Kidonda kinaweza kupona bila ya kupata tiba, lakini si mara zote. Kuna vidonda ambavyo huchukua muda mrefu hadi kikaonekana ni sehemu ya mwili, na hivyo kupachikwa jina la dondandugu. Hiki ni kidonda kinachomla binadamu taratibu bila ya kusikia maumivu makali.
Na katika jamii kuna kasoro ambazo huweza kujirekebisha bila ya kutafuta mkakati mkubwa wa kuzitatua, lakini ziko ambazo zinahitaji hatua madhubuti na thabiti kuzimaliza. Bila ya hatua hizo, kasoro hizo zinakuwa sugu na zinaweza kuiumiza jamii.
Yapo matatizo ambayo huisha kwa vikao vichache, na yapo ambayo yanahitaji vikao vingi kwa ajili ya kutafuta asili, au chanzo, cha tatizo na baadaye kutafuta mbinu za kulimaliza.
Sijui Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) wamechukua njia gani katika kushughulikia tatizo la uahirishaji holela wa mechi ya Simba na Yanga iliyopangwa kuchezwa Machi 8, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini ikaahirishwa saa chake kabla ya muda kuanza kwa kile kilichoelezwa kuwa ni “viashiria vya vurugu na rushwa.”
Viashiria hivyo vilitajwa baada ya Simba kuandika barua kwenda TPLB kueleza kuwa haitacheza mechi hiyo ya Machi 8 kwa madai kuwa ilifanyiwa vurugu na watu wanaosadikiwa kuwa ni walinzi wa Yanga wakati walipokwenda Uwanja wa Mkapa jioni kutumia haki yao ya kikanuni ya kufanya mazoezi mepesi siku moja kabla ya mechi.
SOMA ZAIDI: Simba Inapaswa Kujiandaa, Ushindi Mnono Si Rahisi Katika Fainali
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB ikawajibu Simba kuwa mechi ipo palepale na waliohusika kwenye vurugu hizo wangechukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni. Saa chache baadaye kamati hiyo ikatangaza kuwa mechi hiyo imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
Yanga ikasema ni lazima iheshimu kanuni kwa kuwa mechi haiwezi kuahirishwa kwa sababu zilizotajwa, na hivyo kuahidi kupeleka timu uwanjani. Hata hivyo, uwanjani hakukuwa na waamuzi isipokuwa mashabiki walioanza kuingia kuanzia asubuhi kama ulivyo utamaduni wa mashabiki wa klabu hizo zinapokutana.
Siku iliyofuata Yanga ikaandika barua ya malalamiko TFF ikidai ipewe ushindi katika mchezo huo, lakini haikujibiwa, na hivyo ikalazimika kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kuwahi muda wa kuwasilisha shauri lao baada ya TFF kuchelewa kutoa uamuzi.
Yanga pia ikasema haina imani na viongozi wa TPLB na inataka waondolewe. Lakini rais wa TFF, Wallace Karia, aliporejea nchini kutoka Morocco, alijibu swali la waandishi kuhusu sakata hilo, akielekeza mashambulizi kwa viongozi wa Yanga aliposema “hao wanaodai viongozi wa TPLB wawajibike, wao wako smart (nadhifu)?” jibu lililovuruga zaidi sakata hilo na Yanga kupanua wigo wao wa madai kwa kueleza kuwa hawana imani pia na viongozi wa TFF.
Wakati sakata hilo likitaka waliohusika kuwazuia Simba wasifanye mazoezi, waliohusika kuahirisha mechi wawajibishwe, hakuna lililofanyika hadi sasa na badala yake Bodi ya Ligi imetangaza Juni 15 kuwa ndiyo tarehe mpya ya mchezo huo, lakini Yanga imesema haitapeleka malalamiko popote na haitaingiza timu uwanjani siku hiyo.
SOMA ZAIDI: Betting: Rafiki Mzuri wa Soka Anayehitaji Umakini
Hadi leo kumekuwa kimya kuhusu shauri hilo na inaelekea kinachosubiriwa ni Juni 15 kuona kama Yanga itapeleka timu au la, badala ya kushughulikia changamoto zilizojitokeza.
Hoja za Yanga
Hoja za Yanga ni kwamba itapeleka timu ikiwa viongozi wa TPLB na TFF watawajibishwa na kwa ukubwa zaidi ni kutaka wale waliohusika kuahirisha mechi watawajibishwa.
Kimsingi, takwa la Yanga si kuwaondoa viongozi hao wa TPLB, au kumuondoa Karia, bali kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika kuahirisha mechi bila ya kufuata kanuni. Yanga inaamini kuwa uahirishwaji huo wa mechi ulifanywa kuwanufaisha wapinzani wao, ambao inadaiwa siku hiyo wachezaji wao nyota walikuwa majeruhi.
Simba ilishafanya hivyo mwaka mmoja uliopita wakati ikitakiwa kucheza mechi na Kagera Sugar mkoani Kagera. Ilidai isingeweza kucheza mechi hiyo kwa kuwa wachezaji wake walipatwa na mafua makali. TPLB ikaweka msimamo kuwa mechi ingechezwa kama ilivyopangwa, lakini saa chache kabla ya muda wa mchezo kuanza, ikaahirisha wakati Kagera Sugar imeshafika uwanjani.
Ni kama vile Yanga wanaona mchezo wa kuahirisha mechi kwa ajili ya kunufaisha wapinzani wao umenoga na sasa wanataka kuukomesha.
SOMA ZAIDI: Kuna Dalili za Soka la Tanzania Kurudi Mahakamani
Yanga wanajua fika kuwa uchunguzi huru ukifanywa kujua waliohusika, mambo mengi yatafichuka na itabainika mchezo uliokuwa ukifanyika. Ni wazi kuwa sura za viongozi wakubwa wa soka zitaanikwa na kupoteza heshima yao mbele ya jamii.
Pengine ndio sababu ya ukimywa wa TFF na TPLB katika kushughulikia hoja ya kuwaanika waliohusika na kuwachukulia hatua.
Si rahisi
Si rahisi kwa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kukutana mara mbili ndani ya saa chache kufanya uamuzi. Ni lazima kulikuwa na shinikizo la kuwarudisha wajumbe kikaoni kuahirisha mechi baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya.
Siku ya mechi ya vigogo hao huwa ni purukushani kubwa, kiasi kwamba si rahisi wajumbe wakae karibu na chumba cha mkutano kusubiri wito wa kikao cha pili baada ya kile kilichoweka msimamo wa mechi kuchezwa kama ilivyopangwa.
Si rahisi kwa kamishna wa mechi kuandika ripoti ya mchezo kabla haujafanyika. Si rahisi kwa kamishna wa mechi kuandika ripoti ya mechi kabla ya kwenda uwanjani na kuona viashiria vya vurugu.
SOMA ZAIDI: TFF Isisubiri CAS, Ianze Kujiwajibisha Sakata la Yanga v Simba
Si rahisi kwa Kamati ya Usimamizi kuona viashiria vya vurugu na kuamua kuwa vinaweza kusababisha hatari bila ya idhini ya Jeshi la Polisi, ambalo hutuma maofisa wake katika kikao cha maandalizi ya mechi na kutoa taarifa ya tathmini ya hali ya usalama.
Na si rahisi kwa viashiria vya rushwa kusababisha mechi kuahirishwa.
Kwa hiyo, kuna masuala mengi ambayo TFF na TPLB wanatakiwa kuyashughulikia mapema wakati huu wa kusubiri Juni 15 ili kusiibuke tatizo jingine kubwa zaidi kuliko yote yaliyowahi kutokea katika soka.
Tatizo sugu
Kama nilivyoandika mwanzoni, matatizo hayo hayawezi kujitatua kama kidonda. Inaonekana tatizo la uahirishaji mechi kiholela kwa maslahi ya watu fulanifulani lishakuwa sugu kama dondandugu, na hivyo linaula mpira wa miguu taratibu.
Kibaya zaidi ni kwamba dondandugu limefikia mahali pabaya na kuanza kuleta maumivu makali. Hapa huwezi tena kusubiri lipone lenyewe, au kutumia dawa za kutuliza maumivu, bali kuchukua hatua madhubuti na thabiti kuliponya.
Na mara nyingi dawa za kuponya tatizo kama hilo huwa chungu na kwa sababu ni lazima litibiwe, ni lazima dawa hizo zitumiwe hata kama ni chungu kiasi gani.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.