The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Afrika Imejipanga Kukabiliana na Taathira za Teknolojia ya Akili Unde?

Afrika inapaswa kuandaa sera ya pamoja ya Akili Unde kulinda utu, ustawi, na maendeleo ya watu wake.

subscribe to our newsletter!

Tangu kipindi cha uhuru wa mataifa yake, Afrika imekuwa katika hali ya kujitafuta, hali ambayo imelifanya bara hilo linalokadiriwa kuwa na watu wapatao bilioni 1.4 kupokea kila kitu kinacholetwa mbele yake kwa imani kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya maendeleo. 

Kwa bahati mbaya, njia nyingi zilizoletwa zilizidi kuizamisha Afrika kwenye tope la umaskini, na hata kutishia kupokwa kwa uhuru wake tena. Kwa nini? Kwa sababu Afrika haikuwahi kujitafiti kwa dhati na kuamua kusimama na kujiendesha.

Kwa sasa, kama ilivyojitokeza huko nyuma, Afrika ipo kwenye utaratibu wake wa kupokea teknolojia na sera – kama zilivyo–kutoka mataifa yaliyoendelea duniani.

Teknolojia hii si tu itaamua maendeleo ya watu wa Afrika kwa vizazi vijavyo bali itaamua pia kama kutakuwepo kwa Waafrika wenyewe kwa miaka hiyo ijayo. Teknolojia hii ni ile iitwayo Artificial Intelligence, ambayo wataalamu wa lugha na teknolojia kutoka Afrika Mashariki wameitafsiri kama Akili Unde.

Teknolojia hii ilianza kutumika rasmi mwaka 1956 huko nchini Marekani chini ya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ambapo kompyuta zilianza kutengenezwa kunakili mfumo na utaratibu wa fikra za mwanadamu kwenye kutatua changamoto mbalimbali za kila siku zinazowakumba.

SOMA ZAIDI: Juhudi za Dhati Zinahitajika Kuifikia Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo

Mwezi Julai 2023, mkutano mkubwa ulifanyika jijini Geneva, Uswizi uliofahamika kama AI for Good Global Summit uliohusisha mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UN), viongozi wa Serikali mbalimbali, wataalamu wa teknolojia na makampuni ya uwekezaji kwenye teknolojia hiyo.

Mkutano huo ulilenga kupewa kibali cha uendeshaji rasmi wa shughuli za utengenezaji wa roboti mwenye kutumia teknolojia hiyo na kwa ushawishi wao. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alibariki teknolojia hiyo. 

Sera za pamoja

Tayari Umoja wa Ulaya (EU) umeanzisha sera ya Artificial Intelligence for Europe ambayo msingi wake ni kumlinda na kumfanya mwanadamu kuwa msingi wa mfumo wa uendeshaji wa Akili Unde na siyo teknolojia hiyo kumuendesha mwanadamu.

Sera hii ilitungwa kulinda wananchi wa EU dhidi ya makampuni makubwa ya kiteknolojia yaliyo na uwezo wa kuathiri mwenendo na maendeleo ya binadamu katika umoja huo unaokadiriwa kuwa na watu wapatao milioni 448.4.

Mnamo Julai 2017, China ilitambulisha mpango wake wa New Generation Artificial Intelligence Development Plan (AIDP), ulioweka shabaha ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, taifa hilo lenye watu bilioni 1.412 linaongoza kwenye teknolojia ya Akili Unde duniani. 

SOMA ZAIDI: Tanzania Inaenda Kumuuzia Nani Kahawa Ndani ya AfCFTA?

Mpango huo uliazimia kuwa teknolojia hiyo itakuwa silaha kuu ya ujenzi wa uchumi wa nchi hiyo kwenye kila nyanja, kuanzia uwekezaji viwandani, biashara, afya, ustawi wa jamii, na ulinzi na usalama.

Mpaka sasa, China inaoongoza kwa bajeti kubwa na tafiti nyingi za teknolojia hiyo. 

Tofauti na mataifa ya Ulaya, China imekuwa na sheria chache za kudhibiti matumizi ya teknolojia hiyo, jambo ambalo limekuwa likitazamwa kama hatari ya utekelezwaji kwenye nchi ambazo hazina mkazo wa kudhibiti wa matumizi ya teknolojia hiyo. 

Ikumbukwe kuwa matumizi ya teknolojia hiyo zaidi hutegemea ukusanyaji wa kile kinachojulikana kitaalamu kama Big Data, ambazo ni taarifa zinazohusu tabia, mwenendo na fikra za kila siku za binadamu, jambo ambalo Serikali ya China imekuwa inalifanya kwa kipindi kirefu.

Hapa barani Afrika, nchi ya Afrika ya Kusini inatajwa kama kiongozi wa uwekezaji wa teknolojia hiyo kwa kuwa na zaidi ya makampuni 726 ikifuatiwa na Nigeria yenye makampuni 456. 

SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika

Kwa Afrika Mashariki, Kenya inaongoza, ikiwa na makampuni 204, huku Tanzania na Uganda zikiwa na idadi sawa ya kampuni, ambazo ni 44.

Hatari haijaonekana

Mtazamo wa utendaji kazi na faida na athari ya teknolojia hii barani Afrika bado haujaanza kuonekana, hasa ikizingatiwa kuwa bado haijaanza kutekelezwa kwenye maeneo yanayoathiri ajira na ustawi wa jamii moja kwa moja, tofauti na mataifa yenye uchumi wa juu duniani.

Kwa mfano, hivi karibuni nchini Marekani kumeripotiwa maandamano yaliyohusisha waigizaji, waandishi, pamoja na waongoza filamu yaliyochochewa na makampuni ya filamu kutangaza kuanza kutumia Akili Unde katika tasnia hiyo, jambo lilioonekana kuhatarisha ajira na ustawi wa watu.

Hoja kubwa ya makampuni hayo ilikuwa ni kupunguza gharama za uzalishaji kwa kupunguza idadi ya waajiriwa kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na teknolojia hiyo, pia usahihi wa maamuzi pasipo upendeleo, au kasoro, na urahisishaji wa utendaji kazi.

Barani Afrika, teknolojia hii imeingia kama msaidizi na siyo mbadala, hasa ukizingatia utendaji wake katika shughuli tofauti kama huko nchini Kenya ambapo teknolojia ya Chatbots imekuwa ikitumika kama njia ya kupata ushauri wa afya pasipo kumuona daktari.

SOMA ZAIDI: GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?

Pia, nchini Nigeria, teknolojia ya Zenvus imekuwa ikihusika na kutoa ushauri katika kilimo, huku nchini Afrika ya Kusini, Mama Money na Mukuru zimekuwa zikihusika kwenye maelekezo ya utumaji wa miamala ya fedha.

Ni nchi tano tu barani Afrika – Mauritius, Misri, Afrika ya Kusini, Tunisia na Morocco– ndiyo zimeonekana kuwa tayari kwenye uandaaji, uendeshaji, na mapokeo ya teknolojia ya Akili Bandia. 

Maandalizi haya yanatarajiwa kupunguza athari na kuweka mazingira wezeshi ya kuifanya teknolojia hii kutoathiri uchumi na ustawi wa watu wa Afrika. 

Mazingira hayo ni pamoja na kuwa na mpango wa taifa wa uendeshaji wa teknolojia ya Akili Unde, mifumo ya ulinzi wa taarifa na sheria za faragha, sheria za kutoathiri uhuru na ustawi wa jamii, pamoja na mifumo ya kupambana na wizi wa mtandao.

Kama ilivyo kwa mataifa ya Ulaya na Marekani yalivyoandaa sera ya pamoja ya kulinda utu, ustawi na maendeleo ya watu wao kwa pamoja, ni vyema pia kwa Afrika kufanya hivyo kwani kuacha mataifa yake binafsi yajitegemee kwenye kuendesha, kulinda, na kupambana na teknolojia hii itakuwa sawa na kujidanganya!

Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *