoma, kilichopo umbali wa kilomita tisa kutoka katani hapo. 

“Tungejengewa walau kituo kidogo cha polisi kingeweza kutusaidia,” alisema Musa Masimba, 33, ambaye ni mkazi na Mkonze anayejishughulisha na udereva wa bodaboda. 

“Maana Mkonze ni kata ambayo ndani yake kuna Mkonze yenyewe, Chisichili, Michese, Chikoa, Muungano kule, lakini ukiangalia maeneo yote haya ninayokutajia hakuna kituo cha polisi hata kimoja. Halafu kata ni kubwa sasa hivi, watu wamekuwa ni wengi.”

Ushirikiano

Bochela aliiambiwa The Chanzo kuwa hali ya kata hiyo kukosa kitu cha polisi inawanyima usingizi wao kama viongozi wa kata, na tayari wameshawasilisha maombi kwa halmashauri ya jiji la Dodoma ili waweze kujengewa kituo katani hapo.  

SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji

Hata hivyo, Bochela akaongeza kuwa hata kama kituo hicho kitafanikiwa kujengwa bado wananchi wa kata hiyo wana kazi kubwa ya kuhakikisha watengeneza umoja na ushirikiano baina yao na Jeshi la Polisi, kwani hiyo ndiyo nguzo kubwa ya kutokomeza vitendo vya uhalifu na mauaji. 

“Dawa pekee ya kudhibiti uhalifu ni ushirikiano unaoweza kutokea miongoni mwa wanajamii, kukubali kushiriki kampeni za ulinzi moja kwa moja.”

“Kituo cha polisi kina jengwa eneo moja unajua, kwa hiyo hata kama utakitawanya viwe sehemu tatu bado ulinzi na usalama hautakuwa umeimarishwa kama ambavyo wananchi wakichukua hatua ya kushirikiana na Jeshi la Polisi na sisi viongozi kutokomeza uhalifu,” Bochela aliendela kusisitiza. 

Bochela aliongeza kuwa kuwepo kwa kituo cha Polisi kitasaidia watu kuwa na kituo maalum kwa ajili ya kupeleka taarifa za moja kwa moja au kufika kituoni.

“Kwa uhalifu wa kawaida kituo cha polisi kinaweza kusaidia. Lakini kwa matukio ya kutisha ukisema kituo cha polisi hakiwezi kutosha. Lazima sisi kama wananchi tukubali kushirikiana kufanya operesheni.”

Kituo kila kata

Akizungumza na The Chanzo Novemba 15, 2024, Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alisema kuwa jeshi hilo lina mpango wa kujenga kituo cha polisi kwenye kila kata ikiwemo kata ya Mkonze pia, lakini hakusema ni lini ujenzi huo utakuwa umekamilika.  

“Tunatafuta eneo ambalo tunataka tuainishe kwa kupitia polisi mkaguzi wa kata ya Mkonze na uongozi wa Mkonze,” alisema Katabazi wakati wa mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake. 

“Lakini na kupitia halmashauri, kupitia wakurugenzi nao wameshaanza kuainisha maeneo ambayo vituo vya polisi vitajengwa. Lakini kwa sababu kata ni nyingi lazima tutaangalia maeneo gani tujenge vituo vya polisi. Lakini wananchi wakianza [kujenga] itatupa chachu ya kuweza kuongeza nguvu kujenga kituo cha Polisi kwenye eneo husika.”

Kwa mujibu wa utafiti wa The Chanzo tatizo la upungufu wa vituo vya polisi halipo Dodoma pekee. Mwaka 2022, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, aliwahi kuliambia Bunge kuwa Tanzania inaupungufu wa vituo vya polisi daraja B, 470. 

Upungufu huo ulielezwa kwamba unatokana na uhitaji uliokuwepo wakati huo wa vituo 563 huku vituo vilivyokuwepo vilikuwa ni 93 tu. 

Mtandao umethibitiwa

Kamanda Katabazi alibainisha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu, yaani kuanzia Julai  hadi Oktoba 2024 wastani wa matukio 15 ya mauaji yaliripotiwa mkoani humo. Lakini hadi hivi sasa mtandao uliokuwa ukihusika na matukio ya mauaji tayari wameudhibiti na wahusika wote wamefikishwa mahakamani. 

“Ule mtandao tumeshaumaliza, wahalifu tumeshawafikisha mahakamani. Waliokuwa wanafanya uhalifu wa mauaji kwa maana wanaingia kwenye nyumba za watu, wanavamia watu, wanaua na kuchoma watu, huo mtandao tumeshaumaliza.”

“Karibu watuhumiwa wote waliotekeleza matukio ya mauaji Dodoma wamefikishwa mahakamani. Takribani watuhumiwa 12 hivi wamefikishwa mahakamani. Ule mtandao wa matukio matano wote tumeshawafikisha mahakamani,” alisema Kamanda Katabazi. 

Agosti 30, 2024, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ilisema mauaji yaliendelea kushika kasi nchini licha ya Jeshi la Polisi kufanya jitihada za kuwakamata watahumiwa na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema tume ilibaini visababishi mbalimbali vya matukio ya mauaji, ambapo baadhi yake ni ulipaji kisasi na imani za kishirikina.

Mwaimu akasisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria za nchi na haki za binadamu na kutambua namna bora ya kupata suluhu ya migogoro inayowakabili katika ngazi zote za jamii.

“Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha kunakuwepo na taratibu za kuimarisha ulinzi wa usalama wa raia,” Mwaimu alipendekeza wakati akizungumza na waandishi wa habari. 

“Hiyo ni kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za mapema katika kushughulikia matukio ya uhalifu kwa kushirikiana na mamlaka husika.” 

Jackiline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts