The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Simba Inapaswa Kujiandaa, Ushindi Mnono Si Rahisi Katika Fainali

Kudhani kuwa RS Berkane walishindwa kupata udhindi mpana kwao na hivyo wanaweza kufungika ugenini, ni kujidanganya.

subscribe to our newsletter!

Baada ya kufungwa kwa idadi ndogo ya mabao katika mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba inaonekana imepata ahueni na matumaini ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji la Afrika wakati itakaporudiana na RS Berkane ya Morocco mwishoni mwa wiki.

Simba ilifungwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Berkane, na hivyo itatakiwa ipate ushindi wa kuanzia mabao 3-0 ili iweze kuwazuia wapinzani wao ambao wameshatwaa taji hilo mara mbili.

Iwapo itamudu kushinda kwa mabao 2-0, bingwa ataamuliwa kwa njia ya penati, ambazo kwa kawaida hazina mwenyeji wala mgeni.

Mechi ya marudiano baina ya timu hizo itafanyika Mei 25 kwenye Uwanja wa Amaan jijini Zanzibar baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutofungua Uwanja wa Benjamin Mkapa tangu ilipoufungia mwezi Aprili kutokana na kujaa maji wakati Simba ilipocheza na Al Masry ya Misri katika mashindano hayo.

Matumaini ni makubwa kwa Simba na mashabiki wake kupata ushindi baada ya kuona wachezaji walimudu kuwazuia Berkane kupata zaidi ya mabao mawili nyumbani na hivyo wanategemea kutwaa kombe hilo kwa kupata matokeo mazuri nyumbani.

Mwendo usiyo mzuri

Hata hivyo, Simba haijawa na mwendo mzuri katika hatua ya mtoano. Ililazimika kusubiri ushindi wa penati dhidi ya Al Masry iliyoshinda nyumbani kwa mabao 2-0 na wababe hao wa Mtaa wa Msimbazi kuibuka na ushindi kama huo kwenye Uwanja wa Mkapa.

SOMA ZAIDI: Betting: Rafiki Mzuri wa Soka Anayehitaji Umakini

Haikupata ushindi mzuri dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini katika mechi za nusu fainali baada ya wageni hao kutoka kusini mwa Afrika kushindwa kuziona nyavu za Simba katika mechi zote mbili, na hivyo Simba kunufaika na ushindi wake wa nyumbani.

Hata hivyo, ni nadra sana kuona mechi ya fainali inatoa ushindi mkubwa, iwe ya mchezo mmoja au yote miwili. Kuna kitu katika fainali ambacho husababisha hata timu inayoonekana kuwa ni dhaifu, kukomaa na kutoruhusu ushindi mnono kwa timu iliyokuwa na mwenendo mzuri katika hatua za awali.

Baada ya USM Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa miaka miwili iliyopita, ilionekana kwamba mabingwa hao wa soka wa Tanzania Bara walikuwa wakielekea kupata ‘kipigo cha mwizi’ nchini Algeria katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho.

Lakini hali ikawa tofauti. Yanga ilienda kijasiri nchini Algeria na nusura igeuze matokeo, lakini ikashindwa kuongeza bao kujenga ushindi wa mabao 3-2; ilimaliza mchezo ikiwa imeshinda kwa bao 1-0, na hivyo wababe hao wa jijini Algiers kuibuka na ushindi wa sheria ya bao la ugenini.

Mwaka juzi, Ahly ilipata ushindi finyu nyumbani dhidi ya Wydad Athletic Club ambayo ilifunga bao muhimu la ugenini licha ya kulala kwa mabao 2-1. Matumaini kwamba wababe hao wa Morocco wangegeuza matokeo nyumbani yalitoweka dakika ya mwisho wakati Ahly waliposawazisha na hivyo kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 3-2.

SOMA ZAIDI: Kuna Dalili za Soka la Tanzania Kurudi Mahakamani

Pengine timu iliyonufaika na matokeo mazuri ya ugenini ni Al Ahly katika fainali za mwaka jana na hii ilitokana na kutoruhusu bao ugenini. Ahly, iliyokuwa inatetea ubingwa, ililazimisha sare ya bila kufungana na Esperence du Tunis katika mchezo wa kwanza na haikufanya ajizi jijini Cairo ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 na kutetea taji lake.

Tangu mwaka 2010, ni TP Mazembe pekee iliyopata ushindi mnono wa mabao 5-0 nyumbani, lakini ikiwa ni mechi ya kwanza ya fainali iliyofanyika jijini Lubumbashi dhidi ya Esperence du Tunis. Baada ya ushindi huo katika fainali ya mechi mbili, Mazembe haikuwa na kazi ngumu zaidi ya kulazimisha sare ya baop 1-1 jijini Tunis.

Hata vigogo wa Afrika, Al Ahly walishindwa kugeuza kipigo cha mabao 2-0 walichopewa na Orlando Pirates katika fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2013. Walichoambulia Ahly nyumbani ni sare ya bao 1-1 iliyoipa ubingwa Pirates.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho kumekuwa na matokeo tofauti ingawa si ya kugeuza ushindi wa ugenini. Jaribio lililoonekana kuwa zuri la kubadili ushindi wa mabao 3-0 ambao Raja Athletic Club iliupata dhidi ya AS Vita jijini Casablanca. Ikihitaji ushindi wa mabao 4-0, Vita ilijikuta ikiruhusu bao mapema na hivyo Wamorocco kuwa na ushindi wa jumla wa mabao 4-0. Juhudi za dakika za mwisho ziliipa Vita ushindi wa mabao 3-0, lakini ikaukosa ubingwa kwa kipigo cha jumla ya mabao 4-3.

Matokeo ya ushindi

Kwa hiyo, mechi nyingi za fainali za michuano ya Afrika hazijawa na matokeo ya ushindi mnono au matokeo chanya kwa timu inayoanzia ugenini, wakati mwingine hata pale inaporuhusu bao chache.

SOMA ZAIDI: TFF Isisubiri CAS, Ianze Kujiwajibisha Sakata la Yanga v Simba

Kama ilivyokuwa kwa AS Vita mwaka 2015, mkakati mkuu ulitakiwa uwe kuhakikisha wageni hawapati bao, hasa mwanzoni mwa mchezo kwa kuwa wanazidisha urefu wa mlima, au kupata bao mwisho mwa mchezo kwa kuwa muda wa kurekebisha matokeo unakuwa umeisha.

Ingawa ilionekana shida kwa AS Vita kugeuza kipigo cha mabao 3-0, ari ilikuwa ya juu mbele ya mashabiki wake. Lakini iliporuhusu bao dakika ya 21, ilikuwa imeshajipa kibarua cha ziada; yaani ilitakiwa ishinde kwa mabao 5-1 ndipo itwae kombe hilo.

Kwa Simba, hali ni kama hiyo. Si rahisi kuibuka na ushindi mkubwa unaoweza kubadili matokeo ya kipigo cha mabao 2-0 ugenini ilichopoewa na RS Berkane, ingawa inawezekana.

Ni muhimu kujua kuwa maandalizi ya kimwili na kiakili ni muhimu katika kipindi cha kuelekea mechi hiyo ya marudiano. Kudhani kuwa RS Berkane walishindwa kupata udhindi mpana kwao na hivyo wanaweza kufungika ugenini, ni kujidanganya.

Ni vizuri wachezaji, viongozi na mashabiki wakaona kazi ngumu iliyopo mbele na kujiandaa kwa kila kitu kinachowezekana. Kuwaambia mashabiki kuwa Berkane itafungwa tu kwenye Uwanja wa Amaan ni kuwapa matumaini yasiyo na uhalisia sana. Wakienda uwanjani wakakutana na bao la ugenini, wanaweza kupoteza hata nguvu yao ya mchezaji wa 12 uwanjani.

SOMA ZAIDI: Simba Wameonyesha Njia Ujenzi wa Viwanja

Na hilo halitakuwa tofauti na lile la mwaka 1993 wakati kila shabiki, kila kiongozi na kila mwanachama alipoamini kuwa Simba ingetwaa Kombe la CAF baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana na Stella Abidjan nchini Ivory Coast.

Kuanza kupanga sherehe za ushindi, njia za kulipitishia kombe na mambo mengine, itakuwa ni kuirubuni akili dhidi ya kazi ngumu iliyo mbele yao. Kunahitajika maandalizi ya kimwili, kiakili na kisaikolojia wakati wa kuelekea mechi hiyo nyingine ya kihistoria.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×