The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kwa nini Mwaka wa Uchaguzi 2025 ni wa Kihistoria na Sababu za Hitaji la Muafaka wa Kitaifa Kabla ya Uchaguzi

Nadhani kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na muafaka wa kitaifa, muafaka kama ule uliofanyika mwaka 1960 miezi mitatu kabla ya uchaguzi.

subscribe to our newsletter!

Kusoma kurasa za nyakati za kihistoria ni tofauti na kuziishi. Ukisoma kuhusu nyakati za kihistoria za furaha, hakuna sentensi au aya zinazotosheleza kukuelewesha hisia zilizokuwepo kwa uthabiti wake. Vivyo hivyo, ukizisoma nyakati ngumu za kihistoria zinazoandikwa kwa machozi na damu, mstari mmoja, aya, au kurasa kwenye kitabu cha historia kuhusu maumivu ni tofauti kabisa na  uhalisia, ni vigumu wino kuweza kutafsiri uzito wa hisia za nyakati za kihistoria.

Ninaamini katika mwaka 2025 tuko katika moja ya mwaka wa uchaguzi wa kihistoria; uchaguzi ambao utaenda kuunda au kubadili hatma ya taifa letu katika namna ambayo itagusa walau vizazi vinne vijavyo. Makala hii imekuwa ndefu kidogo, kwa ufupisho nitaeleza mambo kadhaa kwa nini huu ni mwaka wa uchaguzi kihistoria, halafu nitaelezea zaidi:

Kwanza, nii uchaguzi wa kihistoria kwa sababu kurasa za nyakati zetu zitarekodi kama uchaguzi wa kwanza kufanyika baada ya Rais kufariki akiwa madarakani. Aliyekua Makamu wa Rais akawa Rais baada ya kifo cha Rais sasa anaenda kuongoza kampeni za kuwafikia wananchi ili kuchaguliwa, kila maamuzi anayoyachukua sasa ndiyo itakayokuwa kumbukumbu yake kwa vizazi vijavyo.

Pili, ni uchaguzi wa kihistoria kutokana na kuwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani na mgombea wa Urais aliyepita yupo gerezani kwa kesi ya uhaini. Ni uchaguzi wa kihistoria kwa sababu, kwa mara ya kwanza, chama kikuu cha upinzani kimesema hakitashiriki uchaguzi katika mazingira yaliyopo. Chama hiki kimeenda mbali na kufanya kampeni ya watu kutoshiriki uchaguzi. Katika uchaguzi huu, nategemea kama utaendelea kwa namna unavyoendelea, kuna watu wengi watakaochagua kutochagua, hasa kwa kutoamini mifumo ya uchaguzi. Hili lina uzito wake juu ya uhalali wa kisiasa, imani juu ya mifumo ya kisiasa na hata umoja wetu.

Tatu, kila uchaguzi huwa una mambo makuu. Naamini katika uchaguzi huu mambo makuu ni mawili. Kwanza, thamani ya uhai katika nchi yetu na pili ‘Ujamuhuri wetu,’ nikimaanisha nafasi ya sisi wananchi kuamua mambo; kama bado ipo. Hata hivyo, naamini kwa hatua za awali za uchaguzi zinazoendelea mambo haya hayatapewa kipaumbele, na hivyo kutakua na ufa mkubwa kati ya matarajio ya wananchi, na kitu wanasiasa wanachokiwasilisha. Yaani, wanasiasa watakuwa na mambo yao na wananchi watakuwa na mambo yao.

Nne, kuna  viashiria vingi kuwa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), hakiamini, au hakioni thamani tena katika demokrasia ya vyama vingi, na hapa sijasema haiamini katika demokrasia.

Tano, mabadiliko ya kimataifa kutoka siasa za ushawishi mpaka siasa za wenye nguvu na mabadiliko ya kisiasa katika ukanda wetu, Afrika Mashariki, ikiwemo mahusiano mabaya ya raia na wenye madaraka ni mlango unaoruhusu siasa za kimataifa kuwafanya viongozi wa ukanda wetu kuwa viongozi jina; wakiendeshwa huku na kule na mataifa makubwa, hili ni jambo la nyakati za kihistoria.

Andiko hili nimeligawa kwa kuangalia wahusika wakuu, na matukio muhimu, au hali muhimu zinazofanya uwe mwaka wa kihistoria. Nitaanza na CCM pamoja na vyama vingine. Katika matukio nitaelezea ‘Uhunzi wa Jamii,’ au social engineering kwa Kiingereza.

Hii tunaweza kuita ni kama kionjo muhimu kinachotuonesha mwisho unakuwaje, na mwisho tutamalizia na wahusika wa ziada; na mwisho kabisa nitatoa mtazamo wangu wa kwa nini nadhani kuna umuhimu wa muafaka wa kitaifa kabla ya tarehe ya uchaguzi, hoja ambayo naamini kwa sasa haipewi nafasi.

Chama tawala

Mwaka 2017, shirika lisilo la kiserikali la Twaweza lilipotoa utafiti wake na kuonesha kuwa CCM ilikuwa ikikubalika kwa asilimia 65, ilileta mjadala mkali, vyama vya upinzani vikipinga hasa sababu chama kikuu cha upinzani CHADEMA kilikua na asilimia 17 ya kukubalika, kikishuka kutoka asilimia 32 ya mwaka 2013. Kitu ambacho hakikujadiliwa ni kuwa sio CCM ilionekana kuwa maarufu, ilionekana pia kuurudisha umaarufu uliopotea, kwa sababu 2013 na 2014, ilikua imeshuka mpaka asilimia 54.

Nadhani kulikua na umuhimu mkubwa wa kujiuliza CCM, kama chama tawala, kiliwezaje kurudisha umaarufu, na wakafanikiwa. Kwa Afrika, kwa wakati huo, CCM ilikua inatenda miujiza ya kisiasa, hasa kwa kuwa utafiti ule ulikua ni huru na sio wa kubumba.

Sababu kubwa tunayoweza kuielezea ya jambo lile kwa kimombo tunaweza tumia lugha ya Statecraft. Huu ni utaalamu wa kuendesha dola. Neno hilo linabeba dhana ya utalaamu, ubunifu na hata uwezo wa kwenda na nyakati katika uendeshaji wa dola.

Nitatoa mifano kadhaa ya haraka haraka juu ya hoja hii ya Statecraft. Kabla ya 1992, CCM ilipitia vipindi kadhaa vya majaribio hasi. Kwa mfano, mwaka 1969, baadhi ya viongozi waandamizi wa TANU walituhumiwa kutaka kufanya mabadiliko ya kutumia nguvu. Vivyo hivyo mwaka 1982, kulikuwa na jaribio lingine, hili lilikuwa karibu zaidi kufanikiwa. Baada ya hapo kulifanyika mabadiliko makubwa, ikiwemo kwanza kuwekwa kwa ukomo wa uongozi na pia kubadili uongozi.

Badiliko kubwa zaidi ni CCM kujiweka katika hali ya kubadilika. Hii tuliiona mwaka 1992 kwa kuingia kwa vyama vingi ambavyo kimsingi ni suala lililolosukumwa moja kwa moja na Mwalimu Julius Nyerere, baada ya msukumo wa muda mrefu wa wana-mageuzi nje ya CCM. Na waliendelea kujifunza. Kwa mfano, baada ya idadi ndogo zaidi ya watu kujitokeza kupiga kura mwaka 2010, na skendo kadhaa zilizotikisa uhalali wa chama hicho, CCM iliridhia mchakato wa Katiba Mpya, huku ndani ya chama ikija na programu kadhaa za kujibadilisha.

Hata hivyo, kuanzia mwaka 2016 kuendelea, CCM ilichukua mwenendo wa mabadiliko kadhaa katika chama hicho ambapo kuna viashiria vingi vinaonesha Statecraft katika chama hicho imeendelea kupotea. Baadhi ya mambo yaliyotokea ni pamoja na kuona  siasa za ushawishi kupotea, huku siasa za ubabe zikitukuzwa. Ndipo hapa tuliona vijana wengi waliofanikiwa kuchanja mbuga kisiasa ni wale waliokuwa wababe na hata wenye mawazo, kauli na misimamo tata ya kikatili dhidi ya Watanzania wenzao.

Kutoka wakati huo tunaona mabadiliko kutoka kwenye kuwa na ubunifu wa siasa, utaalamu wa siasa mpaka kutegemea mikakati ya kiusalama kwa asilimia kubwa kama nyenzo ya kutimiza malengo ya kisiasa. Katika zama za uongozi wa Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan, kulikua na jitihada za kurudisha siasa za ushawishi. Hata hivyo, jitihada hizo zilififia na kupotea kabisa kuanzia nusu ya pili ya mwaka 2023 kuendelea mbele.

Hali hii ya matumizi makubwa ya mikakati ya kiusalama kutimiza malengo ya kisiasa inatufanya tuishi katika nyakati za kipekee na za kihistoria. Wanasiasa wanafanya siasa, wanaifahamu siasa na wanatatua mambo kisiasa, na msingi wa nguvu ya dola unakuwa ni siasa za kiraia. Uzoefu wa kihistoria unaonesha nyenzo za kiusalama zinapotumika kwa muda mrefu kutimiza malengo ya kisiasa matokeo ya muda mrefu huwa ni tofauti kabisa kwa jamii na hata kitovu cha madaraka hubadilika.

Moja ya mabadiliko ambayo kwa sasa tunaanza kuyaona ni juu ya chaguzi zetu. Kwa muda mrefu, nyakati za uchaguzi, pamoja na mapungufu yake, kulikua kuna hali kwamba kuna kuchagua. Hata hivyo, mwaka 2019 na mwaka 2020, mambo yalibadilika; si mara moja au mbili viongozi waandamizi wa CCM wamekiri mambo hayakuwa sawa. Ni katika hali hii, baadhi ya Wabunge walieleza nafasi zao za Ubunge ni zawadi waliyopewa na Rais John Magufuli.

Nukuu ya Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, Aprili 13, 2021.

Ni wengi pia  wanategemea tena kupata zawadi ya nafasi hizi kuchaguliwa kama wakipita kwenye mchakato wa ndani wa chama tawala. Haya ni mabadiliko ya kipekee. Ndipo hapa nakuja katika hoja kuwa kuna hali ninayoiona ndani ya CCM ya kuacha kuamini katika siasa za vyama vingi; ingawa, kwa mtazamo wangu, naamini CCM ni wanufaika wakubwa wa siasa za vyama vingi kama ambavyo Watanzania wengine walivyonufaika. Toka vyama vingi vilivyoingia, watu wakikasirishwa ndani ya CCM huhamia vyama pinzani; na maisha huendelea, kabla ya hapo ndipo tulipoona majaribio kadhaa hasi.

Hali hii inafanya uchaguzi wa ndani wa CCM kuwa wa muhimu sana. Tunaona mwezi Januari 2025, CCM ilibadili Katiba yake kuongeza wigo wa wapiga kura ndani ya chama hicho. Mabadiliko haya yanaendana na yale ya 2010, yaliyokuja kufutiliwa mbali, ingawa kwa sasa kuna maboresho ya kitaalamu. Kiufupi, tunaweza kusema maboresho ya Januari 2025, ni kama kutengeneza mazingira ya kuwa na uchaguzi ndani ya uchaguzi. Kwa mustakabali wa chama hicho, hili ni jambo zuri na Stephen Wasira, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), aliliongelea kwa undani suala hilo akiwa Mwanza mnamo Februari 11, 2025.

Nukuu ya Stephen Wasira kutoka kwenye mkutano wa hadhara Februari 11, 2025.

Ninaweza kusema mabadiliko haya, kwa maoni yangu, ni kama ‘Jaribio la CCM,’ yaani experiment. Naamini CCM, walivyoangalia mambo ni kuwa kama kutakuwa na ushindani wa kutosha ndani ya CCM, kiu ya wananchi kupata watu wanaowataka itakatwa hata kabla ya uchaguzi.

Hivyo, hakutakuwa na usumbufu mkubwa namna uchaguzi utakavyokuwa sababu  watu wanaopitishwa tayari wamepimwa, wakapimika. Ninaamini hata hatua ya CCM kubadili katiba tena kwa dharura Julai 26, 2025, na kuongeza majina ya wanaokwenda kwenye kura za maoni kuwa zaidi ya watatu ni moja ya jitihada za kuleta ushindani katika hatua za ndani za chama hiki.

Kama kura za maoni za CCM zingeenda, kama ambavyo ilivyoandikwa kwenye vitabu vya kanuni, basi tungeweza kusema CCM experiment imefanikiwa, yaani kuwa na uchaguzi ndani ya uchaguzi. Hata hivyo, mwenendo wa kura za maoni unaonesha hili halijawezekana kwa kiwango kikubwa, kuanzia tuhuma za rushwa, kuharibika michakato, kura feki, fujo mpaka watia nia kupotea na tuhuma za wengine kutekwa. Inaonekana mambo yote yanayotokea kwenye uchaguzi mkuu yametokea kwenye uchaguzi wa CCM.

Na nitaeleza sababu ya hili kutokea. Kutokana na hali inayoonekana CCM kuwa na mkono wa juu katika uchaguzi rasmi, hasa baada ya yaliyotokea 2019, 2020 na 2024, shinikizo kubwa limehamia kwenye uchaguzi wa ndani wa CCM, kwa sababu inategemewa anayepita hapo atapata ‘zawadi ya kuchaguliwa.’

Nukuu kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido | Septemba 01, 2024

Kama mchakato wa uchaguzi rasmi ungetegemewa kuwa walau kama ulivyokuwa kabla ya 2015, wengi wangejua ukipita CCM haimaanishi umepita. Ni vigumu CCM kuwa na chaguzi nzuri kuliko chaguzi rasmi za kitaifa. Unaweza kujaza kikombe kwa maji ya bahari, lakini huwezi kutengeneza bahari kwa maji ya kikombe!

Kwa ufupi, kwa mhusika wa kwanza katika makala hii ninaweza kumalizia kwa kusema kuna viashiria vikubwa CCM haiamini tena katika demokrasia ya mfumo wa vyama vingi. Narudia tena, sijasema haiamini katika demokrasia, na kwa sasa binafsi naona iko katika hatua za kwanza za kujaribu kutafuta suluhu ya mbadala wa demokrasia ya vyama vingi na hili ni jambo la kihistoria.

Uhunzi wa jamii

Nadhani ungetegemea sasa nizungumzie vyama vya upinzani. Hata hivyo, fuatana nami kwanza kwenye suala la uhunzi wa jamii, na nitaelezea pia vyama vingine.

Mpaka leo bado kuna mjadala kwa nini vyuoni kuna masomo yanaitwa sayansi za kijamii, sayansi za siasa. Hata hivyo, ukubali, ukatae, namna jamii ilivyo, mambo tunayoyaita kuwa tamaduni, hulka na silka za jamii haya ni mambo yanayojengeka na kuwa kawaida baada ya maamuzi fulani kufanyika, ni uhunzi ambao haushikiki, hauonjeki, haunusiki, lakini tunauishi na unaathiri kila kitu kwenye maisha.

Nitakupa mfano wa hoja ya uhunzi wa jamii kabla sijaendelea mbali. Mfano wa kwanza ni Tanzania na matumizi ya Kiswahili. Tumejikuta tunatumia Kiswahili kama lugha yetu, hata hivyo hii haikushuka kama mana, ni maamuzi yaliyofanyika kutokana na umaarufu wa lugha hii kama lugha ya biashara. Maamuzi hayo ni kwanza, wakati wa ukoloni wa Ujerumani, baada ya kuona Kiswahili kuwa ni lugha inayoweza kutumika kwa shughuli zao, wakakirasimisha kuitumia shuleni na kuweka ma-akida maeneo mbalimbali walioongea Kiswahili.

Hata hivyo, bado haikua lugha iliyosambaa kona zote kwa asilimia 100, mpaka maamuzi yalivyofanyika baada ya uhuru kuisambaza, kuifundisha na kuipa kipaumbele. Binafsi na wenzangu wa umri wangu hatujui tena lugha za makabila zetu kama wazazi wetu walivyokuwa wanajua, uhunzi kamili wa jamii umefanyika na umetimia.

Nimetoa huu mfano ili iwe rahisi unielewe ninapoizungumzia hii nadharia ya uhunzi wa jamii, au kwa kimombo social-engineering. Kuna matukio, au nadharia kadhaa ambazo ziko katika jamii yetu ambayo naamini tunapitia katika nyakati za social-engineering, uhunzi wa jamii kwa namna ambayo tunabadilisha jamii yetu kwa namna ya kihistoria.

Ukisoma kitabu cha Aili Mari Tripp anachomdadisi Katibu na msaidizi binafsi wa Nyerere, Joan Wicken, utaona anaeleza baada ya Nyerere kurudi kutoka China anasema alikua makini au alishtuka na namna alivyoona Mao alivyokuwa akitukuzwa China, alijaribu kubadili hili, na tunaweza kusema alifanikiwa kwa kiasi.

Hata leo naamini, anavyokumbukwa anaheshimika lakini hatukuzwi. Na matukio kadhaa yalisababisha haya mfano kuomba radhi kwa umma juu ya kuvunja serikali za mitaa, na hata mara kwa mara kushindwa kupata anachotaka, ikiwemo mrithi aliyemtaka; haya yote yalijenga utamaduni wa kuwa na viongozi tunaowaheshimu lakini wanabaki kuwa watu wetu sio miungu.

Kuanzia 2016 mpaka sasa, kumekuwa na msukumo mkubwa sana wa kuwatukuza viongozi wakuu wa nchi; msukumo huu umeenda sambamba na kutengeneza kasumba ya watwana au kwa lugha iliyozoeleka sasa machawa. Kwamba inafanyika ni lazima na ni hitaji la msingi raia kuwasifia viongozi, na inaelekea hata kuwa hata hatari pale usipofanya hivyo. Hali hii ni ya uhunzi wa jamii.

Na kuna jambo ambalo limezua mjadala ndani ya CCM, juu ya siasa za kurithishana. Sasa ukijumlisha huu uhunzi wa kuwapa hadhi ya utukufu, hata hadhi ya kuwaabudu viongozi wetu, na siasa za kurithishana, kama huu ndio uelekeo, naamini tuko katika nyakati za kihistoria; nyakati ambazo tunaweza baada ya muda kugeuka nyuma na kusema, hapa ndipo tulipobadilika. Endelea kufuatana nami nitakupa hitimisho, juu ya haya na uhusiano wa nyakati za kihistoria.

Kuna uhunzi mwingine wa jamii unaendelea, matukio ya utekaji na watu kupotezwa na kupotea. Hata kama tukijifanya kuigiza, hili ni jambo ambalo lipo juu kabisa kwenye ubongo wa Watanzania wengi. Wazazi wana hofu juu ya watoto wao, wake wana hofu juu ya waume zao, marafiki wana hofu juu ya wapendwa wao.

Matukio haya yameendeelea kutengeneza hofu, na kutokana na kuhusishwa na masuala ya siasa, matukio haya yameanza kuunda upya jamii yetu kwa namna ambavyo tunabadilika kabisa. Kwanza, kuna muitikio wa wale wanaojitenga na kuhimizana kuachana na siasa, hasa kutokulalamika au kuongea chochote kwa namna ambayo itawaudhi wenye nguvu. Kwa hapa jamii yetu inagawanyika mara tatu, wako wanaoingia katika kundi la kwanza, la kusifia  na wako wanaoamua kunyamaza kabisa na kunyong’onyea kukubali lolote linalowakumba.

Hata hivyo, kunaibuka pia mazungumzo ya watu wanaoanza kuona sababu kubwa ya matukio haya kuwatokea wao na wapendwa wao ni kwa sababu wanaonekana  ni dhaifu wanaweza kufanyiwa chochote; yaani wako kama swala mbele ya simba, ndipo hapo unaanza kuona lugha ya kuanza kuhimiza kujilinda, na hata lugha za visasi.

Huu uhunzi wa jamii kupitia haya matukio ya utekaji na watu kupotea, unafanya nyakati hizi ziwe za kihistoria sababu zinatengeneza mazingira yasiyotabirika kwa kila mtu kwa picha ya muda mrefu. Hakuna anayeweza kutabiri jamii itakavyokuwa kwa uhakika, ila jambo la msingi ni hakika haya matukio yakiendelea jamii yetu haitakua ilivyokuwa.

Nukuu ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akikabidhi vifaa kwa Polisi, Oktoba 10, 2024

Moja ya dalili za mwanzo ni mfano watu kusherehekea waziwazi viongozi wanapokumbwa na mabaya hasa kifo, kwa kawaida, Watanzania huangalia kifo kwa jicho la upole, huruma, unyenyekevu iwe kwa unafiki au kweli; ila kushangilia kwa nderemo na vifijo ni jambo jipya.

Jambo la tatu ni kampeni ya CHADEMA ya No reform, No Election, kampeni hii wakati ni ya muda mrefu, msingi wake hasa na muelekeo wake uliochukua ni baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024. Uchaguzi wa serikali za mitaa naweza nikasema lilikua ni kosa la kimkakati la CCM, kwa namna yeyote ile, CCM walikua wana uhakika wa kushinda kati ya asilimia 55 mpaka 70 kwenye ule uchaguzi, na hii ni kwa sababu ndio chama pekee chenye mtandao mpana wa uchaguzi kuliko chama chochote.

Maamuzi yaliyofanyika, kuendesha uchaguzi namna ulivyoendeshwa, ulifungua mtiririko wa matukio ambayo, hata pamoja na nyenzo nyingi zilizopo, imekuwa ngumu kwa CCM kuwa na udhibiti wa kisiasa, na hata kimkakati, imejikuta ikilazimika kuitika (ku-react) kwenye mambo mengi.

Nataka nikukumbushe msomaji moja ya kichekesho kuwahi kutokea katika siasa za upinzani, kabla sijaendelea na hoja hapo juu. Kichekesho hiki ni kile kilichotokea mwaka 2014, ambapo Mbunge wa Vunjo Augustine Mrema, alisimama Bungeni kuuliza kama Rais Jakaya Kikwete ambaye alimtaja kuwa ni rafiki yake kama hampendi tena, hii ni baada ya Rais Kikwete kumteua James Mbatia kama Mbunge.

Kwa vyama vya upinzani hii si picha nzuri, inaonesha upinzani unaoendeshwa na chama tawala, lakini kama tukiitazama hili jambo la Mbatia na Mrema kwa macho ya chama tawala, utawapa sifa yao; kuwaendesha wapinzani bila kutumia nguvu ya mabavu, upewe nini tena? Sio tukio hili, na matukio mengi yanaonesha CCM kama chama tawala, kiliweza au kimeweza kutengeneza mikakati na mbinu mbalimbali za kuweza kuendesha upinzani na hata kuruhusu upinzani ambao hauathiri maslahi yake kwa ukubwa.

Sasa tuendelee na mtiririko tuliouanza huko juu, baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, mambo yalibadilika; hasa kwenye chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, uongozi uliokuwepo ukaondolewa na misimamo ilichokuliwa baada ya hapo, tunaweza kusema ilikua tofauti kabisa. Matukio mengi yaliyotokea mpaka leo, yameonesha mahusiano ambayo CCM iliweza kuyajenga ndani ya chama hicho yamevurugika kabisa.

Kampeni ya CHADEMA ya No Reform, No Election, pamoja na kuelezea madai juu ya uchaguzi, unaona pia ina uwezo mkubwa wa kuiunda jamii kwa namna moja au nyingine kutoka misimamo ya kawaida, mpaka kuwa na misimamo mikali, hasa ukijumlisha na matukio yaliyoizunguka.

Ni kawaida katika nyakati za uchaguzi watu kutojitokeza kwa sababu mbalimbali wengi huwa ni uvivu, hali ya hewa, na pia sababu za kisiasa. Na suala la watu kujitokeza, CCM hufanya utafiti wake wa ndani na utafiti ambao CCM iliufanya baada ya watu wengi kutojitokeza kwenye uchaguzi wa 2010 ilionekana sababu kubwa zilikua za kisiasa, yaani kukatishwa tamaa na mwenendo wa chama hicho.

Utafiti wa CCM

Hata hivyo, pamoja na malalamiko ya upinzani, hakukua na sababu yeyote ambayo kwa ujumla ingewezekana kuweka mashaka ya kudumu juu ya uhalali wa mgombea wa CCM aliyeshinda uchaguzi. Tofauti na wakati huu, wakati wa sasa, chama kikuu cha upinzani kimeamua kuweka chaguo ambalo liko wazi kwa wanachama na wafuasi wake, yaani kuchagua kutochagua. Hii ina athari kubwa na ya msingi juu ya uhalali wa kisiasa katika uchaguzi huu, wote ambao hawatajitokeza itahesabiwa ni kwa sababu wamechagua kutochagua.

Kuna wengi ambao nyakati za uchaguzi husukuwa kwenda kupiga kura kwa hamasa ya kampeni, kwa sasa watakutana na hamasa zingine pia.

Katika historia ya chaguzi zetu za vyama vingi, sidhani kama kuna wakati uhalali wa kisiasa umewahi kuwa wa muhimu kama mwaka 2025. Hii ni kwa sababu ni wakati pekee katika historia ya Tanzania, nchi inaenda kuchagua Rais baada ya Rais aliyekuwepo kufariki madarakani. Ukiacha kampeni hii ya No reform, no election, dalili zinaonekana suala la uhalali wa kisiasa litakuwa na mjadala mpana baada ya uchaguzi kwa ujumla na hata ndani ya CCM.

Inawezekana imekuwa ngumu kunifuatilia ninaeleza nini kuhusu uhunzi wa jamii unaotokea basi nitaweka sawa tena. Kwanza jamii yetu iko au inaelekea katika nyakati ambayo yanajengwa mazingira ya kuwatukuza viongozi wetu, watu wetu kwa namna ambayo tuanze kuwaona kama miungu, ikimaanisha sheria, kanuni na katiba zetu hazina maana, katikati ya hii hali utekaji na upotezaji wa watu unaingia ili kuwatia watu hofu.Upande wa pili tunaona moja kuna watu wanaanza kuiangalia hali ya kutekwa na kupotezwa katika jicho la kujihami, na pili tunaona kuna kampeni za kunyima uhalali watu wenye madaraka.

Hizi pande mbili zote zinaelekea kuwa uhunzi wa jamii iliyogawanyika. Tukirudi kule juu, ambapo nilieleza, kama njia za kiusalama zikitumika kwa muda mrefu kutimiza malengo ya kisiasa, kitovu cha madaraka hubadilika; chochote ambacho tunakijenga kwa sasa kwenye jamii yetu, kwa hakika ni kikombe cha mashaka na wasiwasi. Mbaya zaidi, tayari tumeanza kuyaangalia baadhi ya matatizo tuliyonayo kwa jicho la Utanganyika na Uzanzibari, na wengine wanaona mlolongo wa ukosoaji labda una msukumo pia wa kidini. 

Kuna kujidanganya kuwa baada ya uchaguzi, tutatafuta muafaka, tutaanza mchakato wa Katiba mpya. Uzoefu wa kihistoria unaonesha, watu wenye madaraka wanapokabiliwa na msongo wasiwasi juu ya kukubalika na uhalali madaraka yao uwe wa kufirika, kuhisika au kweli, kinachofuata mara nyingi ni matumizi makubwa ya nguvu na ubabe; ndivyo ilivyokuwa Haiti, Sovieti na hata kwa majirani zetu Malawi na Uganda.

Tanzania katika jamii za Kimataifa

Mwanzoni nilieleza nitaiweka hii makala kwa kuwaelezea wahusika mbalimbali, nikaanza wa karibu zaidi na sasa naenda kwa wahusika wa mbali, mambo yote haya yanaungana mwishoni.

Mara nyingi kwa uzoefu wetu wa kihistoria tunaona kwamba mataifa yanayoathiri au yanayoweza kuathiri uelekeo wetu wa kisiasa na hata kiuchumi  ni Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Urussi, China; tunatumiaga mara nyingi Mashariki na Magharibi. Huku mataifa ya karibu hasa Afrika Mashariki tukiyaangalia kwa jicho la majirani yaani, ya kwao yetu na yetu yao.

Moja ya utofauti ambao tunauona katika ulimwengu wa kimataifa kwa sasa ni kuwa mataifa makubwa yanabadili uelekeo wa siasa zao kutoka siasa za ushawishi mpaka siasa za mabavu. Yaani mwenye nguvu za kijeshi au za kiuchumi akisema ruka, unatakiwa kuruka au la sivyo utakiona cha mtema kuni.

Kwa mataifa kama Tanzania, uzoefu wa kihistoria unaonesha tuko katika wakati mbaya zaidi kuwa na jamii iliyogawanyika. Moja ya jambo ambalo lililo-ilinda serikali ya awamu ya kwanza, kwa kiasi kikubwa hasa katikati ya msongo wa kimataifa ni kuwa, watu wake waliiamini, waliamini uthabiti na nia ya viongozi wao; sio kwa sababu ya matukio ya kutekwa au kupotezwa, waliamini viongozi wao na viongozi wao walifanya jitihada kuitikia malalamiko na kurekebisha wanapokosea.

Uzoefu unaonesha hata mataifa rafiki kwa sasa, huangalia mambo kwa namna ambayo hakuna mtu anayetaka kuhangaika saana na matatizo ya wengine, hata pale inapoonekana kuna maslahi ya msingi. Mfano tumeona DR Congo, ambapo China ina uwekezaji mkubwa kuliko nchi yeyote, ngoma ilipohitaji mchezaji, hakutaka mikono yake kuchafuka saana. Na sababu kubwa ni kuwa katika hali yeyote mbaya na nzuri, mataifa makubwa yanaweza kufanya kazi popote.

Sasa kuna nadharia za pande mbili hasa kwenye siasa za kimataifa ambazo naamini ni za mashaka katika nyakati hizi. Kwa wadau wengi wenye nafasi za madaraka, wanaamini, unaweza kukorofisha uhusiano na wananchi ndani hasa kwenye masuala ya msingi ya uhusiano kati ya wananchi na wenye dhamana, na ili kupata uhalali wa kimataifa ukakimbilia kwa China na Urusi, hasa mataifa mengine yakikubagaza.

Lakini kuna nadharia pia kwa wadau wa vyama vya upinzani kwamba kunaweza kuwa na mshikamano wa kidemokrasia kimataifa pale haki za kibinadamu zinapominywa. Nadhari zote hizi mbili naamini zina ukweli kiasi, hata hivyo sio za kutegemea katika dunia ya sasa.

Kwa watu wenye madaraka, unahitaji watu kuwa upande wako sasa zaidi ya wakati mwingine kwa sababu mataifa yote makubwa, bila kujali upande, kwa sasa wakipata nafasi ya kufanya taifa moja kuwa taifa kikaragosi, wataichukua, na hakuna namna rahisi ya kupoteza mamlaka ya nchi, kama kukosa uhalali ndani na kutegemea uungwaji mkono wa nje. Utaendeshwa kama upepo unavyoiendesha tiara, ni njia rahisi ya kuwa Mobutu Seseseko.

Kwa wadau wanaotegemea mshikamano wa kidemokrasia nje ya nchi, nyakati zinaonesha, siasa za nyakati hizi, kutoka Washington, Brussels, mpaka Beijing na Kremlin siasa zinakuwa za kimaslahi kuliko za ki-ideolojia. Kama maslahi yao yanalindwa kwa dhati na watu walio madarakani, mshikamano watakaonesha ni wa maigizo zaidi. Na mbaya zaidi kuna hali ya mataifa makubwa kuelewana kwa kiwango fulani linapokuja suala la mataifa madogo yenye maslahi nayo, hii imeweza kuonekana DR Congo. Ni kama nyakati za Berlin Conference, utofauti ni kuwa kwa sasa tutayaona mataifa ya Asia pia kwenye meza.

Lingine tunaweza kusema kuna mataifa yanayoibukia, madogo, yenye nguvu za kiuchumi na yenyewe yanazunguka huku na kule kutengeneza ushawishi wao.

Tukiangalia hiki kipindi cha miaka mitano, moja ya chachu ya kubadilika kabisa kwa siasa zetu, ilitoka kwenye taifa la nje, taifa ambalo halikuwahi kuhusika kwa kiwango kikubwa kwenye siasa zetu. Kwa wafuatiliaji wa mambo tunafahamu namna siasa zetu zilivyochukua mkondo wa tofauti baada ya mkataba wa bandari, sio lengo la makala hii kuuchambua mkataba, ni mjadala uliopitia.

Lakini baada ya sekeseke lile lililohusisha nchi ya Falme za Kiarabu, ndipo hapo tuliona kuvunjika kwa maridhiano na siasa za maridhiano, mpunga au shekeli zikajaa kwenye siasa zetu, siasa za chochote kitu zikashamiri kweli kweli na hatujawahi kurudi nyuma.

Ukijumlisha haya yote ni kuwa siasa za kimataifa zinabadilika, mgawanyiko wa aina yeyote ndani ya nchi, utatufanya tuwe sehemu ya kutumika, kutumiwa na mwisho wa siku kupoteza uhuru wetu wa kuamua mambo.

La mwisho kabisa, Afrika Mashariki iko katika hatari ya kumezwa na siasa za ulimwenguni. Afrika Mashariki iko katika hatari ya kuwa sehemu ya majaribio ya siasa mpya za ulimwenguni, cheche zimeonekana Congo, na sasa zinaenda kusambaa.

Kwa kawaida, Tanzania imekuwa sehemu ambayo majirani wakiwa na matatizo ya kisiasa wamekuwa wakiiangalia kama rula, yaani wakitolea mfano; kuanzia umadhubuti wa viongozi, mamlaka ya kimaadili na hata misimamo ya kimataifa. Hata hivyo, kwa sasa kwa Afrika Mashariki wote tunafanana kwa kiwango kikubwa. Kenya watu wanatekwa na wenye Subaru, Tanzania watu wanatekwa na wenye Landcruiser, Uganda watu wanatekwa na wenye ‘drone’.

Naelewa hali ya wasiwasi mkubwa miongoni mwa watu wenye madaraka ilizuka baada ya maandamano ya GeN Z ya Kenya. Baada ya maandamano yale, tuliona mabadiliko makubwa katika siasa zetu hasa maonyo na masisitizo kutoka katika vyombo mbalimbali. Lakini pia mashaka yaliongezeka hasa vitendo vya utekaji; tuliona tukio la Sativa, tuliona Soka na wenzake wakipotezwa mpaka leo, tuliona tukio la utekaji na mauaji ya Ali Kibao, matukio ambayo mpaka leo hayajawahi kupata ufumbuzi.

Kwa Tanzania, Ile sura ya mzee mwenye busara Afrika Mashariki imepotea, kwa Afrika Mashariki hakuna wa kumgusa bega mwenziwe. Ni mlango wa fursa kwa mataifa mengine kuiendesha Afrika Mashariki. Kama hakuna mabadiliko, tuko kwenye nyakati za kihistoria sio tu Tanzania, bali hata Afrika Mashariki.

Hitimisho

Kuna siku nilikuwa naongea na mtu mmoja, akawa anaeleza kuwa wakati wa uchaguzi ni kawaida matukio kutokea, hasa mambo mabaya. Kichwani mwangu jambo pekee lililonijia ni kuwa mambo mabaya yanamtokea nani, hata hivyo aliendelea kuelezea, watu mbalimbali hukumbwa na kadhia na hata huzuni kubwa, ila ni mambo yanapita.

Kila nikifikiria yale matamshi ya yule mtu, bado nakumbuka sura yake. Alivyokuwa akiongea naamini alikua akiongea akimaanisha watu wengine, sio yeye wala familia yake, wala wapendwa wake, kama angekuwa ana uhakika mambo mabaya yangemkuta yeye au familia yake, nadhani aisingekaa kuwaza, kusema wala kufikiri, angesisitiza mambo mabaya yasimkute yeyote.

Nadhani kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na muafaka wa kitaifa, muafaka kama ule uliofanyika mwaka 1960 miezi mitatu kabla ya uchaguzi. Baada ya uzoefu wa mwaka 1958, Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Waingereza ilikubaliana na TANU kubadilisha mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa kwenye Katiba,ili kuboresha uchaguzi uliofanyika Agosti 1960.

Nakubali kuwa sio wakati sahihi kuwa na mabadiliko ya Katiba, ila kuna umuhimu wa kuwa na muafaka wa kitaifa. Kwanza, kwa viongozi wa kisiasa wanaoshikiliwa kuachiliwa, pili vyama vyote Tanzania kuruhusiwa kushiriki uchaguzi, tatu viongozi wa kisiasa wa pande zote kukutanishwa mbele ya wazee, viongozi wa dini, na kuwepo na makubaliano ya kuelekea uchaguzi wa 2025.

Kinyume na hapo naamini hali ya sasa italeta hali ya mashaka zaidi katika chaguzi zinazokuja, kama ambavyo hali mbaya ya uchaguzi wa 2020, imezaa hali ya mashaka ya uchaguzi wa 2025; nadhani itakuwa ni kawaida kwa chama chenye nguvu kufungiwa kufanya siasa miezi michache kabla ya uchaguzi, itakuwa ni kawaida kwa kiongozi wa upinzani mwenye ushawishi kufungwa kabla ya uchaguzi.

Na suala la uhalali wa kihistoria litakuwa sio la muhimu, kitovu cha madaraka kitaendelea kuhama kutoka siasa za kiraia kuelekea siasa za kiusalama, kwa sababu, kikombe cha uhalali kikitindika, kwa wengi hujazilizwa kwa ubabe; wanasiasa nao watakutana na mkanganyiko mpya wakigundua hawashikilii nguvu zote za kimadaraka.

Kama hakuna muafaka wa kisiasa, nadhani 2025 inaweza kuwa mwanzo wa nyakati za mashaka zaidi kihistoria kuwahi kuibuka Tanzania.

Tony Alfred K ni mchambuzi anayefanya kazi na The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tony@thechanzo.com  au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×