The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Simulizi za Watoto Walioachishwa Shule na Wazazi Wao na Kulazimika Kuingia Mitaani Kutafuta Maisha

Kwa sasa wanajihusisha na kubeba mizigo pamoja na biashara ndogo ndogo, vitu ambavyo hawakupenda kuvifanya ila imewalazimu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Bariki Matonya alikuwa na umri wa miaka 17 alipoachishwa shule na baba yake mzazi, wakati alipokuwa anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Idifu, iliyopo Mvumi, wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.

Matonya mwenye umri wa miaka 19 hivi sasa alikumbwa na mkasa huo mwaka 2023, ambapo hali hiyo ilitokana na wazazi wake kutokuwa na maelewano mazuri. Hivyo, ilipelekea akose mahitaji muhimu ya shule, na mama yake alikuwa akitaka mwanaye asome huku hali ikiwa tofauti kwa upande wa baba yake.

“Wakati wa kwenda kufanya mtihani wa kidato cha pili nikaacha,” Matonya aliiambia The Chanzo Novemba 6, 2024, alipokuwa kwenye soko la Sabasaba akibeba mizigo majira ya saa mbili asubuhi. “Sikufanya mtihani kutokana na mazingira ya nyumbani yaliyotokana na kukosekana kwa ushirikiano kati ya baba na mama.”

“Baba yangu huwa anakunywa pombe, akinywa anakuwa mkorofi. Sikuelewa kwa nini baba yangu alitaka mimi niache shule. Lakini ni ukweli nilitakiwa niwe shuleni hadi muda huu,” alisema Matonya, mtoto wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto sita katika familia yao.

Baada ya kuachishwa shule Matonya alilazimika kuja Dodoma mjini kutafuta maisha, na akaanza kufanya kazi ya kubeba mizigo katika soko la Sabasaba.

Kijana huyo mfupi wa kimo, aliyekuwa amevalia sweta jeusi, kaptura ya jinsi ya buluu na viatu vya wazi miguuni, huku akiwa amebeba mzigo mabegani mwake alisema, angekuwa na wazazi wenye uwezo na nia ya kusomesha angesoma kama wenzake ili aachane na kazi hiyo ngumu.

Mizigo hiyo anayoibeba haina bei maalum, akionewa huruma kulingana na mzigo aliyobeba hulipwa kiasi cha Shilingi 2,000. Mara nyingi kiasi anachopewa ni Shilingi 500 pekee.

“Kubeba mizigo ni changamoto kubwa sana, sema tu inatulazimu. Kwa siku unaweza kuingiza kiasi cha Shilingi 10,000 kama faida. [Na] kuna siku unakosa kabisa. Kuwa huku inaniumiza kwa sababu ukiangalia na umri wangu na kazi ninayofanya ni ngumu mno.”

SOMA ZAIDI: Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuongeza Ubora wa Elimu Inayotolewa Tanzania

Pamoja na kuwa Matonya anafanya kazi hiyo yenye ujira mdogo, kipato anachokipata kwa sasa anakitumia pia kuihudumia familia yao pindi inapohitaji msaada. Lakini pia, amefanikiwa kununua nguruwe wawili ambao amempa mama yake awafuge.

Nikifaulu nisimjue

Yaliyomkuta Matonya hayana tofauti sana na kile ambacho kilimkuta Steve Thadei mwaka 2020 alipokuwa na umri wa miaka 13. Thadei alilazimika kuacha shule mwaka huo akiwa darasa la sita mara baada ya baba yake mzazi kumwambia kuwa endapo atafaulu mitihani ya darasa la saba basi asimjue yeye kama mzazi wake.

“Nilitamani kuendelea na shule lakini baba aliniambia ukifaulu tafuta mzazi wako,” alisema Thadei huku akiwa anaangalia chini kwa huzuni. “Akasema kama wewe unataka kuendelea kusoma utajua mwenyewe.”

“Hawa baba zetu wanashida,” aliongeza Thadei, mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto saba katika familia yao. Ukiomba hela [tu] ya daftari anakuambia yeye hana. Walitaka tuwe tunawachungia ng’ombe zao.”

Alipoacha shule alikuwa ni mtu wa kulima kwenye mashamba. Kaka yake alipoona mdogo wake anapitia hali hiyo alimchukua na kumleta Dodoma kufanya kazi, ambapo tangu mwaka 2021 amekuwa akibeba mizigo kwenye soko la Sabasaba.

The Chanzo ilibaini kuwa watoto wengi wa kiume wenye umri kati ya miaka 10 na 19 wanaoachishwa shule na wazazi wao, hukimbilia jijini Dodoma kisha huanza kujishughulisha na biashara za kuuza mayai, vitafunwa, karanga, mifuko, pamoja na kubebea mizigo kwenye masoko.

Niache shule nikalime

Doto Frank, 16, mzaliwa wa wilaya ya Mpwapwa alishinikizwa kuacha shule na baba yake wa kambo aliyekuwa akimtaka ajikite kwenye shughuli za kilimo za familia.

“Niliacha shule nikiwa darasa la sita mwaka 2021,” alisema Frank. “Nakumbuka ilikuwa siku ya kwenda kufanya mtihani, nikaambiwa nisiende shule niende shambani. [Nikaambiwa] mimi ni mvivu nataka kwenda shule na sitaki kwenda shamba. Baba akasema kama hutaki kwenda kulima ondoka hapa nyumbani. Nikaamua niende kulima shambani.”

“Siku niliyoenda shule mwalimu alinichapa sana viboko, kutokana na yale maumivu nikaamua kuacha shule,” aliongeza Frank wakati akizungumza The Chanzo kwa huzuni huku machozi yakimlenga.

Kwa sasa Frank yupo mjini Dodoma anatembeza mayai, maisha ambayo hakutegemea kuyaishi kwani alikuwa na ndoto za kusoma sana. Lakini kutokana na baba yake kutotaka aende shule basi imelazimu kuishi maisha hayo yenye changamoto nyingi, ambapo anadai kuwa wakati mwingine amekuwa halipwi ujira wake baada ya kazi.

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa mwaka 2022 wanafunzi 329,918 waliacha shule za sekondari na msingi hapa nchini.

Mkoa wa Dodoma ulishika nafasi ya tano baada ya wanafunzi wa shule za msingi 13,208 kubainika kuacha shule, huku kwa upande wa shule za sekondari ulishika nafasi ya tatu baada ya wanafunzi 8,846 kuacha shule.

Uchunguzi ambao The Chanzo uliufanya mwaka jana ulibaini kuwa sababu kubwa iliyopelekea mkoa wa Dodoma kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule ni ugumu wa maisha.

Lakini pia, wazazi wengi hasa wanotokea maeneo ya vijijini walionekana kutotambua umuhimu wa elimu, hali ambayo imekuwa ikiwasukuma kuwalazimisha watoto wao waache shule ili wakijite kwenye shughuli za kuzalisha kipato kitakachosaidia familia zao.

Venance Kabengwe ni Meneja Miradi wa Shirika la The Living Smile International ambalo linahusika na elimu kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu Dodoma. Akizungumza na The Chanzo kuhusu changamoto ya watoto kuachishwa shule mkoani hapa, Kabengwe amesema kuwa kitendo hicho si tu kina madhara kwa watoto hao bali kwa familia na jamii nzima kwa ujumla.

“Elimu ni kiashiria namba moja cha maendeleo ya jamii yoyote. Hawa watoto walikuwa na ndoto zao wakati wanapelekwa shule, inavyotekea wazazi au walezi kuwaachisha watoto au vijana shule kunawafanya watoto washindwe kufikia ndoto zao.”

Kabengwe akaongeza kuwa ukosefu wa elimu kwa watoto wanaoachishwa shule unawapa ugumu pia wakati fulani kutumia maarifa yao kujiajiri, kwa sababu katika jamii yoyote elimu ni kiashiria cha kwanza cha maendeleo.

“Kinachopaswa kufanyika kuwe na uwajibikaji wa pamoja kuanzia mamlaka za chini, Serikali za Mitaa, na kuwe na ufuatiliaji wa makusudi wa kujua zoezi la uandikishaji wanafunzi shuleni.

“Zirekebishwe sheria au zikazwe sheria kwa wazazi au walezii ambao wanashiriki kwenye kuwaachisha watoto shule kwa makusudi. Hakuna sababu ya msingi ya mzazi au mlezi kushiriki kumuachisha mtoto shule,” Kabengwe alisema kwa msisitizo.

The Chanzo ilizungumza na Rosemary Nicodemus, Afisa Ustawi wa jiji la Dodoma, ili kufahamu kama wanatambua juu ya adha ya watoto kuachishwa shule na kisha kuingia mitaani na wao wamekua wakichukua hatua gani dhidi ya suala hilo?

Rosemary akaeleza kuwa wamekuwa wakifuatilia mara kwa mara juu ya suala hilo na kuchukua hatua ikiwemo kuwakusanya watoto walioachishwa shule na kuingia mitaani na kuwapa msaada maalum.

“Watoto tukishawaondoa kwenye mitaa tunaoutaratibu wa kuwaweka kwenye makao wakati tunafanya upembuzi yakinifu, na kufanya tathmini ya huduma,” anasema Rosemary. Kwa sababu unapo muokoa mtoto lazima umsikilize. Ukisha msikiliza ujue tatizo lake ni nini? Ujue nyumbani ni wapi? Kwa hiyo lazima ufanye tathmini ya mahitaji yake, ili uweze kumpa huduma ile ambayo inastahili.”

“Watoto hawa wakifanyiwa tathimini ndiyo tunajua huyu mtoto sasa anahitajika kurudi wapi? Mwingine anasema kabisa nataka kurudi nyumbani. Mwingine ukimfanyia tathmini anasema mimi sihitaji kurudi nyumbani. Kwa hiyo, huyu sasa unakaa naye na kuendelea kuongea naye, kumshauri mpaka mwisho wa siku ujue lile hitaji la msingi.”

SOMA ZAIDI: Elimu ya Zanzibar Inavyowaacha Nyuma Wanafunzi Wenye Ulemavu Kwenye Masuala ya Teknolojia

Ochola Wayoga ni mdau wa masuala ya elimu hapa nchini, ambapo ameeleza kwamba pamoja na uwepo wa kanuni zinazowawajibisha wazazi kwa kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule, suala hilo limekuwa halizingatiwi kwa asilimia 100.

Wayoga anaeleza kuwa tatizo hilo linatokana na ubovu wa usimamizi wa mfumo wa elimu kuanzia ngazi ya familia hadi ngazi ya Serikali.

“Serikali ya kijiji inawajibu wa kujua watoto ambao hawaendi shuleni na sababu zinazo wafanya wasiende,” anasema Wayoga ambaye amewahi pia kuwa Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET). “Kuna sehemu zingine haijatekelezeka na sheria kama inavyotaka hawajachukuliwa hatua hao wanaohusika.”

“Na siyo kwamba hawa wazazi hajui, wanajua hawa wazazi wana simu janja, wana redio ambazo wanasikiliza. Hawa wazazi wengine wanakwenda misikitini na kanisani ambako habari ya elimu inazungumziwa pia na wanasikia. Kwa hiyo kutokumpeleka shuleni kwa muda huu ni ujinga, siyo ujinga inaweza ikawa ni umaskini.”

The Chanzo iliimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, namna mkoa huo unavyokabiliana na changamoto ya watoto kuachishwa shule, ambapo alisema kwamba kwa sasa wanaomkakati wa kuimrisha elimu ambao ulizinduliwa mwaka jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Senyamule akaongeza kuwa mkakati huo unavyo vipengele vyote ukijumuisha namna ambavyo watahakikisha kila mwanafunzi anayetakiwa kuwa shule anakuwa shuleni.

“Tumekuwa tukifanya hamasa kupitia ofisi ya mkoa, mkuu wa wilaya na maeneo mengine kuwakumbusha wananchi wajibu wao wa kufikisha watoto shule,” alisema Senyamule. “Lakini ziko sheria ambazo tunazichukua kwa wazazi ambao watoto wao hawatafika shuleni.”

“Bahati nzuri ipo sheria ya elimu ambayo ina muwajibisha mzazi ambaye hatafikisha mtoto wake shuleni. Mwaka jana tulizisimamia vizuri sheria hizo. Na mwaka huu tunategemea kuendelea kupunguza zaidi tatizo hilo, au kuliondoa kabisa. Mzazi ambaye hatahakisha mtoto wake anafika shuleni atachukuliwa hatua.”

Kwa upande wa Waziri wa Elimu, Profes Adolf Mkenda, yeye amebainisha kuwa wizara inatambua kuwa kuna tatizo kubwa la wanafuzni kuacha shule. Kutokana na hali hiyo wizara inaendelea kuunganisha mifumo yake ya elimu ili kuweza kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi mara tu anapojiunga darasa la kwanza.

“Sasa hivi idadi ya wanafunzi wanaoacha shule Geita ndiyo kubwa sana. Kwa hiyo, tuna mikakati mbalimbali ya kupambana na hali hiyo. Ukweli ni kwamba watoto wa kiume ndiyo wanaacha shule zaidi siyo wa kike. Kwa hiyo, tunalifanyia kazi kwa nguvu kubwa kuna timu inafanya kazi, hatujalifumbia macho.” Profesa Mkenda anasema.
Jackiline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×