Dar es Salaam. Msimu wa tatu wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu umehitimishwa jijini hapa hapo Aprili 13, 2025, uliofanyika kuendana na siku ya kuzaliwa ya Rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa hilo la Afrika Mashariki, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwenye mjadala uliotangulia hafla ya utoaji wa tuzo hizo kwa washindi wa mwaka huu, iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini hapa, wadau wa Kiswahili na uandishi bunifu nchini walijadili umuhimu na haja ya kubuni mbinu anuwai na madhubuti zitakazosaidia kuikuza lugha hiyo na fasihi yake ulimwenguni.
Moja kati ya mbinu zinazopendekezwa ni kuangalia namna mapinduzi yanayoendelea kutokea ya kiteknolojia yanaweza kutoa mchango wa aina gani kufanikisha lengo hilo, katika nyakati ambapo mataifa mbalimbali ulimwenguni yanawekeza nguvu kubwa katika kukuza lugha na tamaduni zao kwengineko duniani.
Ukiongozwa na Profesa Ibrahim Noor Sharif, gwiji la ushairi wa Kiswahili, ambaye pia ni mhadhiri, mwandishi wa vitabu na mchoraji kutoka Chuo Kikuu cha Sultan Quaboos cha nchini Oman, mjadala huo pia ulihudhuriwa na waandishi bunifu wa vitabu mbalimbali katika nyanja ya hadithi za watoto, riwaya, tamthiliya na ushairi, pamoja na wapenzi na wasomaji wa kazi hizo za fasihi.
Profesa Sharif, aliyezaliwa Zanzibar hapo Oktoba 6, 1947, alidokeza kwamba teknolojia imepanua wigo wa waandishi wa kazi bunifu kutangaza kazi zao na kushirikiana na watungi wenzao – gwiji hilo lilisahihisha kwamba neno sahihi ni “mtungi” au “mtungaji,” na siyo “mtunzi,” akisema mtunzi ni yule aliyepo jumba la makumbusho, anayetunza vitu –, uwezekano ambao haukuwepo miaka michache tu nyuma.
SOMA ZAIDI: Furaha, Hamasa Zatawala Msimu wa Pili wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu
“[Zamani], mshairi mmoja yuko Dar es Salaam, mwingine yuko Kilimanjaro, au Arusha, ilikuwa hakuna ule uhusiano wa pamoja wa kuchokozana, na nini,” Sharif, ambaye kazi zake ni pamoja na Umbuji wa Kiwandeo, alisema kwenye mjadala huo. “Lakini leo, mitandao [ya kijamii] inarahisisha [kazi hiyo].”
Mbali na kuunganisha watungaji wa Kiswahili na wenzao ulimwenguni, teknolojia pia imetajwa kuwa na uwezo wa kuongeza ushawishi wa fasihi ya Kiswahili duniani, na hivyo kuongeza ukubalikaji wake miongoni mwa watu wa mataifa mbalimbali.
Wadau wengi wanaamini kwamba kama itatumiwa vizuri, teknolojia inatoa fursa ya kuwajengea watu imani kwamba inawezekana kutumia Kiswahili kwenye juhudi zao za kusaka maarifa.
Akili Unde
Moja kati ya teknolojia iliyoibuka kwenye mjadala huo ni Akili Unde, au Artificial Intelligence (AI), kwa kimombo, ambayo, licha ya kuwajaza hofu baadhi ya watungaji kutokana na “tishio” lake la kuwaondoa, baadhi wanaamini inaweza kuwa na msaada kwenye namna watungaji wa Kiswahili wanaweza kuitumia kwenye kuboresha uzalishaji wa kazi zao za fasihi na kuzitangaza.
Akichangia kwenye mada hiyo, Fadhy Mtanga, mwandishi na mshairi wa zama za sasa, alibainisha kwamba kigezo kimoja kinachoweza kuifanya kazi ya fasihi ikubalike kwa watu ni uwezo wake wa kuwa na “mashiko” na isiyo na “ukomo wa wakati,” vitu ambavyo vinamlazimisha mwandishi atafute maarifa kutoka maeneo mbalimbali.
SOMA ZAIDI: Washindi Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Watangazwa Dar
“Kwa hivyo sasa, Akili Mnemba inayo nafasi kubwa ya kumsaidia mwandishi, badala ya kutumia muda mrefu kuchakata taarifa ghafi, akazipata zikiwa tayari zimechakatwa,” alidokeza mwandishi huyo wa Huba.
“Uandishi pia ni pamoja na uwezo wa kumudu misamiati, na mbinu nyingine, ikiwemo tamathali za semi, uwezo ambao Akili Mnemba ina fursa ya kumjengea mwandishi,” aliongeza Mtanga.
Tuzo
Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ya kwanza ya aina yake nchini, ilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali kuchochea adhma hii ya kukuza fasihi ya Kiswahili, siyo tu nchini Tanzania, bali duniani kote.
Ikizinduliwa rasmi mwaka 2022, Tuzo hiyo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 2023, mwaka huu ikiwa ni msimu wake wa tatu tangu kuanza kutolewa kwake kwa waandishi bunifu wa Tanzania.
Ikilenga tanzu za riwaya, ushairi na hadithi za watoto, Tuzo hiyo huambatana na fedha taslimu za Shilingi milioni 10 anazopewa mshindi wa kwanza, pamoja na Serikali kufadhili gharama za uchapishaji na usambazaji wa muswada ulioshinda tuzo hizo.
SOMA ZAIDI: Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu: Tumaini Jipya Kwa Waandishi Tanzania?
Mbali na waandishi, Tuzo pia inalenga kuunga mkono wachapishaji nchini, pamoja na kukuza utamaduni wa kujisomea miongoni mwa wananchi.
Washindi wa kwanza kwa mwaka huu ni Maundu Mwingizi (Riwaya); Hussein Kondo Abdallah (Ushairi); Tyatawelu Emmanuel Kingu (Tamthiliya); na Tune Shaban Salim (Hadithi za Watoto). Wote wamepata Shilingi milioni 10, kila mmoja, ngao, cheti, pamoja na miswada yao kuchapishwa kwa kwa gharama ya Serikali na kusambazwa katika shule mbalimbali pamoja na kwenye maktaba za taifa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hizo kwa washindi hao, mgeni rasmi wa shughuli hiyo, aliyekuwa akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliahidi Serikali kuendelea kutoa tuzo hizo ili ziweze kufanikisha malengo yake.
“Maandiko bunifu yenye tija ni yale yanayoisawiri jamii katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za kijamii, za kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia,” alisema Mbunge huyo wa Mkuranga (Chama cha Mapinduzi – CCM).
“Mwandishi aitumiaye kalamu yake kikamilifu kuchora masuala mazito yanayogusa maisha ya watu, huyo ndiyo mwandishi stadi na rafiki wa jamii,” aliongeza. “Aidha, kazi bunifu inayoangazia masuala mtambuka ni muhimu kwa ajili ya kuifunda na kuijuza jamii yetu kwa yale yanayojiri. Ninatoa rai kwa waandishi bunifu kuendelea kulifaa taifa letu kwa kalamu zenu.”