Dar es Salaam. Wananchi jijini hapa wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na wagombea kutoa zawadi kipindi cha uchaguzi, baadhi wakisema kitendo hicho kinaashiria upendo, huku wengine wakikiita kama rushwa ya kumshawishi mpiga kura kupiga kura kwa namna fulani.
Vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi vinakatazwa vikali nchini Tanzania, huku mamlaka kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikitoa onyo kali kwa vyama vya siasa na wagombea wao kutojihusisha na vitendo hivyo, au kuhatarisha kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria wakikaidi katazo hilo.
Kila msimu wa uchaguzi hapa nchini, vyama na wagombea wao hugawa zawadi mbalimbali, kama vile kofia, khanga, vitenge, na kadhalika, kwa wananchi kama sehemu ya kampeni zao kwa ajili ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi, hali inayoibua swali endapo kama hizi ni zawadi tu au ni rushwa ya kuwashawishi wananchi kuchukua uamuzi fulani.
Mwaka huu, wananchi watategemewa kupigia kura Rais, wabunge na madiwani kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na punde baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuteua wagombea wa nafasi hizo, wananchi watafikiwa kwa ajili ya kupewa zawadi hizo.
The Chanzo iliwauliza wananchi kadhaa jijini Dar es Salaam endapo kama watapokea zawadi hizo, ambapo walikuwa na mawazo tofauti.
Upendo kwa wananchi
Martha Kibuga, mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam, ameeleza kwamba yeye hazichukulii zawadi hizo kama rushwa, bali ni zawadi za kawaida ambazo viongozi wameamua kuzitoa kama upendo kwa wananchi wao na kuonyesha kuwajali.
SOMA ZAIDI: Serikali za Mitaa, Halmashauri Zaongoza Kulalamikiwa kwa Rushwa Dodoma 2022
“Nitaipokea kwa sababu imetoka kwa kiongozi wangu na nitaipokea kwa moyo mmoja na kwa upendo kwa sababu hajaja kuileta kama rushwa ila ameileta kama upendo,” alijibu Martha alipoulizwa kama atapokea zawadi hizo akipewa.
Martha aliongeza pia kwamba licha ya kupewa zawadi hiyo, bado atampigia mgombea huyo kwa sababu hata asipotoa kama ametokea kumpenda angempigia kura.
“Ni [zawadi] halali kwa sababu wenyewe wanatoa kwa upendo japokuwa kuna wengine wanaweza kufikiri kama rushwa, lakini kwangu mimi naona tu ni sawa kwa sababu wanatoa kwao kama upendo kama kuonesha upendo kwa wananchi au kupunguza kero kwa wananchi,” aliongeza Martha.
Licha ya kutofautiana kidogo na Martha kwa kuzielezea zawadi hizo kama rushwa, Oscar Kokonyoka, mkazi mwingine wa Mwananyamala, amedogosha uwezo wa zawadi hizo kumshawishi mwananchi apige kura kwa namna fulani, akisema mwananchi anaweza kuzipokea na bado asipimpigie kura mtu aliyempatia.
“Wewe ukiwa kama mwananchi ambaye unajua kiongozi gani anayekufaa, unaweza ukachukua zawadi, halafu vilevile yeye ambaye amekupa hii zawadi ukashindwa kumpitisha pia, na inawezekana pia ukaacha kabisa kuchukua na zawadi yenyewe ambayo wanayoileta kwako,” Kokonyoka ameeleza.
SOMA ZAIDI: ‘Samaki Mkunje Angali Mbichi’: Shule Zinavyoandaa Vijana Dhidi ya Vitendo vya Rushwa
Fikiri Beti, mkazi wa Dar es Salaam, anasema suala la zawadi kama rushwa ya uchaguzi halina mjadala, akihoji kwa nini mgombea atoe rushwa kwenye uchaguzi kama vile utumishi ni kazi inayolipa sana.
Utazirudisha vipi?
“Kiongozi kama kiongozi, wewe una nia ya kugombea uongozi, kwa nini utoe pesa?” anauliza mwananchi huyo. “Je, zile pesa unazozitoa kuna biashara gani ya kuingiza kwenye uongozi ili urudishe pesa zako?”
Beti anaamini mgombea anayefanya hivyo hana sifa za uongozi, kwani anasema kiongozi bora anatakiwa aoneshe maendeleo makubwa katika jimbo lake.
Alipoulizwa endapo kama ataikataa zawadi kutoka kwa mgombea, Beti alijibu: “Mimi akiniletea zawadi napokea kwa sababu sijamuomba, sawa? Yeye atanipa zawadi, nitapokea, nitazitumia. Lakini mimi mwenyewe nitajua jinsi gani, au nitajua nimchague nani kwa sababu zawadi kaniletea kwa hiari yake, sijamuomba.”
Kwa mujibu wa TAKUKURU, si zawadi zote zinaweza kuangukia kwenye kundi la rushwa. Kilicho muhimu, kwa mujibu wa mamlaka hiyo, ni wakati zawadi hiyo inatolewa.
SOMA ZAIDI: CCM Imeongeza Wapigakura Kuzuia Rushwa, Kwa Nini TFF Imewapunguza?
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo kwenye kikao chake na wahariri Aprili 30, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema zawadi wakati wa uchaguzi zinapaswa kuangaliwa kwa makini.
“Kuhusu zawadi, je, unatoa muda gani?” aliuliza Chalamila. “Tunaishi wote eneo hili na hujawai kutoa zawadi, iweje leo uje utoe zawadi ilihali umetangaza kugombea eneo hili hili? Hizo zawadi lazima ziangaliwe.”
Baadhi ya wananchi waliozungumza na The Chanzo wanakubaliana na msimamo huu wa TAKUKURU, wakisema waziwazi kwamba zawadi hizo ni rushwa inayopaswa kudhibitiwa wakati wa uchaguzi.
Siyo sahihi
“Hili suala, wacha niseme ukweli, siyo sahihi kwa sababu ina maana umekaa miaka mitano hukuifanyia chochote, lakini kinakuja kipindi cha uchaguzi, yaani unajua bado miezi miwili uchaguzi ndo unaanza kuleta zawadi, unaleta ukaribu na wananchi,” Ramadhani Kidile, mkazi wa Dar es Salaam, anasema.
“Lakini kipindi cha miaka mitano, miaka minne ya nyuma, yaani unakuwa huonekani, halafu unakuja kuonekana kwenye uchaguzi bado miezi miwili au mitatu, kwa hiyo, afsiri yake ni rushwa, na siyo sahihi,” aliongeza.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ni Muhimu Kwa Ustawi wa Jamii na Kupunguza Umaskini
Destiny Chakupewa, mkazi wa Makumbusho, Dar es Salaam, pia anaamini kwamba suala la zawadi wakati wa uchaguzi haliwezi kuwa ni suala linaloweza kuruhusiwa na sheria, kwani kufanya hivyo kutasababisha jitihada zote za kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi kushindwa kufanikiwa.
“Kwa sababu mara nyingi tunajua kabisa kura ni siri, na watu hawatakiwi kabisa kujua huyu atamchagua mtu fulani na wananvyogawa hivi hizo zawadi wanakuwa wanawashawishi [wananchi] ili waweze kuwachagua, kitu ambacho ni kinyume kabisa na sheria na haifai,” alifafanua Chakupewa.
Veronika Ezekia ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia veronikaezekia22@gmail.com.