Leo napenda tuzungumze jambo ambalo mara nyingi halipewi nafasi kwenye malezi: umuhimu wa kuwasaidia watoto kuelezea hisia zao.
Wengi wetu tulikua kwenye familia ambako hisia hazikupewa nafasi. Tulipolia, tuliambiwa “Nyamaza” au “Usilie kama mtoto mdogo.” Tulipokasirika, tulisukumiwa chumbani na kuambiwa “Nenda kalale.”
Si kwamba wazazi wetu hawakutujali, bali kwa sababu nao hawakufundishwa namna ya kutambua na kuheshimu hisia. Matokeo yake, tulijifunza kuficha hisia badala ya kuzishughulikia.
Utafiti unaonyesha kwamba watu wanaokua bila kujua lugha ya hisia hujipata wakihangaika zaidi na msongo wa mawazo, matatizo ya mahusiano, na hata afya ya mwili. Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kujua na kudhibiti hisia ni sehemu ya msingi ya afya ya akili na ustawi wa kijamii.
Tusome hadithi ya Juma tuwe na uelewa zaidi.
Juma ni mvulana wa miaka tisa. Shuleni anajulikana kwa uchangamfu, lakini nyumbani mara nyingi alijifungia chumbani. Aliposhindwa katika mchezo, alikasirika sana. Akikosea darasani, alikaa kimya siku nzima. Wazazi wake walihisi wasiwasi na walijiuliza, “Kwa nini Juma huficha hisia zake? Tumempa kila kitu, lakini bado anaonekana kubeba mzigo ndani yake.” Walikuwa wanampenda, lakini hawakujua namna ya kumsaidia.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wadogo Huwa na Hofu ya Watu, Hata Watoto Wenzao?
Walipoanza kubadili mtazamo wao, mabadiliko yalipoanza kuonekana. Badala ya kumwambia “Usilie”, walianza kumuuliza, “Unajisikiaje sasa?” Badala ya kumtenga alipokasirika, walimpa nafasi ya kutulia na kisha kumwalika kuzungumza. Polepole, Juma alianza kubadilika.
Alijifunza kusema waziwazi, “Nimehuzunika kwa sababu rafiki yangu hakutaka kucheza na mimi” au “Ninajisikia aibu kwa kuwa nilikosea mbele ya watu.” Mafanikio haya yalikuwa zaidi ya kushinda michezo au kupata alama nzuri darasani; yalikuwa ni ushindi wa utu na afya ya akili.
Wanasaikolojia wanasema kuwa uwezo wa watoto kuelewa na kuelezea hisia zao ni sawa na kujifunza kusoma na kuandika. Daniel Goleman, mtaalamu wa akili ya hisia, anaeleza kuwa watoto wanaojifunza kudhibiti na kueleza hisia zao hujenga uwezo mkubwa wa kushirikiana na wengine na kufanikiwa maishani.
Utafiti kutoka Harvard Center on the Developing Child unaonyesha kuwa watoto wanaopewa nafasi ya kuzungumza hisia zao nyumbani hupunguza hatari ya matatizo ya afya ya akili wanapokuwa watu wazima. Kwa maneno mengine, kila mara tunapomruhusu mtoto kuzungumza kuhusu huzuni, hasira au furaha, tunamjengea kinga ya maisha yake ya baadaye.
Familia ya Juma iliunda utaratibu wa kila jioni kukaa pamoja na kuzungumza kuhusu hisia za siku. Mwanzoni ilikuwa ngumu; wengine walicheka au kukaa kimya. Lakini kadri muda ulivyopita, ikawa desturi yenye thamani kubwa.
SOMA ZAIDI: Leo Tujadili Maumivu ya Kihisia Wazazi Tunawarithisha Watoto Wetu
Kupitia mazungumzo haya, Juma alijifunza kwamba kulia si aibu, kusema “samahani” si udhaifu, na kusamehe ni sehemu ya utu. Mazungumzo hayo madogo ya kila siku yaligeuka kuwa darasa muhimu lililomsaidia kukua akiwa salama kihisia, mwenye ujasiri wa kujieleza, na mwenye huruma kwa wengine.
Tunapojenga utamaduni wa kuzungumza hisia nyumbani, tunawasaidia watoto wetu kukua wakiwa na afya ya akili bora. Hatuhitaji vitabu vingi wala semina nyingi. Tunachohitaji ni muda, subira na huruma. Na tukifanya hivyo, tunabadilisha urithi tulioupokea, tukiwaandalia watoto wetu mustakabali ulio na nguvu ya kuelewa na kueleza nafsi zao.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.