Zanzibar. Sekta ya uchumi wa buluu na uvuvi imekuwa ni moja ya kipaumbele kikubwa sana cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye miaka ya hivi karibuni. Serikali imekuwa ikijidhatiti kwa kusuka mipango madhubuti ya sekta hiyo yenye fursa nyingi kwa lengo la kukuza uchumi wa visiwa hivi va marashi ya karafuu.
Juni 3, 2025 Baraza la Wawakilishi lilipitisha bajeti ya wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 172.03 zilipitishwa. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 14.95 zitatumika kwa kazi za kawaida kama mishahara na uendeshaji wa ofisi, huku kiasi cha Shilingi bilioni 157.08 zinatarajiwa kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Bajeti hii ya mwaka huu imeongezeka kwa kiasi kikubwa sana tofauti na mwaka jana, ambapo mwaka 2024/25, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 66.01, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 10.99 zilikuwa kwa ajili ya kazi za kawaida na Shilingi bilioni 55.02 kwa ajili ya maendeleo.
Kitendo cha bajeti ya mwaka huu kuwa Shilingi bilioni 172. 03 imekuwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 106.02, ambayo ni sawa na asilimia 160.6. Ongezeko hili kubwa linatokana na mipango ya uwekezaji katika miradi ya kimkakati, hususan ujenzi wa bandari za uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya baharini, usambazaji wa gesi, na kuendeleza sekta ya uvuvi wa bahari kuu.
Katika matumizi ya maendeleo bajeti imeweka kipaumbele katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya baharini, ambapo uzalishaji wa samaki unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 78,943 hadi kufikia tani 115,000. Vilevile, sekta ya kilimo cha mwani imepewa msukumo mpya, kwa lengo la kuongeza uzalishaji kutoka tani 19,715 hadi 30,000.
Mbali na kilimo na uvuvi, bajeti hii pia inalenga kuchochea uwekezaji katika utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hii inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi na kusambaza gesi, ikiwa ni sehemu ya mipango ya muda mrefu ya kutumia nishati kama kichocheo cha uchumi.
Bajeti ya 2025/2026, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar imepanga kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu na kuongeza mchango wake katika pato la taifa. Vipaumbele vikuu vya bajeti hii ni pamoja na ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani, utanuzi wa bandari za Mkoani na Shumba, pamoja na ujenzi wa bandari za Kizimkazi kwa ajili ya uvuvi.
SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu
Serikali pia imepanga kuwekeza katika Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO) ili kuongeza uzalishaji wa samaki na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini. Shilingi bilioni 172.03, zimetengwa kwa miradi ya maendeleo.
Samaki na mwani
Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imejipanga kuongeza uzalishaji wa samaki na mwani kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kutekeleza mikakati kabambe ya kiutekelezaji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kisasa, utoaji wa elimu kwa wakulima na wavuvi, pamoja na ugawaji wa vifaa muhimu vya uzalishaji.
Serikali inalenga kukuza thamani ya mazao haya, ambayo ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi wa buluu, kwa lengo la kuongeza kipato cha wananchi na mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.
Katika sekta ya samaki, Serikali imepanga kuimarisha upatikanaji wa vifaranga na chakula bora cha samaki kwa kujenga viwanda na vituo vya kuzalisha rasilimali hizo. Pia, serikali inaendelea na ujenzi wa madiko na masoko ya kisasa ya samaki maeneo ya Fungurefu (Unguja) na Mkoani (Pemba) ili kurahisisha uuzaji na usindikaji wa mazao ya uvuvi.
Kwa upande wa mwani, serikali imetangaza mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wake kwa kuwapatia wakulima mafunzo ya kitaalamu juu ya kilimo bora cha kina kirefu kwa kutumia mbinu ya “kamatia chini” (double loop techniques).
Ili kuimarisha ubora wa mwani na kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeanzisha maabara ya kisasa ya uzalishaji wa mbegu (Tissue Culture Laboratory) katika eneo la Beit el Raas.
Mbali na hilo, mashamba darasa yameanzishwa chanja 140 za kukaushia mwani zimejengwa ili kuboresha uhifadhi na usindikaji wa zao hilo. Serikali pia imeanzisha kamati ya kitaifa ya kushughulikia maendeleo ya sekta ya mwani, ikijumuisha wadau kutoka sekta ya umma na binafsi ili kutatua changamoto za wakulima kwa pamoja.
Kupitia juhudi hizi, Serikali inalenga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya baharini, kuhamasisha uwekezaji, na kuimarisha kipato cha wananchi, hasa wanawake na vijana wanaojihusisha na sekta hizo. Hatua hizi ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar ya mwaka 2022, ambayo imeweka msingi imara wa kutumia rasilimali za bahari kwa njia endelevu.
Mafuta na gesi
Mwaka 2025/2026 kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA), Serikali inalenga kusimamia uwekezaji katika vitalu 10 vya mafuta na gesi vilivyotangazwa, vikiwemo nane vya baharini na viwili vya nchi kavu, kwa kutumia mfumo wa utoaji wa vitalu kwa njia ya moja kwa moja kwa wawekezaji.
Kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo, jumla ya Shilingi bilioni 6.78 ziliombwa na ZPRA katika bajeti ya 2024/2025, ambapo hadi kufikia Machi 2025, walipokea Shilingi bilioni 3.63 pekee, sawa na asilimia 54 ya bajeti iliyopangwa. Fedha hizo zilitumika kujenga kituo cha muda cha kuhifadhia na kusimamia taarifa za mafuta na gesi kununua vifaa maalum vya kuhifadhi taarifa, na kutoa mafunzo kwa watendaji wa mamlaka hiyo.
Kupitia Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Zanzibar (ZPDC), Serikali pia imepanga kuendeleza utafiti wa maeneo ya mafuta na kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bohari ya mafuta.
Mipango hii inalenga kuhakikisha Zanzibar inanufaika kikamilifu na rasilimali zake za mafuta na gesi kwa kuzivuna kwa njia endelevu, kuimarisha mapato ya taifa, na kutoa ajira kwa wazawa.
SOMA ZAIDI: Mkopo wa Dola Bilioni 2.5 Kutoka Korea Kusini: Je, Tanzania Imeweka Rehani Bahari na Madini Yake?
Hata hivyo, utekelezaji wa mipango hii unategemea upatikanaji wa fedha kwa wakati, jambo ambalo limekuwa changamoto katika bajeti za miaka ya nyuma. Serikali imetakiwa kuongeza msukumo wa kifedha na kiutendaji ili sekta hii muhimu iweze kuleta matokeo yaliyotarajiwa.
Fedha kidogo
Kama ilivyokuwa kwenye wizara nyingi, ambapo licha ya Baraza la Wawakilishi kupitisha bajeti kubwa lakini wizara zimeendelea kupokea fedha kidogo kwa ajili ya kutekeleza mipango yake.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 66.01. Hata hivyo, hadi kufikia Machi 2025, wizara ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi bilioni 28.48 tu, sawa na asilimia 43 ya bajeti yote iliyopangwa.
Kati ya fedha zilizopatikana, Shilingi bilioni 6.09 zilihusiana na kazi za kawaida, na Shilingi bilioni 22.39 zikiwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo sehemu kubwa ilitoka Serikalini kupitia SMZ, huku michango ya washirika wa maendeleo ikiwa midogo.
Kiwango hiki kidogo cha fedha kilichotolewa hakitoshelezi kutekeleza kikamilifu malengo makubwa ya Serikali kwenye sekta ya uchumi wa buluu. Miongoni mwa mipango hiyo ni pamoja na ujenzi wa madiko ya kisasa, uzalishaji wa vifaranga, maabara za mbegu za mwani na kuimarisha soko la mazao ya baharini, yote yanayohitaji uwekezaji mkubwa na wa haraka.
Kutokana na changamoto hii ya upatikanaji wa fedha kwa wakati na kwa kiwango cha kutosha, kuna hatari ya miradi mingi kuchelewa au kutofanyika kabisa, hali ambayo itazorotesha juhudi za kuongeza ajira, kipato kwa wananchi na ukuaji wa pato la taifa kupitia sekta ya uchumi wa buluu.
Serikali inapaswa kuweka mkazo zaidi katika utoaji wa rasilimali fedha kwa wakati ili kuhakikisha dhamira ya kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia bahari inatimia kwa vitendo.
Changamoto nyingine ambayo itaikabili wizara hii mwaka huu ni ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo kutokana na changamoto za upatikanaji wa fedha na urasimu katika utoaji wa fedha za bajeti. Ukosefu wa wataalamu wa uvuvi wa bahari kuu umekuwa tatizo sugu, hasa katika kampuni ya ZAFICO, ambapo uvuvi wa bahari kuu unahitaji teknolojia na ujuzi wa hali ya juu ili kufanikisha shughuli za uzalishaji.
Suala la uharibifu wa mazingira ya bahari, unaosababishwa na uvuvi haramu na athari za mabadiliko ya tabianchi, umekuwa kikwazo kikubwa kwa uhifadhi wa rasilimali za bahari na ukuzaji wa sekta ya uvuvi.
Pia, masoko kwa mazao ya baharini, hususan mwani, imeendelea kuwa changamoto, licha ya juhudi za Serikali za kuimarisha uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa hizo.
Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com.