The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Serikali Mara Yaendelea Kuhamisha Wananchi wa Nyatwali, Huku Ukiukwaji wa Haki za Binadamu Ukiripotiwa

Serikali inaondosha wananchi hao kupisha uanzishwaji wa ushoroba wa wanyama kutoka Hifadhi ya Serengeti kwenda kufuata maji Ziwa Victoria.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Serikali mkoani Mara inaendelea na zoezi lake la kuwahamisha wakazi takribani 13,000 kutoka kata ya Nyatwali, wilaya ya Bunda kupisha uanzishwaji wa ushoroba wa wanyama kutoka Hifadhi ya Serengeti kwenda Ziwa Victoria, huku wananchi hao wakiieleza The Chanzo kwamba zoezi hilo limeendelea kugubikwa na kasoro kadhaa, ikiwemo uonevu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Taarifa za uhakika zilizokifikia chombo hiki cha habari zinaeleza kwamba mnamo Julai 26, 2025, gari mbili zilizobeba askari 14 wenye silaha kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) zilifika vijiji viwili vya Tamau na Serengeti, ambapo askari hao waliwapiga watu, kuchoma makazi ya wananchi, kuchoma mazizi ya ng’ombe, na kuondoa wanyama eneo la kijiji na kuwatelekeza, miongoni mwa kadhia mbalimbali walizozifanya.

Mwita Mwikwabe Ng’alale, mkazi wa kijiji cha Tamau, alishuhudia kilichotokea kwenye kijiji chake cha Tamau, na kukielezea kile alichokiona kwa The Chanzo, kwa njia ya simu, kama “uonevu” usiozingatia misingi yoyote ya utu na haki za binadamu.

“Mazizi yanachomwa moto, nyumba zinateketezwa,” Ng’alale, 58, alieleza kwa uchungu na huzuni. “Hii siyo haki hata kidogo. Kuna wananchi wamepoteza zaidi ya ng’ombe 25, mpaka hivi sasa hawajui ziko wapi.”

Talugole Maingu, kutoka kijiji cha Serengeti, ambaye ni shuhuda na mwathirika wa vitendo hivyo, amefananisha kile wananchofanyiwa na Serikali na askari wa TANAPA kama vile wao siyo raia, bali wakimbizi kutoka nchi za mbali, akiomba mamlaka husika kuingilia kati kukomesha vitendo hivyo.

SOMA ZAIDI: ‘Hatuna Sehemu Nyingine ya Kwenda’: Wakazi wa Nyatwali, Bunda Walia Kuhamishwa Kwenye Eneo Lao la Asili Bila Kusikilizwa 

“Sasa kwa nini tuondoke wakati eneo hili tuna ng’ombe?” anauliza Maingu, 35, kwenye mahojiano na The Chanzo. “Sisi tumepata vipesa; wengine wanajenga hawajamaliza kujenga. Maana yake pesa ilikuwa ndogo. Sasa ng’ombe tunaenda kuwaweka wapi?”

‘Lazima wahame’

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, alihalalisha vitendo hivyo kwa kuiambia The Chanzo kwamba tayari wananchi hao wameshalipwa fidia kwa asilimia 100, na kwamba kilichobaki ni wao kuhama eneo hilo ili Serikali iweke mazingira mazuri ya wanyama kutoka Hifadhi ya Serengeti kwenda Ziwa Victoria kufuata maji.

Kwa mujibu wa Serikali, hatua hiyo ni muhimu kwani imegundulika kwamba wakati wa Kiangazi, wanyama kama vile tembo hulazimika kuvuka eneo hilo na kufuata maji kwenye ziwa hilo, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na hata makazi ya watu. 

“Wizara ya Maliasili na Utalii imeshalipa fedha zote,” Kaminyoge ameieleza The Chanzo kwenye mahojiano kwa njia ya simu. “Zilikuwa zimebaki [Shilingi] milioni 172 kwa watu 64; Serikali imewalipa. Kilichopo ni kwamba wananchi wahame.”

Hata hivyo, wananchi ambao The Chanzo imeongea nao wameeleza kwamba sababu kubwa kwa nini hawataki kuondoka eneo hilo ni kushindwa kwa Serikali kuwapa eneo mbadala kwa ajili ya makazi na shughuli zao za kiuchumi, kama vile ufugaji.

SOMA ZAIDI: Mauaji, Ubakaji na Vipigo: Simulizi za Kutisha za Mamia ya Wananchi Tabora Waliobaki Bila Makazi Baada ya Serikali Kugeuza Ardhi Yao Kuwa Hifadhi

Wananchi pia wanasema kwamba hawakulipwa vile ambavyo wao wanastahili, kwani eneo lao liko kwenye halmashauri ya Mji wa Bunda ambako wanastahili kulipwa Shilingi 2,000 kwa mita za mraba, lakini Serikali imewalipa shilingi 490 tu kwa kila mita ya mraba. Wananchi wanasema pesa hii haitoshi kwenda kuanzisha maisha sehemu nyingine.

‘Tunatishwa’

The Chanzo ilipowauliza kwa nini mlipokea pesa hizo licha ya kuwa hazikidhi mahitaji yao, wananchi hao walidai kwamba walilazimika kufanya hivyo kwani Serikali ilikwenda ikiwa na askari waliokuwa na silaha, hali iliyowafanya wasaini makubaliano kishingo upande.

“Tunatishwa [kwa] kuambiwa sasa mtu ambaye hatachukuwa fomu asitathiminiwe, basi yeye  ataachwa kama alivyo basi na kuhama munahama,” Ng’alale anasimulia. “Sasa watu wakabisha, wakaona sasa tutafanyeje? Watu wakachukuwa fomu na kutathiminiwa.”

Hata hivyo, Kaminyoge amesema wananchi hao wanapaswa kuondoka, na wataenda kusubiri malalamiko hayo kufanyiwa kazi wakiwa nje ya eneo hilo. Kiongozi huyo wa Serikali alisistiza kuwa wanyamapori kama tembo, nyumbu, na pundamilia wameanza kuingia Nyatwali, na kuwachunga ng’ombe pamoja nao kunaweza kusababisha magonjwa. 

“Lazima TANAPA ifanye utaratibu wa kuhakikisha ng’ombe hawachungwi hapa,” Kaminyoge alibainisha. “Wengi wa ng’ombe hawa wanatoka nje; sio wa mule ndani. Kwa hiyo, eneo hili halitakiwi kuchungia ng’ombe. Sio eneo la malisho.”

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

Haya yote yanatokea wakati ambapo wananchi takriban 500 wa Nyatwali wanakusudia kufungua kesi dhidi ya Serikali kwa kile wanachodai ni kushindwa kwake kwa kuwalinda dhidi ya madhila na ukatili wanaopitia, na kuiomba mahakama iingilie kati kusitisha uonevu huo.

Daudi Mahemba, wakili anayewawakilisha wananchi hao, ameiambia The Chanzo kwamba kwa sasa shauri hilo liko katika hatua ya mwisho kukamilishwa kwa aajili ya kusajiliwa, lengo likiwa ni kupata zuio la mahakama kuzuia kile ambacho kinafanyika kwa wakazi hao kwa sasa na kuruhusu utawala wa sheria ushike hatamu. 


Joseph Kirati ni mwandishi na mtayarishaji wa maudhui wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia Jkiraty14@gmail.com.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×