The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Je, Mbinu Zote za Malezi Yaliyotulea Sisi Bado Zinafaa?

Malezi si mkataba wa kurithishana bila mabadiliko; ni safari ya kukua pamoja na watoto wetu.

subscribe to our newsletter!

Wengi wetu tumekulia kwenye familia za Kitanzania ambapo maneno kama “Mimi ni mama/baba lazima ufanye ninachokambia,” “kati ya mimi au wewe, nani kamzaa mwenzake,”  au “unadhani mimi na wewe ni sawa?” yalikua ni jambo la kawaida. 

Ilikuwa ni misemo iliyojaa uthabiti, heshima, na maamuzi yasiyo na mjadala. Malezi yetu yamekuwa yakijikita kwenye misingi ya kuheshimu wakubwa zetu na nidhamu inayojengwa kwa ukali. Thamani hizi ndiyo zimejenga kizazi chetu sisi.

Lakini nyakati zimebadilika. Sasa tunalea watoto wanaokua kwenye dunia yenye mitandao ya kijamii, taarifa zisizo na kikomo, tamaduni mchanganyiko na changamoto mpya za maisha na malezi. 

Tofauti na zamani, watoto wetu leo wanakutana na maswali magumu mapema zaidi kuanzia shinikizo la rika, mabadiliko ya mwili, hadi matatizo ya afya ya akili. Swali ni, je, mbinu zote za malezi yaliyotulea sisi bado zinafaa?

Tafiti za kisaikolojia zinaonesha kwamba watoto wanaokuzwa kwa mchanganyiko wa nidhamu thabiti na upendo hujenga ujasiri, mawasiliano mazuri, na uwezo wa kufanya maamuzi bora wanapokua. Mfano wa malezi unaoitwa authoritative parenting ambao unachanganya mipaka iliyo wazi na mazungumzo ya wazi umehusishwa na matokeo bora ya kijamii na kitaaluma kwa watoto.

SOMA ZAIDI: Tuwafundishe Watoto Wetu Urafiki Mzuri ni Upi

Lakini sisi Waafrika mara nyingi tumezoea zaidi mtindo wa malezi wa kimabavu, au authoritarian parenting, ambao ni nidhamu kali inayojengwa na maamuzi kutoka juu kwenda chini. 

Ni mtindo uliofanikisha mambo mengi, lakini katika dunia ya leo, tunahitaji pia kuelewa kwamba watoto wanakua vizuri zaidi tunapowapa nafasi ya kueleza hisia na maoni yao bila hofu.

Tanzania tunakabiliana na changamoto za kipekee. Wazazi wengi tunalea watoto wetu katika mazingira yenye shinikizo la kiuchumi, majukumu mengi ya kifamilia, na wakati mdogo wa kuzungumza kwa undani na watoto. 

Pia, mila zetu mara nyingine hutufundisha kwamba kuzungumza kuhusu hisia au masuala ya afya ya akili ni ishara ya udhaifu mtazamo unaoweza kuathiri ustawi wa watoto wetu.

Hata hivyo, tafiti za zinaonesha kuwa mazungumzo ya wazi nyumbani hupunguza hatari ya matatizo ya akili kwa vijana, hasa msongo wa mawazo na wasiwasi. Vilevile, watoto wanaosikilizwa na kupewa nafasi ya kujieleza hujenga ujasiri wa ndani na uhusiano bora na wazazi wao.

Baadhi ya mbinu

Kwa hiyo, ni muhimu wazazi na walezi tuwe na mazungumzo ya kweli na ya mara kwa mara. Si lazima kila kikao kiwe cha masomo au ushauri; wakati mwingine, kuuliza “Umejisikiaje leo?” kunaweza kuanzisha mazungumzo yenye thamani kubwa.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Mtoto Wako Analia Sana?

Tuweke mipaka na maadili, lakini pia kueleza sababu za hiyo mipaka. Watoto wanapofahamu “kwa nini” nyuma ya sheria tunazotunga, wanaheshimu zaidi mipaka hiyo.

Tuheshimu hisia za watoto wetu.  Badala ya kusema “utazoea tu” pale tunapofanya jambo linaloweza kudhuru hisia zao, tunaweza kusema, “Naona umekasirika, hebu tuzungumze.” Hii inajenga ufahamu wa kihisia na heshima kwa pande zote.

Tujifunze kubadilisha mitazamo yetu. Dunia ya watoto wetu si sawa na ile tuliyokulia sisi. Tukijifunza kubadilisha mitazamo yetu kuhusu changamoto zao, ikiwemo teknolojia na mitandao ya kijamii, tunawasaidia kushinda mitihani ya maisha kwa uelewa zaidi.

Malezi si mkataba wa kurithishana bila mabadiliko; ni safari ya kukua pamoja na watoto wetu. Tunaweza bado kushikilia misingi ya heshima na mshikamano wa jamii, huku tukijifunza kusikiliza, kuelewa na kufundisha kwa upendo.

Kwa kufanya hivyo, tunaunda kizazi kinachothamini asili yake, lakini pia kimejiandaa kukabiliana na changamoto za dunia ya leo. Na labda, miaka ijayo, watoto wetu watakapokumbuka misemo ya utotoni, badala ya “Kwa sababu tumesema,” watasema, “Kwa sababu tulizungumza, tukakubaliana” ndiyo maana tumefikia hapa.  

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×