The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Hoja Siyo Karia Kama Mgombea Bali Kanuni za Uchaguzi Zinazominya Demokrasia

Watu wasizuiwe kwa sheria na kanuni kuingia kwenye uchaguzi, bali mafanikio ya mgombea na mikakati yake ndiyo iamue achaguliwe au aondolewe.

subscribe to our newsletter!

Tangu mchakato wa uchaguzi mkuu wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uanze, na baadaye tatizo la uidhinishaji kuibuka upya kama ilivyokuwa mwaka 2021, kumekuwa na ukosoaji mkubwa unaofanyika kuhusu mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi.

Wapo ambao waliweka pingamizi na wako ambao wamepeleka hoja zao kwa Msajili wa Vyama vya Michezo kupinga ushiriki wa rais wa sasa, Wallace Karia, na kupinga kanuni zinazotumika kwamba kwanza hazikusajiliwa na pili zinakiuka misingi ya haki na demokrasia.

Na wapo waliofikia kutaka Karia aondolewe kabisa kwa madai kuwa Sera ya Michezo ya mwaka 1995 inazuia mgombea kukaa madarakani kwa vipindi vitatu vya miaka minne kila kimoja. Hao wanataka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) litangaze kumuondoa kwa kuwa limeshaviandikia vyama vya Temeke na Ubungo kuondoa sheria inayoruhusu mgombea kukaa madarakani kwa vipindi vitatu vya miaka minne.

Lakini wanaotetea mabadiliko hayo wamekuwa hawayayazungumzii bali kufanya majumuisho kuwa wanaokosoa wanamchukia Karia, na wengine kufikia kusema wana uchu wa madaraka.

Hakuna anayekosoa mabadiliko hayo ambaye ameingia kwenye uchaguzi kutaka agombee, kiasi cha kuweza kuelezewa kuwa anamchukia Karia, au ana uchu wa madaraka.

SOMA ZAIDI: Azimio TFF Lilitakiwa Lifute Uchaguzi 2025

Na wengine, kama mimi, tunaamini kuwa bila ya hata hayo mabadiliko kufanyika, Karia angeshinda kwa kura nyingi hata kama wangepitishwa watu wanane kugombea nafasi ya rais wa TFF. Kwa nini? Ni kwa sababu katika kipindi chake kumekuwa na mafanikio makubwa; awe aliyoyatengeneza yeye au amekutana nayo. Hiyo ilitosha kumrudisha madarakani kwa kishindo.

Kwa hiyo, tatizo si Karia au kumchukia rais huyo wa TFF, bali tatizo ni mabadiliko ya sheria na kanuni zinazofinya demokrasia na kuondoa haki kwenye uchaguzi wa viongozi wa hirikisho hilo. Na ndio maana Karia harushiwi maneno makali na wajenga hoja, isipokuwa wale wa nje wanaoropoka maneno makali kila wanapoona wakosoaji wanajenga hoja muhimu.

Uidhinishwaji wa wagombea

Tatizo kubwa limekuwa ni uidhinishwaji wa wagombea urais au kwa lugha maarufu endorsement. Ni kweli Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) lina sheria inayotaka mgombea wa urais apate angalau vyama vitano vya kumuidhinisha.

FIFA ina wanachama takriban 207, yaani nchi zote zinazotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) zinapata sifa ya kujiunga na shirikisho hilo.

Kwa hiyo, linapoweka idadi ya chini ya waidhinishaji kuwa vyama vitano, hiyo ni asilimia ndogo sana kwa shirikisho lenye wanachama 207. Ukiichukua hiyo kanuni na kuileta kwenye nchi ambayo shirikisho lake lina wanachama 47, unakuwa hujazingatia mazingira ya nchi yako.

SOMA ZAIDI: Ni Rasmi, Waamuzi Wetu Tanzania Hawaaminiki

Ni lazima kuwepo uwiano wa idadi ya waidhinishaji. Kama ina wanachama 207, ni sawa kabisa waidhinishaji wakiwa kuanzia watano kwa kuwa ni vigumu kwa mgombea mmoja kuzunguka na fomu kote duniani kutafuta waidhinishaji zaidi ya 200.

Na kwa ustaarabu wa wenzetu, inakuwa ni vigumu kwa wanachama wote kumuidhinisha mgombea mmoja, isipokuwa pale ambapo ama hajatokea mshindani au ametokea mshindani ambaye ni dhaifu.

Unapoleta kanuni hiyo kwenye uchaguzi kama wetu kunakuwa na hila ndani yake. Kwamba mgombea urais aliye madarakani, akiwalinda viongozi wa mikoa, basi naye atalindwa kwenye uchaguzi wake. Hapo ndipo tatizo linapoanzia.

Siasa

Kwa wale ambao tunafuatilia siasa za mpira wa miguu tumekuwa tukishuhudia tangu chaguzi za viongozi wa mikoa zilipoanza. Wale ambao wanatakiwa na uongozi wa juu wa TFF ndio waliopita mikoani. 

Kilichofanyika ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwenda sambamba na chaguzi zote za mikoani na mara nyingi kufanya maamuzi ambayo yaliengua wale ambao wangeweka upinzani kwa mtetezi au mtu ambaye alitakiwa.

SOMA ZAIDI: Ni Fursa kwa Klabu Kuunda Upya Bodi ya Ligi

Na ukiangalia, ni wagombea wachache wapya walioingia kwenye uongozi wa mikoa, na hao kauli yao ya kwanza baada ya kushinda ilikuwa ni kuunga mkono uongozi wa sasa badala ya kuzungumzia mikakati yao ya kuendeleza soka kwenye eneo lake. Kwa maana nyingine walichaguliwa wapigakura na si viongozi wa mikoa.

Si kila sheria iliyomo kwenye katiba ya FIFA inafaa kutumika katika nchi wanachama kutokana na tofauti ya majukumu na wigo wa utendaji kazi. Kama tunaweza kunakili kila kitu muhimu, basi tungenakili muundo wa Kamati ya Maadili ya FIFA ambayo ina idara kuu mbili zinazojitegemea: idara ya uchunguzi na ya mashtaka.

Mpira wetu una tatizo kubwa la kimaadili ndio maana haikuwa ajabu kuita waamuzi kutoka Misri kuja kuchezesha mechi ambayo ni fahari ya nchi: Simba na Yanga. Kama tatizo ni kubwa kiasi hicho, basi nakili ya kwanza ingekuwa katika muundo na uhuru wa Kamati ya Maadili ya FIFA.

Tujadili hoja

Kwa hiyo, ni muhimu sana kujadili hoja za kimaendeleo zinazohusu misingi ya haki na demokrasia. Kama Rais Julius Nyerere alivyowahi kuonya kuwa katiba tuliyo nayo ina mapungufu makubwa na nchi ikipata kiongozi dikteta, anaweza kuitumia vibaya sana.

Ndivyo tunavyosema sheria na kanuni hizi za soka Tanzania ni mbaya na hazifai. Akija mgombea wa hovyo anaweza kuzitumia vibaya na akishaingia, akaitumia vibaya katiba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa kuweka vipengele vinavyompa rais wa TFF mamlaka makubwa.

SOMA ZAIDI: TFF Ijiepusha na Chaguzi za Wilaya

Kwa hiyo, tunapojadili kasoro za mabadiliko ya sheria na kanuni za uchaguzi, hatumlengi Karia bali hayo matatizo. Na hayo yameanza hata kabla ya wagombea urais kujulikana, na hata kabla ya tarehe ya uchaguzi kutangazwa. Hivyo, si kwamba kuna mgombea anayepigiwa chapuo, la hasha! Kwa sababu hakuna mgombea mwenye nguvu za kushindana na Karia kwa sasa ndani ya TFF.

Lakini hatuwezi kukaa kimya kwa sababu tu Karia ndiye mwenye uwezo wa kushinda, bali ni lazima tujadili kwa kuwa hizi kanuni ni mbovu na zinafinya haki na demokrasia na kupunguza ushindani wa nafasi moja muhimu katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

Anayenufaika na uongozi asijitokeze mbele kuwapachika majina wanaokosoa kuwa hawataki, au hawampendi, Karia, bali ajue kuwa wanapigania mpira wa miguu usitumbukie mikononi mwa waovu watakaoturudisha kule nyuma ambako waziri anayealikwa kufungua mkutano, alikuwa anajibiwa hotuba yake na mjumbe mmoja hapohapo ukumbini. 

Kiwango cha juu cha kiburi kinachotokana na watu kubweteka kiasi hiki!

Watu wasizuiwe kwa sheria na kanuni kuingia kwenye uchaguzi, bali mafanikio ya mgombea na mikakati yake ndiyo iamue achaguliwe au aondolewe. Ndiyo msingi mkuu wa demokrasia.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×