The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tumefikaje Kwenye Hali ya Sasa ya Kutengeneza Miungu Watu Hapa Tanzania?

Katika miaka ya hivi karibuni, dhana ya kuabudu viongozi kupita kiasi imezidi sana Tanzania, ikichagizwa na mambo kadhaa. Hali hii ina athari nyingi kwa mustakabali wa taifa letu.

subscribe to our newsletter!

Wakati wa uzinduzi wa daraja la Busisi, Waziri wa Ujenzi, Abdalla Ulega, alitoa sifa kedekede kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ndoto ya mtangulizi wake, hayati John Magufuli. Akihojiwa na moja ya vyombo vya habari, Ulega alitoa sifa nyingi kwa Rais na kumtaja kama mkweli, muadilifu na mwenye hofu ya Mungu. 

Katika uzinduzi huo wa daraja ambalo limepewa jina John Pombe Magufuli (JPM) kwa heshima ya mchango wake mkubwa katika miundombinu, viongozi wengi wa Serikali walihudhuria hafla hiyo ambayo ilitajwa kama historia kwa taifa la Tanzania. Mbali na viongozi wa Serikali na waandamizi, hafla ilisheheni makada wa Chama cha Mapinduzi, wasanii, waigizaji na watu wengine ambao wanatajwa kama maarufu.

Jambo ambalo kwa sasa sio la kushangaza tena, ni jinsi viongozi wa juu wa Serikali na siasa wanavyowasifia viongozi wa juu wa Serikali, akiwemo Rais Samia. Imekua utamaduni sasa kwa kila kiongozi wa Serikali, na hata watu wa kawaida, kuanza hotuba zao, hata pale rais hayupo, kwa kumshukuru Rais Samia. Barabara nyingi za mikoa ya Tanzania zimepambwa na picha za Rais. 

Mabango ya kumtukuza Rais yamejaa kila kona. Vijiwe vya mitaani, kama vile vijiwe vya drafti, karata, kahawa na gumzo, vimepewa majina ya Rais. Baadhi ya redio nchini zinatukumbusha maneno aliyosema Rais Samia kwenye hotuba zake – mithili ya hotuba za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambazo zilikuwa kizichezwa mara baada ya taarifa ya habari kwenye redio ya Taifa. 

Viongozi wa juu Serikalini, wakiwemo mawaziri wanavaa fulana na kofia ambazo zinachapa ya SSH. Mtangulizi wa Rais Samia, John Magufuli, pia alipewa sifa ambazo zilimkufuru Mungu. Kwa mfano, Mbunge Kangi Lugola akichangia mada bungeni mwaka 2020 alimfananisha Magufuli na Yesu Kristu. Prof Palamagamba Kabudi aliteleza ulimi na kumwita Rais Magufuli “Mheshimiwa Mungu” na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwahi kutamka kwamba “Mungu anatakiwa amshukuru Rais Magufuli.”

Miungu watu 

Swali linaloibuka ni kwa nini Tanzania imejenga utamaduni wa kuabudu viongozi wa juu Serikalini? Je, ni utamaduni wa Watanzania kutengeneza miungu watu, au kile kinachojulikana kwa kimombo kama cult personality? Ama, ni mifumo kandamizi inayochagiza mazingira ya kusifia pasipo kawaida? Na, ni nini athari za kujenga taifa la kuabudu viongozi wa siasa?

SOMA ZAIDI: Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea?

Neno cult personality limetumiwa kuelezea sampuli ya viongozi ambao, kupitia jamii zao, wanainuliwa na kugeuzwa kuwa zaidi ya binadamu wa kawaida. Kiongozi wa namna hii anajua kila kitu, anajiona ana uwezo mkubwa mfano wa Mungu. Mara nyingi, kiongozi wa namna hii anaaminika kubeba dira na mawazo ya watu wake. Baadhi ya sifa nyingine ni kuwa na mvuto wa kipekee, au charismatic, kupendwa na kuhofiwa na watu. 

Katika historia, viongozi kama Fidel Castro wa Cuba, Kim il Sung wa Korea ya Kaskazini, Joseph Stalin wa USSR, Mwenyekiti Mao Zedong wa Uchina, walijenga hulka za kimiungu watu, au cult personality, ambazo walizitumia kuhalalisha tawala zao. Kupitia itikadi za kikomunisti, itikadi za kisoshalisti (Ujamaa), na itikadi za utaifa, viongozi hawa waliweza kujenga nchi zao katika nyakati ngumu. 

Kwa mfano, itikadi ya kikomunisti ilikua ndiyo msingi wa mapinduzi ya Cuba mwaka 1959 na itikadi za utaifa, au nationalism, na ufasisti zilitumiwa sana na viongozi wa aina hii barani Ulaya mwanzoni mwa karne ya 20. Kupitia itikadi hizi za utaifa, viongozi hawa waliweza kusimika tawala zao kwa njia za kimabavu na kujenga tawala za kiimla. 

Tumefikaje hapa?

Kwa tathmini ya kihistoria, kuna baadhi ya wale wanaosema, mbinu hizi zilikua muhimu kwa ajili ya kujenga utaifa na maendeleo ya viwanda. Lakini, athari zake ni kwamba, viongozi wa namna ile walijenga dhana na nadharia ya wakombozi wa mataifa yao na kwamba bila wao nchi hizi zisingekua kitu.  

Tanzania ipo katika mchakato wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ambao unategemewa kufanyika Oktoba. Katika miaka mitatu iliyopita, dhana ya kuabudu viongozi kupita kiasi imezidi. Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, chini ya uongozi wa Rais Samia, dhana ya viongozi kusifiwa kupitiliza imeshamiri sana. Utawala wa Rais Samia umejikuta katika hali hii kwa sababu kuu mbili.

SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket 

Ya kwanza ni kukubali kutekwa na watu ambao waliona kumsifia kama fursa. Mara baada ya kuchukua mikoba ya urais mwaka 2021 kufuatia kifo cha Magufuli, Rais Samia alipata uungwaji mkubwa sana kutoka kwa Watanzania wengi. Kwa wakati ule, Tanzania ilikua katika mpito ambao ulihitaji kiongozi ambaye angeinua matumaini ya Watanzania baada ya kipindi kigumu cha kisiasa. 

Watanzania wengi walimuona Rais Samia kama kiongozi mfano ambaye ataufanikisha mpito ule. Walimuona kama kiunganishi na wakamuita Mama. Jina Mama lilitumika kumpa heshima na kumkabidhi majukumu ya kimama japo kuna wale waliosema jina hilo lilimdunisha.

Watu waliomzingira waliona fursa na kuanza kushusha sifa. Tukaanza kusikia “Mama anaupiga mwingi” au “Mama kaifanya Tanzania kujulikana kimataifa” pamoja na balagha, au hyperbole kwa kimombo, nyingi. Nadhani mtitiriko wa sifa zilizopitiliza na kujipendekeza kwa viongozi na waandamizi ziliambatana na kipindi ambacho Rais Samia alikua katika harakati za kujikita na kuonyesha mamlaka yake ndani ya CCM na katika ngazi za juu za mfumo wa utawala. 

Ni wakati huu machawa – jina la dhihaki ambalo limepewa kwa wale wanaomsifia Rais na chama tawala liliibuka. Machawa wamelikubali jina hilo na kuendelea bila soni kutetea hata mambo ambayo unaona kabisa hayafai. Rais Samia, ama kwa kutojua ama kuzidiwa kete, alikubali sifa hizi ziendelee. Siku hadi siku tukaona anaendelea kupewa sifa pamoja na kuheshimishwa ikiwa ni pamoja na kutunukiwa cheo udaktari wa heshima.

Jambo la pili ni Rais Samia kukubali uhalisia wa sifa kama mtaji wa kisiasa. Katika mahesabu ya kisiasa, hususan wakati ambapo tunaelekea kwenye uchaguzi, viongozi wengi wanafurahia sifa kama ishara ya kukubalika, ama kujenga taswira ya kukubalika, na wapiga kura.

Athari kwa taifa

Athari za kujenga taifa la kuabudu viongozi wa siasa kupitiliza zipo nyingi. Kwanza, athari ya sifa kupita kiasi na kuabudu viongozi kama mashujaa husababisha utawala wa kibinafsi, au personalized governance kwa kimombo, jambo linalofanya uwajibikaji kuwa mgumu. 

SOMA ZAIDI: ‘Animal Farm’ ya George Orwell Inavyotusaidia Kuelewa Dhana ya Uongozi wa Umma na Uwajibikaji 

Pili, jambo hili huzaa taifa la watu waoga, wenye hofu na wasiohoji. Ni kawaida kuwa na mitazamo tofauti, na hakika wote hatuwezi kufikiria sawa. Ila katika mazingira ya kuwa na miungu watu kama viongozi, basi huwezi kumkosoa. 

Tatu, pale kiongozi, ama viongozi, wa Serikali wanapoabudiwa na kutukuzwa kupita kiasi, taasisi ambazo zimewekwa kikatiba, kwa mfano, Mahakama, Bunge, vyombo vya habari, nk., vinashindwa kufanya kazi zao kwa uhuru. Taasisi hizi ambazo zinaongozwa kisheria zinalazimika kutoa maamuzi yatakayomfurahisa kiongozi na sio kwa kuzingatia haki na maslahi ya watu wote. Mataifa ambayo yanajiita ya kidemokrasia kama Tanzania, mfumo wa udhibiti na usawazishaji wa mamlaka, au checks and balances, kwenye taasisi za Serikali ni muhimu. 

Mwisho, viongozi ambao wanakubali kuzingirwa na machawa, wapambe, wanafiki na wanaojipendekeza, mara nyingi hufanya maamuzi mabaya kwa sababu washauri wao wanaogopa kuwaambia ukweli. Na pale anapoambiwa ukweli, kiongozi anajikuta anapuuza ama kumwajibisha yule mshauri kwa kumfukuza kazi.

Nihitimishe kwa kutahadharisha kwamba historia inatuonesha kwamba uongozi wa kimungu mtu ni mbaya kwa taifa na ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na utawala bora. Kiongozi wa siasa, hata akiwa na cheo kikubwa, ni mtumishi wa wananchi. Anapaswa kukubali kukosolewa na pale anapofanya vizuri anapongezwa – sio kama nabii bali mtumishi wa watu. 

Mohandas Gandhi, mwanaharakati aliyeamini kutotumia nguvu kama njia ya kupigania haki na mpigania uhuru wa India aliwahi kusema, “Sio vizuri kwetu kumwabudu mtu binafsi. Ni mawazo au maadili tu yanayoweza kuabudiwa.”

Tubadilike, hatujachelewa!

Nicodemus Minde ana Shahada ya Uzamivu kwenye mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani – Afrika, Nairobi, Kenya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia nminde96@gmail.com au X kama @decolanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×