Dar es Salaam. Jumatano ya Februari 19, 2025, Dk Willibrod Slaa anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kesi yake ambayo imekuwa na panda shuka nyingi tangu alivyokamatwa.
Dk Slaa ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alikamatwa Januari 10, 2025, kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X, na tangu hapo amekuwa akisota rumande, ambapo mpaka siku ya leo ametimiza siku 38 akiwa huko.
Hali hii imekuwa ikiwafanya wadau mbalimbali wa masuala ya haki jinai kuibuka na kupaza sauti zao wakitaka upande wa Jamhuri utende haki katika shauri hilo, hasa kwenye suala la kumpatia dhamana kwani kosa analokabiliwa nalo lina haki hiyo.
The Chanzo imekukusanyia matukio yote muhimu yaliyotokea tangu Dk Slaa alipokamatwa, ambapo unaweza kuyasoma matukio hayo kuanzia hapa;
Januari 10, 2025: Usiku wa kuamkia siku hiyo taarifa yenye sauti ya Dk Willibrod Slaa inaanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa anakamtwa na polisi na kupelekwa kituo cha polisi Mbweni. Asubuhi yake Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, anathibitisha taarifa hizo na kueleza kuwa wanamshikilia kwa ajili ya mahojiano naye kwenye baadhi ya mambo.
Januari 10, 2025: Dk Slaa afikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X, zamani ukifahamika kama Twitter,kupitia jukwaa lililofahamika kama Maria Sarungi Tsehai, kosa ambalo alilidaiwa kutendwa Januari 9, 2025. Baada ya shtaka kusomwa, Dk Slaa anarudishwa rumande baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa umewasilisha mahakamani kiapo cha kuzuia dhamana.
Januari 13, 2025: Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yashindwa kusikiliza kesi ya Dk Slaa baada ya kutofikishwa mahakamani hapo.
Januari 17, 2025: Dk Slaa aletwa mahakamani kusikiliza maombi mawili. Moja, ni kuhusu dhamana na la pili ni la kesi kufutwa kwa kuwa imewasilishwa bila uhalali. Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, akubaliana na jopo la mawakili wa upande wa mashtaka kwamba wasubiri uamuzi wa pingamizi la uhalali wa hati ya mashtaka, ndipo maombi ya kupinga dhamana yasikilizwe.
Uamuzi huu wawakasirisha mawakili wa upande wa utetezi, ambapo wakaeleza kwamba wanakwenda kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kesi hiyo Mahakama Kuu, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wake.
Januari 22, 2025: Mahakama Kuu yasimamisha uamuzi wa Mahakama wa Hakimu Mkazi Kisutu uliopangwa kutolewa Januari 23, 2025, pamoja na kesi yote kwa ujumla. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Dk Slaa kufungua kesi mahakamani hapo kupinga uamuzi wa kutopewa dhamana, huku akihoji uhalali wa hati ya mashtaka katika kesi ya msingi inayomkabili.
Januari 24, 2025: Mahakama Kuu yasikiliza kesi iliyofunguliwa na Dk Slaa kupitia mawakili wake, akipinga uhalali wa kesi ya msingi iliyofunguliwa na upande wa Jamhuri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokana na mawakili wake kufungua kesi ambayo upelelezi wake haujakamilika. Baada ya kusikiliza mahakama hiyo ikaiairisha hadi Januari 27, 2025, itakapoitwa kwa ajili ya kutoa maamuzi.
Januari 25, 2025: Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, akiambatana na viongozi wengine wa chama hicho wanamtembelea Dk Slaa katika gereza la Keko, jijini Dar es Salaam.
Januari 27, 2025: Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati uliofanyika Dar es Salaam, Januari 27 na 28, 2025, wakamisha Mahakama Kuu kutoa maamuzi ya kesi ya Dk Slaa.
Januari 30, 2025: Mahakama Kuu yarudisha shauri la Dk Slaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kutoa maelekezo kwamba mahakama hiyo inapaswa kulipa kipaumbele suala la dhamana.
Uamuzi huo umetolewa leo Januari 30, 2025, baada ya mawakili wake kufungua shauri katika Mahakama Kuu wakitaka mahakama hiyo ipitie mwenendo wa suala la dhamana ya kiongozi huyo mkongwe wa siasa mara baada ya upande wa Jamhuri kupinga kwamba asipewe dhamana.
Januari 31, 2025: Mawakili wa Serikali wanaiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba wanakusudia kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya Mahakama Kuu. Hivyo, wanamtaka Mheshimiwa Hakimu, asisome uamuzi aliopanga kusoma na asifanye jambo lolote lile kwa sababu hana mamlaka mpaka Mahakama ya Rufani itakaposikuliza rufaa yao. Kesi hiyo ikahairishwa kwa muda wa masaa mawili kabla ya kuendelea.
Akizungumza na vyombo vya habari nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakili wa Dk Slaa, Peter Madeleka, akasema kwa hatua ilipofikia, kwa sababu Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikieleza kuwa kipo tayari kwa maridhiano, basi mawakili wa Dk Slaa wanafikiria kutumia njia ya maridhiano ili kupata muafaka wa kesi inayomkabili kiongozi huyo mkongwe wa siasa za upinzani.
Baada ya masaa mawili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inarejea na kutoa maamuzi kuwa. inakubaliana na upande wa Jamhuri kuwa kama wanakusudia kukuta rufaa basi mahakama hiyo inakuwa imefungwa mikono. Kwa hiyo haiwezi kufanya jambo jingine lolote linalohusiana na kesi ya Dk Slaa, mpaka rufaa yao itakaposikilizwa.
Februari 6, 2025: Kesi ya Dk Slaa inasikilizwa tena kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na upande wa Jamhuri unaieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Februari 14, 2025: Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, akizungumza kwenye moja ya mkutano wa hadhara anahoji endapo Dk Slaa akipoteza maisha akiwa gerezani kutokana na uzee wake, Rais Samia Suluhu Hassan atamtoaje na atawaambia nini Watanzania kuhusu kifo hicho.