Familia ya Al-Hajj Nourdin Mushi (25) imeendelea kumtafuta baada ya kuchukuliwa na watu wenye silaha maeneo ya Tegeta Kibo mnamo Septemba 05, 2025.
Al-Hajj Mushi anayeishi na kaka yake, Ally Mushi, alimuaga kaka yake kuwa anaenda kukutana na mteja wa kukodisha gari maeneo ya Tegeta Kibo Complex mnamo Septemba 05, 2025.
Hata hivyo majira ya saa moja jioni,alichukuliwa kinguvu na watu wenye silaha walioodoka naye katika gari aina ya Toyota Wish. Al-haji alikipiga kelele kuwa anatekwa katika jitihada za kukabiliana na watu hao, hata hivyo walimzidi nguvu na kuondoka naye. Hakukua na yeyote katika kadamnasi aliyeweza kutoa msaada wa moja kwa moja kudhibiti watu hao.
“Ni kijana mdogo tu wa miaka 25, aliniomba ruhusa anaenda Kibo Complex kibiashara, alivyoenda pale hakurudi tena. Sasa kesho asubuhi tukaenda hiyo sehemu-Kibo Complex, [mashuhuda] wakatuambia kumbe nyie ni ndugu ya yule jamaa aliyetekwa,” anaeleza kaka yake ndugu Ally.
Al-Hajj ni maarufu katika mtandao wa Instagram kupitia ukurasa wake wa @kings_hot_riders ambao husambaza picha kuhusu magari ya kifahari Tanzania. Sehemu kubwa hupiga picha na kusambaza picha hizo kwa ridhaa za wamiliki wa magari hayo.
Tukio hili limeripotiwa polisi kituo cha Mbweni na kupewa RB namba: MBN/RB/2209/2025, kama una taarifa zozote unaweza kuwasiliana na familia kupitia namba 0683772862.