The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

TFF Ijiepusha na Chaguzi za Wilaya

TFF ni lazima iheshimu mamlaka za mikoa na kuacha kuingilia shughuli zake kwa kisingizio kwamba ngazi hiyo haijaunda vyombo vyake.

subscribe to our newsletter!

Kuna uwezekano uchaguzi mwingine wa viongozi wa soka wa wilaya ukaingia kwenye mgogoro mwingine mkubwa kutokana na siasa za uchaguzi za kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa na, kwa namna fulani, siasa za uchaguzi mkuu ujao wa wabunge na madiwani.

Tumeshuhudia mpambano huo wa madaraka na wa kisiasa ukichukua nafasi kubwa katika uchaguzi wa viongozi wa soka wa wilaya ya Temeke, TEFA ambako ilibidi waliokiuka taratibu na kanuni za uchaguzi waadhibiwe na Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), badala ya mamlaka yake ya nidhamu, yaani kamati ya maadili ya Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA).

Yaani wakati chombo cha kusimamia soka nchini, Chama cha Soka Tanzania (FAT) kilipobadili muundo wake kutoka chama kwenda shirikisho, kilikuwa kimebadili muundo wa madaraka kwa kuachia madaraka katika ngazi ya mikoa badala ya FAT ambayo ilikumbatia madaraka yote kutoka wilaya hadi taifa.

Kwa maana hiyo, vyama vya soka vya mikoa vikawa vinashirikishwa tu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vikiwa na mamlaka kamili yasiyoingiliwa na uongozi wa shirikisho. Maana halisi ya shirikisho, kama ilivyo Serikali ya Shirikisho ya Marekani, kwa maana kwamba inaundwa na Serikali huru za majimbo, ambazpo zina mamlaka kamili isipokuwa yale yaliyoanishwa kwenye Serikali ya Shirikisho.

Ndivyo ilivyo kwa Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani. Na kwa ufahamu zaidi, ndivyo ulivyo muundo wa uongozi wa Shirikisho la KImataifa la Soka (FIFA), ambalo linashirikisha vyama huru vya soka vya nchi vilivyo na mamlaka kamili ya kuendesha shughuli zake, hasa zile muhimu kama za kupata viongozi wake. Pia, zina vyombo vya haki, kama kamati za maadili za nchi kwa ajili ya kushughulikia uadilifu.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Msimu wa Ligi Uwe Miezi 12 Badala ya Tisa ya Kawaida? 

Kwa hiyo, FAT ilipobadilika kuwa TFF iliondoa mamlaka ya kusimamia shughuli za uendeshaji mpira katika ngazi ya mikoa ili ijikite zaidi na masuala ya kitaifa na shughuli nyingine za maendeleo.

Tafsiri tofauti

Inaonekana katiba hiyo sasa inatafsiriwa vingine, na TFF inashika mamlaka yote katika ngazi ya mikoa, na zaidi inaelekea hadi katika ngazi ya wilaya, kitu ambacho kinaweza kusababisha uongozi ukawa wa aina moja, yaani wa watu wenye mrengo wa aina moja, na hivyo kwenda kinyume na ile kanuni kuu ya mawazo tofauti yanavyosaidia kuleta maendeleo.

Kwa hiyo, siasa za ubunge za wilayani Temeke ziliingilia uchaguzi. Mgongano wa maslahi unaotokana na TEFA kuwa na vyanzo vizuri vya mapato, ukazidi kuchochea mgogoro wa uchaguzi na nguvu ya viongozi wa shirikisho ndio ikazidi kuuchafua uchaguzi huo. Hivi sasa wapo waliopata adhabu maarufu ya kufungiwa maisha kujishirikisha na soka, adhabu ambayo, hata kama wahusika wana hatia, huenda inatolewa Tanzania tu.

Hali hiyo imeanza kujitokeza wilayani Ubungo ambako uchaguzi wa kipindi kilichopita haukuwaacha salama baadhi ya wanafamilia. Wako waliokumbana na ile adhabu maarufu ya kifungo cha maisha na hadi leo wanapambana mahakamani.

Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwishoni mwa wiki, lakini haukufanyika baada ya mamlaka za juu kuuzuia kutokana na baadhi ya wagombea kuwasilisha malalamiko yao kwa kamati za kitaifa.

SOMA ZAIDI: Sakata la Yanga, Simba Haliwezi Kuisha Kama Kidonda. Viongozi Wawajibike

Ndivyo ilivyokuwa Temeke ambako mamlaka husika haikuwasilishiwa shauri lolote kwa sababu kubwa moja tu: mkoa wa Dar es Salaam bado haujaunda kamati yake ya maadili kushughulikia uadilifu katika mamlaka yake.

Na ndivyo itakavyokuwa kwamba mashauri yaliyojitokeza wilayani Ubungo hayatashughulikiwa na mamlaka ya mkoa kwa sababu kamati ya maadili bado haijaundwa.

Maajabu

Cha ajabu, Kamati ya Maadili ya TFF inaona ni sawa kushughilikia mashauri ya uadilifu yawanafamilia ambao si wanachama wake, kama ilivyofanya wilayani Temeke. Vyama vya soka vya wilaya si wanachama wa TFF, bali ni wanachama wa vyama vya mikoa. Iweje shauri la wilaya likatolewe maamuzi na chombo cha kitaifa? Katika utawala bora hii si sawa.

Ingawaje kwa utawala bora hilo si sawa, lakini siasa za uchaguzi ujao wa viongozi wa soka wa mikoa, husababisha kuwepo na migogoro mikubwa katika ngazi za wilaya. Na kwa sababu kunakuja pia uchaguzi wa viongozi wa shirikisho, wanaowania uongozi katika ngazi ya taifa, nao wanaingiza figisu zao ili wapatikane wapigakura watakaowafaa na si viongozi wanaofaa kuongoza mpira kwa miaka minne ijayo.

Hii inaondoa ufanisi katika uendeshaji soka kuanzia ngazi za wilaya hadi mikoa kwa kuwa wanaochaguliwa kuongoza ni wapigakura na si watu wenye maono, sifa na uwezo wa kuongoza mpira katika ngazi hizo.

SOMA ZAIDI: Simba Inapaswa Kujiandaa, Ushindi Mnono Si Rahisi Katika Fainali

Ndio maana zile ligi maarufu za wilaya na hatimaye mkoa ni kama zimekufa. Macho na masikio ya watu wilayani na mikoani ni kwa Simba na Yanga na si kuona vijana wao wakipambana katika ngazi za juu kitaifa.

Na kwa sababu wanaenda kwenye vikao vya mikoa na kitaifa kupiga kura tu, hakuna mijadala mizito ya kuhoji mipango ya maendeleo kwa kuwa wanapokwenda kwenye mikutano mikuu kazi yao ni ama kupiga kura ama kuunga mkono ajenda.

Na ndio maana kila uchaguzi wa mkoa unapomalizika, kauli ya kwanza ya mshindi wa kiti cha uchaguzi ni kuunga mkono mgombea wa urais wa shirikisho na si kuueleza umma mikakati yake ya kusukuma mbele maendeleo ya soka katika ngazi yake.

Tunusuru soka

Ni muhimu haya yakaonekana mapema na wale wenye nguvu wakaanza kuyashikia bango ili kuunusuru mpira wetu dhidi ya ongezeko la machawa wasio na uchungu na maendeleo, bali matumbo yao.

TFF ni lazima irudi nyuma na kuangalia mwelekeo huu kama ni afya kwa mpira wa miguu. Mamlaka ambayo inashindwa kuunda vyombo vyake vya haki kushughulikia mashauri katika ngazi yake, ziwajibishwe badala ya kutumia upenyo huo kushughulikia watu wanaonekana kuwa si wapigakura bali viongozi.

SOMA ZAIDI: Betting: Rafiki Mzuri wa Soka Anayehitaji Umakini

Tunahitaji viongozi wanaohoji na si wanaoenda kushiriki kampeni za wagombea wa uongozi katika nafasi za kitaifa. 

TFF ni lazima iheshimu mamlaka za mikoa na kuacha kuingilia shughuli zake kwa kisingizio kwamba ngazi hiyo haijaunda vyombo vyake. Badala yake, isisitize kuwa kila mkoa ni lazima uunde vyombo vyake vya haki ili vile vya kitaifa vijikite na mashauri ya kitaifa tu.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×