Kila kizazi kina changamoto zake. Wazazi wa jana walikuwa na vikwazo vyao, nasi wa leo tunavyo vyetu. Lakini swali linabaki: Je, kuwa mzazi katika ulimwengu wa leo ni kazi ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa zamani?
Miaka ya nyuma, mtoto hakuwa wa mzazi mmoja tu, alikuwa wa kijiji kizima. Majirani walikuwa ni sehemu ya familia. Bibi, babu, shangazi, mjomba, hata mama mwenye duka wa mtaa wa pili, wote walihusika katika kumkuza mtoto.
Kulikuwepo na mfumo usio rasmi wa msaada; mzazi hakuhitaji kujua kila kitu kwa sababu jamii ilimsaidia kulea. “Mtoto ni wa jamii” ndiyo imani iliyokuwa imejengeka katika jamii. Lakini je, jamii hiyo bado ipo kwa sura ile ile?
Leo, mazingira ya maisha yamebadilika sana. Wazazi wengi wanaishi mijini, mbali na familia zao za asili. Wengine wamehamia maeneo mapya kwa ajili ya kazi au masomo, na hawana ushirikiano na umoja wa kijamii wa kuaminika. Majirani hawajuani. Na katika miji mikubwa, hata kuomba jirani akusaidie kumchunga mtoto kwa dakika kumi ni kazi.
Wakati huohuo, watoto wetu wamezaliwa katika dunia yenye taarifa nyingi kuliko uwezo wao wa kuzichakata. Wana simu mikononi, televisheni chumbani, na marafiki wa mtandaoni wanaowapa ushauri ambao mara nyingine hauendani kabisa na maadili ya familia.
SOMA ZAIDI: Wazazi Waliopo Kimwili Lakini Wasiopatikana Kihisia Hukuza Watoto Wasiojali Thamani ya Upendo
Ukweli ni kwamba, “Hatuwezi tena kuwalea watoto wetu kwa namna tulivyolelewa na wazazi wetu kwa maana wazazi wetu walitukuza kwa ajili ya dunia tofauti na ya sasa.”
Wengi wetu tulilelewa kwa adhabu kali, maneno makali, na hofu kama njia ya nidhamu. Lakini sasa tunajifunza kuwa malezi yenye kuzingatia utu, mazungumzo, na usikivu yanazaa matunda bora zaidi. Na hiyo si kazi ndogo, ni kujifunza upya na kubadili njia tulizojifunzia wenyewe.
Mfano halisi: Baba mmoja mwenye mtoto wa miaka 14 aligundua kuwa kijana wake hana hamasa shuleni. Badala ya kumtishia, au kumpiga, alianza kwa upole: “Umechoka au kuna kitu kinachokusumbua?”
Katika mazungumzo haya, alijifunza, kwa mara ya kwanza, kuhusu afya ya akili ya kijana wake na mzizi wa tatizo lake. Ni ushuhuda wa wazi kwamba sauti ya mtoto haipaswi kukandamizwa bali kusikilizwa.
Changamoto zinazotukumba wazazi wa sasa ni pamoja na kuelimisha watoto kuhusu usalama wa mtandaoni, hasa ukatili wa kingono mtandaoni na ushawishi wa watu wasiojulikana juu ya tabia kadha wa kadha hatarishi.
SOMA ZAIDI: Wazazi na Walezi, Uelewa Juu ya Mahusiano Yenye Afya ni Muhimu kwa Watoto Wetu
Pia, kupata muda wa kuwa na watoto huku tukipambana na majukumu ya kazi na maisha, pamoja na kujifunza teknolojia na ulimwengu wao wa kidijitali bila kuwahukumu, au kuogopa, mabadiliko yatokanayo na teknolojia
Ingawa hatuna tena kijiji cha kihalisia, bado tuna nafasi ya kujenga kijiji kipya cha kusaidiana kinachoendana na muktadha wa mazingira yetu ya sasa. Hii inaweza kuwa: vikundi vya wazazi kwenye WhatsApp, jumuiya za wazazi shuleni, marafiki wanaoshirikiana na kusaidiana, au hata mahusiano ya karibu na majirani wa karibu.
Katika miji mikubwa, mahusiano haya hayaji kwa urahisi, lakini yanahitaji kujengwa kwa makusudi. Maana mzazi anayebeba kila kitu peke yake, huchoka haraka kimwili, kihisia, na kiakili na hali hii huathiri hata uhusiano wake na mtoto na huweka maisha ya mtoto hatarini. Inahitaji kijiji kumlea mtoto, lakini katika zama hizi inahitaji dhamira ya kweli kukijenga kijiji upya.
Hakuna kizazi kilicholea bila changamoto. Lakini tofauti ya sasa ni kwamba dunia inabadilika kwa kasi ya ajabu na imegeuka kuwa kijiji. Na mzazi asiye tayari kubadilika, hujikuta akipotea katika wimbi la mabadiliko hayo.
Ni muhimu tukumbuke kwamba si lazima tuwe wakamilifu, kukosea ni sehemu ya safari, upendo, uelewa, na usikivu na uvumilivu bado ni silaha kuu za mzazi.
SOMA ZAIDI: Ubongo wa Mwanamke Hupungua Ukubwa Kipindi cha Ujauzito. Hii ni Habari Njema, Siyo Mbaya
Kama kuna jambo moja tunaweza kurithi kutoka kwa vizazi vilivyopita, ni hili: Upendo wa kweli na nia njema ya mzazi vinaweza kubadili kabisa maisha ya mtoto bila kujali tamaduni na mazingira.
Na kwa kila hatua tunayochukua leo, tunatengeneza kesho yenye msingi bora zaidi kwa watoto wetu.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.