Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imevitaka vyama kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kwamba Ofisi hiyo haitosita kuchukua hatua endapo itabaini kuna sheria au kanuni zinakiukwa na vyama hivyo.
Akizungumza kwenye warsha ya vyama vya siasa juu ya Sheria ya Gharama za uchaguzi iliyofanyika Jumatatu, Agosti 18, 2025, CPA jijini Dar es Salaam, Edmund Mugasha ambaye ni Mkuu wa Ruzuku katika Ofisi ya Msajili amevisihi vyama kuwa makini katika hatua za awali za uteuzi wa wagombea kwa kuwa ofisi yao inaweza kuwasilisha taarifa za ukiukwaji kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kabla ya uteuzi.
“Sasa ndugu viongozi, wakati mnaendelea na michakato yenu ya ndani ya kuteua wagombea, msajili yuko macho. Yeyote atakayevunja au kwenda kinyume na masharti ya kifungu cha 21, 22 na 23 kuhusu makatazo, moja kwa moja anaweza kukosa sifa za kuteuliwa na INEC. Msajili ana nguvu hiyo kisheria, na sheria imeweka utaratibu huo kwa uwazi,” alisema Mugasha.
Warsha hiyo iliandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kwa lengo la kuwajengea uelewa viongozi wa vyama kuhusu masharti ya sheria h na wajibu wa kila chama na mgombea katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na wa uwazi.
Kuhusu gharama za uchaguzi Mugasha amesema kuwa sheria imempa Msajili nguvu na wajibu mkubwa wa kuhakikisha utekelezaji wa masharti yake na amebainisha kuwa tayari fomu za kutangaza gharama za uchaguzi zimesambazwa katika maeneo yote nchini kuanzia kwenye majimbo 272 na kata 3,960.
“Ndugu viongozi, kifungu cha 4 cha sheria kinampa nguvu Msajili wa Vyama vya Siasa na wajibu wa kusimamia sheria hii. Ukiangalia kifungu cha 36, 50 na hata 62 cha Sheria ya Uchaguzi kinasema wazi kuwa mgombea au Tume itakataa kumteua mtu yeyote iwapo itaridhishwa na Msajili kwamba amekiuka sheria ya gharama za uchaguzi. Hivyo basi, msajili ana mamlaka ya kufanya uchunguzi na hata kuweka pingamizi kwa mgombea yeyote atakayekwenda kinyume na masharti,” alifafanua Mugasha.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila chama na mgombea kuhakikisha fomu za gharama za uchaguzi zinajazwa na kurejeshwa kwa wakati kama Sheria inavyomtaka kabla ya siku ya uteuzi, na kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha mgombea kukosa sifa.
Naye Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohammed Ally Ahmed amesema kuwa uwepo wa sheria ya gharama za uchaguzi inalenga kuweka mazingira ya usawa kwa wagombea, bila kujali uwezo wao wa kifedha.
“Lengo ni kuhakikisha kwamba mashindano ya kisiasa hayatakiwi kuwa ni mashindano ya fedha, bali ya sera na sera pekee. Ndiyo maana msajili amepewa nguvu ya kuhakikisha masharti haya yanazingatiwa,” alisema Ahmed.
Ofisi ya Msajili imevitaka pia vyama vya siasa kuhakikisha wagombea wao wanakuwa wazi juu ya vyanzo vyao vya mapato binafsi pamoja na vyanzo vya mapato ya fedha watakazozitumia kwenye uchaguzi.