Dodoma. Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, utiaji saini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu kati ya Benki Kuu ya Tanzania na makampuni ya uchimbaji madini na kiwanda cha usafishaji dhahabu cha GGR, itawezesha Benki Kuu kupata vyanzo vya uhakika katika kufanikisha programu yake ya ununuzi wa dhahabu.
Akizungumza wakati wa zoezi la utiaji saini amesema hatua hiyo itasaidia viwanda vya ndani vya usafishaji wa dhahabu kufikia malengo ya kupata ithibati ya kimataifa ya London Bullion Market Association (LBMA).
“Mpango huu wa ununuzi wa dhahabu ni dhamira ya Serikali inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan inakuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, kuongeza mchango wa madini katika pato la taifa, pamoja na kuongeza thamani ya madini nchini,” amesema Nchemba.
Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu nchini kwa kimombo Domestic Gold Purchase Programme – DGPP ulioanza katika mwaka wa fedha 2022/23 ni fursa kwa wauzaji wa dhahabu kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu kwa bei ya ushindani ya soko la kimataifa.
Kupitia mpango huu, Benki Kuu imelenga kuongeza kiwango cha dhahabu kinachotumika kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uhimilivu wa akiba ya fedha za kigeni nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya taifa ya kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje kama chanzo kikuu cha akiba ya fedha za kigeni, na hivyo kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea kifedha kwa kutumia rasilimali asilia zilizopo ndani ya nchi.
“Hadi kufikia Juni 13, 2025, Benki Kuu imefanikiwa kununua kilo 5,022.85 za dhahabu safi, zenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani milioni 554.28, Ikiwa imezidi lengo lake la mwaka la kuongeza akiba ya fedha za kigeni kiasi cha dola za Kimarekani 350 million kwa 2024/25,” amesema Tutuba.
Kuanzia Oktoba 1, 2024 hadi 13 Juni 2025, Benki Kuu imenunua dhahabu kupitia viwanda vya usafishaji wa dhahabu nchini kwa kufuata misingi ya uwazi, bei ya ushindani, na ufanisi, sambamba na malengo ya kuhakikisha dhahabu inapatikana kwa viwango vya kimataifa.
“Dhahabu hii imesafishwa katika viwanda vifuatavyo Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) kilo 3,181.3, Eyes of Africa (EOA) kilo 979.5) na Geita Gold Refinery (GGR] kilo 385.6.”
Naye Waziri wa Madini Antony Mavunde mesema utiaji saini mikataba hiyo itapelekea Benki Kuu kupata madini ya dhahabu ya kutosha kwa ajili ya hifadhi zake lakini pia kuchochea uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi.
“Kifungu cha 100 D cha Sheria ya madini kinazuia usafirishaji wa madini nje ya nchi pasipo kuongezwa thamani,” amesema Mavunde.
Pamoja na mafanikio hayo, Tutuba amesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo changamoto za Kisheria kuhusu ununuzi wa madini ambata (By-products) ambapo ametaja Sheria ya Madini kama kikwazo kwa kuwa haitambui Benki Kuu kama mnunuzi na muuzaji wa madini ambata kama vile madini fedha.
“Tunapendekeza marekebisho ya haraka ya sheria ili kuiwezesha Benki Kuu kununua na kuuza madini ambata na kuweza kuongeza ufanisi katika zoezi zima la ununuzi wa dhahabu nchini,” amesema Tutuba.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa ithibati ya LBMA kwa viwanda vya kusafishia dhahabu nchini hali inayosababisha Benki Kuu kufanya mabadilishano ya dhahabu (gold swaps) kwa gharama kubwa ili kupata dhahabu fedha (monetary gold) inayotambulika kimataifa.
Kuhusu changamoto hizo, Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inatambua changamoto hizo na nyinginezo zinazohusiana na masuala ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gharama za usafishaji dhahabu pamoja na gharama za kubadilisha dhahabu kwa ajili ya kuhifadhiwa nje ya nchi. Amesema Serikali itazifanyia kazi changamoto zote kwa mujibu wa sheria.
“Lengo ni kwamba kama taifa tunakuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni katika dhahabu, kwani kwa muda mrefu sasa imedhihirika kwamba bei ya dhahabu imekuwa ni nzuri na inayozidi kupanda mwaka hadi mwaka,” amesisitiza Mwigulu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa viwanda vya kuchenjua dhahabu, kutumia fursa hiyo ya kiasi kikubwa cha dhahabu kinachouzwa nchini, kuongeza uwezo wao wa kusafisha dhahabu, ili viweze kukidhi vigezo vya kimataifa vya kupata ithibati ya ubora ya LBMA.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia jaquelinevictor88@gmail.com