Mahakama Kuu ya Tanzania leo Juni 23, 2025, imewatia hatiani maofisa wawili wa Jeshi la Polisi na kuwahukumu kunyongwa kwa kosa la mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis (25), ambaye aliuawa Januari 5, 2022 mkoani Mtwara.
Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Hamidu Mwanga, wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa watuhumiwa waliopatikana na hatia ni Gilbert Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa (OC-CID) wilaya ya Mtwara, na Charles Onyango, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara.
Watuhumiwa wengine watano wa kesi hiyo Nicholaus Kisinza, Mkuu wa Kikosi cha Intelejensia ya Jinai mkoa wa Mtwara, John Msuya Mganga, Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Marco Mbuta, Shirazi Mkupa na Salimu Juma Mbalu wameachiliwa huru.
Mauaji ya Hamis yaligonga vichwa vya habari mwaka 2022 hadi kumpelekea Rais Samia Suluhu Hassan kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aunde kamati ya kuchunguza mauaji hayo. Rais Samia alifanya uamuzi huo kwa kile alichoeleza kuwa kuwa hakukubaliana na suala la jeshi hilo kudaiwa kuhusika na mauaji na kisha kujichunguza lenyewe.
Waziri Majaliwa alitekeleza agizo hilo, ambapo Februari 26, 2022, kamati aliyoiunda alimkabidhi ripoti yake, lakini mpaka hukumu hii inatolewa leo matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo yalikuwa hayajawekwa wazi.