The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Azimio TFF Lilitakiwa Lifute Uchaguzi 2025

subscribe to our newsletter!

Ni kawaida ya jumuiya, au taasisi yeyote, kuweka kwenye katiba yake vipindi vya uchaguzi kwa ajili ya kupata viongozi, ama walewale waliopo madarakani waendelee, au kuingiza sura mpya.

Hii imewekwa ili kuwe na ushindani, au kusiwepo na kubwweteka, kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza kwa kuwa pale wanapobweteka tu na mambo kuenda mrama, wapigakura hushtuka na kusubiri kipindi cha uchaguzi ili watumie haki yao kufanya mabadiliko.

Hata kwenye nchi za chama kimoja, bado uchaguzi ni kitu muhimu ili jamii iweze kusonga mbele. Hata kwenye nchi zenye utawala wa kifalme, bado kuna taratibu zinazowekwa kwa ajili ya wananchi kuchagua Serikali inayojihusisha na maisha yao ya kila siku.

Ni katika nchi ambazo kuna utawala wa kijeshi ndiko uchaguzi hakuna. Huko ni amri moja tu kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu. Bila utawala wa kijeshi au wa kidikteta, uchaguzi ni muhimu sana katika kuwafanya viongozi wawajibike kwa wananchi wanaowatumikia.

Ndivyo inavyotakiwa kuwa katika vyama vyote: viwe vya michezo, vya starehe, vya kiuchumi, vya misiba na vinginevyo ili mradi vinakutanisha watu tofauti wenye malengo au nia zinazofanana.

SOMA ZAIDI: Ni Rasmi, Waamuzi Wetu Tanzania Hawaaminiki

Kwa hiyo, ni kitu cha kipuuzi kuweka uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halafu kuweka vizingiti vya kuzuia watu tofauti kugombea. Hakuna maana ya uchaguzi katika mazingira hayo na kwa vyovyote, viongozi hawawezi kuwa wawajibikaji zaidi ya kuzingatia maslahi ya wapigakura wao na si mchezo wenyewe.

Mabadiliko ya katiba

Tumeona jinsi TFF ilivyofanya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2019 yaliyoujenga urais na kuufanya uwe kila kitu katika uongozi na uendeshaji wa mpira wa miguu, huku ukimjengea ukuta mpana wa kuzuia wengine kujaribu kushindana naye.

Tumeona mabadiliko ya kanuni za uchaguzi ya mwaka 2021 yalivyogongomea msumari wa lango la kuzuia wengine kumpa changamoto rais wa sasa, kiasi kwamba imekuwa ni vigumu kwa wale wenye nia ya kugombea kupata sifa zote za kuingia kwenye boksi la kura.

Kanuni iliyoondoa wanafamilia, ambao wameelezwa vizuri kwenye katiba, kuweka pingamizi dhidi ya wagombea, hasa wa urais na kutaka wanachama pekee ndio wawe na sifa za kuandika pingamizi, imeondoa mambo muhimu ambayo wadau wangeweza kuisaidia TFF kuchuja wagombea wachafu.

Wanafamilia ndio wanaoishi au kufanya shughuli za kikazi au kibiashara na watu wanaotaka kuongoza mpira. Kama mgombea alikuwa na kesi ya ukwepaji kodi na akabainika mahakamani kuwa alikutwa na hatia lakini hakuna mwanachama anayetaka kumuwekea pingamizi, huyu atapita na kuchaguliwa kuongoza shirikisho pamoja na uchafu wake.

SOMA ZAIDI: Ni Fursa kwa Klabu Kuunda Upya Bodi ya Ligi

Kama kuna njama kama hizo zilizofanyika Moshi wakati wa Mkutano Mkuu wa kufikia azimio batili la kumuidhinisha mgombea mmoja, uwezekano wa mtu mchafu kama mkwepa kodi wa hapo juu, kupita na kuwa rais ni kitu rahisi sana.

Haiwezekani watu 80 tu ndio wakaamue kila kitu kuhusu wagombea katika taifa ambalo lina wendawazimu wa mapenzi ya mpira wa miguu. Wale watu wapatao 80 wakiopewa dhamana ya kuingia Mkutano Mkuu na Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa TFF, ni wawakilishi tu na si genge la mafia linalojiamulia kila kitu.

Ni wawakilishi wa maslahi mapana ya Watanzania na hivyo wanatakiwa kuheshimu taratibu zilizowekwa katika kutafuta viongozi. Hata kama wanamtaka mgombea mmoja, ni bora waende kwenye boksi la kura kuonyesha mapenzi yao na si kutengeneza kanuni za kuzuia wengine.

Udhaifu mkubwa

Kutumia sheria na kanuni kuzuia wagombea ni udhaifu mkubwa wa uongozi wenyewe na wajumbe wa Mkutano Mkuu. Haiwezekani wajumbe wa Mkutano Mkuu wakaweka kanuni ambayo inaweza kuja kuwageuka hata wao pindi watakapoona wamekomaa na kutaka kushika nyadhifa kubwa TFF.

Ni dhahiri kuwa yule atakayekuwa madarakani, atatumia mbinu hiyohiyo iliyotumika Moshi. Kwamba mtu mmoja anayeamua kujitoa akili, akapendekeza kwenye Mkutano Mkuu eti tufikie azimio la kumuidhinisha mgombea mmoja na wengine wakakubali bila ya kuhoji iwapo watajitokeza wenye uwezo zaidi itakuwaje.

SOMA ZAIDI: TFF Ijiepusha na Chaguzi za Wilaya

Haya basi. Kapitishwa mmoja, inakuwaje wale walioidhinishwa na kanuni kuwa ndio wenye haki ya kuweka pingamizi, wachezewe akili?

Kama mabadiliko ya kanuni yaliondoa wanafamilia kuweka pingamizi na kutaka vyama wanachama ndio viwe na haki hiyo, imekuwaje tena tafsiri ya kanuni hiyo ikarudi kulekule kwa watu binafsi?

Maana ya mabadiliko hayo ni kwamba hakuna mtu yeyote binafsi anaruhusiwa kuweka pingamizi, isipokuwa vyama 26 vya mikoa, vyama vitano shiriki na klabu 16 za Ligi Kuu.

Lakini tafsiri ya Kamati ya Uchaguzi katika kanuni hiyo ni kwamba yule aliyewasilisha pingamizi ndiye anayetakiwa afike mbele ya kamati kulitetea. Yaani kama hayupo na pingamizi lake halisikilizwi wala kujadiliwa.

Ndivyo ilivyotokea katika pingamizi lililowasilishwa na klabu ya Yanga, ambayo ndio mwanachama pekee ambaye hakumuidhinisha rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia, kutetea kiti chake. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andrew Ntine, ndiye aliyewasilisha pingamizi hilo, lakini kikaoni akaenda Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Msimu wa Ligi Uwe Miezi 12 Badala ya Tisa ya Kawaida? 

Kamati ikakataa kumsikiliza kwa kuwa eti si yeye aliyewasilisha pingamizi. Yaani pingamizi likawa na Ntine na si Yanga!

Kuna haja gani basi ya kuandika pingamizi? Kulikuwa na haja gani basi ya kuondoa wanafamilia katika kuwasilisha pingamizi kama pingamizi la mwanachama linageuzwa kuwa la mtu binafsi?

Genge

Kwa kifupi kuna genge la watu pale kwenye Mkutano Mkuu wa TFF ambalo halikupenda kuwepo kwa uchaguzi, lakini halikujua lifanye nini badala ya hadaa hizi zilizofanyika za kusumbua wanafamilia wa mpira wa miguu.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa kawaida kule Moshi, wangefikia azimio la kutoitisha uchaguzi hadi mwaka 2028 badala ya sinema waliyoifanya ambayo inaelekea kuvuruga soka letu. Hii sinema isiposhughulikiwa vizuri, inaweza kuturudisha mahakamani wakati huu tunajiandaa kwa fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zitakazoanza mapema mwezi ujao.

Kama wanavyosema Mkutano Mkuu ndio kila kitu, azimio la kutoitisha uchaguzi 2025 lingeswihi na kama ni usumbufu ungekuja kwa njia nyingine, lakini si hii ya kudhani Watanzania wote ni wapuuzi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×