Kwenye tasnia niliyopo, hii ya habari, kuna mazingira magumu sana ya kufanya kazi. Kwa mfano, na hili nimelizungumza sana, ili uweze kufanya uandishi wa habari Tanzania, ni lazima upewe kibali na Serikali, ambayo wao wanaiita “ithibati.” Hii ni leseni, kutoka kwa Serikali, kwenda kwa mwandishi, inayomuwezesha kufanya kazi yake ya uandishi.
Utaratibu huu ni wa ajabu kwa sababu mbalimbali, ikiwemo hiyo inayohusu uwezo unaoipa Serikali ya kuingilia uhuru wa mtu wa kufanya kazi, unaohakikishwa na Katiba na sheria zingine za nchi. Ingeeleweka kama Serikali ingeweka utaratibu kwamba kama unataka kuhudhuria idara mahususi za Serikali ili kuandika habari zake – Bunge, Ikulu, Mahakama, n.k., – basi uwe na hiyo ithibati. Hivyo ndivyo inavyofanyika ulimwenguni kote.
Lakini kuweka utaratibu kwamba huwezi kufanya kazi ya uandishi kabisa kabisa, hata kama ingekuwa ni kuandika kuhusu miti na wanyama, bila kuwa na hicho kinachoitwa “ithibati,” ni kitu kingine kabisa kisichoingia kabisa akilini. Kwenye tasnia ya sheria, kwa mfano, haiko hivyo. Leseni utapewa kama unataka kuwakilisha wateja mahakamani. Kama hilo siyo lengo, leseni si lazima, na huzuiwi kufanya kazi zinazohusiana na sheria.
Hata inapokuja kwa chombo cha habari kama taasisi pia kuna mambo ya ajabu ambayo nadhani yapo kwenye tasnia hii tu ya habari. Kwa mfano, leo ukianzisha kampuni ya habari ukaiita XYZ Co. Ltd, ukapata usajili kutoka kwa mamlaka husika na ukawa na uwezo wa kufanya kazi kisheria, ukitaka tu kuchapisha habari mtandaoni, lazima upate usajili na leseni mpya kutoka mamlaka moja ya Serikali, na ukitaka kuwa na gazeti, lazima upate leseni mpya kutoka kwa mamlaka nyingine ya Serikali!
Ni mambo ya ajabu kweli kweli ambayo, kama nilivyosema, hayaingii akilini hata kidogo. Licha ya mazingira kuwa magumu kiasi hiki, Watanzania mbalimbali wameendelea kuingia na kuwekeza nguvu, akili, muda na mali zao kwenye uandishi wa habari. Hawa siyo kwamba ni wajinga, kwamba labda hawajuwi hatari inayowakabili, la hasha! Wanajua, lakini wameamua kuchukua uamuzi huo licha ya uwepo wa hatari hizo.
SOMA ZAIDI: ACT Wazalendo Walitaka Jeshi la Polisi Kumuachia Makamu Mwenyekiti Wao Mchinjita
Swali linakuja, je, kama ulijua kwamba mamlaka inaweza kukuamrisha ushushe maudhui fulani uliyoyapandisha, kwa sababu itakatazozitaja, ukifanyiwa hivyo tunapaswa kukuhurumia? Kama tulikuonya kwamba Serikali inaweza kufungia gazeti lako, bila ya amri ya Mahakama, na muda mwingine bila hata kukusikiliza, kwa nini tukae upande wako pale hatua hiyo inapochukuliwa dhidi yako?
Sakata la ACT Wazalendo
Nimeona ni muhimu kutoa huu mfano ili niweze kuelezea vizuri kile kinachotokea kwa ACT Wazalendo, na ukosoaji ambao, kwa maoni yangu, naona si wa haki, na hauna ishara ya kutusaidia, kwa namna yoyote ile, kwenye harakati zetu za kudai mageuzi muhimu kwenye nchi yetu.
Kwa sababu, moja kati ya ukosoaji mkubwa unaoelekezwa kwa chama hicho cha siasa kwa sasa, hususan kufuatia kuenguliwa kwa mgombea wake wa Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Luhaga Mpina, ni kwamba chama hicho hakipaswi kulalamikia hatua hiyo kwani walijua, au angalau walipaswa kujua, kwamba ingetokea.
Wengi wetu tumeelekeza nguvu kubwa kwenye kuikumbusha ACT Wazalendo, “Mnaona, tuliwaambia,” katika hali ambayo, kwa mtazamo wangu, inatokosesha fursa ya kuona nini haswa hii hatua inamaanisha, ambayo kimsingi ni kusafishiwa njia kwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, aingie kwenye uchaguzi huo bila mpinzani yeyote wa maana.
Jambo moja kubwa linalonitatiza mimi binafsi ni kwamba, kweli, sisi kama wapigania mageuzi, katika mazingira ambapo chama tawala na vyombo vya dola vinapambana na chama cha upinzani tunaona ni busara kukikandia chama hicho, hata kama tuna mashaka juu ya lengo la kuanzishwa kwake? Kwamba kati ya pande hizi mbili, zenye kuzidiana ubavu na nguvu kwa viwango vikubwa, tunaona ni vyema kuelekeza ukosoaji wetu kwa pande dhaifu na nyonge?
SOMA ZAIDI: ACT Wazalendo: Miaka 11 na Dira ya Mapambano ya Ukombozi wa Umma
Tuchukulie shutuma tunazozielekeza kwa ACT Wazalendo ni za kweli, je, si kwa maslahi yetu kwamba pale inapodhihirika, kama hivi sasa, Dola limetangaza vita na chama hicho, kusimama nacho, na hata kama siyo kwa kukiunga mkono hadharani, basi angalau kujizuia kuchukua hatua zinazoweza kukoleza moto wa dola dhidi yake?
Nadhani tunaweza kufanya vizuri zaidi badala ya kutoa fursa kwa watesi wetu kufahamu udhaifu wetu kwamba tunaweza kugawanyishwa kirahisi, na hivyo kutengeneza mazingira wezeshi ya hilo kufanyika kwa kiwango kikubwa zaidi. Maana kugawanyika kwetu hakuwezi kuwa ni hasara kwa watesi wetu, bali faida kubwa.
Mapambano
Nimalizie safu hii – ambayo awali nilikusudia niandike tu kwa ufupi kwenye mtandao wa X, lakini nikaona bora nieleze kwa upana kwa hofu ya kueleweka vibaya, kitu ambacho si cha nadra sana siku hizi kutokea – kwa kurudia jibu ambalo hupenda kuwapa watu wanaonukuu kauli ya Serikali kwamba Tanzania kuna uhuru wa habari, na ndiyo maana tunaona vyombo vingi vya habari vikianzishwa.
Jibu langu, siku zote, limekuwa kwamba hapa Tanzania, angalau kwa ufahamu wangu, watu hawaingii kwenye tasnia ya habari, na kuweza kufanya wanayoyafanya, kwa sababu eti wanaona, au wanaamini kuna uhuru wa habari Tanzania.
Ukweli wa mambo ni kwamba wengi makini waliopo kwenye tasnia wameingia, na wameendelea kufanya kazi zao, licha ya kutokuwepo kwa huo uhuru. Kwa maneno mengine, wengi wao wanaelewa vizuri hakuna uhuru wa habari Tanzania, na hiyo ndiyo sababu iliyowasukuma kuingia, wakiamini wanaweza kuchangia kwenye jitihada za kupatikana kwa uhuru huo.
SOMA ZAIDI: Kwetu Sisi ACT Wazalendo, Mahakama ni Ulingo Mwingine wa Mapambano, Tutaitumia Ipasavyo
Watu kama hao wapo pia kwenye sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali, na wapo pia kwenye vyama vya siasa, na maoni yangu ni kwamba hatutakuwa tunawatendea haki, na kimsingi, hatutakuwa tunajitendea haki, pale inapotokea wanapigwa rungu na dola, tukajitokeza, siyo kuwaunga mkono na kuwatia moyo, bali kuwauliza: “Kwani si tuliwaambia, mkajifanya wajuaji?”