Mwaka 1994, beki wa Colombia, Andres Escobar, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa mjini Medellin baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo kurejea nyumbani ikitokea Marekani ambako ilitolewa katika hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia.
Escobar alikuwa mmoja wa mabeki wa timu hiyo wakati ilipofungwa mabao 2-1 na Marekani. Katika mechi hiyo, Escobar alijifunga wakati akijaribu kuzuia krosi ya chini kutoka upande wa kushoto na kujikuta akiusukumia wavuni mpira, kuipa Marekani ushindi wa mabao 2-1 ulioinyima Colombia tiketi ya kuingia hatua ya mtoano.
Escobar akaonekana ndio sababu ya Colombia kuondolewa mapema, tena na Marekani ambayo ni taifa dogo katika soka duniani. Mara baada ya timu kurejea Colombia, beki huyo alipigwa risasi na mtu asiyejulikana na ndio ukawa mwisho wake.
Wengi wanahusisha kifo chake na tukio la kujifunga, ingawaje hakuna ushahidi wa kutosha kwa kuwa hata muuaji hakujulikana, lakini kutokana na nchi hiyo kujaa wacheza kamari ambao ni wauza dawa za kulevya wenye nguvu, inawezekana kabisa moja ya magenge hayo ya biashara hiyo haramu ndilo lililohusika kutekeleza mauaji hayo.
Kosa la Escobar lilikuwa la kawaida sana kimpira, lakini katika nchi ambayo ina uendawazimu wa mapenzi na mpira wa miguu, tukio hilo liliudhi wengi, na inawezekana kabisa, ama magenge ya wauza dawa za kulevya au mashabiki, waliamua kufanya unyama huo baada ya timu yao kuondolewa mapema na majirani zao.
Ingekuwa ni kosa kama lililofanywa na kiungo Ladack Chasambi, sijui magenge hayo, au mashabiki, wangechukua uamuzi gani kuhusu maisha ya chipukizi huyo. Labda wangefurahia kumuua kwa kumchoma moto ili waone raha wakati akiteseka na maumivu ya kuungua.
SOMA ZAIDI: Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka
Lakini kadri siku zinavyokwenda mashabiki wa soka wanazidi kustaarabika na hata magenge hayo ya dawa za kulevya yanachukua mwelekeo tofauti katika kushiriki kubashiri matokeo na uwanja wa kubashiri sasa umekuwa mpana kwa kuwa mikeka inahusisha timu nyingi.
Ustaarabu huo pia unatokana na mashabiki na wadau kuzidi kuelewa vizuri mchezo wa mpira wa miguu na masuala mengine kama ubinadamu. Zamani ilikuwa shida kwa mechi za mitaani kuisha bila ya vurugu; kumpiga refa au wachezaji na mashabiki wao kupigana na timu pinzani.
Siku hizi, refa asiye na ulinzi wowote anachezesha mechi za mitaani zenye upinzani mkali, lakini anaondoka salama bila ya kurushiwa hata kofi.
Chasambi
Tulitegemea ustaarabu huu ndio ungetawala tukio la Chasambi kujifunga kwa bahati mbaya wakati Simba ikitoka sare ya bao 1-1 na Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu iliyofanyika katikati ya wiki na kusababisha Simba ishindwe kurudi kileleni.
Chasambi alipokea pasi kutoka kwa Abdulrazack Hamza akiwa pembeni, upande wa kushoto, huku wachezaji wa Fountain Gate wakielekea kumzonga. Badala ya kuutuliza, Chasambi aliamua kuurudisha golini kwa kipa. Lakini alipiga mpira wa juu ambao kipa Tintin Camara alishindwa kuuzuia kwa mwili wake kwa kuwa asingeweza kudaka pasi ya beki wake.
Juhudi zake za kutaka kuuzuia mpira kwa kiwiliwili zilishindikana na mpira ukapitiliza kwenda wavuni na kuipa Fountain Gate bao la kusawazisha. Na ingawa kipa wao alionyeshwa kadi nyekundu, Simba walishindwa kupata bao jingine ambalo lingeweza kusahaulisha machungu ya kujifunga.
SOMA ZAIDI: Uraia kwa Viungo Watatu wa Singida Big Stars Haukidhi Maslahi Yoyote ya Kisoka au Kitaifa. Ubatilishwe
Ladack, ambaye siku hiyo angeweza kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi kama asingefanya kosa hilo baada ya kucheza vizuri kwa muda mwngi na kutoa pasi ya bao, alishikwa na butwaa wakati akishuhudia mpira ukijaa wavuni.
Mikono yote miwili akaipandisha juu kwenda kushika kichwa, huku miguu yake ikianzaa kujikunja kuupeleka mwili ardhini. Sekunde chache baadaye akawa amekaa chini, mikono kichwani akionekana kujutia alichofanya.
Ni baada ya sekunde chache mchezaji wa Fountain Gate akamfuata kumfariji na baadaye mchezaji wa Simba akamfuata kumuinua.
Kwa matukio hayo unaona jinsi Chasambi alivyostushwa na mpira alioupiga kupitiliza wavuni, huku mikono na kichwa chake vikionyesha ni jinsi gani haamini kilichotokea na kukijutia. Ilikuwa ni siku nzuri kwake iliyoisha kwa majonzi ambayo hakutegemea.
Risasi za maneno
Kama ilivyokuwa kwa magenge ya wauza dawa za kulevya na mashabiki wa Colombia, ndivyo ilivyo kwa baadhi ya mashabiki wa Simba wanaomrushia Chasambi risasi za maneno kujaribu kumuua.
Inawezekana kabisa kwa maneno yaliyorushwa tangu tukio hilo litokee, yameshamuua kabisa mchezaji huyo mdogo na kunahitajika juhudi kubwa za ushauri ili kumfufua arejee kwenye njia sahihi aliyokuwa akiifuata.
Na kwa kuwa maneno hayo yamekuwa kama milipuko ya risasi zinazolengwa kwake, kuna uwezekano mchezaji huyo akahofia hata kubeba majukumu katika kikosi kitakachoanza mechi inayofuata ya wawakilishi hao wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho.
SOMA ZAIDI: Yanga Haikufanya Uamuzi Sahihi kwa Wakati Sahihi Ilipoamua Kuachana na Miguel Gamondi
Na akiangalia huko nyuma kama kuna mfano wake, anaona matukio ya kutisha yanayowahusu wachezaji wa Simba waliofungisha. Wapo waliopotea kabisa, wapo waliopumzishwa kwa muda na wapo walioachwa baada ya usajili.
Anaweza kupuuzia kelele za baadhi ya maofisa wa Yanga na mashabiki kushangilia kosa lake, lakini ni vigumu kwake kustahimili kelele za mashabiki na wanachama wa klabu yake.
Faraja
Kwa hiyo, inafaa kwa mchezaji kama huyo, ambaye ameanza kuaminiwa katika kikosi cha kwanza na kupewa majukumu makubwa kwenye timu yenye wachezaji wengi nyota kutoka sehemu mbalimbali Afrika, kuwa naye karibu kumfariji na kumpa moyo kuwa bado anaweza kufikia ndoto zake.
Inategemea benchi la ufundi lina washauri wa namna gani wa masuala ya kisaikolojia, wakiongozwa na kocha mkuu, David Fadlu, ambaye ameshaonyesha kukubali kuwa alichofanya Chasambi ni kosa la kimpira.
Lakini jamii nayo haina budi kuwajibika kumlinda. Kitendo cha baadhi ya wachambuzi kusema kwa uhakika kuwa Chasambi alifanya makusudi bila ya kuwa na ushahidi wowote, kinaweza kumuumiza zaidi na kuporomosha kiwango chake.
Ni vigumu kuthibitisha kusudio la mtu ambaye amefanya jitihada kutafuta bao katika mazingira magumu, halafu akaonekana anajifunga. Kuonyesha kusudi hilo ni ngumu sana hata zijengwe hoja nyingi kiasi gani.
SOMA ZAIDI: ‘Ilala ni Soka’ Ina Lengo Zuri Kukuza Soka Ngazi ya Vitongoji. Lakini Kuna Kasoro za Msingi
Pili ni vyombo vya habari vya mtandaoni ambavyo vimeshawajenga watu wanaojitoa akili kuwa ndio wasemaji wakuu wa masuala ya klabu za Simba na Yanga. Hawa huhojiwa kila baada ya tukio au mechi ili watoe maoni yao.
Pamoja na kwamba hawawakilishi chombo au taasisi yoyote, hupewa kipaumbele na hutoa maneno makali. Na wameshatoa maneno makali dhidi ya Chasambi kuonyesha kuwa alikusudia kujifunga na kwamba Simba haimtaki tena.
Kundi gani la Simba lisilomtaka Chasambi analoliwakilisha? Hawa wanaweza kusababisha migogoro isiyo na ulazima au kuvuruga timu au kumvuruga mchezaji.
Wote hao watasababisha Chasambi acheze kwa tahadhari mechi zinazofuata, na kila kosa atakalofanya litaangaliwa kwa mapana na marefu, kiasi kwamba itakuwa shida kwake kujitoa mhanga kama alivyofanya katika mechi ya Fountain Gate kabla ya kujifunga.
Jamii haina budi kukilinda kipaji chake kwa kuacha kutoa tuhumu zisizo na ushahidi wowote kwa ajili ya kumdidimiza.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.