Leo Jumamosi ya Aprili 12, 2025, Tume ya Uchaguzi pamoja na vyama vya siasa vinategemewa kusaini maadili ya uchaguzi, ambapo Mkurugenzi wa UchaguziRamadhani kailima akiongea na kituo cha UTV, jana Aprili 11, 2025, ameeleza kuwa chama kisichosaini hakitashiriki uchaguzi.
“Chama cha siasa kisiposaini maadili ya uchaguzi kesho [Aprili 12] kwa mujibu wa kifungu namba 162 kifungu kidogo cha pili cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hakitapata fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu. Kwa sababu kifungu hicho kinasema maadili hayo yanapaswa kusainiwa na kuzingatiwa na kutiiwa na cha chama cha siasa mgombea tume na serikali,” alieleza Kailima.
Aliendelea kufafanua: “Sasa kama chama cha siasa hakijasaini maadili hayo kesho hakitapata fursa ya kusimamisha mgombea kwa sababu hata mgombea wa chama chochote cha siasa anayetaka kugombea nafasi ya kiti cha Rais, Mbunge na Diwani wakati wa kuwasilisha fomu zake za uteuzi atapaswa ajaze fomu namba kumi ya kukiri kuyazingatia maadili hayo ya uchaguzi, hatopata fomu namba kumi kwa sababu chama chake cha siasa kitakuwa hakijasaini maadili hayo ya uchaguzi.”
“Kwa hiyo chama kama hakikusaini maadili hayo ya uchaguzi hayo kesho, basi kitapata haki yake ya kutokusimamisha wagombea. Kwa sababu kusimamisha wagombea ni haki pia, sio lazima,” Kailima alisisitiza zaidi.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika ameeleza umma kuwa chama hicho hakitakuwepo Dodoma kusaini maadili hayo ya uchaguzi.
“Katibu Mkuu sitakuwepo kwenye kikao cha tarehe 12 Aprili 2025 cha kushauriana na kusaini maadili ya uchaguzi ya 2025. Ifahamike kuwa mwenye mamlaka ya kusaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya chama cha siasa ni Katibu Mkuu. Katibu Mkuu sijateua kiongozi au afisa yoyote kwenda kushiriki kwa niaba yangu katika kikao hicho kitakachofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alifafanua Mnyika kupitia ukurasa wake wa X.
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 inataka Kanuni za Maadili ya Uchaguzi kuchapishwa baada ya mashauriano na vyama vyote vya siasa. Kifungu 162 cha sheria hiyo inaeleza:
“Kwa madhumuni ya kusimamia uchaguzi wa haki, huru na amani, na baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, Tume itaandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake. (2) Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitasainiwa na- (a) kila chama cha siasa; (b) kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi; (c) Serikali; na (d) Tume, na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini. (3) Mtu ambaye atakiuka masharti ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni hizo.”
CHADEMA imeendelea kusisitiza kuwa haitashiriki uchaguzi kama hakutakuwa mabadiliko katika uendeshaji wa uchaguzi huku ikitaja vitendo vya mauaji yaliyotokea kwa wagombea wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ukatwaji wa wagobea, pamoja na malalamiko mengine ikiwemo matumizi ya nguvu wakati wa uchaguzi.
Kailima alipoulizwa kuhusu hoja ya mabadiliko alieleza kuwa tume haihusiki na utungaji wa sheria, bali wenye malalamiko waelekeze katika mamlaka sahihi.