Ni jambo la kawaida kabisa: tunafika kwenye sherehe, au mkutano wa kifamilia, mtoto wetu mdogo anashikamana na mguu, anafunika uso au analia mtu anapojaribu kumsemesha.
Wengine hata wakiona wenzao wakicheza, wanakaa pembeni wakiogopa kujiunga. Wazazi wengi hujiuliza, “Kwa nini mtoto wangu anaogopa watu au watoto wenzake?”
Kwanza, ni vizuri tujue kwamba hii ni sehemu ya kawaida ya ukuaji wa mtoto. Wataalamu wa malezi wanasema kati ya miezi 18 na miaka mitatu, watoto wengi huanza kutambua tofauti kati ya watu wanaowazoea na wageni.
Hapa ndipo tunapoona tabia ya hofu kwa watu wasiojulikana, au stranger anxiety kwa kitaalamu. Ni kama mfumo wa asili wa ulinzi wa mtoto anakuwa makini zaidi ili ajilinde.
Utafiti wa Profesa Jerome Kagan kutoka Chuo Kikuu cha Harvard umeonesha kuwa karibu asilimia 15 hadi 20 ya watoto huzaliwa wakiwa na hulka ya aibu au woga. Hawa ni wale wanaoonesha tabia hizo haraka wanapokutana na mazingira mapya iwe ni mtu mpya, sehemu mpya au kelele zisizotarajiwa.
SOMA ZAIDI: Leo Tujadili Maumivu ya Kihisia Wazazi Tunawarithisha Watoto Wetu
Wazazi wengi hushangaa: “Lakini kwa nini aogope hata watoto wenzake?” Ukweli ni kwamba watoto wenzao pia wanaweza kuonekana kama changamoto.
Watoto wadogo huwa hawana ustadi mkubwa wa kijamii, na wanaweza kuchukua vitu ghafla, kupiga kelele, au kukimbia bila kutarajiwa. Kwa mtoto mwenye woga, haya yote ni ya kutisha kama vile kukutana na mgeni asiyejulikana.
Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Child Development mwaka 2018 ulionesha kuwa watoto wadogo wanahitaji muda na mazoezi ya mara kwa mara kabla ya kuzoea kucheza na wenzao. Hii ni safari, kama kujifunza kutembea – hatua kwa hatua.
Wazazi tufanye nini?
Hali hii inaweza kutufanya tujisikie vibaya au hata aibu, lakini sio kosa letu wala kosa la mtoto. Badala ya kumlazimisha “aende acheze,” au aongee na watu tunaweza kumsaidia kwa njia za upole.
Tunaweza kumpa muda na nafasi aangalie kwanza kabla ya kushiriki, kumuonesha mfano – tukiwa wenyewe tukisalimiana na kuongea kwa urafiki, watoto hujifunza kupitia sisi, au kuanza na hatua ndogo ndogo, kama vile kupanga michezo midogo midogo.
Au tunaweza kumkutanisha na mtoto au mtu mmoja mmoja badala ya kundi kubwa, au kumsaidia mtoto kutambua hisia zake – tunaweza kusema, “Naona unaogopa mwanangu. Ebu tukae pamoja kidogo kwanza.”
SOMA ZAIDI: Namna Wazazi Tunavyoua Ujasiri wa Watoto Wetu Bila Kujua
Kwa msaada, upendo na uvumilivu, watoto wengi hukua wakishinda hofu hizi. Wanapofika miaka ya awali ya shule, wale waliokuwa wakijificha nyuma ya miguu yetu wanageuka kuwa watoto wanaokimbia na kucheka na wenzao uwanjani.
Na hata kwa wale wenye hulka ya aibu zaidi, mara nyingi tabia hiyo hujenga tabia muhimu ukubwani wanapokua kama huruma, umakini na fikra za kina.
Kwa hiyo, mtoto anapokuwa na hofu ya watu au watoto wenzake, tusione kama ni tatizo kubwa. Ni sehemu ya ubongo wake unaokua na kutafuta njia salama ya kukabiliana na ulimwengu.
Kazi yetu kama wazazi ni kumpa moyo, uvumilivu na nafasi ya kujifunza taratibu. Hatua ndogo ndogo za leo ndizo zitakazomsaidia kesho awe na ujasiri wa kujitokeza na kushirikiana na wengine.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.