Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza kuwa Makamu Mwenyekiti wake wa Tanzania Bara ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli Isihaka Mchinjita, aliyekuwa katika ziara ya kujionea madhila wanayopata watumiaji wa Usafiri wa Mwendo Kasi jijini Dar esSalaam leo Ijumaaa tarehe 23, Mei 2025 amekamatwa na Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hiko, Mchinita amekamatwa katika kituo cha mabasi ya mwendokasi kilichopo Kimara Mwisho, jijini Dar es Salaam mara baada ya kukata tiketi na kutaka kutumia usafiri huo wa umma.
“ACT Wazalendo tunalaani hatua hiyo ya Jeshi la Polisi kumkamata kiongozi wetu na tunawataka wamuachie mara moja bila masharti yoyote,” imeeleza taarifa hiyo.
Bado Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote ya kukamatwa kwa kiongozi huyo, na The Chanzo inaendelea kufuatilia kutoka Polisi juu ya sakata hili.
Viongozi mbalimbali wa ACT Wazalendo, wafuasi wa chama na watu wengine mbalimbali wametoa rai kupitia mitandao ya kijamaa wakilitaka Jeshi la Polisi kumuachia huru Mchinjita.
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amelaani kukamatwa kwa Mchinjita na kulitaka Jeshi la Polisi kumuachia mara moja bila masharti yoyote.
“Kumekuwa na malalamiko makubwa ya wananchi wa Dar es Salaam kuhusu huduma duni za usafiri wa mabasi ya mwendokasi. Leo asubuhi Waziri Mkuu Kivuli na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa Ndugu Mchinjita alikwenda stendi ya mabasi hayo Kimara kujionea adha wanazopata wananchi. Polisi wamemkamata,” ameandika Zitto.