Agosti 12, 2008, Rais wa Ufaransa wa wakati huo, Nicolas Sarkozy, hakuamini masikio yake kwa alichokuwa anakisikia kutoka kwa mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Urusi wa wakati huo, Vladimir Putin.
“Yule [Mikheil] Saakashvili,” Putin anadaiwa kusema, akimzungumzia kiongozi huyo wa Georgia kwa wakati huo. “Nitamnyonga.” Sarkozy, akipigwa na butwaa, akamuuliza kwa mshangao, “utamnyonga!” “Ndio,” Putin alijibu, na kuongeza: “Mbona Wamarekani walimnyonga Saddam Hussein.”
Hayo yalikua mazungumzo kati ya viongozi hao wawili kwenye kikao cha usuluhishi baada ya Urusi kuivamia nchi ya Georgia, mwaka 2008, na kuzuka kwa vita baina ya nchi hizo mbili ambapo Urusi iliwazidi nguvu kirahisi Georgia.
Mapema mwaka 2008, aliyekuwa Rais wa Marekani, George Bush Jr, alitangaza kampeni ya kuweka mpango wa kuzisaidia nchi za Georgia na Ukraine kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO. Kauli hiyo ilishutumiwa vikali na Urusi, kwa kile walichodai, kukaribiwa na NATO kwenye mipaka yake ni tishio la kiusalama wa nchi yao.
Hivyo, Urusi ikaanza maandalizi na hatimaye kuivamia Georgia, na miaka 14 baadae, yaani mwaka 2022, Urusi wakaivamia Ukraine, kwa kile kile walichodai kulinda usalama wa nchi yao.
SOMA ZAIDI: Undani Kuhusu Mtanzania Aliyefariki Nchini Ukraine. Familia Yazungumza
Urusi ni taifa kongwe, kubwa na lenye hadhi ya kuwa superpower, kwa kimombo. Unaweza kushangaa kwa nini wanajihami hivi.
Hata hivyo, ukirudi kwenye historia, Urusi ina uzoefu wa kuvamiwa na mataifa mengine toka kuanzia karne ya 13, ambapo Himaya wa Mongolia ilipowavamia, na baadae kwenye historia kuvamiwa na mataifa mengine kama vile Uswidi, Poland, Ufaransa chini ya Napoleon na baadae mara mbili na Ujerumani.
Hivyo, kutilia mashaka kwao na majirani zao ni wasiwasi wenye uhalisia nyuma yake, haswa wanapoona mahasimu wao wakubwa kutoka kile kinachoitwa Magharibi, yaani Marekani na washirika wake, kwa kutumia kivuli cha NATO, wakiongeza wanachama ambao ni majirani wa Urusi. Na hakuna jirani anamnyima Urusi usingizi kuliko Ukraine.
Jiografia ya Ukraine
Jiografia inamuhukumu zaidi Ukraine kuliko majirani wengine kwa sababu kuu mbili. Sababu ya kwanza ni kwamba Urusi ni nchi iliyozungukwa na milima, misitu minene na barafu kali maeneo ya kaskazini kwake, hivyo kutengeneza ugumu wa kuivamia kupitia maeneo hayo, isipokua ni rahisi kuivamia kupitia Ukraine, ambapo ardhi yake kwenda Urusi ni ya tambarare inayotoa urahisi kwa adui yoyote anayetaka kuivamia Urusi.
Sababu ya pili ni kwamba Urusi ina changamoto ya bandari zake kubwa kuwa kwenye eneo lenye barafu nyingi, kupelekea bandari yake kubwa kwenye bahari ya Pasifiki, iitwayo Vladivostok, kuganda kwa miezi minne kila mwaka na kushindwa kupitika.
SOMA ZAIDI: Nini Maana ya Ukimya wa Afrika Kwenye Mgogoro wa Urusi na Ukraine?
Hili inaifanya Urusi kupata changamoto wanapopata tishio la kuvamiwa kwa Jeshi lake la maji kushindwa kutumia bandari hizo, lakini pia ugumu wa kuweza kutumia bandari hizo kibiashara.
Kwa bahati mbaya tena kwa Ukraine, Urusi iliona eneo la Ukraine la Crimea lina bandari ambayo haigandi na mwaka 2014, Urusi ilivamia Ukraine na kulimega eneo hilo wanaloliona la kimkakati kwa Jeshi lao la maji na usalama wao.
Kumekuwepo na lawama zikielekezwa kwenda kwa viongozi wa Ukraine, kwamba ukaribu wao na nchi za Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Marekani, ndio umechochea kwa kiasi kikubwa kuifanya Urusi iamini pengine iko hatarini.
Japo, baada ya Ukraine kupata Uhuru mwaka 1991, na shirikisho la Usovieti kuvunjika, na kuifanya Urusi kua kwenye hali mbaya sana ya kiuchumi, Ukraine ililazimika sana kua karibu na Umoja wa Ulaya ili kuweza kupata mitaji, teknolojia pia masoko kwa bidhaa zake.
Pia, Umoja wa Ulaya iliona Ukraine kama moja ya nchi ambayo wangefaidika nayo kiuchumi moja kwa moja. Mfano, kwa sasa, Ukraine ni moja kati ya wazalishaji wakubwa wa chakula kama ngano, alizeti, mahindi, nakadhalika, kwa ajili ya kuuza umoja wa Ulaya.
SOMA ZAIDI: Nini Kimesababisha Mgogoro wa Urusi na Ukraine?
Pia, ni nchi yenye hifadhi kubwa ya madini ya kimkakati ndani ya bara la Ulaya. Hali hii ikaifanya Umoja wa Ulaya waone faida ya kutaka ‘kuhodhi’ mahusiano na Ukraine kuliko kuwaachia Urusi. Jiografia yake imetokea kuiponza Ukraine na kufanya wawekwe mtu kati ya pande mbili za miamba.
Kosa kubwa
Binafsi naamini kosa kubwa la kimkakati ambalo Ukraine wamelifanya sio kuchagua kua karibu na Urusi dhidi ya Marekani na washirika wake wa Ulaya, au kua karibu na Marekani na washirika dhidi ya Urusi, naamini machaguo yote hayo yana changamoto zake.
Kujiweka karibu na Urusi na kutochangamkia mahusiano ya kiuchumi na kibiashara na Umoja wa Ulaya na Marekani, kungewarudisha nyuma kiuchumi, lakini pia kua karibu na upande mwingine dhidi ya Urusi, pia matokeo tumeyaona japo naamini yangekuja tu siku moja kwenye historia japo yangechelewa.
Naamini, kosa la kimkakati kwa Ukraine, walilifanya Disemba 5, 1994, jijini Budapest, Hungary.
Tarehe hiyo ndio siku Ukraine ilisaini makubaliano ya kisiasa na Urusi, Marekani na Uingereza ya kuhakikishiwa usalama wake kama taifa huru, kuheshimiwa mipaka yake, na pia kupewa ulinzi na mataifa hayo makubwa matatu, kwa kubadilishana na Ukraine kusalimu na kurudisha silaha zake za Nyuklia kwa Urusi, maarufu kama Budapest Memorandum.
SOMA ZAIDI: Balozi wa Ukraine Nchini Kenya Kukutana na Raia wa Ukraine Waliokwama Zanzibar
Kabla ya hapo, Ukraine, ikiwa sehemu moja kati ya nchi inayounda shirikisho la iliyokua Umoja wa Kisovieti, silaha nyingi za nyuklia zlihifadhiwa huko Ukraine, na walipojitenga na kupata Uhuru, bado walikua nazo. Binafsi, naamini kama Ukraine ingekua na silaha zake za nyuklia mpaka sasa, bado wangekua salama.
Mpaka sasa hatujawahi kuona taifa lenye silaha za nyuklia likionewa kijeshi na nchi nyingine, sababu hakuna nchi isiyoogopa kushambuliwa kwa silaha hizo toka dunia ilivyoshuhudia mkasa uliowapata Japan.
Naamini viongozi wa Ukraine wakiangalia namna nchi yao inavyoshambuliwa na Urusi na huku Marekani, moja kati ya nchi iliyoahidi kumlinda, wakisuasua chini utawala wa Rais Donald Trump, kwa hakika watakuwa wanaikumbuka Disemba 5, 1994, kwa uchungu mkubwa sana.
Zahoro Muhaji amejitambulisha kama mchambuzi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zahoromuhaji@gmail.com au X kama @ZMuhaji. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.