Kila mwaka, Tanzania inatumia Dola za Marekani bilioni moja kuagiza bidhaa za chuma kutoka nje kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa madaraja, ujenzi wa majumba, ujenzi wa reli na mahitaji mengine mengi. Hata hivyo, Tanzania ina hifadhi kubwa ya madini ya chuma ambayo yakivunwa na kuchakatwa yanaweza kuzalisha bidhaa hizo zinazoagizwa kutoka nje.
Pamoja na kuokoa fedha za kigeni kuagiza bidhaa hizo, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini hayo ya chuma yatazalisha ajira nyingi sana katika mnyororo wa thamani katika fungamanisho la mbele na nyuma, au forward and backward linkages kwa kimombo. Vilevile, kuongeza mauzo ya bidhaa nje na kupata mapato ya fedha za kigeni.
Tanzania ina hifadhi ya madini ya chuma yenye mashapo yanayofikia tani bilioni mbili zilizopo chini ya ardhi katika eneo la Liganga. Ili kupata chuma kutoka kwenye udongo unaochimbwa, nishati kubwa ya umeme inahitajika.
Kwa bahati nzuri ilipo hifadhi ya chuma ndipo pia kuna hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambayo yanaweza kuzalisha umeme wote unaotakiwa kuyeyusha chuma. Aina hizi mbili za madini ndiyo nguzo ya viwanda vya msingi – viwanda vya kuzalisha vidhaa za viwanda. Tanzania ina hifadhi ya makaa ya mawe katika eneo la mchuchuma inayofikia mashapo ya tani bilioni moja na milioni 200.
Hazina
Mchuchuma na Liganga ni hazina ya Tanzania. Maeneo haya yapo wilayani Ludewa, Njombe. Hata hivyo, jirani na mkoa wa Njombe, mkoa wa Ruvuma, Tanzania pia imejaaliwa makaa ya mawe ambayo hivi sasa yanachimbwa na kuuzwa nje.
Mwaka 2024, jumla ya tani milioni tatu za makaa ya mawe zilichimbwa na kuuzwa nje. Mwaka huo Tanzania ilipata fedha za kigeni Dola za Marekani milioni 340. Nchi inayoongoza kununua makaa ya mawe kutoka Tanzania ni Poland.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu
Kutokana na mipango, ambayo naweza kusema ni isiyotekelezeka, ya Serikali, tunatarajia kuzalisha na kuuza nje tani milioni moja ya chuma kwa mwaka. Kiwango hiki cha uzalishaji kitahitaji umeme wa kiasi cha 300MW. Vilevile, Serikali inataka kuzalisha 300MW zingine za umeme kwa ajili ya kuingiza kwenye gridi ya taifa.
Kwa namna yeyote ile, Tanzania inaweza kuweka lengo la kuzalisha tani milioni mbili za chuma na tani milioni tano za makaa ya mawe kila mwaka. Makaa ya mawe yazalishe umeme 1000MW kwa ajili ya matumizi ya kuyeyusha chuma na kuingizwa kwenye gridi ya taifa, ikiwemo kuuza nje umeme wa ziada.
Kulingana na mashapo ya chuma na makaa ya mawe yaliyopo eneo la Mchuchuma na Liganga, itachukua miaka 1,000 kumaliza chuma chote na miaka 250 kumaliza makaa ya mawe yote. Kwa bei za sasa za chuma katika soko la dunia, fedha za kigeni zitakazopatikana kutokana na kuuza nje chuma na bidhaa za chuma zaweza kufikia Dola za Marekani 1.5 bilioni mpaka bilioni mbili. Mapato mengine yatatokana na kuuza nje makaa ya mawe na Umeme utakaozalishwa.
Faida kubwa
Faida kubwa kabisa ya mradi huu ni mabaki yanayotokana na uchenjuaji wa chuma. Ndani ya mashapo ya chuma tulichonacho kuna madini mengine yanaitwa vanadium, pentoxide, na mengine mengi. Haya madini ya vanadium ni madini ghali sana duniani kwani yanahitajika kwenye uzalishaji wa ndege, meli na vifaa vya teknolojia mpya.
Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa katika kila tani milioni moja ya chuma inayochenjuliwa kuna takribani tani 80,000 za vanadium zinazopatikana. Mchakato wa kuchenjua chuma lazima uondoe madini haya na mengine ili kupata chuma peke yake, hivyo ni mchakato wa lazima kufanyika.
Madini haya ni uchafu kama uchafu wa pumba za mahindi baada ya kuyakoboa. Hata hivyo, uchafu huu unathamani kubwa sana. Hivi sasa tani moja ya vanadium kwenye soko la dunia inauzwa kwa kati ya Dola za Marekani 30,000 na 50,000.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hili la Wamachinga Linanisononesha Sana
Ukiuza chuma tani milioni moja unapata mpaka Dola za Marekani milioni 600, lakini ukiuza tani 80,000 za vanadium zinazotokana na hiyo tani milioni moja ya chuma unapata Dola za Marekani bilioni 2.4. Fedha mara nne ya upatazo kwa chuma!
Kwa lengo la uzalishaji wa tani milioni mbili za chuma kwa mwaka, mapato ya fedha za kigeni kutoka vanadium peke yake yataweza kuliingizia taifa Dola za Marekani bilioni 4.8 kila mwaka.
Kwa ujumla, mradi mzima wa Mchuchuma na Liganga unaweza kuliingizia taifa fedha za kigeni zinazofikia mpaka Dola za Marekani bilioni saba. Kuweka katika muktadha sawa wa uelewa ni kwamba dhahabu yote tunayouza hivi sasa ni Dola za Marekani chini ya bilioni nne.
Pamoja na faida za mapato hayo ya fedha za kigeni, mradi huu kama ilivyoelezwa hapo awali, utaongeza ajira zaidi ya 100,000 katika mnyororo mzima wa thamani kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuanzisha viwanda vingine vinavyohusiana, ikiwemo mahitaji ya viwanda vya kuyeyusha chuma, vyakula, vinywaji, malighafi, vipuri, na huduma kama vile sekta ya usafirishaji kama reli kutoka Ludewa mpaka Mtwara, makazi na mengine mengi sana.
Kusuasua kwa mradi
Mradi huu wa Mchuchuma na Liganga haujaanza licha ya Serikali kuingia makubaliano na Kampuni kutoka China ili wawekeze na kuanza tangu mwaka 2011. Waziri aliyefanikisha kusainiwa kwa mkataba wa uwekezaji, Dk Cyril Chami, ameshatangulia mbele ya haki.
Tangu mwaka 2015, mradi ulipaswa kuanza kujengwa, Serikali ikahitaji mazungumzo mapya ya mkataba na mazungumzo hayo hayakwisha. Mmiliki wa kampuni iliyotaka kuwekeza naye ameshafariki, na Sichuan Hongda, kampuni ya uwekezaji huo, inasemekana iliingia mgogoro na Serikali ya China na hivyo inawezekana isiweze tena kuwekeza katika mradi huo wa thamani ya ujenzi inayofikia Dola za Marekani 3.6 bilioni.
SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Taasisi za Kimataifa Zina Nguvu Sana Tanzania Kuliko Watanzania
Tanzania inajenga reli itakayofikia gharama ya Dola za Marekani bilioni 15 kwa kuagiza mataruma ya reli kutoka nje. Tunaendelea kupeleka ajira nje na fedha za kigeni. Hakika, hasara ya uchelewaji huu sio tu pesa za kigeni tunazotumia kuagiza bidhaa za chuma, bali pia pesa za kigeni ambazo tungepata iwapo mradi ungeanza.
Ni hasara ya Dola za Marekani bilioni nane kila Mwaka katika miaka kumi iliyopita, na miaka yote inayokuja bila kutekelezwa kwa mradi huu. Ni hasara ya kuua ndoto za malaki ya vijana wa Kitanzania ambao hawana ajira, wakimaliza vyuo wanaishia kuendesha bodaboda ambazo zinaongoza kwa vyanzo vya vifo hapa nchini.
Gesi Asilia
Wakati huohuo, dunia ina mahitaji makubwa ya nishati kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchumi na hata idadi ya watu. Gesi Asilia imekuwa chanzo tegemezi cha nishati duniani. Nchi mbalimbali zinahangaika kutafuta vyanzo vya uhakika vya nishati. Tanzania ina mradi wa kuipa dunia gesi kimiminika, au LNG kwa kimombo, huko Likong’o, Lindi. Mradi huo pia umecheleweshwa kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
Tanzania ina hifadhi ya Gesi Asilia inayofikia mita za ujazo trilioni 57 katika bahari kuu. Makampuni makubwa ya kutoka Norway, Marekani, Uingereza na Uholanzi yaliwekeza mabilioni ya Dola za Marekani kutafuta gesi hiyo kwenye bahari kuu kusini mwa Tanzania.
Sehemu kubwa ya gesi hii imegunduliwa kati ya mwaka 2007-2012. Mradi wa kuzalisha gesi kimiminika ulipaswa kuanza kujengwa mwaka 2014. Mazungumzo ya mikataba yanaendelea mpaka sasa.
Mradi huu ungewezesha Tanzania kuuza nje tani milioni kumi za Gesi Asilia kila mwaka na kuliingizia taifa mapato ya fedha za kigeni yanayofikia Dola za Marekani bilioni kumi.
Mradi huu pia una fungamanisho kubwa haswa wakati wa ujenzi, ujenzi ambao ungegharimu Dola za Marekani bilioni 42 katika kipindi cha miaka takribani saba.
Inatarajiwa kuwa ajira zaidi ya 21,000 zingezalishwa katika mnyororo mzima wa thamani ya mradi.
Kama ilivyo kwa bidhaa za chuma, Tanzania inatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza nje mbolea na gesi ya kupikia, yaani LPG. Mwaka 2024, kwa mfano, zaidi ya Dola za Marekani milioni 400 zimetumika kuagiza mbolea kutoka nje na Dola za Marekani milioni 240 kuagiza gesi ya kupikia.
Malighafi za kuzalisha mbolea na gesi ya kupikia ni uchafu, au by product kwa kimombo, katika uzalishaji na uchakataji wa gesi. Kutokana na mradi huu, Tanzania ingeweza kuwa na kiwanda kikubwa cha mbolea Afrika Mashariki na Kati, na kuuza mbolea kwa mataifa yote yanayotuzunguka.
Vilevile, tungewezesha kuzalisha gesi ya kupikia hapa nchini na kuhakikisha kila nyumba inatumia gesi na kutunza mazingira yetu. Tungeuza gesi ya kupikia kwa nchi zote zinazotuzunguka.
Zaidi ya hapo, hivi sasa Gesi Asilia ina matumizi mengi, ikiwemo kuendesha magari na mitambo ya viwanda ambayo hivi sasa tunatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya magari na mitambo. Tafiti zinaonesha kwamba iwapo Serikali ikiamua kutumia gesi (CNG) kuendesha nusu tu ya magari yake ingeokoa zaidi ya Dola za Marekani milioni 500 zinazotumika kuagiza mafuta ya petroli na dizeli kutoka nje.
Hakika, hasara ya uchelewaji huu sio tu pesa za kigeni tunazotumia kuagiza mafuta, mbolea, gesi ya kupikia, nakadhalika kutoka nje, bali pia pesa za kigeni ambazo tungepata iwapo mradi ungeanza, ikiwemo Dola za Marekani bilioni 11 kila mwaka unaopita bila kutekelezwa mradi huu.
Maelezo hayatoshi
Hakuna linaloweza kueleza vya kutosha kwa nini Serikali ya Tanzania, hususan Serikali za Rais John Magufuli na Samia Suluhu Hassan, zinachelewesha miradi hii ambayo kwa pamoja ingeingiza fedha za kigeni nchini zaidi ya fedha zote za Kigeni zinazoingia sasa kwa mauzo ya bidhaa zote na huduma zote.
Miradi hii miwili ingeingiza kila mwaka Dola za Marekani bilioni 17 kama mapato ya fedha za kigeni, ilhali hivi sasa kwa takwimu za mwaka 2024 Tanzania inaingiza Dola za Marekani bilioni 16. Miradi hii ingeokoa fedha za kigeni tunazotumia kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje. Miradi ingezalisha ajira nyingi sana. Miradi hii ingebadilisha kabisa uchumi na maisha ya watu wa Njombe na Lindi na mikoa jirani.
Miradi hii ingechochea sana kufikia shabaha ya uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja kutokana na multiplier effect yake katika fungamanisho na sekta nyengine za uchumi kama kilimo, viwanda, usafirishaji, nishati ya umeme na hata utalii.
Ni nini kilichonyuma ya pazia kinachopelekea viongozi wetu kutoona umuhimu wa miradi hii?
Zitto Kabwe ni Kiongozi Mstaafu wa chama cha upinzani ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zittokabwe@gmail.com au X kama @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.