Zanzibar. Sleem Khamis ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Vitongoji iliyopo shehia ya Vitongoji, wilaya ya Chakechake, mkoa wa Kusini Pemba. Licha ya kuwa shule hiyo inachumba maalum cha wanafunzi kujifunzia kompyuta, Khamis, 14, hajawahi kabisa kupata fursa ya kujifunza kitu chochote kinachohusiana na kompyuta.
“Sijawahi kuingia kwenye chumba hicho na sijawahi hata kushika kompyuta, ila natamani kujifunza lakini ndiyo hivyo mimi sisikii.”
“Huwa naiona kompyuta kwa mjomba wangu, ila hata nyumbani sijafundishwa kwa hiyo sijui jinsi ya kutumia,” Khamis ambaye anapenda sana somo la Hisabati na ana ndoto za kuwa mwalimu wa somo hilo anasema kwa sauti kubwa wakati akizungumza na The Chanzo wakati tukiwa nyumbani kwao.
Anayopitia Khamis hayatofautiani na yale yanayomkumba Fatma Ali, 12, mwanafunzi wa darasa sita katika shule ya msingi Kiswaduni, iliyo wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi.
SOMA ZAIDI: Ubakaji Unavyowajaza Hofu Watoto wa Kike Mjini Magharibi, Z’bar: ‘Tunaogopa, Hatuko Salama’
Ukimtazama Fatma utagundua kuwa anatabasamu muda wote, lakini nyuma ya tabasamu hilo anakabiliwa na changamoto ya ulemavu wa kutokuona. Kutokana na hali hiyo, wakati wenzake wakijifunza teknolojia za kisasa kama kompyuta na programu za mawasiliano, Fatma huishia kusikia tu na mpaka sasa hakuna alichoambulia kwenye masuala hayo.
“Ninapenda shule, lakini teknolojia ambayo ingeweza kunisaidia haipo shuleni kwetu, sifahamu na sijui inafafanaje hiyo kompyuta mwalimu anayoisema,” anasema Fatma huku akiwa na tabasamu lake mwanana ambalo limetamalaki usoni mwake.
Fatma ambaye ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu nyumbani kwao, anatamani kuwa daktari wa watoto, lakini anafikiria kuwa anaweza asiyafikie malengo hayo kwani kwa kiasi kikubwa dunia inayokwenda kwa kasi kwenye mabadiliko ya teknolojia inaelekea kumwacha nyuma.
“Nasikia vizuri ila kuona ndiyo sioni. Sasa nitawezaje kujifunza kompyuta wakati shuleni hakuna kifaaa cha kueleza kompyuta ipoje? Kingine sijui kama mama ataweza kuninulia kifaa cha kutumia zaidi ili niweze kujifunza kuhusu kumpyuta,” Fatma anazungumza wakati akiwa amekaa kwenye sofa la sebuleni kwao maeneo ya Saataeni.
Nimekosa kazi
Wakati Khamis na Fatma wakiwaza ni kwa namna gani wataishi baada ya kumaliza shule huku wakiwa hawajui namna ya kutumia vifaa vya kiteknolojia kama kompyuta, tayari Aisha Soud Fakih, 19, mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi aliyehitimu masomo yake ya kidato cha nne mwaka 2022 anakumbana na changamoto hiyo.
Aisha amekosa fursa ya kuuza duka kwa sababu hajui kutumia kompyuta na simu janja, hali ambayo inamfanya awe mtu ambaye hana ajira.
“Pengine ningesoma shuleni haya mambo ningeweza hata kujiajiri kuandikia watu barua hapa kijijini,” amesema Aisha ambaye kwa sasa anatamani kufanya kazi kama mtu wa mapokezi, ila kwa sababu hana ujuzi huo muhimu basi ameshindwa kufanya hivyo.
“Serikali ingaalie suala hili kwa kuweka mkazo kwenye masomo hayo ya teknolojia kwa wanafunzi wote, na kusiwe na ubaguzi maana ndiyo maana inapelekea wengine sasa hatujui kitu kwa sababu hakukuwa na mazingira mazuri ya sisi kusoma,” amesema Aisha wakati akizungumza na The Chanzo nyumbani kwao kisiwani Pemba.
SOMA ZAIDI: Ukatili wa Wenza Kusambaza Picha na Video za Faragha Baada ya Kuachana Waliza Wanawake Zanzibar
Takwimu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar zinaonesha kuwa wanafunzi wenye ulemavu kwa shule za Serikali ni 8,858. Wanafunzi wa chekechea wakiwa 1,032, huku wa shule za msingi wakiwa 4,440 na sekondari ni 3,386.
Idadi hiyo inajumuisha ulemavu wa viungo, usikivu, ulemavu wa ngozi, uziwi na ulemavu wa kutokuzungumza, na wanafunzi wa kiume idadi yao ni kubwa kwa makundi ya chekechea wapo 622 katika ya 1,032, shule za msingi ni 2,343 kati ya 3,386 isipokuwa sekondari, ambapo wapo 1,121 katia ya wanafunzi 4,440.
Nadya Mohamed ni mwalimu wa shule ya msingi Kisiwandui iliyopo mkoa wa Mjini Magharibi. Nadya anawafundisha wanafunzi wasioona masomo ya Kisababti na Kiswahili.
Mwalimu huyu ambaye naye pia ni haoni ameiambia The Chanzo kuwa Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya uwepo wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu vitakavyowawezesha kujifunza masuala ya teknolojia.
“Inatakiwa tutumie hii teknolojia ya Obit Reader 20, ambacho ni kifaa kinachosaidia sisi kuandika kazi zetu na kupata urahisi wa kuwafundisha watoto kuhusiana na masomo ya kompyuta, lakini bado hatujaanza kuwafundisha.”
Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni kutokuwepo kwa vifaa hivyo, kwa hiyo tunaiomba Serikali iwezeshe upatikanaji wake, kwani haki ya kujifunza ni ya watoto wote,” Nadya anasema.
SOMA ZAIDI: Afrika Imejipanga Kukabiliana na Taathira za Teknolojia ya Akili Unde?
Jamila Bora Afya ni mwanaharakati na mtetezi wa masuala ya watu wenye ulemavu hususani watoto kutoka visiwani hapa. Jamila amesisitiza kuwa suala linalowakwamisha wanafunzi wenye ulemavu kujifunza masuala ya teknolojia ni ukosefu wa vifaa maalum.
Kwa mujibu wake hali hiyo imekuwa ikipelekea kundi hilo la watoto kuachwa nyuma kwenye eneo hilo na ndiyo maana wao kama wadau wamekuwa wakiipigia kelele Serikali ihakikishe kwamba inachukua hatua ili kulimaliza tatizo hilo.
“Mtoto anasoma shule mpaka anamaliza haijui hata hiyo kompyuta, na wakati mwengine hata akijifunza inakuwa ni kidogo tu na hakuna muendelezo wa mafunzo hayo,” Jamila anaiambia The Chanzo.
“Dunia kwa sasa inaendelea, kila kitu ni teknolojia, ikiwa watoto wenye ulemavu hawatapata elimu na ujuzi basi wataendelea kupata tabu kwenye soko la ajira.”
Juma Salim Ali ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Ali amekiri kuwa kuna changamoto kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza masuala ya teknolojia, na Serikali inalitambua hilo ndiyo maana imekuwa ikichukua hatua kulimaliza tatizo hilo.
“Watoto wenye mahitaji maalum wanatakiwa kupatiwa kila aina ya nyenzo katika kujifunza na kusaidiwa, na ndiyo maana Serikali imekuwa ikitoa msaada wa vifaa maalum vya kuwawezesha wanafunzi hao kusikia na kusomea, japo kuwa bado havitoshi.”
SOMA ZAIDI: Kutana na Kijana Aliyepania Kuleta Mapinduzi ya Kiteknolojia Tanzania
Ali akaongeza kuwa hata suala la walimu wenye taaluma ya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum ni changamoto ambayo wanaitambua, na wataifanyia kazi ili idadi yao iongezeke.
“Walimu ambao tulionao bado elimu zao kwenye suala la ujumuishwaji wa wanafunzi ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum tulio nao. Serikali ina mpango wa kuendelea kutoa mafunzo kazini kwenye upande wa elimu jumuishi ili waweze kuwasaidia zaidi kundi hilo la wanafunzi,” Ali anamalizia kusema.
Wasiachwe nyuma
Adil Mohamed Ali ni Mratibu wa Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), taasisi isiyo ya kiserikali inayolenga kuwasaidia watu wasioona. Ali amesema ulimwengu wa sasa ni wa teknolojia na ndipo tunapokwenda huko sasa ikiwa kunakosekana ushirikishwaji wa masuala ya teknoljia kwa watoto wenye ulemavu basi kutakuwa na athari za kimaendeleo kwa upande wao.
“Watoto wenye ulemavu wasiwachwe nyuma kwa sababu tu ya hali yao ya ulemavu waliyokuwa nayo na tunahitaji kuihimiza zaidi Serikali juu ya kuwezeshwa watoto hawa kwenye masuala hayo.”
“Katika mabadiliko ya sekta ya elimu kwenye ujenzi wa shule za maghorofa bado kuna changamoto wa ufikiwaji wa sehemu kama maabara na hata vyumba vya kompyuta kwa baadhi ya shule, suala ambalo pia linarudisha nyuma juhudi za ujumuishwaji wa wanafunzi wenye ulemavu,” Ali anasema.
Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com