Taarifa za kifedha za Benki Kuu ya Tanzania za Agosti 2025, zinaonesha Benki hiyo imeimarisha akiba yake ya dhahabu kufikia dhahabu zenye thamani ya shilingi Bilioni 821.8 kufikia Agosti 31, 2025.
Ongezeko hili ni kubwa zaidi kutokea toka Oktoba 2023, BoT ilipoanza kununua dhahabu kwa ajili ya akiba. Mpaka kufikia Julai 31, 2025, Benki Kuu ilikua na akiba ya dhahabu yenye thamani ya Bilioni 171.9, hata hivyo ndani ya mwezi mmoja, Benki Kuu imeweza kuwa na akiba inayofika Bilioni 821.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 377.8.
Akiba hii ya dhahabu ni sehemu ya mkakati wa Benki Kuu katika kukabiliana na mabadiliko ya dunia, ikiwemo vita ya kibiashara kati ya mataifa makubwa.Pia mabadiliko ya kisera katika biashara za dunia yanayoathiri hali ya kiuchumi katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Katika ripoti yake ya sera ya uchumi ya mwezi Julai 2025, Benki Kuu ilieleza kuwa manunuzi ya dhahabu yalilenga kuimarisha nguvu ya shilingi katikati ya changamoto za kidunia.
“Mvutano wa kisiasa unaoongezeka duniani, migogoro ya kibiashara, na mabadiliko katika sera za misaada ya nje ya Marekani vimeongeza hali ya wasiwasi duniani, na kusababisha Mabenki kuangalia upya uwekezaji wao wa kifedha kukabiliana na viashiria hatarishi,” ripoti ya sera ya uchumi ya BOT ya mwezi Julai 2025 inaeleza.
“Ununuzi wa dhahabu wa ndani uliofanywa na Benki umeongeza ukwasi, jambo ambalo kwa sehemu limepunguza shinikizo kwenye shilingi,” BOT imeeleza zaidi.
Shilingi imeendelea kuimarika katika siku za hivi karibuni kutokana na hatua mbalimbali ikiwemo ya manunuzi ya dhahabu. Mambo mengine yaliyosababisha kuimarika kwa shilingi ni pamoja na utalii, mauzo ya mazao, pamoja na mauzo ya dhahabu nje.
Kutokana na changamoto mbalimbali za kidunia, ikiwemo hali ya wasiwasi baada ya vita vya Ukraine, mabadiliko ya mara kwa mara ya sera za Marekani, lakini pia na mabadiliko ya kasi ya kisiasa za kidunia yanayoendana na vuta nikuvute za kikanda, Benki Kuu nyingi duniani zimehamia katika manunuzi ya kasi ya dhahabu toka mwaka 2023. Wengi wakipunguza utegemezi wa uhifadhi wa akiba kupitia dola kama ilivyozoeleka.
Kwa mujibu wa Baraza la Dhahabu Duniani kwa mwezi Juni nchi zilizoongoza kwa kununua dhahabu ni pamoja na: Uzbekistan (tani 9), Kazakhstan (tani 7), Singapore (tani 6), China, Uturuki na Cheki; tani mbili kila moja. Na kwa nchi za Afrika Ghana iliongozo kwa kununua tani 1. Kwa mwezi Julai nchi zilizoongoza ni pamoja na Kazakhstan iliyonunua tani 3, Uturuki, China na Cheki walionunua tani mbili kila moja, Uganda nayo imetangaza kuanza kuhifadhi dhahabu.
Kwa mwaka 2025 nchi iliyoongoza katika kununua dhahabu ni Poland, ambapo imenunua tani 67. Poland ni moja ya nchi ambayo iko katika mvutano mkubwa na Urusi, ambapo mnamo Septemba 10, 2025, ndege nyuki (drone) takribani 19 kutoka Urusi ziliingia katika anga la Poland, huku ndege nyuki tatu zikiangushwa. Urusi imesisitiza haikua na nia ya kuivamia Poland, jambo ambalo Poland imeendelea kulipinga, na kusisitiza Urusi ina njama dhidi yake.
Dhahabu imeendelea kuwa bidhaa inayokimbiliwa wakati wa mashaka, na kwa sasa duniani dhahabu imeendelea kupanda thamani kutokana na mahitaji kuongezeka.
Tanzania imeendelea kunufaika ikiwa kama moja ya mzalishaji mkubwa wa dhahabu Afrika, mkakati wa BoT kununua dhahabu unakuwa na manufaa mara mbili katika uchumi; kwanza kuimarisha shilingi lakini pili kupunguza utegemezi na shinikizo juu ya kuhitaji fedha za kigeni katika kuleta mizania ya sera za kiuchumi.