The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Uchaguzi Mkuu 2025: Fursa ya Kubadili Maisha ya Vijana Tanzania

Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni zaidi ya tukio la kisiasa; ni fursa ya kuandika upya historia ya taifa.

subscribe to our newsletter!

Leo, Agosti 12, 2025, dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana. Hii ni siku maalum ya kutambua mchango wa vijana katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Kauli mbiu ya mwaka huu nchini Tanzania ni “Kuelekea 2030: Tanzania ya viwanda – Boresha elimu kwa vijana kwa maendeleo ya taifa.”

Siku hii ni zaidi ya kumbukumbu; ni tafakuri ya nafasi ya vijana katika mustakabali wa taifa. Nchini Tanzania, kundi hili ndilo nguvu kuu ya idadi ya watu na rasilimali muhimu isiyo na kifani. Lakini, je, vijana wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayogusa maisha yao?

Takwimu zinaonesha kuwa vijana wa umri kati ya miaka 15 na 35 ni takribani milioni 21.9, sawa na asilimia 34.1 ya Watanzania wote. Kwa jumla, watoto na vijana wanaunda asilimia 77.5 ya idadi ya watu nchini. Kwa lugha rahisi, Tanzania ni taifa la vijana.

Hata hivyo, changamoto ni kubwa. Kila mwaka, zaidi ya vijana milioni moja huingia kwenye soko la ajira, lakini ni takribani 100,000 pekee ndiyo hupata ajira rasmi. Ripoti ya hali ya ajira ya mwaka 2023 inaonesha kuwa idadi ya wote walioajiriwa kwenye sekta rasmi ni milioni 3.6 pekee, huku zaidi ya milioni 31 wakiwa hawana ajira, au wakiwa katika ajira zisizo rasmi.

Vijana wengi wamejikuta wakitegemea shughuli zisizo na uhakika wa kipato kama bodaboda, biashara ndogondogo, au kazi za vibarua. Wakati huohuo, sekta zinazokua zaidi mara nyingi hazina uwezo wa kutoa ajira nyingi, jambo linaloongeza pengo la kipato kati ya matajiri na vijana wengi masikini.

SOMA ZAIDI: Mchakato Uchukuaji Fomu CCM Washika Kasi: Vijana CCM Wajitosa Majimbo ya Mawaziri 

Swali kuu ni: Vijana wafanye nini ili kushika hatamu za maendeleo ya taifa lao?
Jibu ni moja tu: Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Kupitia ushiriki wa moja kwa moja katika uchaguzi, vijana wana nafasi ya kuwachagua viongozi wanaotambua changamoto na ndoto zao, kuamua sera zitakazogusa ajira, elimu, teknolojia na huduma za kijamii, na kujenga ari ya uongozi na ushawishi wa kisiasa miongoni mwao.

Licha ya umuhimu huo, takwimu za UNESCO za mwaka 2022 zinaonesha kuwa takriban asilimia 40 ya vijana hawashiriki katika uchaguzi. Wengi wanaamini kura yao haina thamani, huku changamoto kadhaa zikitajwa.

Hizi ni pamoja na hofu ya vurugu wakati wa chaguzi, vikwazo vya kikatiba vinavyowazuia kugombea licha ya kuhitimu kupiga kura, ukosefu wa elimu ya uraia na uhamasishaji endelevu, mitazamo ya kitamaduni inayowapokonya vijana nafasi ya kufanya maamuzi na changamoto za kiuchumi zinazowafanya baadhi kutoona tija ya kushiriki.

Changamoto hizi hazipaswi kuwatisha vijana bali ziwe ngazi ya mabadiliko. Kura moja inaweza kubadili sera ya elimu, afya, miundombinu, na uchumi. Kukosa kupiga kura ni kukabidhi mustakabali wa taifa mikononi mwa wengine.

SOMA ZAIDI: Vijana Wenzangu, Tusiruhusu Kisingizio Chochote Kituzuie Kushiriki Kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Mkuu 

Mwanafalsafa wa Kigiriki, Plato, aliwahi kusema: “Moja kati ya adhabu za kukataa kushiriki siasa ni kutawaliwa na watu wasio bora kuliko wewe.”

Kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi, vijana wanaimarisha demokrasia, uwajibikaji na uwazi wa uongozi. Wanatoa sauti kwa mahitaji ya kizazi chao na kuhakikisha yanazingatiwa katika ngazi zote za maamuzi.

Kesho bora ya Tanzania inategemea kura ya kijana leo. Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni zaidi ya tukio la kisiasa; ni fursa ya kuandika upya historia ya taifa. Vijana wanapaswa kujitokeza, kupiga kura, na kulinda kura zao. 

Kesho bora ya Tanzania inategemea maamuzi ya kura moja ya kijana leo; ni muda wa vijana kufanya maamuzi sahihi yatakayoiweka nchi yetu katika ramani.

Ruqayya Nassir ni Naibu Katibu Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Taifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ruqayyanassir95@gmail.com au X kama @RuqayyaNassir. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×