The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi: Jitihada Inayolenga Kuondoa Unyanyapaa Dhidi ya Watoto Wenye Kigugumizi Tanzania 

Kwa kuwajengea watoto wanaogugumiza kujiamini na uvumilivu, kambi hii huwafundisha kuwa na mawasiliano bora na kuchechemua katika jamii inayowazunguka.

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi, watoto wenye kigugumizi, pamoja na familia zao, huambiwa kwamba lazima wakishinde, au kupunguza, kigugumizi chao ili kufanikisha ndoto zao. Wazo hilo, hata hivyo, si sahihi, na linawadhuru, na ndilo hasa Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi, au Camp Dream. Speak. Live kwa kimombo, inajaribu kulibadilisha. 

Kwa kuwajengea watoto wanaogugumiza kujiamini na uvumilivu, kambi hii huwafundisha kuwa na mawasiliano bora na kuchechemua katika jamii inayowazunguka.

Kwa mara ya kwanza Afrika, kambi hii ilifanyika Zanzibar mwaka jana, 2024, katika Kituo cha Makuzi na Maendeleo ya Watoto, ikiratibiwa na mimi na wenzangu kupitia Chama cha Mitindo Maalum ya Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA), taasisi niliyoianzisha kusaidia mapambano dhidi ya unyanyapaa wa watu wenye kigugumizi Tanzania.

Programu ya mwaka jana imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kihisia na kisaikolojia kwa watoto 12 walioshiriki, kutoka hali ya uoga hadi kuwa na ujasiri na kujieleza waziwazi.

Mwaka huu, CHAMMUTA kimepanga kuendesha Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi jijini Dar es Salaam katika wiki ya Juni 23 – 27, 2025. 

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Watu Wenye Kigugumizi Wangependa Uongee Nao

Camp Dream. Speak. Live ilianzishwa na Dk Courtney Byrd katika Kituo cha Arthur M. Blank cha Elimu na Utafiti kuhusu Kigugumizi katika Chuo Kikuu cha Texas, huko Austin, Marekani, kupitia msaada mkubwa wa kifadhili mnamo 2014. Kambi hii ina orodha ndefu ya wanaosubiri, huku watoto na familia zao wakitoka kote nchini kushiriki —bila gharama yoyote.

Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi. ni programu ya kipekee inayolenga kusaidia watoto wenye kigugumizi kuanzia umri wa miaka mine hadi 17. Kambi hii huwasaidia watoto kujifunza kujikubali, kujiamini, na kuwasiliana kwa ufanisi bila kujaribu kuficha au kuondoa kigugumizi chao. 

Badala ya kuwalazimisha kuacha kugugumiza, kambi hii huwahimiza kuwa wao wenyewe na kutumia mawasiliano ya kweli na ya wazi.

Licha ya kuwepo na michezo mbalimbali, lengo kuu la kambi ni kuendeleza mbinu za mawasiliano kwa watoto na kuwapa ujasiri wa kuzungumza bila hofu. Watoto hujifunza jinsi ya kujieleza kuhusu kigugumizi chao na kutetea haki zao za kusikilizwa kwa nafasi stahiki.

Mojawapo ya vipengele muhimu vya kambi ni kuwafundisha watoto kuelewa kuwa kigugumizi si kasoro, bali ni sehemu ya maisha yao. Wanahimizwa kutokubali shinikizo la kuzungumza “kama roboti” kama baadhi ya wataalamu wanavyopendekeza. 

Badala yake, wanapaswa kuzungumza kihalisi. Wanafunzi wa shahada ya kwanza katika sayansi ya mawasiliano wanatarajiwa kushiriki katika kambi na kupata uzoefu wa kiutendaji kwa kushirikiana moja kwa moja na watoto.

Programu hii pia inawashirikisha wazazi na familia. Siku ya mwisho katika programu, watoto huonyesha vipaji vyao na kuwaelimisha wazazi kuhusu kile walichojifunza.

Kwa ujumla, Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi ni harakati ya kijamii ya kuondoa unyanyapaa kuhusu kigugumizi na kujenga kizazi kipya cha watoto jasiri, wanaojielewa na kujiamini.

Wazazi na walezi ambao wangependa watoto wao wenye kigugumizi washiriki katika Kambi ya Ota. Zungumza. Ishi wanakaribishwa kujaza fomu ya usajili inayopatikana hapa kabla ya Aprili 23, 2025.

Ally Baharoon Ni  mwanzilishi wa Chama cha Mitindo Maalum ya Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA). Kwa mrejesho, anapatikana kupitia allybaharoon@gmail.com au X kama @venturally. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×