The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Msamiati wa Kiswahili Usipotumiwa Vizuri Hudhihirisha Weledi Hafifu wa Lugha na Kupotosha Ujumbe

Hatuwezi kukiuka misingi, taratibu na kanuni za lugha kama kweli tunataka taarifa tunazokusudia kuzifikisha kwa hadhira, zifike kama tulivyokusudia na zilete athari inayostahiki.

subscribe to our newsletter!

Moja kati ya dhima kubwa ya lugha ni kuwasilisha mawazo yaliyomo katika fikra za msemaji, mzungumzaji au mwandishi. Lengo kuu la mawazo yanayowasilishwa ni kufikisha taarifa maalum ambayo mwasilishaji hukusudia iifikie hadhira yake. 

Taarifa tunazozipata baada ya kusoma au kusikiliza, ndizo tunazoziita ujumbe. Ujumbe kupitia lugha tunaweza kuupata katika nyanja au fani nyingi za lugha, kama vile za fasihi, barua, habari, makala, insha, matangazo, risala, hotuba, mahubiri na mazungumzo tunayoyafanya kila siku na kila mahali.

Kwa kuwa ujumbe ndiyo stahabu ya kila msikilizaji na msomaji, ndiyo azma ya kila msemaji na mwandishi, ndipo kila lugha ikawekewa misingi na kanuni zinazomuongoza mtumiaji, hususan anayeitumia lugha katika shughuli rasmi, ili awe fasaha katika usarifu wa matamshi yake, usahihi wa maumbo ya maneno, upangiliaji faafu wa maneno na kujenga tungo sahihi zitakazokamilisha kifungu cha habari. Hatimaye kupatikana maana iliyokusudiwa ambayo hutazamiwa kutoa ujumbe unaotarajiwa.

Moja katia ya stadi muhumu za usemaji na uandishi, inayopaswa kuwekewa akmali ya uangalifu na uzingatifu ni matumizi ya msamiati wa lugha. Msamiati wa lugha usipotumiwa mahala panapostahiki huweza ama kupotosha au kutofikisha kabisa ujumbe unaokusudiwa na mwandishi au msemaji wa lugha. 

Makala hii inakuletea uchambuzi wa kisayansi wa baadhi ya maneno yanayodhihirisha utajiri wa lugha ya Kiswahili lakini yanahitaji weledi katika misingi ya matumizi yake, hususan kwa wanahabari na waandishi wengine.

Miongoni mwa watumiaji rasmi na wakubwa wa lugha ni wanahabari. Kwa wanahabari lugha si kama sehemu tu ya kazi yao, kiasi cha kupewa hadhi duni, bali ni nyenzo, mtaji na tunu ya kazi zao. Ndiyo wanayoitumia kusuka, kuchambua, kuhoji, kujadili, kuhukumu, na hata kusambaza kazi zao kama vile habari, makala, vipindi na matangazo mbalimbali.

SOMA ZAIDI: Uvamizi Dhidi ya Tasnia ya Habari? Tuzungumze Matumizi Mabovu ya Kiswahili Yafanywao na Waandishi wa Habari

Ukichunguza habari, makala na hata baadhi ya matangazo ya vyombo vingi vya habari, utagundua makosa mengi katika matumizi ya lugha sanifu na fasaha, yakiwemo matumizi mabovu ya baadhi ya msamiati wa lugha. Jambo hili licha ya kupigiwa kelele kila uchao, bado linaonekana kuithakili tasnia ya habari nchini na wakati mwingine hata vyombo vya habari vya kimataifa.

Matumizi ya viunganishi

Kiswahili, kama zilivyo lugha nyingine, kina viunganishi vingi ambavyo hutumiwa kwa namna tafauti kuunganisha maneno, tungo, sentesi, dhana, ibara na hata vifungu vya habari. Miongoni mwavyo ni na, pamoja na, sawa na, licha ya, lakini, ingawa, mithili ya, kama, ambapo, wakati, au, laiti, vyenginevyo, hivyo, kwa hivyo, vilevile, hata hivyo, aidha na halikadhalika.

Viunganishi hivi hugawanyika katika aina mbambali na hudhihirisha mantiki tafauti za kisemantiki. Mgawanyo huo na mantiki zinazobainishwa ndivyo vinavyomuongoza mwandishi, au msemaji, kutambua wapi atumie kiunganishi hiki na wapi atumie kile. Kiunganishi kipi kinaweza kuanza mwanzo wa sentesi na kwa kigezo gani. Kadhalika kipi hakiruhusu hali hiyo. Sidhani kama wanahabari wengi wameeledika katika sayansi hii ya lugha.

Kwa mfano, habari ya DW Kiswahili iliyotumwa katika akaunti ya Facebook ya chombo hicho cha habari, Januari 21, 2025, ilisomeka hivi: “Donald Trump tayari ameanza kazi kama rais wa 47 wa Marekani…” Hapa kuna matumizi yasiyo sahihi ya kiunganishi ‘kama.’ 

Kiunganishi hiki kinaweza kutumiwa kwa dhima tafauti katika tungo. Miongoni mwazo ni kuonesha ushuruti, kwa mfano; Kama atakuja, nitampa; kufananisha; Alipita kwa kasi kama umweso; hutumika kuchuka nafasi ya ‘kuwa’ na ‘kwamba.’ Kwa mfano, badala ya kusema ‘Sikujua kuwa atakuja’ ninaweza kusema ‘Sikujua kama atakuja.’

Kwa namna kiunganishi hiki kilivyotumika katika habari hiyo, kinafanya kazi ya kufananisha au kwa niaba. Yaani, uanzaji wa kazi wa Dodald Trump umefananisha na ule wa Rais wa Marekani au Donald Trump ameanza kazi kwa niaba ya rais wa Marekani. 

SOMA ZAIDI: Hatutegemei Shirika Kubwa la Habari Kama ZBC Lifanye Makosa ya Kizembe ya Lugha

Hivyo, matumizi mabaya ya kiunganishi hiki yametoa si tu maana potofu bali pia maana tata. Tungo hiyo haikutakiwa kutumia kiunganishi ‘kama.’ Badala yake, kiunganisha ‘akiwa’ na hivyo kusomeka: “Donald Trump tayari ameanza kazi akiwa rais wa 47 wa Marekani …”

Mfano mwengine ni habari iliyotumwa katika akaunti ya Fecebook ya Shirika la Utangazi la Tanzania (TBConline) inayohusu hotuba ya Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko, akizindua Mashindano ya Kimataifa ya Qur’aan Tukufu, Februari 9, 2025. Katika taarifa hiyo kuna kifungu kinachosomeka hivi:

“Aidha amesema mashindano hayo mbali na kuwa yanachochea usomaji wa Qur’aan Tukufu pia hujenga uelewa wa hofu ya Mwenyezi Mungu lakini pia yanaitangaza Tanzania katika taswira chanya.”

Kifungu hiki cha habari kina makosa mengi lakini hapa tutaangazia kosa la matumizi ya kiunganishi ‘lakini.’ Kiunganishi hiki hutumika kuunganisha tungo au mawazo yanayokinzana. Yaani mtu anapoeleza jambo kisha akataja neno ‘lakini’ tunatarajia aeleze kinyume cha yale aliyoeleza kabla. 

Katika kifungu hicho, mwandishi ametaja faida za mashindano ya Qur’aan Tukufu kwa mujibu wa msemaji. Baaada ya kutaja faida mbili, ametumia kiunganishi ‘lakini,’ ambacho kinaashiria kuwa mwandishi atageuka upande wa pili wa faida. Yaani atataja hasara, dosari au changamoto kuhusiana na alichokisema kabla.

Hata hivyo, mwandishi ameendelea kutaja faida. Haya ni matumizi yasiyo sahihi ya viungnishi kama vile lakini, hata hivyo, pamoja na bali. Kwa mantiki hii, mwandishi alitakiwa kutumia kiunganisha na au pia, kadhalika, vilevile, halikadhalika. Hivyo, ingelisomeka, kwa mfano: “… hujenga uelewa wa hofu ya Mwenyezi Mungu kadhalika yanaitangaza Tanzania katika taswira chanya.”

SOMA ZAIDI: Uchanganyaji R na L na Makosa Mengine ya Kiswahili Yafanywayo na Wanahabari

Baadhi ya waandishi hupenda pia kutumia kiunganishi ‘lakini’ mwanzoni mwa sentesi. Jambo ambalo si sahihi kabisa. Viunganishi vyenye dhima sawa na ‘lakini’ vinavyoweza kuanza mwanzo wa tungo au sentesi ni pamoja na hata hivyo, pamoja na, na kwa upande mwengine.

Kategoria ya maneno

Baadhi ya waandishi kwa kutoupa umuhimu ujuzi na weledi wa lugha wanayoitumia, hujikuta wakiwa katika mkanganyiko wa matumizi ya kategoria za maneno. Kategoria hapa ni aina za maneno kama vile Nomino (N), Kitenzi (T/Ts/t), Kivumishi (V), Kielezi (E) na Kiwakilishi (W). 

Maneno ya Kiswahili yana sifa ya kunyumbulika na hivyo kubadilika katika kategoria mbalimbali. Mwandishi asipokuwa makini anaweza kulitumia neno katika hali ya kitenzi huku akiwa amekusudia nomino au kinyume chake, bila ya kujua. Kwa mfano, tazama picha hizi tatu namna DW Kiswahili wanavyolitumia neno ‘Tafakari’ wakikusudia Nomino (N), ilihali neno hilo ni Kitenzi (T):

Nomino ya kitenzi ‘tafakari’ ni ‘tafakuri.’ Hivyo, katika taarifa zinazoonekana kwenye picha hizi, neno sahihi lilitakiwa kuwa Tafakuri na si Tafakari.

Wanahabari na lugha

Haiyumkiniki kutangaza au kuandika chochote pasi na kutumia lugha. Hivyo kwa vyovyote iwavyo, hatuwezi kukwepa umuhimu wa matumizi sanifu na fasaha ya lugha, ikiwa kweli tunakusudia kufanya kazi kitaaluma na kitaalamu. 

Halikadhalika hatuwezi kukiuka misingi, taratibu na kanuni za lugha kama kweli tunataka taarifa tunazokusudia kuzifikisha kwa hadhira, zifike kama tulivyokusudia na zilete athari inayostahiki.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Umuhimu wa matumizi bora ya lugha haupewi nafasi stahiki na wanahabari wengi. Pengine hali hii inaweza kuwa inasababishwa na bezo, weledi hafifu wa lugha na wakati mwengine kukosekana kwa wahariri mahususi wa lugha katika vyombo vingi vya habari, kama si vyote.

Mifano michache tuliyoibainisha hapo juu, iwe chachu kwa wanahabari na waandishi wa fani nyingine kujihimu katika kujifunza zaidi lugha na misingi yake, ili kazi zao ziwe bora na ziwasilishe kile kinachokusudiwa kuwakilishwa kwenye mbavu za kauli na maandishi yao.

Usalama wa mawimbi ya sauti za wanahabari, bembelezo la upepo wa kauli zao na uzito wa wino wa kalamu zao hutegema mno ufundi, weledi, ubunifu na ustadi wa lugha wanayoitumia. Kuanzia kwenye matamshi, maumbo na mpangilio wa maneno, muundo wa tungo, uteuzi wa msamiati na ufaraguzi kisemantiki na kimantiki.

Ni wajibu usiyoakidi udhuru kwa wanahabari kuwa na shauku, muhu na kariha binafsi ya kujifunza misingi, taratibu na kanuni za lugha. Kwa kutambaa kwenye nyayo hizo watastafidi weledi, ustadi na ubunifu katika kuisarifu lugha na kumudu ufaraguzi wa matumizi yake chini ya mievuli ya ubora, usanifu na ufasaha wake.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×