The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kwa Kuifokea Yanga, Karia Ameonesha Upande Kwenye Sakata Kati ya Klabu Hiyo na Simba

Tulitegemea kiongozi wa juu wa kariba yake, atulie wakati huu mgogoro haujaisha ili juhudi za kuumaliza zifanyike na mambo hayo ya kuahirisha mechi hivyo yafikishwe mwisho.

subscribe to our newsletter!

Kwa kawaida, kama taasisi ina vyombo vya haki, viongozi hujiepusha kuzungumzia masuala ambayo yanashughulikiwa na vyombo hivyo ili kuepuka kutoa maneno yanayoweza kuchukuliwa kuwa ni maagizo.

Kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lina kamati ambazo zinafanya kazi kwa niaba ya Kamati ya Utendaji, basi ni mwiko kwa rais wa shirikisho kuzungumzia kitu chochote ambacho kiko mezani mwa moja ya kamati hizo hadi hapo uamuzi utakapotolewa ndipo anaweza kuuzungumzia na hasa kama shauri limeshafika mwisho.

Lakini hii imekuwa tofauti kwa rais wa TFF, Wallace Karia, ambaye wakati sakata la Yanga na Simba linatokea alikuwa nje ya nchi kuhudhuria mkutano wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Simba walitangaza kugomea mechi yao dhidi ya Yanga wakidai kuwa walizuiwa kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufanya mazoezi ya mwisho kama kanuni zinavyotaka kwamba timu itakayokuwa mgeni ipewe nafasi ya kutumia uwanja kwa muda ambao mechi itachezwa siku inayofuata.

Yamezungumzwa mengi kuhusu kilichotokea siku hiyo usiku lakini baadaye Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ambayo kimsingi ni Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kutokana na viongozi wake wakuu kuwa ndio viongozi wa kamati hiyo, ikatoa tamko la kusisitiza kuwa mechi itachezwa kama ilivyopangwa.

SOMA ZAIDI: Ni Kupoteza Muda Kujadili Kanuni Sakata la Simba, Yanga

Lakini saa chache baadaye, kamati ikaitishwa tena na kutangaza kuahirisha mechi, uamuzi ambao Yanga iliupinga na kuahidi kutocheza mechi itakayopangwa upya, ikidai kanuni hazikufuatwa katika kuahirisha mechi.

Ukiangalia sana, utaona chanzo cha mgogoro mpya wa timu moja kusema haitacheza, na nyingine kusema haitacheza, utabaini kuwa ni Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kutokana na kuyumbishwa na tishio la Simba hadi kufikia kuahirisha mechi kwa sababu iliyoitwa ya dharura, ambayo kwa utamaduni wa mpira haipo.

Kwa kuwa kamati hiyo ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuvuruga mchezo huo, ni lazima shirikisho zima liwe katika harakati za kutafuta ufumbuzi ambao unaweza kukubalika na pande zote mbili.

Ungetegemea kiongozi wa juu kabisa wa shirikisho asitoe kauli yoyote wakati huu kwa hoja kwamba suala hilo bado linashughulikiwa, hasa baada ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi kusema kuwa kuna mambo ambayo bado inayachunguza.

Hata kabla ya kamati kutoa ripoti ya mambo hayo, tayari Rais Karia ameshaifokea Yanga kwa kusema hoja yao kwamba viongozi wawili wa TPLB, yaani mwenyekiti Stephen Mghuto na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Almasi Kasongo, wawajibike, haikubaliki.

SOMA ZAIDI: CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?

Haikubaliki kwa ripoti ipi iliyotoka hadi sasa inayoonyesha kuwa hawakuwa na makosa? Karia amesimamia wapi hadi anaona hakuna tatizo kwa viongozi hao? Ametumia hoja ipi? Au kwamba viongozi na watendaji wa shirikisho la taasisi zake hawawezi kuadhibiwa kwa kuwajibishwa?

Ndivyo Karia anavyotaka kuwaambia wadau wa soka maana hajatuambia kuwa hawawezi kuwajibishwa kwa sababu gani. Tulitegemea kiongozi wa juu wa kariba yake, atulie wakati huu mgogoro haujaisha ili juhudi za kuumaliza zifanyike na mambo hayo ya kuahirisha mechi hivyo yafikishwe mwisho.

Mwaka juzi kipindi kama hiki ndicho kamati hiyo ilitangaza kubadili muda wa mechi baina ya timu hizo na kusababisha taharuki kubwa, baada ya Yanga kushikilia kanuni kwamba uahirishaji wa mechi haukufuata kanuni inayotaka uamuzi huo ufanyike kabla ya saa 24.

Ilikuwa ni aibu na fedheha siku hiyo maana mashabiki, ambao huanza pilikapilika za kwenda uwanjani kuanzia alfajiri, walijazana uwanjani kwa kuwa uamuzi wa kubadili muda ulifanywa saa chache kabla ya mechi kuanza.

Hakuna aliyewajibishwa hadi sasa kwa kusababisha taharuki hiyo na fedheha kwa nchi, usumbufu na hasara kwa mashabiki na wadhamini.

SOMA ZAIDI: Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti

Leo kunatokea tatizo kama hilo, bado rais wa shirikisho haonyeshi kukerwa na badala yake analaumu walioathirika na uamuzi wa kuahirisha mechi?

Hata tishio la Yanga, rais alitakiwa atumie busara kulizungumzia kwa kuwa limetokana na watendaji wa TFF kuvurunda. Kusema kwamba kama “hawataki waende kucheza sinema” ni matusi kwa klabu ya Yanga na mashabiki wake.

Usingetegemea kiongozi wa juu wa TFF kutoa maneno ya kejeli na kashfa kwa moja ya taasisi zilizo chini yake.

Kama wana Yanga wataona Karia ameshasimamia upande mmoja kutokana na kauli hizo, atawalaumu? Kama Wana-Yanga wataongeza nguvu katika madai yao na kusema hata Karia hawana imani naye, atawalaumu?

Ni muhimu kwa viongozi kuficha hisia zao hata kama kumetokea jambo lililowakera kuhofia kutoa maneno yatakayotafsiriwa kuwa ni maelekezo.

SOMA ZAIDI: Uwakilishi wa Wazanzibari Unahitajika Uongozi wa Michezo Kitaifa

Baada ya kauli yake, inawekanaje Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ukatoka na uamuzi ambao unatofautiana na kauli hizo za Karia, hata kama ndio utakuwa sahihi?

Wakati mwingine, hata kukaa kimya wakati jambo kubwa limetokea ni busara pia. Kila jambo lina wakati wake wa kulizungjmzia.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

One Response

  1. Moja ya matatizo yaliyochangia mpira wetu kudumaa ni watu kama Osiah kuwahi kutumikia TFF kama mtendaji mkuu. Si tu uwezo mdogo, ila siku zote anaendeshwa na mahaba na mtu anayehusudu kubishana hata pasipo na sababu ya mabishano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×